Watoto Wadogo (Ambao Hawajabaleghe) Kuifuata Dini ya Baba Yao
Question
Mimi si mwislamu, na nimeelewa kuwa kuna baba mwenye watoto watatu, naye amesilimu, kisha akawachukua watoto wake bila ya mama yao kujua na akawabadilisha majina yao na kuwasilimisha. Je jambo hili linafaa? Na hasa kwa kuzingatia sheria za Kiislamu? Na je jambo hili linapingana na maneno yake Mwenyezi Mungu {Hapana kulazimisha katika dini} (AL BAQARAH; 256)?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Ijulikanavyo katika Sheria ni kuwa iwapo watoto bado hawajafikia rika la kubaleghe na baba yao akawa mwislamu, basi nao humfuata baba yao katika Uislamu.
Mwandishi wa kitabu cha: [Badaiu Swanai 7/104, chapa, Dar Al Kutuub Al Ilmiyah], mwanazuoni wa Madhehebu ya Imam Hanafi, anasema: “Mmoja ya wazazi wawili akisilimu basi mtoto humfuata aliyesilimu”.
Na sayyid Khalil anasema katika ufupisho wake wa madhehebu ya Imamu Malik [Sherhu Dardiyr Wa Hashiya Dusuwk, 4/303, chapa, dar fikr]: “Na huhukumiwa kuwa ni mwislamu yule ambaye hajawa mtambuzi kutokana na udogo au wendawazimu wake kwa kuwa baba yake tu ni mwisilamu.”
Na Imamu Shafi anasema katika kitabu cha: [Ummu 6/40, chapa, Dar Maarifa]: “Iwapo wazazi wa mtoto watakuwa makafiri na mmoja wao akasilimu na mtoto bado ni mdogo, atahukumiwa kuwa mwislamu kwa kusilimu mmoja wa wazazi wake.”
Na Al Mardawi anasema –madhehebu ya Imamu Hanbali katika kitabu cha: [Inswaf 6/453, chapa, Dar Ihyaa Aturaath Al Arabiy): “Huhukumiwa mtoto kuwa ni mwislamu kwa kusilimu mmoja wa wazazi wake wawili”.
Na dalili ya hayo ni kuwa wazazi wawili wana nafasi iliyo sawa katika kufuatwa –ambayo ni kuzaa na kuungana- hapo mwislamu huwa na nguvu kwa Uislamu wake, kwani Uislamu huwa juu na wala hakuna chochote juu yake, nao ni dini ya Mwenyezi Mungu aliyoiridhia kwa waja wake na kutuma kupitia dini hiyo wajumbe wake, dini ambayo hupatikana utulivu ndani yake duniani na akhera, na kuiamini dini hii imani yake inakusanya (kuamini) vitabu na Mitume yote.
Ufupisho: Watoto ambao hawajabaleghe huhukumiwa kuwa ni waislamu kisheria kwa kumfuata mmoja wa wazazi wake ambaye ni mwislamu, na hutekelezewa hukumu zote za kiislamu, kama vile kurithi na kurithiwa. Na anaefariki huzikwa kwa kuoshwa na kuzikwa katika makaburi ya waislamu, na jambo hili halipingani na lengo la kisheria la kwamba hakuna kulazimisha katika dini.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.