Hakika – Maana yake katika Utamadun...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hakika – Maana yake katika Utamaduni wa Kiislamu

Question

Nini maana ya hakika katika Utamaduni wa Kiislamu? 

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
1. Hakika neno la “Al Hak” ni mojawapo ya majina ya Mwenyezi Mungu ambayo Amejiita katika Qurani Tukufu kama ilivyo katika maneno yake: {Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki}[AL-AN-AM, 62], aidha {Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu wa haki} [YUNUS, 32], licha ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mola wa haki aidha Yeye ndiye chimbuko la kila kitu tunachokiona hapa duniani kiambatanacho na haki au hakika; kwani Yeye ndiye Muumbaji wa hayo yote kwa haki kama Alivyobainisha kwa maneno yake: {Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki} [AL-AHQAF, 2].
2. Uongofu kwa haki – nao unatokana na Mwenyezi Mungu – hauwezekani kuwa ni uongofu tu wa hakika ya kinadharia au fikra sahihi peke yake, bali lazima uongofu huo ujumuishe uongofu kwa maadili mema; kwani haiwezekani kutengana baina ya mtazamo na kazi katika utamaduni wa Kiislamu tena hakuna heri katika elimu ila ikiambatana na kazi. Kwa maana nyingine utafiti juu ya hakika au haki katika utamaduni wa Kiislamu hauwezekani kuwa ni utafiti wa kimaarifa tu, bali lazima uambatane na utafiti kwa misingi ya mienendo kwa upande wa kimaadili.
3. Hiyo ni sifa ya kwanza miongoni mwa sifa zionekanazo zaidi ambazo tunaweza kuzitaja katika utafiti wa Kiislamu kuhusu “Hakika”: kutotenga baina ya mtazamo na kazi, au baina ya nadharia na utendaji. Utamaduni wa Kiislamu hauweki bure neno la “Batili” mkabala wa neno la “Haki”; kwani haki katika mtazamo wa utamaduni wa Kiislamu haimaanishi tu usahihi wa fikra za kimantiki za kinadharia bali inadokeza wigo wenye jumulisho na upana wenye kuingiliana na wigo wa heri, kadhalika neno la “Batili” halimaanishi “Ufisadi” katika namna ya kutafakari, bali linadokeza wigo wenye jumlisho na upana zaidi wenye kuingiliana na wigo mwingine; shari.
4. Uislamu sio dini ya kiitikadi tu – kwa mujibu wa maana dhahania ya kifalsafa – bali pia ni mfumo kamilifu wa kijamii unaojengeka juu ya msingi wa kidini. Hali ya kuwa hatuwezi kutenganisha baina ya nadharia na utendaji au baina ya itikadi na utungaji wa sheria.
5. Tena jambo linalosisitiza uingiliano ulio baina ya nadharia na utendaji katika utamaduni wa Kiislamu ni cheo cha pekee ambacho utamaduni huo uliipa kazi. Hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Mbona, (kwa nini) mnasema msiyoyatenda? * Ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda} [AS-SAFF, 2,3]. Imani aghalabu inatajwa katika Qurani Tukufu pamoja na kazi. Aya za Qurani Tukufu zinazosifu kazi ni nyingi na wingi wake unarejea katika sababu ya kuumba binadamu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Lakini mwanadamu amekizidi kila kitu kwa ubishi} [AL KAHF, 54], {Je, mwanadamu hatambui ya kwamba tumemuumba kwa tone la manii? Amekuwa hasimu yetu aliye dhahiri} [YA-SIN, 77].
6. Katika uwanja huu unaohusika na kutotenganisha baina ya nadharia na kazi katika utafiti wa hakika kwa mujibu wa mtazamo wa utamaduni wa Kiislamu, hapa tunaweza kuchochea suala lingine nalo ni kukurubisha pamoja hekima na sheria, nalo ni mojawapo ya masuala yenye umuhimu katika utamaduni huu. Wanafikra Waislamu wameafikiana kwamba lengo la sheria na lengo la hekima ni moja, nalo ni kuleta furaha kwa binadamu kutokana na njia ya itikadi sahihi (ya haki) pamoja na kuyatenda mema, kwa hiyo sheria inaafikiana kikamilifu na hekima hii, aidha kwa hiyo Waislamu wamefungua uwanja kwa njia zote zinazowapeleka katika hekima hiyo.
7. Dhana ya “Hakika” katika utamaduni wa Kiislamu inapanuka na kukusanya hakika ya kielimu ambayo Maulamaa wanaweza kuipata, kila mmoja katika uwanja wake husika. Aidha inakusanya hakika ya kisheria kama wanavyoiona watu wa sheria na hakika ya kielimu kama wanavyoipata Maulamaa kutokana na akili zao, aidha hakika ya kidhati kama Masufi wanavyoifahamu kutokana na njia ya kukimbilia kwa kujua Mwenyezi Mungu, basi “Hakika” kwao ni kujilazimisha kuabudu Allah, na kushikamana na hukumu za kisheria, hivyo jitihada za kiroho ni mchanganyiko wa mtazamo pamoja na kazi. Hiyo ndiyo sifa ya kwanza katika sifa za “Hakika” katika utamaduni wa Kiislamu.
8. Hiyo inatupeleka katika kuzungumzia sifa ya pili: Nayo ni kuwa kila utafiti katika “Hakika” lazima binadamu aainishe nafasi ya binadamu kwa ulimwengu. Binadamu ndiye khalifa ya Mwenyezi Mungu katika ardhi yake naye ndiye aliyechukua na kuibeba amana kama Alivyosema Mwenyezi Mungu: (Kwa yakini Sisi Tulizidhihirisha amri zetu na makatazo yetu, (tukaziuliza) mbingu na ardhi na milima (kuwa zitachukua madaraka ya kufuata amri hizo na kujiepusha na makatazo hayo ili zipate Pepo zikifuzu, na Moto zikifeli), vikakataa kuichukua (ahadi hiyo) na vikaiogopa, lakini mwanadamu akaichukua. Bila shaka yeye ni dhalimu mkubwa {wa nafsi yake kwa kuwa amechukua dhamana hii wala haitekelezi}, mjinga sana. [AL AHZAAB, 72]. Naye binadamu ndiye kiumbe ambacho Mwenyezi Mungu Amemdhalilishia Ulimwengu wote kwake: {Je! Hamuoni ya kwamba Mwenyezi Mungu Amekudhalilishieni vilivyomo mbinguni na ardhini, na Akakukamilishieni neema Zake zilizo dhahiri na za siri? Na wako watu wanaobishana katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu pasipo elimu wala uongofu wala Kitabu chenye nuru} [LUQMAN, 20] pamoja na Aya nyingine.
9. Aidha kuna Aya nyingine zinazoainisha hali kwa binadamu asije kutakabari, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Hebu waulize, “Je, wao (binadamu) ni wenye umbo gumu zaidi au wale (wengine) tuliowaumba (kama tulivyokuumbeni nyinyi, kama Malaika na Majini …)?” Bila shaka sisi tuliwaumba (wanadamu) kwa udongo unaonata. (Wana nguvu gani za kujivunia)?} [AS-SAAFFAT, 11].
10- Hivyo, inamaanisha kwamba Qurani Tukufu baada ya kuinua cheo cha binadamu, ilimtaka asipindukie mipaka ikamfahamisha kwamba Ulimwengu ndio mkubwa zaidi kuliko yeye, naye binadamu yuko ndani ya ulimwengu. Na hiyo ndio sifa nyingine miongoni mwa sifa za “Hakika” katika utamaduni wa Kiislamu.
11- Qurani Tukufu ina hamu kubwa ya kumkumbusha binadamu daima asili yake ya udongo, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Ambaye Ametengeneza umbo la kila kitu, na Akaanzisha umbo la mwanadamu kwa ugongo * Na kisha Akakifanya kizazi chake kwa mchujo wa maji yaliyo madhalilifu} [AS-SAJDAH, 7,8]. {Basi (tazameni namna tulivyokuumbeni): kwa hakika Tulikuumbeni kwa udongo} [AL-HAJJ, 5], {Bila shaka sisi tuliwaumba (wanadamu) kwa udongo unaonata. (Wana nguvu gani za kujivunia)?} [AS-SAAFFAT, 11], {Na Tulimuumba mwanadamu kwa udongo mkavu unaotoa sauti (unapogongwa), unaotokana na matope meusi yaliyovunda} [AL HIJR, 26].
12- Hayo yote yanaweza kutufikisha katika picha halisi kuhusu binadamu kama Qurani Tukufu ilivyotuonyesha, Qurani Tukufu ilikuwa na hamu siyo tu kumwambia binadamu kuwa anaambatana na ulimwengu ambao yeye ni sehemu tu ya ulimwengu huo, bali Qurani Tukufu ilitaka kutuonyesha binadamu katika picha ya kuwa Mwenyezi Mungu Amemuumba kwa kumpulizia roho na jambo linalotupeleka kutazama tena katika dhana ieneayo kuhusu binadamu katika mazingira ya fikra za kiislamu kuwa ni kiumbe cha kiroho tu na kutomtenga na mazingira ya uhalisia unaoonekana.
13- Binadamu huyo ambaye aliwekwa katika nafasi yake ulimwenguni na aliambatana na historia yake ya kimumbile, ndiye aliyewezeshwa na Mwenyezi Mungu kutafuta “Hakika”, naye ndiye aliyechukua amana. Lakini ni nini madhumuni ya hakika? Inapatikanaje? Binadamu anaelekea wapi katika kuitafuta kwake hiyo hakika?
14- Katika kuyajibu hayo, tunaweza kusema: Binadamu akitaka kutafuta “Hakika”, Qurani Tukufu inamwelekeza kwa ulimwengu na mazingira yanamyozunguka ili azizingatie Aya za Mwenyezi Mungu Ulimwenguni; kwani mazingira kama ilivyo katika Qurani, ni chimbuko la yakini na kuamini wala siyo vivuli au mzuka au chimbuko la maarifa ya kudhani kama ilivyo katika utamaduni wa kiyunani, tofauti na utamaduni wa Kiislamu, ambapo mazingira yawe yanaendelea daima, ardhi iliyokufa Mwenyezi Mungu Anaifufua tena, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na alama ya kuonesha moja ya rehema za Mwenyezi Mungu) juu yao ni ardhi iliyokufa: Tunaifufua na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila * Na Tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu na kupitisha chemchem ndani yake * Ili wale katika matunda yake; na haikuyafanya (matunda) hayo mikono yao; je, hawashukuru? * Ametukuka Mwenyezi Mungu aliyeumba dume na jike katika (vitu) vyote; katika vile ivioteshavyo ardhi, na katika nafsi zao (wanadamu), na katika vile wasivyovijua * Na usiku ni alama kwao (vile vile ya neema za Mwenyezi Mungu juu ya viumbe vyake); tunauvua humo mchana; mara wao wanakuwa kizani * Na jua (pia ni alama kwao); linakwenda (maisha) mpaka kituoni pake. Hayo ni matengenezo ya (Mwenyezi Mungu) Mwenye nguvu (na) Mwenye kujua * Na mwezi (kadhalika ni alama kwao); Tumeupimia vituo, (hiki baada ya hiki); mpaka unakuwa (mwembamba) kama chaparare la mtende kuukuu lililonywea * Haliwi jua kuufikia mwezi, (wakati wa nguvu zake) wala usiku kuupita mchana, (ukaja kwa ghafla kabla ya wakati wake). Na vyote vinaogelea katika njia zao} [YA-SIN, 33: 40].
15- Lazima kusisitiza kwamba ingawa utamaduni wa Kiislamu unaelekea kutafuta “Maana ya hakika” mpaka ukafikia mfumo wa kimajaribio wenye kupinga mwelekeo dhania wa kiakili kama ulivyo katika utamaduni wa kiyunani ila haiwezekani kuusifu utamaduni wa Kiislamu kuwa ni utamaduni hisia kama ulivyo katika baadhi ya mielekeo ya utamaduni wa kimagharibi inayotegemea hisia kimsingi, maana utamaduni wa Kiislamu unajumuisha kwa uwiano na ufahamu wa mbali baina ya mielekeo miwili: Mwelekeo wa kihisia na Mwelekeo wa kiakili.
16- Miongoni mwa sifa za kiujumla za dhana ya “Hakika” katika utamaduni wa Kiislamu: Ni kwamba kutafuta kwake kunaambatana kikamilifu na dini ya Kiislamu kama ni Akida, Sheria inayojumlisha makundi ya amri na makatazo ambayo Mweka Sheria Ameyafaradhisha, aidha utafiti wa “Hekima” katika utamaduni wa Kiislamu haukuwa utafiti kwa ajili ya kupata ladha ya utafiti wa kinadharia peke yake kama tulivyoona katika mielekeo ya baadhi ya wanafalsafa, bali ni utafiti wa kuhudumia Akida kwanza, pili: Binadamu, tatu: Kuhudumia “Hakika”.
17- Hapa lazima tutoe mwangaza zaidi juu ya Akida ya kiislamu na uhusiano ulio baina yake, na kutafuta hakika kwani inawezekana kufahamika kutokana na neno “Akida” kwamba inajumuisha ndani yake mambo yasiyoweza au yasiyokubali majadiliano ya kiakili; maana mkabala wa akili na mambo ya kiakili, kama hali ilivyo katika tamaduni zisizokubali kutumia akili katika kuthibitisha hakika za mambo; kwani katika tamaduni za aina hizo mambo yaliyolazimishwa na kufaradhishwa na Akida haiwezekani kujadiliwa na akili, tofauti na Akida katika dini ya Kiislamu ambayo kimsingi inategemea akili. Kuna Aya katika Qurani Tukufu zinahimiza kuiweka mbele akili na kuzingatia ufalme wa mbingu na ardhi ili binadamu afikie Akida sahihi yenye kuanzishwa juu ya misingi ya upweke wa Mwenyezi Mungu kama ilivyotajwa katika Qurani Tukufu: {Mwenyezi Mungu) Ambaye Amekufanyieni hii ardhi kuwa kama bustani (mliotandikiwa mstarehe), na mbingu kuwa kama paa, na Akateremsha maji kutoka mawinguni; na kwa hayo Akatoa matunda yawe riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua (kuwa hana mshirika} [AL BAQARAH, 22]. Kwa hiyo, wengi wa wataalamu wa elimu ya Al-Kalaam (wanafalsafa wa maandiko ya dhana) na mafaqihi walielekea kwa kuainisha suala la mtazamo wa kiakili kuwa ni wajibu kifaya.
18- Hivyo, tunaweza kusema kwamba mjumuiko baina ya hakika na Akida au baina ya akili na dalili za kunukuliwa katika utamaduni wa Kiislamu ni jambo linalolazimika kutokea kama ilivyoamrisha dini ya Uislamu.
19- Kwa upande mwingine, tunaweza kuzungumzia ufungamano wa dhana ya hakika katika utamaduni wa kiislamu na makundi ya dhana nyingine kama vile ukweli katika maneno na vitendo pamoja na kufanya Ikhlasi na bidii. Zaidi ya hayo, mkabala katika Kiarabu baina ya ukweli “Haki” na Batili unaonesha kwamba kuondosha haki au hakika hutokea kwanza kwa kufanya la Batili, aidha inaonesha kwamba mwenye kutafiti hakika lazima awe mwenye maadili mema, kwani utafiti wa hakika katika utamaduni wa Kiislamu unafungamana na kutenda mema na kujitenga na shari, kwani elimu katika Uislamu ni amana naye atakayechukua ile amana lazima awe na amani ya kiroho. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Mungu) humpa hekima (akili yenye nafuu) amtakaye, na aliyepewa hekima bila shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili} [AL BAQARAH, 269].
20- Na kuambatana kwa haki na ukweli halisi katika utamaduni wa Kiislamu kunatuwezesha kuzungumzia kifungu kingine cha dhana zinazofungamana naye, basi hakika inayochimbua na ukweli huo si ya jumla au ni lazima iwe na uimara, bali inapaswa iwe tofauti kidogo, ambayo inabadilika kutokana na mabadiliko ya hali halisi, kwani haki haiwi bila ya sharti, bila ya ukomo isipokuwa wakati wa kuzungumzia Mwenyezi Mungu na Manabii wake, Mitume wake, vitabu vyake, mambo yenye ukweli katika Imani na kisheria, ama katika Ulimwengu wetu halisi kwani mtazamo kwa haki ni masuala yanayohitilafiana kutoka mtu kwenda kwa mwingine, na hapa hakuna uwanja wa kuzungumzia udharura usiyo na sharti au yakini halisi, hakuna hakika halisi isipokuwa katika uwanja wa kiakida na misingi ya kidini, na kwa hiyo utamaduni wa Kiislamu ulifahamika sana, kama ambavyo utamaduni wa kiyunani ulijengeka juu ya uthibiti wa vitu katika maumbile, na kuuimarisha kwake ulimwenguni, na jambo hili linasababisha kutoendelea kwa sayansi na na kutofika kwa vumbuzi mpya, maadamu kila kitu duniani na maumbile kimewekwa thabiti, yaani bila ya kubadilika. Na kwa hiyo Ibn Kaldun anasema (vipimo vya kimantiki ni hukumu za kiakilini, na vilivyomo katika mazingira ya nje viwe na umbo, basi usawe wa kiyakini baina yake si wenye yakini, kwani mada inakataza usawe, isipokuwa unaokiri hali halisi, dalili ni shahidi yake, siyo dalili za kimantiki).
21- Hakika ufunguzi wa utamaduni wa Kiislamu kwa sifa yake hasa ni jambo ambalo liliufanya uweke uzani kwa hali halisi kwa kuzingatia hali halisi siyo kama jaribio la kielimu tu bali kwa dhana ya matumizi ya mchakato katika hali halisi, yaani kutenda. Kwa sababu kuamini mabadiliko, maendeleo, kidinamiki, kunapaswa kufungamana na kuamini kwa nyenzo zitakazotusaidia kuzifahamu na kuishi nazo. Na nyenzo hizo zinapatikana katika jaribio la kielimu na matumizi ya mchakato. Kuhusu jaribio la kielimu tunaweza kusema kuwa ustaarabu wa Kiislamu umetolea maulamaa wakubwa sana wamekuwa wenye athari kubwa katika maendeleo ya elimu. Kuhusu matumizi ya mchakato yanawakilisha msingi muhimu sana kati ya misingi ya jitihada ya kisheria ya Kiislamu, na maulamaa wameeleza matumizi hayo ya mchakato kwa (masilaha ya watu), na huo si msingi wa manufaa katika hali halisi tu (kiutendaji), bali inatupasa kufahamu kuwa kuangalia masilaha hayo ni nyenzo ya kubadilika hali halisi, kwa njia ya kutekeleza na matumizi ya mchakato, na kwa njia ya vitendo vya watu wote vyenye ufahamu mkubwa. Tunaweza kuita namna hiyo ya matumizi ya mchakato ya watu wote ni mchango wa jamii katika kubadilika kwa hali halisi na kusahihisha makosa yake pamoja na kurekebisha upungufu.
22- Kufungamana kwa utamaduni wa Kiislamu na mchango wa jamii katika kubadilika ni miongoni mwa sifa za dhana ya ukweli katika utamaduni huo, kwani utamaduni wa Kiislamu unajumuisha baina ya akili na hisia na kubadilika kwa njia ya jamii. Nadharia zote mpya mwishoni zilisisitiza sana mchango wa taasisi za jamii husika katika kubadilika na kusahihihisha.
23- Na kwa kuangalia utamaduni wa Kiislamu kwa hali halisi kwa namna hiyo kuliufanya uwe na umuhimu mkubwa kwa chanzo kimoja muhimu cha maarifa, katika kutafuta kwake hakika; nacho ni Mlolongo wa mapokezi (Tawaatur) ambao unasisitizia yakini na simulizi za watu Waaminifu (thiqaatu) Wasema kweli, wenye Uadilifu Madhubuti. Na chanzo hicho ni msingi wa maarifa ya kihistoria na Mapokezi ya Hadithi za Mtume S.A.W. Na waislamu wameweka dalili, nakala, vipimo, na vigezo ambavyo wamevitumia kwa mbinu ya kihistoria tangu wakati huo hadi sasa. Na Waislamu wakapata hamu kubwa mno ya chanzo hicho muhimu cha ukweli, kwa kutokana na umuhimu wake mkubwa katika kunukuli, na hasa hasa Sunna ya Mtume.
24- Ibn Kaldun ni miongoni mwa maulamaa walioshughulikia sana upande wa hali halisi katika kutambua na kujua ukweli na hivyo kwa kupitia masomo aliyoyatoa kwa watu na kuzungumza kwake kuhusu mazingira na athari zake na kutegemea kwake juu ya maangalizi na majaribio na Uchanganuaji (Istiqrai), na kuchunguza kwake kwa vyanzo vya kuzalisha ambavyo vinatawala mapinduzi ya kiuchumi katika jamii ya kibinadamu, hasa hali halisi na kazi ya kibinadamu, na kuchunguza kwake kwa sura za kuishi katika jamii, kama kilimo na biashara na kiwanda, na maoni yake kuhusu kuhozi.
25- Na kushughulikia kwa utamaduni wa Kiislamu kwa hali halisi kwa namna hiyo inatuelezea umbali na utengano wake na mielekeo yote ya maumbo tu katika kutafuta hakika. Utamaduni huo unaona kuwa ukweli ni wenye usawe na hali halisi, hiyo inamaanisha kwamba ukweli katika utamaduni wa Kiislamu uko mbali na ukweli kwa mtazamo wa wanafalsafa wa uchambuzi wanaotaka kukata uhusiano wowote kati ya ukweli na hali halisia, na wanaitikadi kwamba suala lenye ukweli ni suala lenye uwezo wa kuyazalisha masuala mengine ya kimatamshi, lakini maulamaa wa Kiislamu hawafungamanishi ukweli wa masuala na kuzalisha kwa matamshi, bali unafungamana na usawe na kuwafikiana na hali halisia.
26- Inaonekana kwetu mwishoni kama waislami katika kutafuta hakika hawaelekei mwelekeo wa kimaumbo bali kwa utamaduni wao wamejaribu kufikia hakika yenye faida, siyo hakika ya kimantiki tu ambayo inajengwa na wanafalsafa tu, bali hakika inayofungamana na elimu na hali halisia, na ambayo inalenga kimsingi kwa yakini inayofungamana na ukweli kwa maana yake tulioitaja hapo juu, na inayofungamana vile vile na kiitikadi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote
Rejeo la kimsingi: Utangulizi katika falsafa ya kiujumla, Prof. Yahaya Huwidi, Profesa wa Falsafa, Chuo Kikuu cha Cairo, Dar al Thaqafa, 1974, uk. 199: 222.

 

Share this:

Related Fatwas