Namna ya Kuteremka Kusujudu Kwenye Sala.
Question
Ni namna gani iliyo sahihi ya kuteremka kwa ajili ya kusujudu? je kwa kutanguliza magoti au kwa kutanguliza mikono?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Neno kuteremka kwa upande wa lugha: linatokana na neno teremka, kwa mfano husemwa: ameteremka mteremko, kwa maana ya kuwa ameshuka kutoka juu kwenda chini. [Kamusi ya Al-Wasit, 915, mada: ameteremka, chapa ya Majma' Al-Lugha Al-Arabiya].
Na wala haiachani maana ya kiistilahi na maana ya kilugha.
Wanachuoni wametofautiana namna ya kuteremka kwa ajili ya kusujudu kwa kauli mbili:
Kauli ya Kwanza: madhehebu ya Jamhuri ya wanachuoni, kama vile Abi Hanifa, Shafiy, Ahmad, An-Nakhaa, Sufyani At-Thaury, Is-Haq Ibn Rahawih na Muslim Ibn Yasar Al-Baswriy, wanasema ni kutanguliza magoti badala ya mikono wakati wa kuteremka kwa ajili ya kusujudu. [Al-Majmuu Sharhi Al-Muhadhab, 3/427, chapa ya Dar Al-Fikr, na Nihayat Al-Muhtaj, 1/515, chapa ya Dar Al-Fikr, na Al-Mughniy, 1/370, chapa ya Maktabat Al-Kahira, na Al-Inswaf cha Al-Mardawiy, 2/65, chapa ya Dar Ihayaa At-Turath Al-Araby, na Kashaf Al-Iqnaa cha Bahwaty, 1/350 chapa ya Al-Kutub Al-Ilmiya].
Na madhehebu haya yamepokea Hadithi kutoka kwa Umar Ibn Khattab na mtoto wake R.A. (kitabu: Musannaf Ibn Abi Shaiba, 1/236 – 239, chapa ya Maktabat Ar-Rushd) na kuteuliwa hukumu huu na Ibn Al-Qiyam [Kitabu: Zaad Al-Maad, 1/219 chapa ya Muassasat Ar-Risala].
Na dalili yao ni Hadithi ya Waail Ibn Hujru, ambapo amesema R.A. kuwa: “Nimemwona Mtume S.A.W. pindi anaposujudu alikuwa anatanguliza magoti yake kabla ya mikono yake, na anapoinuka alikuwa anainua mikono yake kabla ya magoti yake” imetolewa na Abu Daud katika suna yake.
Na imepokelewa pia kutoka kwa Saad Ibn Abi Wiqaas R.A. kuwa amesema: “Tulikuwa tunatanguliza mikono kabla ya miguu na tukaamrishwa kutanguliza magoti kabla ya mikono” Hadithi hii imetolewa na Ibn Khuzaima katika sahihi yake.
Na kutoka kwa Anas R.A. amesema: “Nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. anasema Allah Akbar…. Kisha akateremka na takbira magoti yake yakaitangulia mikono yake” Hadithi hii imetolewa na Ad-Dar Qutniy katika suna yake na Al-Baihaqiy katika Sunan Al-Kubra.
Na dalili zitokanazo na Hadithi hizi ni kuwa, zenyewe zimebainisha kutanguliza magoti kabla ya mikono.
Kutokana na Abu Hurairah R.A. kutoka kwa Mtume S.A.W. amesema: “Pindi anaposujudu mmoja wenu basi na aanze na magoti yake kabla ya mikono yake, na wala asiteremke mteremko wa ngamia” Hadithi hii imetolewa na Al-Baihaqiy katika Sunan Al-Kubra.
Na dalili zitokanazo na Hadithi hizi ni kuwa zenyewe zinaelezea kutanguliza magoti kabla ya mikono.
Kauli ya Pili: nayo ni ile waliyokubaliana nayo Imamu Malik, Al-Auzai na Ahmad katika mapokezi, na wazungumzaji waliopendekeza kutanguliza mikono kabla ya magoti wakati wa kwenda kusujudu.[Angalia: kitabu cha Sharh Mukhtasar Khalil Al-Kharshy, 1/287, chapa ya Dar Al-Fikr, na Majmuu Sharha Al-Muhadhab, 3/421, chapa ya Dar Al-Fikr, na Insaf cha Mardawiy, 265, Nail Al-Autar cha As-Shaukaniy, 2/293, chapa ya Dar Al-Hadith].
Wakajenga hoja kwa Hadithi iliyopokelewa na Abu Hurairah R.A. kutoka kwa Mtume S.A.W. kuwa amesema: “Pindi anaposujudu mmoja wenu basi wala asiteremke kama vile anavyoteremka ngamia, na atangulize mikono yake kabla ya magoti yake” imetolewa na Abu Dawud katika sunna zake.
Amesema Ibn Hazm: "Ni lazima kwa kila mwenye kusali kuweka - pindi anapo sujudu – mikono yake kwenye ardhi kabla ya magoti yake, na ni lazima". [Ibn Hazm, 3/44, chapa ya Dar Al-Fikr]
Na ametaja Az-Zarkashiy katika kitabu cha: [Shurut At-Tarjih] kuwa pindi wanapo tofautiana wapokezi katika moja ya Hadithi mbili na wakakubaliana wapokezi wengine, basi mapokezi ambayo hayana tofauti hiyo ndiyo bora zaidi, akasema: “Na mfano wake ni Hadithi ya Waail kuwa Mtume S.A.W, alikuwa anatanguliza magoti yake kisha mikono yake kisha paji la uso wake kisha pua yake” wapokezi wala hawakutofautiana katika Hadithi hii. Imamu Shafiy amekubaliana na rai hii, na imepokelewa Hadithi na Abu Hurairah mfano wa Hadithi hii, imepokelewa kutoka kwake juu ya katazo la kuteremka kwenye sujudu kama vile mteremko wa ngamia, kwa maana: kutanguliza magoti kabla ya mikono, akasema Shafiy: Hadithi ya Waail imejitenga na upingaji, nayo ni bora zaidi kuliko Hadithi ya Abu Hurairah, [kitabu cha: Al-Bahr Al-Muhiit, cha Zamarkashiy, 8/183 – 184, chapa ya Dar Al-Kutub].
Na amesahihisha Ibn Al-Qayim kauli ya Jamhuri ya wanachuoni na kujibu kwa dalili nyengine na akasema: “Alikuwa Mtume S.A.W. anatanguliza magoti yake kabla ya mikono yake kisha inafuata mikono yake baada ya magoti kisha uso wake na pua yake, hivi ndio sahihi…
Na kwa upande wa Hadithi ya Abu Hurairah, "Pindi anapo sujudu mmoja wenu basi asiteremke sujudu kama vile anavyoteremka ngamia na atangulize mikono yake kabla ya magoti yake," Hadithi hii Mwenyezi Mungu ndiye Anayejua zaidi. Ndani yake kuna hali ya kutofahamika kwa baadhi ya wapokezi, kwani Hadithi ya kwanza inatofautiana na nyengine, kwa sababu pindi anapoweka mikono yake kabla ya magoti yake basi anakuwa ameteremka mteremko wa ngamia, kwani ngamia huwa anatanguliza mikono yake kwanza. Baada ya watu kuifahamu kauli hii wakasema: magoti mawili ya ngamia yapo mikononi mwake na wala sio miguuni mwake, anapoteremka chini huwa anatanguliza magoti yake kwanza, na hili ndilo lililokatazwa, nalo ni lenye kuharibu… na ninachokiona mimi ni kuwa Hadithi ya Abu Hurairah kama tulivyoitaja ni katika Hadithi iliyogeuzwa maneno yake na baadhi ya wapokezi, lakini asili yake huenda ikawa ni: “Na aweke magoti yake kabla ya mikono yake”
Kisha wakaipa nguvu kauli ya kutanguliza magoti na wakazungumza sana katika hilo na kusema: “….. Hadithi ya Waail Ibn Hujru ni bora kwa sura kadhaa.
Sura ya Kwanza: ni kuwa imethibitisha Hadithi ya Abu Hurairah, ameisema Al-Khatwabiy na wengineo.
Sura ya Pili: Hadithi ya Abu Hurairah ni yenye mgongano wa maandiko, kama ilivyotangulia kusemwa, baadhi wanasema kuwa (Na atangulize mikono yake kabla ya magoti yake) na wengine wanasema kinyume, wengine wanasema: (Na atangulize mikono yake juu ya magoti yake) na miongoni mwao wapo wanaoifuta jumla hii.
Sura ya Tatu: ni ile iliyoelezwa na Imamu Bukhary na Dar Al-Kutniy na wasio kuwa hao.
Sura ya Nne: kuwa ipo kwenye makadirio ya kuthibiti kwake, ambapo wapo wanachuoni waliodai kufutwa kwake. Amesema Ibn Al-Mundhir: baadhi ya watu wetu wanadhani kuwa kuitanguliza mikono miwili kabla ya magoti ni jambo lililofutwa, kama ilivyoelezwa.
Sura ya Tano: inakubaliana na makatazo ya Mtume S.A.W. ya kuteremka kwenye kusujudu, kwa mteremko wa ngamia, tofauti na Hadithi ya Abu Hurairah.
Sura ya Sita: maelezo yanakubalina na maelezo ya Sahaba Umar Ibn Khattab na mwanawe pamoja na Abdillah Ibn Masuud, hakunukuliwa yeyote kati yao kwa yale yanayo kubaliana na Hadithi ya Abu Hurairah.
Sura ya Saba: hakuna ushahidi kutoka Hadithi ya Ibn Umar na Anas kama zilivyotangulia, na wala hakuna ushahidi kwenye Hadithi ya Abu Hurairah, lau zitagongana, basi itatangulizwa Hadithi ya Waail Ibn Hujru kutokana na ushahidi wake.
Sura ya Nane: watu wengi wana mtazamo huo. Na kauli nyengine kwa hakika inalinda kauli ya Al-Auzai na Malik, ama kauli ya Ibn Abi Daud ni kauli ya watu wa Hadithi, kwa hakika wametaka hivyo baadhi yao, na kinyume na hivyo basi Ahmad, Shafiy na Is-haka wapo kinyume na hivyo.
Sura ya Tisa: ni kuwa Hadithi ambayo ndani yake kuna kisa kilichohadithiwa na kimeelezea kisa cha kitendo chake Mtume S.A.W, ambapo kitendo hiko ni bora zaidi kuwa ni cha kuhifadhiwa, kwa sababu ikiwa ndani ya Hadithi kuna kisa kilichohadithiwa huwa kinajulisha kuwa Hadithi yenyewe imehifadhiwa.
Sura ya Kumi: vitendo vyote vya kuhadithiwa huuthibitisha usahihi wa mapokezi yake kuliko zengine, kwani vitendo vyenye hufahamika na ni sahihi, na hili ni katika yenye hukumu yake, na mwenye kulipinga si mwenye kulipigania, basi huangaliwa lile lenye kupewa nguvu. Naye Mwenyezi Mungu ndiye Anayejua zaidi [kitabu cha: Zad Al-Maad, 1/223 na kuendelea].
Na katika hili tunaona kuwa mtazamo wa Jamhuri ya wanachuoni – ambao ni kutanguliza magoti – ndio wenye nguvu zaidi, na hii ni kutokana na nguvu ya dalili zao, isipokuwa sisi tuna tahadharisha kuwa hii ni katika mapambo ya Sala na ambayo hayaleti athari ya kusihi kwa Sala, mwenye kutanguliza magoti yake kwanza Sala yake ni sahihi, na mwenye kutanguliza mikono yake Sala yake pia ni sahihi, na masuala haya yenye tofauti yanafaa kufuata kauli yoyote pasi na yeyote kupinga kauli ya mwengine.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.