Hukumu ya Kumiliki Mitungi ya Gesi na Kuiuza kwa Bei ya Juu.
Question
Baadhi ya maeneo nchini Misri yamekuwa na shida kubwa ya mitungu ya gesi, baadhi ya watu wanatumia nafasi hiyo na wanaingia makubaliano na wale wenye kuhifadhi mitungi ya gesi ili wanunue kwao yote na kuwauzia watu kwa bei ya juu. Ni nini hukumu ya hilo katika sharia?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Mitungu ya gesi ni katika bidhaa muhimu ambazo serikali inafadhili sehemu ya gharama zake, na kulazimika kuimarisha upatikanaji wake na kuiuza kwa bei ya chini kwa wananchi hata kama bei ya gharama zake itapanda, serikali inabeba gharama zake kwa lengo la kusaidia sehemu kubwa ya jamii inayokumbwa na hali ngumu ya maisha, riziki ya tabu na kipato kidogo, nayo pia ni moja ya njia za kukidhi mahitaji ya wenye kipato kidogo na kuinua viwango vyao vya kipato kwa kupata mali kwa sura isiyo ya moja kwa moja, nayo ni ile sura ya ufadhili wa serikali. Hii yote ni katika wajibu wa kisheria kwa serikali na jamii kuelekea kwa wananchi wake hasa wale wenye kipato cha chini.
Kinachotokea katika madirisha ya kuuzia mitungi hii ya gesi ni pamoja na kushikiliwa na baadhi ya walanguzi wakisaidiana na watu wasio na uaminifu miongoni mwa wale wauzaji – ambao wamepewa usimamizi na serikali wa kuuza gesi hiyo kwa bei nafuu – maana yake: Kudhibiti mali ya umma ambayo kwenye Sharia huitwa “Mali ya Mwenyezi Mungu”, kwa sababu kila mtu ndani ya jamii ana haki na fungu kwenye mali hiyo, na maana nyengine ni kutofika ulipiaji wa serikali wa mitungi hii kwa wananchi wanaostahiki, hasa wale wenye kipato kidogo ambao wanataabika sana na kununua mitungi kwa bei ya juu. Yote hayo yanazingatiwa kuwa ni uadui dhidi ya mali za watu, na uharibifu kwenye ulimwengu, pamoja na kuwaingiza kwenye matatizo wale wenye mahitaji kwa kushikilia haki zao na kuwazuia kuzifikia. katika hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma} [AN NISAA: 29]. Na anasema Mtume S.A.W.: “Hakika damu zenu na mali zenu na heshima zenu kwenu ni vitukufu, kama ilivyo tukufu siku yenu hii, ndani ya mji wenu huu, katika mwezi wenu huu”. Hadithi hii imepokelewa na Maimamu wawili kutoka kwa Abi Bakr R.A.
Kuingilia kati kwa hawa watu wenye kushikilia mitungi hii pamoja na hawa walanguzi inazingatiwa kwa mujibu wa Sharia ni ukosefu wa uaminifu na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W., na kukosa uaminifu kwa jamii ambayo imeishi kwenye upotovu wao, pasi na kulinda mali ya jamii na kula heri za jamii, kisha kufanya vitendo vyenye madhara kwao, wanaingia ndani ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua} [AL ANFAAL: 27]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini} [AL ANFAAL: 58]. Kama ambavyo vitendo vyao hivyo ni uharibifu wa mali ya umma, kwa sababu wanashikilia bidhaa hii inayolipiwa na serikali kwa ajili ya wananchi ili wapate kuchuma pasi na shida yeyote. Kukosa kwao uaminifu na kuwarahisishia walanguzi kupata mitungi ya gesi ili wapate kuwauzia watu kwa bei ya juu, ni kushiriki kwao katika dhulma na uovu pamoja na kushikilia haki za watu. Na kufanya hivyo ni dhambi na ni uhalifu, na ni utendaji wa madhambi makubwa yasiyoweza kubebwa na mtu yeyote. Kama ambavyo, vitendo vyao hivi ni kwenda kinyume na vyombo vyenye mamlaka ambavyo Mwenyezi Mungu ameamrisha kuzitii mamlaka hizo na kutokwenda nazo kinyume. Mola Mtukufu anasema: {Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, namt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi} [AN NISAA: 59].
Pindi inaposhikiliwa hii mitungi ya gesi inayofadhiliwa na serikali na hawa walanguzi kutoka kwa wale waliouza dhamira zao miongoni mwa wasimamizi, kisha walanguzi hao wakauza kwa bei ya juu ambayo wanailazimisha kwa watu, basi hao kwa hilo wanakuwa wamekusanya dhambi kwa milango mingi, ambapo wanakuwa wamekwenda kinyume na serikali na kushikilia mali ya umma, na kuwazuia watu kupata haki yao, na kuingia kwenye kauli ya Mtume S.A.W.: “Mwenye kujiingiza kwenye bei za Waislamu ili kupandisha bei hizo, basi inakuwa ni haki kwa Mwenyezi Mungu kumkalisha ndani ya moto Siku ya Kiyama”. Hadithi hii imepokewa na Imamu Ahmad. Watu hao wanakuwa wameingia katika mambo ambayo Sharia imeutilia mkazo uharamu wake, ikiwa ni katika Ulanguzi. Na Ulanguzi katika lugha ni: Kuzuia kitu kwa lengo la kusubiri thamani yake ipande – kama ilivyokuja kwenye [Kamusi ya Al-Muheetw” 1/378 Ch. Taasisi ya Risala], na [Shams Al-Uluum ya Hameery 3/1539 Ch. Dar Al-Fikr], na yaliyokuja katika maelezo ya baadhi ya watu wa lugha kuwa: Kuzuia chakula, uwazi ni kuwa haikusudiwi kuhusisha uelewa wa kuhodhi kwenye chakula tu, isipokuwa kwa kuzingatia chakula ndicho kinachokusudiwa zaidi kwenye uelewa huu, kutokana na watu kukihitaji zaidi, na mahitaji haya kuwa endelevu kila siku, kwa upande mwingine ni kuwa chakula ndicho kinacholanguliwa sana kuliko vitu vingine, kwani kilikuwa katika mahitaji muhimu sana katika zama za kale.
Ama kwa upande wa istilahi ya Kifiqihi: Miongoni mwa wanachuoni wamekufanya kuhodhi huku bidhaa ni maalumu nako ni kitendo cha kuzuia chakula na nafaka. Miongoni mwao wapo walioipanua zaidi maana yake katika kila bidhaa inayohitajika katika Jamii.
Zimepokelewa Hadithi nyingi zinazoutahadharisha Ulanguzi na kuukataza, kutokana na matokeo yake mabaya kwa watu na kwa jamii. Miongoni mwa Hadithi hizo ni pamoja na ile iliyopokelewa na Imamu Muslim kutoka kwa Maamar Ibn Abdillah R.A., Hakika ya Mtume S.A.W., amesema: “Hakuna mwenye kufanya ulanguzi isipokuwa ni mwenye kufanya makosa”.
Na imepokelewa na Imam Ahmad kutoka kwa Abu Huraira R.A., kuwa: Hakika ya Mtume S.A.W., amesema: “Mwenye kuhodhi bidhaa akawa anataka kuwauzia waislamu kwa bei ya juu, basi mtu huyo yuko makosani”.
Jopo la wanachuoni limepitisha kuwa hii ni dalili ya uharamu wa Ulanguzi kupitia Hadithi hii, katika vitu vinavyohitajiwa na watu katika maisha yao bila ya kuuhusisha upande wa chakula tu, kwa kuwa lengo ni kuwasababishia watu madhara, na hili linahusisha kila kitu wanachokihitaji watu, na ikawa maisha yao hayaendi isipokuwa kwa kitu hicho.
Amesema Shaukaany katika kitabu cha: [Naili Al-Autwaar 5/262 – 263, Ch. Dar Al-Hadith: “Uwazi wa Hadithi ni kuwa Ulanguzi ni haramu pasina kutofautisha kati ya chakula cha binadamu na cha wanyama na kati ya chakula kingine. Na kutumika neno “chakula” katika baadhi ya mapokezi Haifai kuhusisha na mapokezi mengine, bali hili ni tamko la mmoja kwa kusudio la wengi, na hii ni kwa sababu kuzuia hukumu hiyo kwa kisichokuwa chakula, ni katika uelewa wa kupachika, ambao Wanachuoni hawaufanyii kazi. Na matokeo yake ni kuwa pindi sababu inapokuwa ni kuleta madhara kwa Waislamu, kuhodhi huko kwa bidhaa hakumishwi isipokuwa kwa sura yenye kuleta madhara kwao. Na katika hukumu hiyo, zinalingana bidhaa za vyakula na zinginezo, kwa kuwa wao wanadhurika kwa bidhaa zote zinazohodhiwa na kulanguliwa.
Ulanguzi ni sababu ya kuenea kwa chuki pamoja na mgawanyiko wa jamii, lakini pia kuporomoka kwa mahusiano kati ya watu, na kupelekea matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii, kama vile ukosefu wa ajira, kupanda kwa bei, rushwa, unafiki, wizi na ulaghai.
Kutokana na maelezo hayo na kupitia swali ni kwamba: Yale yanayofanywa na wahusika wa kuhifadhi na kusimamia mitungi ya gesi kwa kushirikiana na baadhi ya walanguzi kwa kuwauzia wao ili watumie vibaya mahitaji ya watu pamoja na kuwapandishia bei, kwa upande wa Sharia, hii inazingatiwa kuwa ni usaliti wa uaminifu na ni kwenda kinyume na amri ya serikali, lakini pia kurahisha kushikiliwa kwa mali ya umma, na kula mali za watu kwa njia batili, na pia kupoteza haki zao, na ni usumbufu mkubwa kwa wenye kuhitaji na wale wenye kipato kidogo, ambapo kila moja kati ya hayo ni miongoni mwa makosa makubwa. Ama kwa wale walanguzi ambao wanafanya juhudi ya kuongeza bei za mitungi ya gesi wanakuwa wameingia kwenye mlango mzito wa makosa maovu na uharibifu katika ardhi, na kushikilia mali za umma, pamoja na kula mali za watu kwa njia batili, na kufanya vitendo vya ukiritimba wa bidhaa muhimu ambazo zinahitajika sana na watu lakini pia ni kwenda kinyume na mamlaka ya nchi.
Na mwenye kuwafahamu watu hawa au hao wengine, anapaswa kusimamia jukumu lake la kuamrisha mema na kukataza mabaya, kwa kutoa nasaha kwa wale wenye kunasihika miongoni mwao, au kufanya juhudi ya kuondoa shari zao kwa kufikisha taarifa kwenye mamlaka husika ili mamlaka hizo zisimamie wajibu wake kuondosha uovu wao.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.