Hukumu ya kufunga hirizi

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kufunga hirizi

Question

Je, inaruhusiwa kufunga hirizi? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Hirizi ni kitu kilichofungwa kinachovaliwa kiunoni, shingoni au mkononi, kwa imani ya kuwa chaleta manufaa au kumkinga mtu na mabaya, ambapo huwa ni mizizi, mifupa, kucha za wanyama mbali mbali, maandishi n.k
Katika istilahi hirizi ina maana mbili:
Ya kwanza: Mashanga ambayo Waarabu walikuwa wakiwavalisha watoto wao ili kuwakinga na jicho baya katika madai yao, lakini Uislamu umeyabatilisha. [Al-Nihaya fii Gharib Al-Hadith wa Al-Athar: 1/197, Al-Maktaba Al-Elmiyah].
Ya pili: Ni karatasi zinazoandikiwa ndani yake aya kutokana na Qur'ani ili ziwekwe kichwani kwa ajili ya kupata baraka zake. [Hashiyatul Gamal ala Sharhul Manhaj: 1/76, Darul Fikr].
Na miongoni mwa misingi ya itikadi ya Waislamu ni: Hakuna athari ya kibinafsi inasababishwa na kiumbe yeyote, na anayefikiri kuwa ipo athari ya kibinafsi inasababishwa na yeyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi amefanya ushirikina, Ibn Hajar Al-Haytami amesema: “Jambo Hili ni la ujinga na upotovu, nalo ni miongoni mwa madhambi makubwa mno, nalo kama si ushirikina, basi linasababisha ushirikina, ilhali hakuna anayeleta faida na madhara na anayeyazuia isipokuwa Mwenyezi Mungu tu.” [Al-Zawaajir an Iqtiraf Al-Kabair, Ibn Hajar Al-Haytami: 1/274 Darul Fikr]
Lakini kama haikuaminiwa kwamba hirizi ina taathira yenyewe, basi kuna hali mbili: Ama hirizi hizi zinachukuliwa kutokana na Qur’ani au kutoka katika kitu kingine ambacho siyo Qur’ani, nazo hizi ama zimechukuliwa kutokana na Dhikr, Wirdi na maneno mazuri na hali hii inaruhusiwa, au kuwa kinyume cha hali hii yaani ni Matalasimu na maneno yasiyofahamika katika Kiarabu au kwa lugha nyingine, na hali hii hairuhusiwi.
Basi hirizi ambazo zimechukuliwa kutokana na Qur’ani au ambazo zinaingia katika hukumu ya Dhikr, Wirdi, na maneno mazuri, wanavyuoni wengi kutoka madhehebu ya Hanafi, Maliki na Shafii, vile vile imepokelewa kutoka kwa Imam Ahmad, kwamba wote hawa wamesema kuwa jambo hili linaruhusiwa na dalili yao ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.} [AL ISRAA: 82].
Imamu Al-Qurtubi alisema: “Maulamaa wamekhitilafiana kuhusu kuwa Qur’ani ni uponyaji katika maoni mawili: Moja yao ni: Kuwa Qur’ani ni uponyaji kwa mioyo kwa kuondoa ujinga wake na kuondoa mashaka yake, na kwa kuondoa ugonjwa wa ujinga ambao uko moyoni kwa ajili ya kuelewa miujiza na mambo yanayothibitisha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu. Ya Pili: kuwa Qur’ani ni uponyaji kutokana na magonjwa ya kweli kwa kuomba dua na kujikinga na kadhalika” [Jamii li ahkam Al-Qur'ani: 10/316, Darul Kutub Al-Masriyah].
Na hirizi zinazochukuliwa kutokana na kujikinga kulikoandikwa -kama yaliyotangulia hapo juu- si mbaya, na kama mwislamu amezifunga kwa ajili ya kupata baraka zake, basi hakuna tatizo lolote, Mwenyezi Mungu anasema: {Na hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha, kilicho barikiwa. Basi kifuateni, na mcheni Mungu, ili mrehemewe} [Al-Anaam: 155].
Dalili yao pia ni iliyopokelewa kutoka kwa Al-Tirmidhi, Ahmad na Al-Hakim kutoka kwa Muhammad Ibn Abd Al-Rahman Ibn Abi Layla kutoka kwa ndugu yake, Issa alisema: Nilikwenda kwa Abdullah Ibn Abi Akiim Abi Maabad Al-Juhani ili kumzuru nilimwona kuwa ana rangi nyekundu mwilini mwake tulimwambia kuwa: Je, kwanini usifunge hirizi zozote? Akasema: kifo ni karibu zaidi ya kufanya hivyo, Mtume S.A.W alisema: ((Mwenye kutegemea kitu,basi ataelekezwa katika kitu hicho)).
Basi anayetegemea Qur’ani Mwenyezi Mungu atamhifadhi na hatamwacha kwa mwingine; kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye anayehitajika kwake na hutegemewa katika kuomba matibabu kwa Qur’ani [Al-Jaamiu Liahkam Al-Qura’n, Al-Qurtubi, 10/320].
Kama ilivyopokelewa kutoka kwa Abu Daud na Al-Tirmidhi kutoka kwa 'Amr ibn Shuaib kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, alisema: ((Yeyeto kama akiamka ghafla kutoka katika usingizi wake, aseme najikinga kwa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyo kamili kutokana na hasira yake, adhabu ya waja wake, na kutokana na wasiwasi wa mashetani na wasinikaribie, itakuwa hakuna madhara kwake)). Akasema: Abdullah Ibn Amr alikuwa akimjulisha mwanawe aliyebaleghe dua hii, lakini kuhusu asiyebaleghe, Abdullah alikuwa akiandika dua hii katika hati, kisha kuifunga katika shingo yake.
Basi wamechukua kitendo hicho cha Abdullah Ibn Amr R.A kama dalili kwao.
Na ikawa katika kitabu cha Ibn Abi Shaybah [5 / 43-44, Maktabit Al-Rushd] Said Ibn Al-Musayyib aliulizwa kuhusu kujikinga, akasema: “Hakuna kitu kibaya kama kikiwa katika ngozi”, na kutoka kwa Ataa alisema: “Hakuna kitu kibaya kama Qur’ani ikinyongwa”, na Mujahid alikuwa akiwaandikia watu maneno yenye kujikinga na akawafungia, na kutoka kwa Al-Dhahhaak kwamba alikuwa hakuona kitu kibaya kwamba mtu anafunga aya kutokana na Qur’ani lakini kwa sharti aiache mbali katika wakati wa kuosha na wakati wa kujisaidia, pia Abu Ja'far Muhammad Ibn Ali aliruhu kujikinga kwa kuwafungia wavulana, na Ibn Sirin alikuwa haoni kitu kibaya kuhusu kufunga aya kutokana na Qur’ani.
Na miongoni mwa yaliyopokelewa kutoka kwa wanavyuoni kuhusu kuruhusiwa kwa suala hili, ni yaliyoandikwa katika kitabu cha Al-Durr Al-Mukhtar: hirizi zilizochukizwa ni zisizokuwa Qur’ani, na ilisemekana: Haya ni mashanga yaliyofungwa na watu wa zama za ujinga, na katika kitabu cha Al-Mujtaba: Watu walifuata hukumu ya kuruhusiwa siku hizi, na imepokelewa katika Hadithi [Radd Al-Muhtar ala Al-Durr Al-Mukhtar: 6/363, 364, Darul Fikr].
Pia katika Kifayatul Taalib Ar-Rabani ala Risalati Ibn Abi Zayd Al-Qayrawani [2/492, Darul Fikr]: “(Hakuna kitu kibaya kuhusu hirizi zinazofungwa) katika shingo (na ambazo Qur’ani imeandikwa ndani yake) na watu wote ni sawa katika hali hii kama akiwa mgonjwa, asiye mgonjwa, ana Janaba, ana Hedhi, anatokwa na damu kufuatia kujifungua, na hata kwa ng'ombe”, imefahamika kwamba hirizi zinazokuwa kutokana na Qur’ani zinaruhusiwa kama zilifanywa katika kitu kinachozilinda.
Imamu Malik alisema: “Hakuna kitu kibaya kuhusu kuvifunga vitabu ambavyo vina majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu shingoni mwa wagonjwa kwa nia ya kupata baraka yake” [Al-Jamii Li Ahkam Al-Qur’an, Al-Qurtubi: 10/319].
Katika vitabu vya madhehebu ya Shafi: tunaona kwamba Imam Al-Nawawiy alisema katika kitabu cha: [Al-Majmuu 9/66, Darul Fikr] Hadithi ya Mtume wa Allah S.A.W: "Mwenye kufunga hirizi, basi Mwenyezi Mungu hatatimiza chochote kwake, na mwenye kufunga kombe ya baharini, basi Mwenyezi Mungu hatafanya chochote kwake", kisha imepokelewa kutoka kwa Al-Bayhaqi kauli yake kuwa: Kuzuia kunafuata maana iliyotajwa na Abu Obeid- yaani hirizi zisizoandikwa kwa Kiarabu, kisha Al-Bayhaqi alisema: Inawezekana kuwa hivyo na hali hii inafanana na karaha na kuzuia kwa anayezifunga hirizi kwa nia ya kuwa mzima sana na kuondoa kwa ugonjwa kama ilivyokuwa katika zama za ujinga, lakini anayezifunga hirizi kwa nia ya kupata baraka za kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu ambapo yeye anajua kwamba hakuna anayeondoa hiyo isipokuwa Mwenyezi Mungu, na hakuna anayelinda isipokuwa Mwenyezi Mungu tu, basi hakuna kitu kibaya kwa hali hiyo. Imam Al-Nawawiy hakupinga mtazamo huu.
Inafahamika kwamba kufunga hirizi ambazo zimeandikiwa Qur’ani au kumkumbuka Mwenyezi Mungu inaruhusiwa kama zikiwekwa ndani ya kitu kinachoweza kuzihifadhi, ama kuhusu Hadithi zilizopokelewa kuhusu kuzuia kwa kuzifunga hirizi hizi, basi Hadithi hizi zinaelekezwa kuwa hirizi hizi ni za zama za ujinga (Ujahili) ambazo inadhaniwa kuwa zinaleta kheri na zinaondoa shari, hali hii ni haramu, na hakuna uponyaji kwa kufanya jambo la haramu, na pia hirizi za makuhani na wachawi ambazo zisizoandikiwa Qur’ani ndani yake.
Al-Hafidh Ibn Hajar alisema katika kitabu cha Al-Fath -Baada ya kutaja Hadithi inayohusu kuzuia kwa kufunga hirizi: “Haya yote kuhusu kufunga hirizi na nyingine ambazo hazikuandikiwa Qur’ani, ama kuhusu hirizi ambazo zina kumkumbuka Mwenyezi Mungu hakuna kukataza, lakini hirizi hizi zina nia ya kupata baraka zake na kujikinga kwa majina yake Mwenyezi Mungu na kumkumbuka” [Fathul Bari Sharhu sahihi Al-Bukhari: 6/142, Dar Al-Maarifa].
Al-Qadhi Abu Yala Ibn Al-Firaa miongoni mwa wanavyuoni wa madhehebu ya Ibn Hanbal alisema kuwa: “Inawezekana kufahamu mtazamo wa kukataza kwa tofauti ya hali mbili, basi hairuhusiwi kama ikiaminiwa kuwa hirizi hizi zina manufaa kwake na zinaondoa madhara mbali yake, na hali hii hairuhusiwi, kwa sababu hakuna isipokuwa Mwenyezi Mungu tu ambaye ni mwenye manufaa kwa waja wake. Na mtazamo ulioruhusisha jambo hili unaamini kwamba hakuna isipokuwa Mwenyezi Mungu tu ambaye ni mwenye manufaa kwa waja wake. Pengine jambo hili lilichukuliwa kama kawaida ya ujinga, kama inaaaminika kwamba dahari (zama) inawabadilisha watu, kwa hivyo walikuwa wakiitukana” [Kashaaf Al-Qinaa ala Matn Al-Iqnaa, Al-Bahwati: 2/77, Darul Kutub Al-Elmiyah].
Kutokana na hayo yaliyotajwa hapo huu: Kufunga hirizi zinazoandikiwa Qur'ani Tukufu na Dua inaruhusiwa katika sheria sharti Muislamu anaamini kwamba Mwenyezi Mungu tu ni mwenye manufaa na madhara, na kwamba hirizi hizi ni miongoni mwa sababu tu, na kwa kuzingatia kuwa hirizi hizi zihifadhiwe kutoka tusi, pia lazima tutahadhari kuwa kufunga hirizi ambazo ni halali kwa kuomba uponyaji hakutofautiani na kuwepo kwa dawa za matibabu, lakini lazima tuchukue faida yao pamoja pasipo na ziada kwa njia moja au kwa upungufu katika nyingine.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas