Hukumu ya Kuotesha Nywele.

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Kuotesha Nywele.

Question

Ni ipi hukumu ya kuotesha nywele za asili? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba zake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kupenda mapambo na kuondosha yale yanayomtia aibu mtu ni jambo la kimaumbile linalokubalika kisheria, kwa mujibu wa maelezo yaliyotajwa katika Hadithi iliyopokelewa na Maimamu Wawili kuhusu mgonjwa wa mbalanga, Kipara na Kipofu. Na yaliyomo katika Hadithi hiyo: "Na akaja, (yaani Malaika) kwa mwenye kipara akasema: Nini unachokipenda zaidi? Akasema: Nywele nzuri, sitaki sifa ya mwenye kipara kwa kuwa watu wananitia kasoro, akasema: Alimgusa kwa mkono wake, naye akapata nywele nzuri”. Hapa ufahamu wa dalili ni Malaika kukubali ombi la mtu huyo pamoja na kulijibu.
Abu Dawud akapokea kutoka kwa Abdul Rahman bin Turfa kwamba babu yake A’rfaga bin Asa’d alikatwa pua yake, akatengeneza pua ya karatasi ikamsababishia kuoza, basi Mtume S.A.W. akamwamrisha atengeneze pua ya dhahabu.
Hadithi hii ilipokelewa na Al-Tirmizy na alisema: “Hadithi hii ina hukumu ya Hasana Gharib… Na ilipokelewa na zaidi ya mwanazuoni mmoja miongoni mwa wanazuoni kuwa walifunga meno yao kwa dhahabu, na katika Hadithi hiyo ni hoja kwao”.
Tena Hadithi hii ni dalili kuu katika mlango wa mapambo, na waliotangulia walitegemea Hadithi kama alivyoitaja Al-Tirmizy kutoka kwa baadhi yao.
Ama kuhusu kitendo cha kuotesha nywele ni kufanyiwa upasuaji wa kisasa ambapo daktari anachukua sehemu ya ngozi ambayo ina nywele na kuipandikiza katika sehemu nyingine ambayo haina nywele, nayo inawezekana kuwa ya mtu mwenyewe au ya mtu mwingine. [Hukumu ya nywele katika Fiqhi ya Kiislamu, Taha Muhamad Fars, Uk. 182, Ch. Dar Al Bohuoth wa Ad Derasat Al Islamiyah na Ihiyaa At Turaath, Imerits].
Suala hilo katika sura yake, linabainika kwamba sura iliyotajwa haiingii katika kitendo cha kuunganisha ambacho kilikatazwa katika Hadithi iliyopokelewa na Maimamu wawili, Bukhari na Muslim, kutoka kwa Aisha R.A. kwamba Mtume S.A.W. anasema: “Mwenyezi Mungu Amemlaani mwenye kuunganisha au kuunganishwa nywele”. Na katika mlango huo ni kutoka kwa kundi la maswahaba R.A.
Al Badri Al Ainiy akasema katika kitabu cha: [Sharhu Sahihi Al Bukhariy], "Muunga nywele ni yule anaye anaeunganisha nywele zake na nywele nyingine ili kuzifanya ziwe nyingi kwazo, na yeye ni mtendaji, na muunganishiwaji ni yule mwenye kutaka afanyiwe hivyo". [Umdat Al Qaari' 296/19, Ch. Dar Ihiyaa At Turath Al Arabiy, Bairut.]
Kwa hivyo, kuotesha nywele hakuchukui hukumu ya kuunganisha nywele, kwani hakuambatani kisheria na wala kilugha.
Kitendo cha kuotesha nywele kina hali kadhaa:
1. Hali ya kwanza ni: Kuotesha nywele kutoka kwa mtu mwenyewe:
Na hukumu yake ni kuwa inajuzu kisheria, maana mtu ana haki ya kuchukua kiungo kutoka mwilini mwake kwa ajili ya manufaa yake mwenyewe akitanguliza masilahi yanayomfaa zaidi. Ikiwa yule aliyepigwa juu ya uso wake kwa kitu kinachoweza kusababisha kuua au kuvunja au kumtia kasoro akaondosha kwa mkono wake, basi ana haki ya kufanya hivyo katika hali zote, hata ikiwa mkono wake utapata madhara. Na ikiwa hivyo, basi suala la kunyoa nywele kutoka katika baadhi ya sehemu za mwili na kuotesha katika sehemu nyingine ni halali pia.
Ibn Nagm Mfuasi wa Madhehebu ya Hanafi anasema: Mabaya mawili yakikutana, hutazamwa lenye madhara makubwa zaidi, na kutendwa lenye madhara madogo zaidi, Azaila'iy akasema….. halafu aina katika masuala hayo, kwamba mtu akipatwa na madhara miwili yanayolingana, anaweza kuchukuwa lolote atakalo katika mawili hayo. Na yakitofautiana basi atachagua lililo jepesi zaidi.
Na Maelezo yalitolewa na Baraza la Fiqhi ya Kiislamu – la Taasisi ya Mkutano wa Kiislamu mjini Jida – uliofanyika tarehe 18 mpaka 23 mwezi wa Mfungo tano, mwaka wa 1408 Hijrah, sawa na tarehe 6 mpaka 11 mwezi wa Februari mwaka wa 1988, baadhi ya maamuzi miongoni mwayo ni kwamba: Inajuzu kuhamisha kiungo cha mtu kutoka sehemu moja na kukipeleka sehemu nyingine katika mwili wake pamoja na kuhakikisha kwamba manufaa yanayotarajiwa kwa kitendo cha kuhamisha yanazidi madhara yatakayoweza kusababishwa na kitendo hicho, kwa sharti kwamba kitendo hicho kifanyike kwa kurudisha kiungo kilichopotea au kuboresha sura yake au kazi yake au kurekebisha kasoro au kuondosha ubaya unaosababisha madhara ya kisaikolojia na ya kimwili kwa mtu.
Hali ya Pili: Kitendo cha kuotesha nywele kutoka kwa mtu mwingine:
Nacho ni halali kwa mujibu wa kauli za wanaosema: Kupata manufaa kwa nywele za binadamu; nayo ni madhehebu ya Muhammad bin Al-Hassan.
Al Badriy Al-A’ny anasema katika kitabu cha: [Sharh Al Hidaya], kitabu hichi ni miongoni mwa vitabu vya wanazuoni wa Madhehebu ya Hanafi: “Haijuzu kuuza wa nywele za binadamu wala kuzitumia katika kujinifaisha nazo” na wala hakuna hitilafu baina ya wanachuoni katika suala hili isipokuwa riwaya kutoka kwa Muhammad – Mwenyezi Mungu Amrehemu, - yeye anasema “Inajuzu kunuafaika na nywele za binadamu”, na anasema hivyo kwa kuchukua dalili kutoka kkatika Hadithi: “Mtume S.A.W. alipozikata nywele zake aliwagawia Masahaba zake”, na wao walikuwa wanapata baraka kwa nywele hizo, na kama zingelikuwa najisi basi Mtume S.A.W, asingelifanya hivyo kwa kuwa huwezi kupata baraka katika najisi”. [Kitabu cha: Al Binayah fee Sharh Al Hedayah 166/8, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]
Jambo linaloitia nguvu kauli hii ni kuwa suala la kuzika nywele za binadamu haliwajibiki; kwa kuwa hakuna maandiko yaliyo wazi katika suala hili, na kwa hivyo basi hakuna rai nyingine katika mlango huu kama alivyotaja Baihaqy katika kitabu cha: [Shua’b Al Iman 232/5, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah, Bairut]. Kwa hivyo, suala la kuzika nywele ni miongoni mwa mambo yanayopendeza tu.
Imamu Nawawiy anasema: "Inapendeza kuzizika ardhini nywele zilizonyolewa na kucha zilizokatwa. Hadithi hii ilipokelewa na Ibn Omar R.A. wote wawili, kwa makubaliano ya wanazuoni wetu”. [Al-Majmu’ Sharhu Al Muhazab, 1/289, 290, Ch. Dar Al Fikr]
Na Ibn Qudamah; mwanachuoni wa Madhehebu ya Hanbali anasema: "Inapendeza kuzizika ardhini kucha ziliyokatwa na nywele zilizonyolewa". [Al Moghniy 66/1, Ch. Maktabat Al Qaherah]
Ama zikiwa hazikupatikana nywele kutoka kwa mtu mwenyewe, au mtu mwingine bila ya malipo yoyote, basi inajuzu kununua nywele kwa pesa katika hali ya dharura au kuhitaji. Hata ikiwa hakuna mtu yeyote aliyezungumzia kuhusu kujuzu kuuza nywele za mwanadamu, lakini msingi wa: "Kuchukua fedha kwa kuondosha haki ya umiliki wa kitu", inayojulikana kwa wanazuoni wa Madhehebu ya Shafi inaweza kutumiwa katika sehemu hii.
Ibn Hajar Al Haitamiy mwanachuoni wa Madhehebu ya Shafi, anasema: "Inajuzu kuhamisha umiliki maalumu kwa pesa". [Tuhafat Al Menhaaj 238/4, Ch. Al Maktabah At Tojariyah Al Kubra]
Hali ya Tatu: Kuotesha nywele zisizo kuwa za mwanadamu (Nywele za bandia):
Inajuzu kuotesha nywele za bandia, na hilo haliingii katika hukumu ya kuunganisha nywele ambayo imekataliwa.
Ibn Qudamah anasema katika kitabu chake: [Al Mughniy]: "Ni wazi kuwa lililoharamishwa ni kuunganishwa nywele kwa nywele, kwani kufanya hivyo kuna udanganyifu, na kutumia nywele zenye hitilafu katika unajisi wake, na zaidi ya hayo hakuna kinachoharamishwa kwani hakuna maana kama hiyo ndani yake na pia hakuna madhara ndani yake". [Al Mughniy 70/1]
Na kuotesha nywele kwa ujumla wake hakuzuii udhu na josho; kwani nywele zinaoteshwa katika maoteo yake na chini ya ngozi na kitendo hicho hakibatilishi josho, kwani kinafanywa chini ya ngozi siyo juu yake. Ama kuhusu udhu, lengo lake ni kupaka maji baadhi tu ya sehemu yoyote ya kichwa na hilo linapatikana.
Kuhusu suala la kupunguza nywele wakati wa kutekeleza ibada ya Hija, ikiwa nywele hizo ni nywele za binadamu basi zina hukumu zile zile za nywele zake mtu huyo. Na ikiwa ni nywele za bandia basi hazichukui hukumu za nywele za asili, na inatosheleza kwa kuchukua nywele tatu tu za asili kama zitapatikana, au inatosha kupitisha wembe juu ya sehemu ya kichwa katika sehemu ambazo kwa kawaida zinazoota nywele, hata kama hakuna nywele, kwa kupendeza kufanya hivyo na sio Kuwajibika.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas