Hukumu ya Kuotesha Nywele
Question
Nini hukumu ya kuotesha nywele za asili?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kupenda mapambo na kuondosha yale yanayomtia aibu mtu ni jambo la kimaumbile linalokubalika kisheria, na katika Hadithi walitajwa wale watu watatu walioingia katika pango: “Akaja “Malaika” kwa mwenye kipara akasema: Nini unachokipenda zaidi? Akasema: Nywele nzuri, sitaki sifa ya mwenye kipara kwa kuwa watu wananitia aibu, akasema: Alimgusa kwa mkono wake naye akapata nyewele nzuri”. Ilipokelewa na Imamu Bukhari na Imamu Muslim kutoka kwa Abu Huraira. Hapa ufahamu wa dalili ni kukubali Malaika ombi lake pamoja na kulijibu.
Na katika Sunna yenye kutakaswa, kuna Hadithi iliyopokelewa na Abu Dawoud kutoka kwa Abdul Rahman bin Turfa kwamba babu yake A’rfaga bin Asa’d alikatwa pua yake, akatengeneza pua ya karatasi ikamsabibishia uozo, basi Mtume S.A.W. akamwamrisha atengeneze pua ya dhahabu.
Hadithi hii ilipokelewa na Al-Tirmizy na alisema: “Hadithi hii ni Hasana Gharib … na ilipokelewa na zaidi ya mmoja miongoni mwa wanazuoni kuwa walifunga meno yao kwa dhahabu, na katika Hadithi hiyo ni hoja kwao”.
Tena Hadithi hii ni dalili kuu katika mlango wa mapambo, na waliotangulia walitegemea Hadithi kama alivyoitaja Al-Tirmizy kutoka kwa baadhi yao.
Na kitendo cha kuotesha nywele ni operesheni ya kisasa ambapo daktari anachukua sehemu ya ngozi ambayo ina nywele na kupandikiza katika sehemu nyingine ambayo haina nywele nayo inawezekana kuwa ya mtu mwenyewe au ya mwengine [Hukumu ya nywele katika Fiqhi ya Kiislamu,Taha Muhamad Fars, uk. 182].
Kitendo cha kuotesha nywele kina hali kadhaa:
1. Kuotesha nywele kutokana na mtu mwenyewe: Na hukumu yake ni kujuzu kisheria, maana mtu ana haki ya kuchukua kiungo kutoka mwili wake kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe akitanguliza masilahi yanayomfaa zaidi. Ikiwa yule anayepigwa juu ya uso wake kwa kitu kinachoweza kusababisha kuua au kuvunja au kumtia aibu akaondosha kwa mkono wake, basi ana haki ya kufanya hivyo katika hali zote hata ikiwa mkono wake utapata madhara, na ikiwa hivyo basi suala la kunyoa nywele kutoka baadhi ya sehemu za mwili na kuotesha katika sehemu nyingine ni halali pia.
Na yalitolewa na Baraza la Fiqhi ya Kiislamu –lililofuata taasisi ya mkutano wa Kiislamu mjini Jida– baadhi ya maamuzi tunayataja kama ni: Inajuzu kuhamisha kiungo cha mtu kutoka sehemu mpaka sehemu nyingine katika mwili wake pamoja na kuhakikisha kwamba manufaa yanayotarajiwa kwa kitendo cha kuhamisha yanazidi madhara yatakayosababishwa na kitendo hicho, sharti kitendo hicho kifanyike kwa kurudisha kiungo kilichopotea au kuboresha sura yake au kazi yake au kurekebisha kasoro au kuondosha ubaya unaosababisha madhara ya kisaikolojia ya kimwili kwa mtu [Hukumu za nywele, uk. 184].
2. Kitendo cha kuotesha nywele kutoka mtu mwengine: nacho ni halali kwa mujibu wa kauli za waliosema: Kupata manufaa kwa nywele za binadamu nayo ni madhehebu ya Muhammad bin Al-Hassan.
Al-A’ny Al Hanafy alisema katika kitabu cha: [Sharh Al Hidaya, 8/166, chapa ya Dar Al Kotub Al-Elmiya]: “Haijuzu uuzaji wa nywele za binadamu wala kuzitumia kupata manufaa” na wala hakuna hitilafu baina ya mafaqihi katika suala hili isipokuwa riwaya kutoka kwa Muhammad –Mwenyezi Mungu Amrehemu- “Inajuzu kupata manufaa kutokana na nywele za binadamu”, na hivyo kwa kupata dalili kutoka kwa Hadithi: “Mtume S.A.W. alipokata nywele za kichwa chake akazigawa baina ya Mashahaba wake”, nao walikuwa wanapata baraka kwa nywele hizo, na zingelikuwa najisi asingelifanya hivyo kwa kuwa najisi huwezi kupata baraka”.
Jambo linalotiaa nguvu kauli hii ni kuwa suala la kuzika nywele za binadamu haliwajibiki; kwa kuwa hakuna maandiko yaliyo wazi katika suala hili, basi hakuna rai nyingine katika mlango huu kama alivyotaja Al-Baihaqy katika kitabu cha: [Shua’b Al Iman “Sehemu za Imani”, 8/444, chapa ya Mak-tabat Al-Rushd], basi suala la kuzika nywele ni niongoni mwa mambo yanayopendezwa tu.
Al-Nawawiy alisema katika kitabu cha: [Al-Majmu’, 1/289, chapa ya Dar Al Fikr]: “Inapendeza kuzizika ardhini nywele zinazoanguka na kucha”. Hadithi hii ilipokelewa na Ibn U’mar R.A. kwa makubaliano ya wanazuoni wetu”.
Ama wale wanaokataza kitendo cha kuhamisha kwa ajili ya kuona nywele za mwanamke asiye ndugu na kadhalika, basi hapa linakuja suala la “kuona kiungo kitengewacho”: kwa maana: Inajuzu kuona kiungo cha binadamu kinachotengwa , na suala hili lina hitilafu baina wa maulamaa ambapo kundi lao walielekea kusema hakuna uharamisho wa kiungo cha mwili wa binadamu baada ya kukitenga. Al-Rahibany alisema katika kitabu cha: [Matalib Auli Al Nuha fi Sharh Ghayat Al-Muntaha, 5/19, chapa ya Bairut]: “Haiharamishwi kuona kwa makusudi nywele zitengwazo kwa kuondosha uharamu wake”. Nayo ni maoni yaliyo sahihi zaidi kwa wafuasi wa madhehebu ya Shafi [Raudhat Al-Talebeen, Al-Nawawiy, 7/26, chapa ya Al-Maktab Al-Islamiy].
Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kwamba sura iliyotajwa haiingii katika kitendo cha kuunganisha ambacho kilikatazwa katika Hadithi iliyopokelewa na Al Bukhari na Muslim kutoka kwa Aisha R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: “Mwenyezi Mungu Amelaani mwenye kuunganisha na mwenye kuunganishwa”.
3. Kuotesha nywele za bandia: Inajuzu kuotesha nywele za bandia, na hilo haliingii katika hukumu ya kuunganisha nywele ambayo imekataliwa kama ilivyotangulia, vile vile ni hukumu yake ni karibu zaidi na halali kuliko suala lililotangulia; kwa kuwa watu wa elimu hawajahitalifiana sana juu yake.
Ibn Qudama alisema katika kitabu cha: [Al-Mughniy,1/96, chapa ya Ihiyaa Al Turath Al Araby]: “ni wazi kuwa lililoharamishwa ni kuunganishwa nywele kwa nywele … zaidi ya hayo hayaharamishwi kwani hakuna madhara ndani yake”.
Tanabahi: Kitendo cha kuotesha nywele kwa ujumla hakina kizuizi cha udhu na kuoga; kwa kuwa nywele zinaotesha chini ya ngozi na kwa hiyo haibatilishi kuoga licha ya udhu.
Kuhusu suala la kufupisha nywele wakati wa kutekeleza ibada ya Hija, ikiwa nywele ni za binadamu basi zinachukua hukumu ile ile ya nywele asili za mtu mwenyewe, na ikiwa ni nywele bandia basi hazichukui hukumu za nywele asili.
Hitimisho: Kitendo cha kuotesha nywele ikiwa nywele zitaendelea kudumu kama vile nywele asili basi hauna ubaya wowote na wala hakizingatiwi kama ni udanganyifu, ama zikiwa nywele zinaota kwa muda mfupi halafu zinatoka tena, basi hukumu yake ni sawa na nywele bandia; hasa zikikusudiwi udanganyifu na hadaa katika posa kwa mfano au kuathiri wanawake ili kuchuma madhambi basi ni haramu kisheria. Ama ikiwa kwa nia nzuri mbali ya hayo basi si haramu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.