Kufanya Kazi Katika Pahala pa Kuuza...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kufanya Kazi Katika Pahala pa Kuuza Pombe na Nyama ya Nguruwe Katika Nchi Zisizo za Kiislamu

Question

Mimi ni kijana wa kiislamu, nafanya kazi nchini Uholanzi katika Duka kubwa (Super market) la Mwislamu ambapo zinauzwa baadhi ya chupa za pombe na nyama za nguruwe, na nimetafuta kazi nyingine lakini kwa bahati mbaya sijapata kwa wakati huu. Nifanyeje kwa sasa? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Hakika Wafuasi wa madhehebu ya Abu-Hanifa wanahalalisha suala la kuamiliana na wasio Waislamu katika nchi zisizo za Kiislamu kwa mikataba batili ikiwa hivyo kwa ridhaa zao na mapatano ya kukubaliana kama vile uuzaji wa pombe na nyama za nguruwe na riba na kila vinavyofanana na hivyo miongoni mwa miamala batili, jambo ambalo linaafikiana na swali la muulizaji kwa kuwa asili ya wale wanunuzi wa vitu hivyo katika hilo Duka kubwa ni makafiri, na wafuasi wa madhehebu ya Abu-Hanifa wamepata dalili nyingi juu ya suala hili. Miongoni mwa dalili hizo ni Hadithi yenye hukumu ya Mursal ya Makhul kutoka kwa Mtume S.A.W.: "Hakuna riba kati ya Waislamu na watu wa vita katika nchi ya vita" ilitajwa na Al-Shafi katika kitabu cha: [Al-Umm, 7/359], na Al-Zailai’i katika kitabu cha [Nasb Al-Raya, 4/44], na Ibn Hajar katika kitabu cha [Al-Diraya fi Takhrij Ahadith Al-Hidaya, 2/158], na Ibn Kudama katika kitabu cha: [Al-Moghny, 4/47] ingawa alisema: Habari yao ni Mursal usahihi wake haujulikani, na inawezekana yeye alikuwa anataka kulikataza suala lile.
Na miongoni mwa dalili zao ni kwamba Mtume S.A.W alipowakomboa Bani Qainuqai walisema: Sisi tunawadai watu bado hatujapata mali zetu, basi Mtume S.A.W. aliwaambia: "Muwe na haraka kupata mali zeni au mziache" na alipowakomboa Bani An-Nadr walisema: Sisi tunawadai watu basi Mtume S.A.W. aliwaambia: "Mziache mali zenu au muwe na haraka ya kuzipata", na inajulikana kwamba miamala ya aina hiyo baina ya Waislamu ni miongoni mwa milango ya miamala ya riba kwa hiyo ni batili.
Kadhalika wamepata dalili juu ya suala hili kwa mashindano yalikuwa baina ya Mtume S.A.W. na Rukana alipokuwa bado Makka na Rukana alikuwa kafiri na Mtume S.A.W alimshinda na kila akimshinda Mtume alikuwa anachukua thuluthi ya kondoo wake, na Makka wakati huo ilikuwa nchi ya ukafiri, na Mtume S.A.W alirejesha kondoo wake baadaye kwa ufadhili na ukarimu wake, na kisa hicho kilipokelewa na Abu-Dawood, 4/55 na At-Tirmiziy 4/247, lakini hawakutaja kondoo ingawa kisa cha kondoo kilitajwa katika kitabu cha: [Marasil Abu-Dawood 1/235 ]na wengineo.
Aidha wamepata dalili juu ya suala hili kutokana na ile Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abass na wengineo kwamba Mtume S.A.W. alisema katika Hotuba ya wadaa (kuaga): kila riba ilikuwa katika zama ya ujahili basi inaachwa, na ya kwanza ni riba ya Al-Abass Ibn Abdul-Mutalib" na ufahamu wa dalili ni kwamba Al-Abass aliingia katika Uislamu wakati wa vita vya Badr baada ya kutekwa na alirudi Makkah na alikuwa anaamiliana na riba wala hakuyaficha haya juu ya Mtume S.A.W. na wala Mtume S.A.W. hakumkataza asifanye hivyo, basi kutokana na hayo tunapata dalili juu ya uhalali wa suala hili, na kinachoachwa katika riba ni yale matendeano ambayo yalikuwa hayajatimizwa mpaka siku ya ukombozi wa Makka na ikawa ni nchi ya Kiislamu.
Na pia walipata dalili juu ya suala hili kwamba Abu Bakr alishindana na watu wa Makka kabla ya Hijra wakati wa Mwenyezi Mungu alipoteremsha kauli yake: {Alif Lam Mim * Warumi wameshindwa}[AR-RUM,1-2] makafiri wa kikuraishi walimwambia: Mnadhani kwamba Warumi watashinda? Alisema: Ndiyo, wakasema: Unashindana nasi? Akasema: ndiyo, basi alishindana nao, na alimwambia Mtume S.A.W naye Mtume alimwambia: "Nenda kwao na uzidishe rehani" naye Abu Bakar akafanya, na Warumi walishinda Wafursi na Abu Bakr aliwashinda akachukua rehani, na Mtume S.A.W. hajakataza jambo hilo na kamari hiyo ilifanyika kati yao katika Makka ilipokuwa ni nchi ya ukafiri [Tazama Al-Mabsuut, 14/57 na Fat-h Al-Kadeer 6/178]
Na kwa dalili hizi na nyinginezo Muhamad Ibn Al-Hasan alisema: Mwislamu akiingia katika nchi ya vita kwa salama basi hakuna ubaya azichukue mali zao kwa ridhaa yao kwa hali yeyote. [Tazama Sharh Al-Siyar Al-Kabeer, 4/141].
Al-Sarkhasiy alisema: Hakuna riba kati ya Waislamu na watu wa vita katika nchi za vita, na hiyo - inamaanisha Hadithi ya Mak-hul “Al Mursal”- ni dalili ya Abu-Hanifa na Muhamad - Mwenyezi Mungu Awarehemu - katika uhalilisho wa uuzaji wa Mwislamu Dirhamu moja kwa mbili kutoka kwa mtu wa vita katika nchi ya vita, hali kadhalika akiwauzia nyamafu au akishindana nao kwa pesa ili kuipata fedha yao ya kamari, basi fedha hiyo ni halali kwake kwa mujibu wa madhehebu ya Abu-Hanifa na Muhamad Mwenyezi Mungu Awarehemu [Tazama Al-Mabsuut, 14/56]. Na kauli ya Maimamu wawili Abu-Hanifa na Muhamad ni kauli iliyozingatiwa na iliyochaguliwa kwa wafuasi wa madhehebu ya Abu-Hanifa.
Hitimisho ni kwamba Abu-Hanifa na Muhamad - mbali na Yussuf - wameona kwamba miamala ya mikataba batili katika nchi zisizo za Kiislamu baina ya Mwislamu na wasio Waislamu ni halali, kinyume na wafuasi wa madhehebu mengine wanaoona kwamba miamala ya aina hiyo ni haramu katika nchi zote ziwe za Kiislamu au za kivita, na mwulizaji anaweza kufuata maoni ya Abu-Hanifa na Muhamad – Mwenyezi Mungu Awarehemu – katika suala lake, hasa ikiwa yeye bado hajapata kazi nyingine ya halali, na misingi ya kisheria inajuzisha hilo; kwani wanachuoni wa Fiqhi wanasema kwamba mtu aliyebaleghe ana haki ya kufuata rai ya aliyehalalisha suala lenye hitilafu ikiwa kufuata rai ya kukataza na kuharamisha inaweza kumsababishia kero au taabu, basi wanasema: Aliyetahiniwa na na suala lenye hitilafu ana haki ya kufuata yeye mwenye kuhalalisha.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas