Sheria ya Mvuto wa Binadamu
Question
Je,ni kweli ipo Sheria ya mvuto wa binadamu?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Sheria ya Uislamu imeleta matumaini mema na kuwa na dhana nzuri. Mtume S.A.W alibainisha kuwa kama mtu akiwa na dhana nzuri na kutumaini mema, basi atakuta kheri, furaha, na baraka katika maisha yake, na Mtume S.A.W alitaja Hadithi nyingi kuhusu jambo hili, miongoni mwao ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah Ibn Abbas R.A. kuwa Mtume S.A.W aliingia kwa bedui (aliekuwa anaumwa) kumjulia hali, na ilikuwa kawaida ya Mtume S.A.W. kila anapoingia kwa mgonjwa alikuwa akisema “Hapana neno, ni twahara akipenda Allah”. Yule bedui akasema, "Kutwaharishwa?, Hapana hii ni homa inayochemka, au inayomsumbua mwanamume mkongwe, na itamsababishia mauti" Akasema Mtume S.A.W., “Basi ni neema pia”. Pia Mtume S.A.W. alisema : “Dhana nzuri ni miongoni mwa ibada nzuri”, Hadithi hii imepokelewa kutoka kwa Abu Dauud na Al-Hakim kutoka kwa Abu Hurairah.
Imetajwa katika Hadithi Qudsi kuwa : “Hakika Mwenyezi Mungu anasema: Mimi nipo mbele ya dhana ya mja wangu kwangu, kama akidhani dhana nzuri basi ni nzuri, na kama akidhani dhana mbaya basi ni mbaya”. Imepokelewa kutoka kwa Al-Tabarani kutoka kwa Wathilah.
Na katika Hadithi nyingine : “Mwenyezi Mungu ameamuru mja mmoja aje ili kusimama ukingoni mwa moto wa Jahanam, aliposimama ukingoni mwake akasema : Ewe Mola wangu nilikuwa na dhana nzuri kwako, Mwenyezi Mungu akawaambia Malaika wake : Mrudisheni kwani Mimi nipo mbele ya dhana ya mja wangu kwangu”.
Vile vile imetajwa katika baadhi ya Hadithi kuwa : “Mwenye kuambiwa jambo zuri lolote kuhusu Mwenyezi Mungu na akalifanya akimwamini na akilenga thawabu yake, basi Mwenyezi Mungu atampa thawabu hii hata kama hali haikuwa hivyo”, mwishoni mwa Hadithi alisema kuwa: “Kama mmoja wenu akiwa na dhana nzuri kwa jiwe, Mwenyezi Mungu atamnufaisha nalo”.
Hadithi zinazobainisha maana ya jambo hili ni nyingi sana na zinaithibitisha zaidi. Kwa hivyo, Uislamu uliwahimiza wafuasi wake kuomba dua. Na kwa kawaida dua inakuja baada ya kutarajia kheri iliyopeleka mtu kuiomba kutoka Mwenyezi Mungu. Mtume S.A.W. alibainisha kuwa dua inaboresha hali ya mwanadamu na inageuza yaliyoandikwa katika majaaliwa ya Mwenyezi Mungu; yaani pengine mwanadamu mmoja atapata jambo la shari, akiomba dua Mwenyezi Mungu atamondoshea shari hii na atambadilishia kheri. Imetajwa katika Hadithi kuwa watu wawili walikuwa na usawa katika kazi zao duniani, mmoja wao akamwona mwenzake katika Pepo ya Firdaus ya juu kabisa Siku ya Kiyama, mtu yule akamwuliza Mola wake kuhusu jambo hili ingawa walikuwa na usawa katika kazi, Mwenyezi Mungu alisema : “Yeye alikuwa akiniomba Pepo ya Firdaus ya juu kabisa”.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu alitujaalia Waislamu, alitujulisha mambo tusiyoyajua, alitufungulia milango ya furaha ulimwenguni ili tugundue Sheria za ulimwengu zinazoafikiana na aliyokuja nayo Mtume S.A.W. ili tuseme kwa ndimi zetu na nyonyo zetu kuwa: Mwenyezi Mungu alisema kweli na Mtume wake S.A.W. pia.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote