Wito wa Swala ya Kupatwa kwa Jua na Mwezi.
Question
Watu huitwa vipi kwa ajili ya kuswali Swala ya kupatwa kwa Mwezi na Jua? Je, watu huitwa kwa kusema (Asalatu Jami’ah) au kwa adhana?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu:
Wito wa Swala ni ujulisho wa wakati wa Swala, na maana ya Adhana kwa upande wa lugha ya Kiarabu ni: ujulisho, Mola Mtukufu Amesema: {Na watangazie watu Hija}[AL-HAJJ: 27], kwa maana ya kuwajulisha watu juu ya Hija.
Ama kwa upande wa Sharia ni: kujulisha kuingia wakati wa Swala ya lazima, kwa kutumia matamshi na maneno yanayofahamika na kwa sifa maalumu.
Na neno Kusuf kwa upande wa lugha: hutumika kwa maana ya matukio mawili ya kupatwa kwa jua na mwezi, lakini lililokuwa maarufu kwa wanachuoni, lina maana ya tukio la kupatwa kwa jua, na neno Khusuf linahusishwa na tukio la kupatwa kwa mwezi, kama ilivyoelezwa na Al-Jauhariy katika kitabu cha As-Sahah kuwa hivyo ndiyo sahihi zaidi [Kitabu Al-Majmuu, Shareh ya Al-Muhadhab 5/37, chapa ya Maktabat Al-Munira].
Ni Sunna kuswali pamoja kwa Swala ya kupatwa kwa jua na mwezi, kutokana na mapokezi kuwa Mtume S.A.W. amesema katika Hadithi iliyokubaliwa na wanachuoni wa Hadithi, ni Hadithi iliyotokana na Bi. Aisha R.A. amesema: “Hakika ya jua na mwezi ni alama mbili miongoni mwa alama za uwezo wa Mwenyezi Mungu, hayatokei matukio ya kupatwa kwao kwa sababu ya kufa kwa mtu au kwa ajili ya uhai wake, ikiwa mtaziona hali hizo, basi swalini”, Mtume S.A.W. akaamrisha kuswali kwa sababu ya matukio hayo kwa amri moja tu, na kutoka kwa Ibn Abbas amesema kuwa: Yeye aliswali na watu wa Basra katika Swala ya kupatwa kwa mwezi rakaa mbili, na akasema: “Kwa hakika nimeswali kwa sababu nimemwona Mtume S.A.W. akiswali”, na hiyo ni moja ya matukio hayo mawili hivyo akafananisha pia na tukio la kupatwa kwa jua, na ni Sunna kuiswali kwa pamoja au mtu mmoja mmoja. [Kitabu Al-Mughniy cha Ibn Qudama, 2/142, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy]
Na Adhana imewekwa kwa sababu ya Swala za Faradhi tu pasi na kuwepo tofauti yoyote ile lengo ni kujulisha kufika kwa wakati wake, kwa sababu Swala za Faradhi au za Lazima zimehusishwa na wakati maalumu, amesema Mtume S.A.W. katika Hadithi ambayo imepokelewa na Imam Bukhariy na Muslim kutoka kwa Malik Ibn Al-Huwairath: “Pindi unapofika muda wa Swala, basi mmoja wenu ainue Adhana na awaswalisheni aliyemkubwa kiumri zaidi yenu”, Mtume S.A.W. akahusisha Adhana na tukio la kufika kwa muda wa Swala ya Faradhi au Swala ya Lazima, wala hakuna Adhana kwa Swala ya Jeneza au Swala ya Maiti wala kwa Swala za Sunna, na katika yale yaliyopokewa katika hilo ni pamoja na Hadithi iliyopokewa katika kitabu cha Imam Muslim kutoka kwa Jabir Ibn Samra amesema: “Nimeswali pamoja na Mtume S.A.W. Swala ya Idd zaidi ya mara moja pasi na kuwepo Adhana wala kukimu Swala”.
Amesema Imam An-Nawawiy katika kitabu cha [Majmuo’] kuwa: “Adhana na kukimu Swala vimewekwa kwa ajili ya Swala tano za kila siku kwa tamko lililo sahihi na kwa kubaliana pia wanachuoni, wala haijawekwa Adhana na kukimu Swala pasina Swala tano na hukuna tofauti katika hilo, ni sawa sawa hakuna Adhana na kukimu Swala kwenye Swala ya Nadhiri au Swala ya Jeneza au Swala ya Sunna, ni sawa sawa pia Swala ya Sunna inayoswaliwa kwa pamoja kama vile Swala za Idd mbili, Swala kupatwa kwa jua na mwezi, Swala ya Kuomba mvua au Sunna isiyoswaliwa kwa pamoja kama vile Swala ya Adhuha”. [Majmuu ya Annawawiy, 3/83, chapa ya Maktabat Al-Munira].
Ama Swala ya kupatwa kwa jua na mwezi: zenyewe hutolewa wito wake kwa kusema “As-Salat Al-Jami’ah” kutokana na yale yaliyokuja ndani ya vitabu viwili sahihi vya Hadithi vya Imam Muslim na Imam Bukhariy kutokana na Hadithi ya Abdillah Ibn Amr Ibn Al-Aas amesema: (Pindi lilipopatwa jua zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. palilinganiwa kwa kusema: Inna Swalata Jami’ah), amesema Imamu Shafiy katika kitabu cha: [Al-Umm “1/269, chapa ya Dar Al-Maarifa]: “Inapendeza kwa Imamu kumwamrisha mwadhini kusema katika Swala za Idd, na katika kuwakusanya watu kwa ajili ya Swala: As-Salat Al-Jamia”.
Amesema Sheikh Zakaria Al-Answariy Al-Shafiy: “Na hulinganiwa kwa ajili ya kuswali pamoja kwa Swala ya Idd mbili pamoja na Swala za Kukamatwa kwa mwezi na jua kwa kusema: As-Salat Al-Jamia’ ” kwa kupokelewa kwake ndani ya vitabu viwili sahihi vya Hadithi katika Swala ya kupatwa kwa jua hivyo linganisha hivyo na Swala zengine zilizobaki” [Kitabu Asmaa Al-Matalib, sherehe ya Raudh Twalib, 1/126, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Na amesema Al-Murdawiy Al-Hanbaliy: “Mlango wa nne: kilicho sahihi katika madhehebu ni kuwa hulinganiwa kwenye Swala ya kuptwa kwa jua kwa kusema: As-Salat Al-Jamia’ ”. [Kitabu Al-Insaaf cha Murdawiy, 1/428, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Na amesema Ibn Qudama: “Inasuniwa kutoa wito kwa ajili ya Swala ya kupatwa kwa Jua kwa kauli hii: As-Salat Al-Jamia’, kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Amr, amesema: llilipatwa jua enzi za Mtume wa Mwenyezi Mungu - S.A.W. - na ukatolewa wito wa kusema As-Salat Al-Jamia’ ” Hadithi imekubaliwa na wanachuoni wote wa Hadithi, “wala haijasuniwa Swala hizo kuletwa Adhana na kukimu, kwa sababu Mtume S.A.W. ameziswali pasi na Adhana wala kukimu, na kwa sababu Swala hizo si katika jumla ya Swala tano za kila siku, hivyo kufananishwa na Swala zengine tu za Sunna”. (Kitabu Al-Mughniy cha Ibn Qudama, 2/142, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy)
Amesema Al-Bahawatiy Al-Hanbaliy: “Hulinganiwa kwenye Swala ya Idd, kupatwa jua na mwezi na Swala ya Kuomba mvua: as-salat Al-Jamia’ ”, amesema kwenye kitabu cha Al-Furuu: hulinganiwa kwenye Swala ya kupatwa kwa jua kwani Hadithi imo kwenye kitabu cha Bukhariy na Muslam”. [Kitabu Kashaf Al-Qinaa kutokana na Matn Al-Iqnaa, 1/233, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Kutokana na maelezo hayo, na kutokana na uhalisia wa swali ni kuwa: Swala za kupatwa kwa jua na mwezi huswaliwa kwa pamoja na watu huitwa kwa ajili ya kuziswali Swala hizo kwa kusema “Swalat Al-Jamia’ ”, wala hakuna wito kwa kutumia Adhana, kwani Adhana ni kwa ajili ya Swala za Lazima tu.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufuni Mjuzi zaidi