Kuainisha Umri wa Kichinjo Udh-hiya.
Question
Je, Kuna umri maalumu kwa mnyama anayechinjwa kama Udh-hiya au hapana? Na kama umri huu usipopatikana, je, inajuzu kumchinja mnyama wa umri mdogo kuliko huo, hasa kwa sasa kwa kuwa kuna aina za malisho yenye nguvu zaidi kwa mnyama ambayo yanamfanya kuwa mnene zaidi japokuwa ni mdogo?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Udh-hiya ni miongoni mwa Sunna zilizotiliwa mkazo, na sheria yake ndiyo kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuihuisha Sunna ya Bwana wetu Ibrahimu Al-Khalil SAW, na kwa ajili ya kutukuza ibada za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Namna hivi; anayezihishimu alama za (dini ya) Mwenyezi Mungu, basi hilo ni jambo la katika utawa (ucha Mungu) wa nyoyo}. [AL HAJJ: 32], na akasema pia: {Nyama zao (wanyama hao wanaochinjwa) hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini inamfikia (kwake Mwenyezi Mungu) taa, (Utawa)}. [AL HAJJ: 37].
Wanazuoni walishurutisha masharti ya Udh-hiya, na baadhi ya masharti yanaambatana na udh-hiya yenyewe, na mengine ni ya mwenye Udh-hiya. Na miongoni mwa masharti ya Udh-hiya ni mifugo yaani: ngamia, ng’ombe, nyati, na mbuzi na kondoo, na haijuzu aina nyingine ya mifugo au ndege; kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na kila uma tumewafanyia mahali pa kuchinjia mihanga ya Ibada ili kulitaja jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile alivyowaruzuku katika wanyama hao wenye miguu minne}. [AL HAJJ: 34].
Imamu Al-Qurtubiy anasema: “Wanyama waliokusudiwa hapa ni: ngamia, ng’ombe, na mbuzi. [Tafsiir Al-Qurtubiy; 12/44, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Masriyah], pia akasema: “Wanyama waliochinjwa kama Udh-hiya, katika kauli ya pamoja ya Waislamu, ni namna nane za wanyama (madume na majike) ya kondoo, mbuzi, ngamia, na ng’ombe”. [Tafsiir Al-Qurtubiy: 15/109].
Al-Baghawiy anasema: “Alisema; {wanyama} yaani ni mifugo; kwa sababu baadhi ya wanyama sio wa kufuga, lakini wa kubeba, kama vile: mafarasi, nyumbu, na punda, na hao haijuzu kuwachinja kama Udh-hiya”. [Ma’aalim At-Tanziil: 3/340, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy]
Na miongoni mwa masharti ya Udh-hiya pia ni kusalimika kwa kasoro mbaya inayopunguza nyama au mafuta yake, isipokuwa kidogo. Na miongoni mwa masharti yake pia ni kuwa mnyama wa Udh-hiya anatakiwa afikie umri maalumu ili ijuzu kumchinja kama Udh-hiya, kwa sababu wanyama kwa ujumla wao hawafai kuwa Udh-hiya kwa ajili ya kujitolea kwa Mwenyezi Mungu; na wengi wa wanazuoni wamekubaliana kuwa: haijuzu kuwa Udh-hiya miongoni mwa ngamia isipokuwa mwenye umri wa miaka mitano au zaidi, na miongoni mwa ng’ombe na mbuzi wawe na umri wa miaka miwili au zaidi, na inajuzu kondoo awe na umri wa mwaka mmoja au zaidi.
Imamu Muslim amepokea katika Hadithi sahihi, kutoka kwa Jabir RA, alisema; Mtume S.A.W, alisema: “Msichinje isipokuwa mnyama wa umri mkubwa, na kama mtapata shida basi mchinje kondoo wa mwaka mmoja”. Yaani haijuzu kama Udh-hiya isipokuwa mnyama wa umri mkubwa, yaani umri wa (Athaniy) kwa ngamia, ng’ombe, na mbuzi; na kuhusu kondoo, haijuzu isipokuwa (Jadha’a), na wanazuoni wamehitilafiana kuhusu (Athaniy) na (Jadha’a); katika madhehebu ya Imamu Shafiy: (Jadha’a) ni wa umri wa mwaka mmoja, na (Athaniy), ni wa umri wa miaka mitano kwa ngamia, na miaka miwili kwa mbuzi na ng’ombe. [Rejea; Tuhfat Al-Muhtaj: 9/348, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy].
Na wafuasi wa madhehebu ya Imamu Malik wamewafikiana na wafuasi wa madhehebu ya Imamu Shafiy kuhusu umri wa (Athaniy) na (Jadha’a), isipokuwa ng’ome ambapo wafuasi wa madhehebu ya Imamu malik wanaona kuwa (Athaniy) ya ng’ombe ambaye ana umri wa miaka mitatu, na kuanzia mwaka wa nne. [Rejea: Hashiyat Ad-Disuuqiy; 2/119, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy]
Na wengi wa wanazuoni pia wanaona kuwa: haijuzu kupunguza umri huu, na kauli zao zinaashiria hivi. Al-Kasaniy katika kitabu chake [Badai’u As-Sanai’i] anasema: “uainishaji wa umri maalumu wa Udh-hiya ni jambo halijuliwi isipokuwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume S.A.W, basi ifuatwe”. [5/70, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]
Katika kitabu cha: [Al-Binayah Ala Al-Hidayah] na Badrud-Diin Al-Ainiy: “Inajuzu kumchinja Kondoo wa mwili mnene, akiwa (Jadha’a) na haijuzu akiwa na mwili mwembamba isipokuwa umri wake ni mwaka mmoja na kuanzia mwaka wa pili, na kuhusu mbuzi haijuzu isipokuwa awe na umri wa mwaka mmoja na kuanzia wa pili, na kuhusu ng’ombe haijuzu isipokuwa na umri wa miaka miwili na kuanzia mwaka wa tatu, akiwa na mwili mnono au la”. [12/47, Ch. ya dar Al-Kutub Al-Elmiyah]
Ibn Abdiin anasema: “Katika kitabu cha Al-Badai’i: Kuainisha umri huo huo, kwa kuangalia mkubwa na mdogo; kama akimchinja wa umri mdogo zaidi basi haijuzu, lakini inajuzu umri mkubwa zaidi, tena nayo ni bora zaidi”. [Radul-Muhtar; 6/322, Ch. ya Dar Al-Fikr]
Al-Kharashiy baada ya kubainisha umri wa wanyama wanayojuzu kuwachinja kama Udh-hiya, anasema: “Hakika umri wa aina hizi za wanyama umetofautiana kutokana na tofauti yake kuhusu uja uzito unaotokea kwa kawaida katika umri uliotajwa, na kwa sababu binadamu kabla ya kufikia umri wa kubalehe ni mwenye upungufu, kadhalika mnyama, kwa hiyo haifai kumchinja kama Udh-hiya”. [3/34, Ch. ya Dar Al-Fikr]
Al-Mawardiy katika kitabu cha [Al-Hawiy] anasema: “ikiwepo kuwa Udh-hiya ni miongoni mwa ngamia, ng’ombe, na kondoo na mbuzi, na isipokuwa aina nyingine za wanyama, basi umri wa Udh-hiya huo unatakiwa, na haijuzu mdogo zaidi miongoni mwake. Na tumekubaliana kwa pamoja kuwa haijuzu kama Udh-hiya mdogo zaidi kuliko (Jadha’a) kwa aina zote, na hailazimiki mkubwa zaidi kuliko (Athaniy) kwa aina zote”. [15/76, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah]
Katika kitabu cha [Asna Al-Mataalib]: “Haijuzu mdogo kuliko (Jadha’a) wa kondoo, wala (Athaniy) wa mbuzi, ngamia, na ng’ombe. Na (Jadha’a) ni wa umri wa mwaka kamili”. [1/535, Ch. ya Dar Al-Kitaab Al-Islamiy]
Ibn Qudamah katika [Al-Mughniy anasema: “Haijuzu isipokuwa (jadha’a) wa kondoo, wala (Athaniy) wa wengine”. [9/439, Ch. ya Maktabat Al-Qahirah]
Na wengi wa wanazuoni walieleza walivyoielekea kwa Hadithi ya Al-Baraa’ Ibn A’azib, alisema: “Mtume S.A.W. alituhutubia Siku ya Idi Kubwa, baada ya Swala akisema: Aliyeswali swala yetu, na kuchinja kichinjo chetu, basi amefanya ibada sahihi, na aliyechinja mnyama wake kabla ya Swala, basi huwa kabla ya Swala na hakutekeleza ibada sahihi, hapo Abu Burdah Ibn Niyar, naye Mjomba wa Al-Baraa’ alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Mimi nilichinja kondoo wangu kabla ya Swala, na nikajua kuwa leo ni siku ya kula na kunywa, nikapenda kuwa kondoo wangu ni wa kwanza wa kuchinjwa nyumbani kwangu, kwa hiyo nilichinja kondoo wangu, nikapata chakula cha adhuhuri kabla sijaja Swali, na Mtume akasema; kondoo wako ni kondoo wa nyama tu, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Tuna mbuzi (jadha’a) mnene zaidi kuliko kondoo wawili, Je, inajuzu kumchinja? Akasema: Naam, lakini haijuzu kwa mtu mwingine yeyote baada yako”. [Muttafaq]
Na kauli yake: “lakini haijuzu kwa mtu mwingine yeyote baada yako” ni dalili ya kuhusishwa kwa Abu Burdah, kwa kupunguza umri ulioainishwa kuhusu Udh-hiya; na pia ni dalili ya kutojuzu kuchinja (Jadha’a) ya kondoo, isipokuwa kwa Abu Burdah, kutokana na hayo, haijuzu kuwachinja ngamia na ngo’mbe wenye umri mdogo. Na kauli yake: “kondoo wako ni kondoo wa nyama tu” yaani siye udh-hiya na hana thawabu ya Udh-hiya, lakini ni kichinjo cha kawaida cha kula, na huenda ni dalili ya kuwa kupata nyama si kusidio la kwanza la kumchinja, na ingelikuwa nyama ni kusudio, basi Mtume angelikubali kondoo wa Abu Burdah, tena Abu Burdah asingelimuulizia kujuzu kwa kumchinja mbuzi wake.
Na Mtume S.A.W., aliruhusia Uqba Ibn A’amir RA., achinje mnyama wa umri mdogo kuliko wa kisheria wa Udh-hiya, na katika vitabu sahihi viwili vya Sunna, kutoka kwa Uqba Ibn A’amir RA., kuwa Mtume S.A.W., alimpa kondoo wengi kwa ajili ya kuwagawa kati ya Masahaba wake, kisha mbuzi au beberu (mwenye umri wa mwaka mmoja) amebaki, na huyu mtu amemwambia Mtume S.A.W., akasema Mtume: “Wewe mwenyewe mchinje kama Udh-hiya” na katika mapokezi ya Al-Baihaqiy: “hapana ruhusa kama hiyo kwa mtu yeyote baada yako”.
Na inafahamika kuwa maoni ya wengi wa wanazuoni kuwa kulazimika na umri unaoainishwa kwa wanyama si suala la akili peke yake, kwa hiyo haijuzu kuupunguza kuliko huo; ingawa wengi wa wanazuoni walihitilafiana na baadhi ya wanazuoni wa Salaf, kama vile: Tawuus, Attaa’, na Al-Awzai’iy, ambao walijuzisha kupunguza kuliko umri huo, wakajuzisha (Jadha’a) miongoni mwa ngamia, ng’ombe, na kondoo kwa jumla, bila ya kumhusisha mtu huyu au yule. [Rejea: Al-Mughniy: 9/348; na Al-Majmuu’: 8/366, Ch. ya Maktabat Al-Irshaad].
Imamu Ibn Hazm anasema: “Kwa njia ya wakii’, Umar Ibn Dhar Al-Hamadaniy alituambia, nilimwambia Tawuus: Ewe Abu Abdul-Rahman: Hakika tuliingia sokoni, tukawakuta (Jadha’a) miongoni mwa ng’ombe wanono na wakubwa, tukawachagua (Athaniy) kwa ajili ya umri wake; na Tawuus akasema: nilipendelea wanene zaidi na wakubwa zaidi” [Al-Muhalla: 6/26, Ch. ya Dar Al-Fikr]. Na (Jadha’a) miongoni mwa ng’ombe, aliyetimia umri wa mwaka.
Rai ya wengi wa wanazuoni yenye nguvu zaidi kwa upande wa dalili, na kwa upande wa maoni yetu, inaweza kusemwa kuwa: kuainisha umri maalumu wa Udh-hiya ni dhana ya atakuwa mnono na mwenye nyama nyingi, kwa kuzingatia hali ya mafakiri na maskini, na katika wakati wa kuwa mwenye umri ulivyo lakini ni mwembamba na nyama chache; na wakati kuwa mwenye umri mdogo, yaani hakufikia umri ulivyo kisheria, lakini ni mwenye nyama nyingi, kama inavyotokea kwa sasa kwa kulisha mnyama malisho yenye nguvu zaidi, ambayo yanazidisha nyama, wakati anapofikia umri ulivyo huenda atakuwa mwembamba na kuendelea kupungua.
Hapa Uislamu unaangalia masilahi ya watu, ambayo ni lengo kuu lililo muhimu miongoni mwa malengo Makuu ya Sharia Tukufu; na kama hakujapatikana mnyama mwenye umri unaotambulika kisheria na mwenye nyama nyingi, na wakati huo akawepo mnyama mdogo kuliko huyo, lakini ana nyama nyingi, basi inajuzu kumchinja kama Udh-hiya, kwa kauli yake Mtume S.A.W.: “Msichinje isipokuwa mnyama wa umri mkubwa, na kama mtakuwa na uzito basi mchinje kondoo wa mwaka mmoja”. [Ameipokea Muslim]
Na kulingana na hayo, basi inajuzu kwa mujibu wa hitajio, na hitajio ndilo linalozingatiwa katika hali ya dharura kwa ujumla au kwa sifa maalumu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.