Hukumu ya Kuzungumza Kati ya Wana...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Kuzungumza Kati ya Wanaume na Wanawake Kupitia Mtandao wa Tovuti

Question

Nini hukumu ya kisheria kuhusu mazungumzo ya mwanamke na mwanaume kwa kuandikia kupitia kuchati au kupitia barua pepe? Ikiwa jambo hili linaruhusiwa, basi ni kwa kiasi gani? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kwa mujibu wa Sheria hakuna kikwazo chochote katika kuzungumza tu kati ya mwanamke na mwanamume kama wanafuata vidhibiti vya kisheria, na kama hakuna kukaa faragha kati yao tu. Kufuatana na hali hii dalili kutoka katika Qur`ani, Sunna na maneno ya Wanavyuoni zimesisitiza hivyo. Kutoka katika Qur`ani na katika kisa cha bwana wetu Musa pamoja na wasichana wawili tunaona aya hii: {Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana.}[Al-Qasas : 23]. Na katika Hadithi ya Mtume iliyopokelewa kutoka kwa Imam Al-Bukhari kutoka kwa Abu Juhaifa R.A alisema: Mtume S.A.W. aliwafanya kama ndugu kati ya Salman na Abu Ad-Dardaai. Salman akamzuru Abu Ad-Dardaai, alipofika akamkuta Ummu Ad-Dardaai huku amevaa nguo zisizo na thamani. Akamwambia: Una khabari gani? Akamwambia: Nduguyo Abu Ad-Dardaai hana haja na dunia. Akaja Abu Ad-Dardaai akamwandalia chakula … mpaka mwisho wa Hadithi. Al-Hafidh Ibn Hajar anasema katika kitabu chake “Fathul Bari”: “Miongoni mwa faida za Hadithi hii ni kuwa inaruhusiwa kuzungumza na mwanamke asiyekuwa ndugu wa damu na inaruhusiwa kuuliza kuhusu jambo lolote linalosababisha maslahi”. Vile vile Imepokelewa kutoka kwa Imamu Bukhari na Imamu Muslim na wengine kutoka kwa Anas Ibn Malik R.A. anasema: Mwanamke miongoni mwa Ansar alimjia Mtume S.A.W. akakaa pamoja naye, akasema: “Nyinyi nakupendeni zaidi kuliko watu wote”. Na katika mapokezi mengine: “Akakaa pamoja naye njiani”, Imamu Bukhari aliweka anuani akisema: (Mlango wa kuruhusiwa kwa mwanamume kukaa yeye na mwanamke mbele ya watu). Al-Hafidh Ibn Hajar anasema katika kitabu chake “Fathul Bari”: “Kuzungumza na mwanamke kwa siri inaruhusiwa kama hakuna fitina”. Al-Mulla Ali Al-Qari alisema katika kitabu chake “Mirqatul Mafatiih”: “Hadithi hii inazindua kwamba kukaa kwa mwanaume na mwanamke peke yao njiani siyo kama kukaa faraghani nyumbani”. Wake zake Mtume S.A.W, walikuwa wakieneza elimu na Dini, Al-Hafidh Ibn Hajar anawazungumzia wanawake elfu moja na mia tano arubaini na tatu, katika kitabu chake [Al-Isabah fii Tamiiz Al-Sahabah]. Miongoni mwa wanawake hawa ni wanavyuoni wa Fiqhi, Hadithi na wanafasihi.
Jambo hili linaruhusiwa kwa mujibu wa vidhibiti vya Sheria, na kwa hivyo basi pasiwepo na ulaini katika kuzungumza. Na wala hakuna kusema maneno mabaya.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas