Hukumu ya Kuchorwa Michoro.
Question
Ni ipi hukumu ya kuchorwa michoro mwilini?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba zake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Michoro ya Mwilini katika lugha ni alama na kubadilisha rangi ya ngozi kutokana na kupigwa au kuanguka, pia kutokana na kudungwa sindano mwilini na kuweka rangi ya buluu au kijani juu yake. [Al-Misbaaah Al-Muniir: 2/661, Kidahizo: WA SHA MA, Ch. ya Al-Maktabah Al-Ilmiyah].
Na katika maana ya istilahi ni: Kudungwa sindano ngozini mpaka damu ikatoka, kisha kuweka rangi ya buluu au wanga mpaka rangi yake ikawa buluu au kijani. [Hashiyat Al-Jamal Ala Sharh Al-Manhaj: 1/417, Ch. ya Dar Al-Fikr]
Na kuchorwa michoro mwilini ni haramu kisheria, kwa mujibu wa Hadithi Sahihi zilizopokelewa kuhusu mwanamke anayechorwa Michoro na yule anayepigwa chapa ya Michoro, na miongoni mwake ni zile Hadithi zilizopokelewa na Imamu Bukhariy na Muslim, kutoka kwa Ibn Umar RA, alisema: “Mtume S.A.W., amemlaani mwenye kuunga nywele na mwenye kuungwa (nywele), na mwenye kuchorwa michoro mwilini na mwenye kutaka kuchorwa michoro mwilini”.
An-Nafarawiy mfuasi wa madhehebu ya Malik katika kitabu cha [Al-Fawakih Ad-dawaniy] anasema: “Wanawake wanakatazwa Kuchorwa Michoro usoni au mkononi au katika sehemu nyingine za mwili. Na katazo hili ni kwa ajili ya kuharamisha, na linalingana kwa wanaume na wanawake. Bali katazo hili kwa wanaume ni kubwa mno. Na Ibn Rushd anasema: dalili ya kuharamisha ni Hadithi iliyopokelewa katika Vitabu Viwili Sahihi kauli yake Mtume S.A.W.: “Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kuunga na kuungwa nywele, na mwenye kuchonga na mwenye kuchongwa meno, na mwenye kuchora michoro mwilini, na mwenye kuchorwa michoro mwilini, na wanaochonga nyusi, na wanaochonga meno, wakaacha mwanya kwa sababu ya uzuri, na wanaobadilisha maumbile aliyoyaumba Mwenyezi Mungu”.
Kwa hiyo Michoro ya Mwilini ni haramu, kutokana na uwazi wa Hadithi, hata wanazuoni, Ibn Rushd na Ibn Shaath wameeleza kuwa ni miongoni mwa dhambi kubwa, ambapo mtendaji wake hulaaniwa. [Al-Fawakih Ad-Dawaniy Bi Sharh Risalat Al-Qairawaniy; 2/314, Ch. ya Dar Al-Fikr]
Na Al-Mardawiy mfuasi wa madhehebu ya Hanbal anasema: “kuchorwa mwilini kunaharamishwa kwa rai sahihi ya Madhehebu”. [Al-Insaaf: 1/126, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy]
Sheikh wa Uislamu Zakariya Al-Ansariy mfuasi wa madhehebu ya Shafi anasema: “Michoro ya Mwilini ni kupiga sindano ngozini, mpaka damu ikatoka, kisha kuwekwa rangi juu yake. Na kufanya hivyo ni haramu kwa uwazi kutokana na Hadithi ya Vitabu viwili Sahihi: ““Mwenyezi Mungu amemlaani mwenye kuunga na kuungwa nywele, na mwenye kuchora Michoro ya Mwilini, na mwenye kuchorwa Michoro ya Mwilini, na mwenye kuchonga na mwenye kuchongwa (meno), na mwenye kuchonga nyusi, na mwenye kuchongwa nyusi”, kwa maana ya mtendaji na mtendewa hivyo. [Asna Al-Mataalib: 1/172, Ch. ya Dar Al-Kitaab Al-Islaamiy]
Na kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia ni kuwa: Michoro ya Mwilini kwa sifa yake iliyotajwa katika maelezo yaliyotangulia ni haramu kisheria.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.