Hukumu ya kujifunza michezo ya kivi...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kujifunza michezo ya kivita

Question

Je, inaruhusiwa kwa Mwislamu kushiriki katika michezo ambayo mshindani anajaribu kumshinda mpinzani wake kwa kumjeruhi kichwani na mwilini mwawake? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Hakuna ubaya wowote katika kujifunza michezo tofauti ya kivita kwa njia isiyo ya hatari. Ama ikiwa kujifunza huko kunaleta madhara makubwa na kusababisha ulemavu basi ni haramu kwa mujibu wa Sheria.
Baraza la Fiqhi la Kiislamu lilipitisha azimio moja katika mkutano wake wa kumi uliofanyika Makkah mwezi wa mfungo tano, mwaka wa 1408, sawa na mwezi wa Oktoba, mwaka wa 1987, kuwa mchezo wa ndondi ni haramu; kwa sababu mchezo huu unaruhusu kumdhuru mmoja wa washindani katika mwili wake na hata kumsababishia upofu au kupata madhara makubwa kwenye ubongo wake, au mvunjiko wa mifupa, au kifo, pasipo na jukumu lolote kwa mshindani wake aliyempiga na kumsababishia madhara hayo, ukiongezea na furaha ya washabiki kwa aliyeshinda na kuyafurahia madhara haya. Na kitendo hiki kimepigwa marufuku kabisa kwa mujibu wa Sheria ya Uislamu; kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo}[AL BAQARAH : 195], na kauli yake pia : {Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukurehemuni}[AN NISAA: 29]. Na Hadithi ya Mtume S.A.W: “Hakuna kuleta madhara wala kudhuriana”.
Kutokana na hayo yaliyotangulia hapo juu, Wanavyuoni wa Fiqhi wanasema kuwa mwenye kuhalalisha umwagaji wa damu ya mwingine akamwambia: Niue, hairuhusiwi kumuua, na akimwua atabeba jukumu la kuua na ataadhibiwa. Kutokana na hayo, Baraza la Fiqhi lilipitisha azimio kuwa si ruhusa kuuita mchezo wa ndondi mazoezi ya viungo, na hairuhusiwi kuucheza; kwani maana ya michezo na mazoezi ni kutokuwepo au kutosababisha madhara ya aina yoyote.
Mwisho wa azimio la Baraza la Fiqhi. Na azimio hili kwa maana hii linakusanya aina zote za michezo ya kivita ya mikono au ya mwili mzima yenye madhara au yenye kusababisha ulemavu.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi ya wote

 

Share this:

Related Fatwas