Kazi za Udalali.
Question
Ni ipi hukumu ya Uislamu kwenye kazi za udalali?
Answer
Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimwendee Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, pamoja na watu wake na Masahaba wake na wale waliomfuata. Baada ya utangulizi huo,
Neno dalali kwa upande wa lugha: ni kazi ya udalali, nayo ni kiunganishi kati ya muuzaji na mnunuzi ili kurahisisha kazi za manunuzi. Dalali wa masuala ya ardhi maana yake ni mtu anaejua zaidi mambo ya ardhi. Na hili ni neno lenye asili ya lugha ya kifursi. “angalia: Alwasiitw uk. 448 chapa ya Dar Ad-da’awa”.
Amesema Al-Khatwabiy: “dalali ni neno la kiajemi, na lilitumika mara nyingi kwa maana ya watu wanaosimamia kazi za mauzo na walikuwa ni watu wa kiajemi, hivyo jina hili likapatikana kutokana na watu hao. Mtume akalibadilisha neno hili na kuita biashara, ambapo jina biashara ni katika majina ya Kiarabu, na katika Hadithi ambayo imepokelewa na Imamu Daud na Tirmidhy kutoka kwa Qais Ibn Abi Ghurza amesema: “Tulikuwa enzi za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. tukiita madalali, Mtume alipita na kutuita kwa jina zuri zaidi kuliko hilo na akasema: “Enyi wafanya biashara hakika kazi za biashara mara nyingi zina upotoshaji na uongo basi changanyeni biashara zenu na kutoa sadaka” (Kitabu Ma’alim As-Sunan, 3/53, chapa ya Al-Matiba’a Al-Elmiya - Halab).
Udalali ni uelekezaji, na uelekezaji kilugha unatokana na: mwenye kuelekeza kitu. Kwa upande wa kimsamiati: ni kuwa mtu wa kati, kati ya muuzaji na mnunuzi, na huyu dalali: ndiye ambaye anakuwa kati, kati ya muuzaji na mnunuzi ili kufanikisha suala zima la uuzaji na ununuzi, ndio huitwa dalali, kwa sababu humuelekeza mnunuzi kuhusu bidhaa, na humuelekeza muuzaji kuhusu bei na thamani. (Kitabu Al-Bahr Al-Raiq Sherh Kanz Al-Daqaaiq cha Ibn Najim Al-Hanafiy, 6/119, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy).
Udalali ni makubaliano yenye malipo: Muuzaji anamuhitaji dalali ili kutangaza bidhaa zake, na mnunuzi pia anamuhitaji dalali ili kufahamu sehemu inayopatikana hiyo bidhaa, au kwa maana nyengine mnunuzi hafahamu njia za majadiliano kwenye kuuza na kununua, au kwa sababu anakuwa hana uwezo wa kutambua bidhaa nzuri na mbovu, lakini moja ya sharti kuu ya udalali ni kuwa mkweli na mwaminifu, na kuelezea kasoro ya bidhaa na uzuri wake kwa uaminifu mkubwa na kwa ukweli. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na atayelileta atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni mdhamini wa hayo} [YUSUF, 72].
Amesema Ibn Al-Arabiy: “Maana ya aya, ni tamko la mambo ya malipo, nayo ni aina ya kazi ambayo ndani yake kuna malipo kwa mfanyaji, na kazi ya aina hii aliifanya Mtume S.A.W. pamoja na Masahaba wake bila ya tofauti yoyote ile”. (Kitabu cha Ahkaamu Al-Qurani cha Ibn Al-Araby 3/65, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya).
Jopo la Maimamu limeelezea kufaa kwa kazi hii ya udalali, na inafaa pia kuchukua malipo yanayotokana na kazi hii, amesema Sahnuun: “Niliuliza: je inafaa kuchukua malipo kwenye kazi ya udalali kwa kauli ya Malik? Akasema Ibn Qaasim: ndio kwani nilimuuliza Malik kuhusiana na muuza nguo, mtu anatoa pesa kununuliwa nguo kisha anayenunua anaongeza Dinar tatu katika kila Dinar mia moja anayoitumia kununulia nguo? Akasema: hakuna ubaya kwa hilo, na akasema: hii ni katika kazi ya malipo” (Kitabu Al-Mudawana, 3/466, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah).
Amesema Imamu Bukhari katika kitabu chake: Mlango wa malipo ya udalali, “hajaona Ibn Syreen, Atwaa, Ibrahim na Hassan malipo ya kazi ya udalali kuwa kuna ubaya, na akasema Ibn Abbas: hakuna ubaya wowote kusema: uza hii nguo, na kile kitakachozidi zaidi ya pesa fulani basi hicho ni chako, akasema pia Ibn Syreen: ikiwa atasema: uza kwa thamani hii, na kitakachozidi ni chako, au tutagawana mimi na wewe basi hakuna ubaya wowote ule”. Na amesema Mtume S.A.W: “Waislamu wana utekelezaji wao”. (Kitabu: Sahih Al-Bukhariy, 3/92, chapa ya Dar Tuq An-Najat).
Amesema Ibn Qudama katika kitabu cha Al-Mughniy. “Inafaa kumlipa dalali anayemnunulia mtu nguo” na akaruhusu pia Ibn Syreen, Atwaa na An-nakhay, na akaichukiza At-Thauriy na Hamada rai hiyo.
Na dalili yetu katika hili ni kwamba ndani yake kuna manufaa yaliyo halali. Inafaa pia kufanya uwakilishi, na inafaa kumlipa dalali kama vile kwenye ununuzi wa jengo, na inafaa kumlipa kwa muda unaofahamika, mfano wa kumlipa ndani ya siku kumi akiwa anamnunulia mtu vitu, kwa sababu muda unafahamika na kazi pia inafahamika, na akamlipa katika kila Dirhamu elfu moja kitu chenye kufahamika, inafaa pia ikiwa atasema: kila unaponinunulia nguo basi nitakulipa Dirhamu moja, na nguo ikawa inafahamika kwa sifa, au yenye kukadiriwa kwa thamani, basi inafaa”. (Kitabu Al-Mughniy cha Ibn Qudama, 5/270, chapa ya Dar Ihyaa Al-Turath Al-Araby).
Amesema Al-Murdawiy katika kitabu cha Tas-hih Al-Furuu kuwa: “Uuzaji wa dalali na ununuzi wake ni sawa na kazi ya mshonaji, na fundi seremala pamoja na malipo mengine ya wadau wengine, kila mmoja anaweza kutaka uwakilishi, hata kama mwakilishwa hana wa kumwakilisha”. (Kitabu: Tas-hih Al-Furuu cha Murdawiy, 7/113, chapa ya Dar Al-Risala).
Amesema Al-Bujairamiy katika kitabu chake: “Alikuwa Umar Ibn Al-Khattab R.A. ni dalali akifanya kazi kati ya muuzaji na mnunuzi” (Kitabu Hashiyat Al-Bujairimy, 3/299, chapa ya Dar Al-Fikr).
Katika jibu la swali ni kuwa: Udalali kisheria ni kazi inayofaa madamu tu kinachofanyika ni halali, na wala hakuna ubaya wowote kufanya kazi ya udalali. Nayo (kazi ya udalali) inazingatiwa kuwa ni halali kwa makubaliano yenye malipo kisheria.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.