Misingi ya Kuzitabiri Ndoto za Usi...

Egypt's Dar Al-Ifta

Misingi ya Kuzitabiri Ndoto za Usingizi.

Question

Je, Misingi ya kuzitafsiri ndoto ni elimu? Na yapi marejeo yake? Na je, jambo hili lilikuwepo katika Mataifa yaliyotangulia? Na wakati upi ni sahihi kwa mtu kuzitafsiri ndoto, na hasa kwa kuwepo onyo la kufanya hivyo kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya utangulizo huo:
Asili ya kutabiri katika lugha ya Kiarabu ina maana ya kuvuka na kuondoka, na makusudio yake ni kuvuka kwa matukio ya jambo fulani.
Na Al-Fayumiy anasema: “niliuvuka mto yaani: niliukatisha hadi upande mwingine, na niliitabiri ndoto yaani: niliifasiri, na katika Uteremsho: {ikiwa nyinyi mnaweza kufasiri ndoto}. [YUSUF: 43], na nilivuka njia yaani: niliipita, na mvukaji njia ni mpitaji. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: {isipokuwa mmo safarini}. [AN NISAA: 43], na Al-Azhariy anasema: msafiri huenda anahitaji maji, na pia imesemekana kuwa makusudio yake: isipokuwa mkiwa mmepita msikitini bila ya kunuia Swala”. [Al-Misbaah Al-Muniir: 2/389, kidahizo: (A’a- Ba –Ra), Ch. ya Al-Maktabah Al-Ilmiyah].
Al-Qurtwubiy anasema: “Kauli yake Mwenyezi Mungu: {Enyi wakubwa! Niotoleeni ndoto yangu} [YUSUF: 43], yaani: niambieni hukumu ya ndoto hii {ikiwa nyinyi mnaweza kufasiri ndoto}. [YUSUF: 43], na ibara hii imechukuliwa kutoka katika kuvuka mto, na maana ya niliuvuka mto: nilifikia ufuko wake, kwa hiyo mtabiri ndoto anaelezea matukio yake”. [Aj-Jamii’ Li Ahkaam Al-Quran: 9/200, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Misriyah]
Kuhusu uhakika wa ndoto, Imamu An-Nawawiy anasema: “Madhehebu ya watu wa Sunna kuhusu hakika ya ndoto kuwa: Mwenyezi Mungu anajenga imani ndani ya moyo wa mwenye kulala usingizi, kama anavyoijenga kwa aliye macho, na Mwenyezi Mungu anafanya anayoyataka, ambapo hazuiliwi kwa usingizi wala uamkaji, na alipoziumba imani hizi alizijaalia ishara za mambo mengine ambayo yatadhihirika baadaye, au alikuwa akiziumba kabla ya hapo, na kama akiumba ndani ya moyo wa mwenye usingizi kuwa anaruka, na hakika yake asiruke, basi ni dhahiri kuwa anaamini jambo kinyume chake, na imani hii itakuwa ishara ya jambo jingine, kama Mwenyezi Mungu aliyaumba mawingu yawe ishara ya mvua, na vyote ni viumbe vya Mwenyezi Mungu, lakini anaziumba nďoto na imani ziwe ishara ya kupendeza mbali na kuwepo Shetani, na anaziumba zinazodhuru pamoja na kuwepo Shetani, kwa hiyo kunasibishwa kwa Shetani kwa njia ya majazi, kwa sababu ya kuwepo kwake, na hana kazi ya kweli hapo, na hii ni maana ya kauli yake Mtume S.A.W.,: “ndoto njema zinatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ndoto mbaya zinatoka kwa Shetani”, si kwa maana ya kuwa Shetani anafanya kitu.
Basi ndoto njema ni za kupendezwa, na ndoto mbaya ni za kuchukiwa; na haya ni maneno ya Mtaalamu Al-Maziriy; na wengine walisema: kunasibishwa nďoto ya kupendeza kwa Mwenyezi Mungu ni kwa njia ya heshima, kinyume cha ya kuchukiwa, na hakika zote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, uangalizi wake na amri yake, na hakuna kazi ya Shetani hapo, lakini anahudhuria ndoto ya kuchukiwa na kupata furaha kwake”. [Sharh An-Nawawiy Ala Muslim: 15/17, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turaath Al-Arabiy]
Al-Hafidh Ibn Hajar anasema: “ndoto ni mitazamo aliyoitundika Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya moyo wa mtu, kwa mikono ya Malaika au Shetani, ama iwe kwa majina yake yaani kwa hakika yake, au kwa kinaya yake, au kwa mchanganyiko, na mfano wake katika hali ya kuamka ni mawazo ambayo huenda yakatokea kwa sura ya kisa, au kwa sura ya jumla bila matukio maalumu.
Na huu ni muhtasari wa kauli ya Ustadh Abu Is-haaq, aliyesema: Kadhi Abu Bakr Ibn At-Twayib alielekea kuwa hizi ni itikadi na akatoa hoja kuwa mwenye ndoto huenda akajiona mnyama au ndege kwa mfano, na huo sio mtazamo, kwa hiyo inawajibika kuwa itikadi, kwa sababu itikadi huenda kuwa kinyume cha ukweli wake, na Ibn Al-Arabiy anasema: rai ya kwanza ni bora zaidi, na iliyotajwa na Ibn At-Twayib ni aina ya kutoa mfano tu, kwa sababu mtazamo uliopo hapo unaambatana na mfano wenyewe, na sio wa kitu kingine. Mwisho kwa ufupi” [Fat-h Al-Bariy: 12/352, Ch. ya Dar Al-Maa’rifah]
Wanazuoni wa tafsiri walizungumzia utabiri wa nďoto kwenye Aya zilizotaja jambo hili, hasa katika Surat Yusuf. Na wanazuoni wa sasa wameweka milango ya utabiri wa ndoto katika vitabu vya Sunna.
Na hukumu ya tafsiri ya ndoto ni kwamba iikatik kisharia kwa anayeifahamu elimu hii, kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu aliiumba ndoto kwa faida ya watu, kwa njia ya anayejua kuitabiri kati yao, na hali kadhalika kuhusu Qur`ani na Sunna, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{Na kama wangalilipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka kwao, wale wanopeleleza (wanaojua kupima mambo) miongoni mwao wangalijua (kuwa hilo ni jambo la kutangazwa au si la kutangazwa)}. [AN NISAA; 83], na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
{Basi waulizeni wenye kumbukumbu (ya mamabo ya zamani) ikiwa nyinyi hamjui} [AL ANBIYAA: 7], na asiyekuwa miongoni mwa watu wenye elimu kuhusu suala hili, basi hairuhusiwi kwake kulizungumzia, lakini ni jambo la wataalamu wa hilo tu.
Ibn Abdilbar anasema: “Imamu Malik, Mwenyezi Mungu amrehemu, aliulizwa: Je, inawezekana kwa mtu yeyote kutabiri ndoto? Akajibu: Je, Utume wa kuchezewa? Na akasema pia: haitabiri ndoto isipokuwa anayeielewa, kwa hiyo akiona heri anaieleza, lakini akiona shari basi atasema heri au anyamaze.
Na imesemwa: Je inajuzu kuitabiri kwa maana ya heri ingawa asili yake ni shari; kwa kutegemea kauli ya baadhi ya wanachuoni kuwa: matukio yake yanaambatana na kutabiri kwake? Akajibu; la. Kisha akasema: ndoto ni sehemu moja ya Utume, na Utume hauchezewi”. [At-Tamhiid Lima Fil Muwatta’ Minal Maa’aniy wal Asaaniid: 1/288, Ch. ya Wizarat U’muum Al-Awqaaf Wash-Shuu’un Al-Islamiyah, Moroko]
Abul Waliid Al-Baji anasema: “Haitabiri ndoto isipokuwa anayeifahamu, lakini asiyeijua na kuelewa aache”. [Al-Muntaqaa Sharh Al-Muwatwa’: 7/278].
Na Mtume S.A.W., alijuzisha Abu Bakr aitabiri ndoto, na akamwambia kuwa yeye mara alifanya sahihi na mara nyingine alikosa. Kutoka kwa Ibn Abbas kuwa alikuwa akipokea kuwa mtu mmoja alikuja kwa Mtume S.A.W., akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Mimi niliona usingizini kuwa usiku huu wingu litanyesha mvua ya samli na asali, nikaona watu wanachota kwa mikono yao, baadhi walichukua nyingi na wengine walichukua chache, na nikaona kamba inayounganisha kati ya Mbingu na Ardhi, na nikakuona ukipanda kamba hii kwenda juu, kisha mtu akapanda juu baada yako, kisha mtu mwingine akapanda juu, kisha mtu mwingine akapanda lakini kamba ilikatika, kisha kamba ikaungwa na mtu kapanda juu.
Hapo Abu bakar akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nakuomba uniruhusu niitafsiri ndoto hii, na Mtume S.A.W., akamwambia alitafsiri hiyo ndoto na Abu Bakar akasema: Wingu maana yake ni Uislamu, na samli na asali hunyesha ni Qur`ani pamoja na uzuri wake na ulaini wake, na yaliyochukuliwa na watu na hivyo maana yake walioyachukua kutoka kwenye Qur`ani yakiwa mengi au machache, na kamba inayounganisha kati ya Mbingu na Ardhi maana yake ni haki uliyo nayo, wakati ulipoichukua basi Mwenyezi Mungu akakupandisha kwa sababu yake, kisha mtu akaichukua baada yako, akapanda juu, kisha mwingine akapanda juu, kisha mwingine akapanda lakini kamba ikakatika, kisha kamba ikaungwa tena kwa ajili ya kupanda juu.
Hapo Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, niambie: Je nimefanya sahihi au kosa? Na Mtume S.A.W., akajibu: “umefanya sahihi sehemu na umefanya kosa sehemu nyingine” akasema: Ewe Mtume Wallahi niambie nilipokosea? Akajibu: usiape”. [Muttafaq, na tamko hili ni la Imamu Muslim].
Na watungaji wa vitabu vya Sunna walizoea kuweka kitabu cha kuitafsiri katika migawanyo yao ya vitabu hivi, yaani kitabu cha kuitafsiri ndoto.
Na kwa kawaida mwenye jitihada katika elimu anaweza kufanya kosa, basi mwenye kuitabiri ndoto ni mfano wake, kwa hiyo kuitabiri ndoto si hoja ya kisheria, lakini kuna faida kwake katika fadhila za kazi, watu, na mambo yenye asili ya kisheria.
Imamu Az-Zarkashiy anasema: “Rai sahihi kuwa ndoto ya usingizi haithibiti hukumu ya kisheria wala hoja, ingawa ndoto ya kumuona Mtume S.A.W usingizini ni kweli, kwa sababu Shetani hawezi kuonekana kwa sura yake, na mwenye usingizi hana yakini ya kuinukulu elimu, na ndoto inayosimulia suala la Adhana ya Swala, na Mtume S.A.W aliamuru kutekelezwa, hoja yake siyo kuwa ruya, lakini hoja yake ya kweli ni amri ya Mtume S.A.W, kutekelezwa, kama ipatikanavyo katika elimu”. [Al-Bahr Al-Muhiit Fi Usul Al-Fiqh: 8/118, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]
Kuhusu aina za ndoto: imepokelewa na Abu Huraira R.A, alisema: Mtume S.A.W., alisema: "Utapokuja mwisho wa dunia ruya ya muumini takriban haiongopi, na mwenye ruya ya kweli kabisa ni mwenye mazungumzo ya kweli kabisa, na ruya ni aina tatu: ruya ya habari njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ruya ya mtu anayejizungumza, na ruya ya kuhuzunisha ya Shetani, na mmoja wenu akiona la kuchukiza basi asilizungumzie, asimame na kuswali, na kuiona pingu usingizini ni dini thabiti, lakini nachukia ruya ya pingu shingoni”. [Muttafaq]
Imamu Al-Baghawiy anasema: (kauli yake: ndoto ni aina tatu) inabainisha kuwa si kila analoliona mtu usingizini litakuwa sahihi na anaweza kulitabiri, bali sahihi miongoni mwake ni lililokuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Malaika ya ndoto, kutoka kwa Nakala ya Hukumu Asili (Ummul Kitaab), na zisizo kuwa hizi ni ndoto za uwongo, ambazo hazina utabiri.
Na hizi zina aina kadhaa; huenda ni kitendo cha Shetani anayechezea mwanadamu, au anamuonesha yanayomhuzunisha, na Shetani ana mbinu mbaya anazozitumia kwa kuhuzunisha wanadamu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwake: {Kwa yakini mazungumzo (mabaya) yanatokana na Shetani ili wahuzunike wale walioamini}. [AL MUJADILAH: 10]. Na miongoni mwa mbinu hizi za Shetani ni kutoka manii usingizini ambapo inawajibika kuoga, na hii haina utabiri; na huenda ni miongoni mwa mazungumzo ya nafsi, mfano wake ni mtu wa kazi maalumu anaona nafsi yake usingizini ndani ya kazi hii, na anayependa mwanamke anamuona usingizini, n.k.; na huenda hii ni kutokana na tabia yake tu”. [Sharh As-Sunnah; 21/211, Ch. ya Al-Maktab Al-Islamiy]
Kuhusu chimbuko la elimu ya kuitabiri ndoto, asili yake ni uwezo wa akili, na mfano wake elimu ya Fiqh, na tangu zamani elimu hii haikutegemea Qur`ani na Sunna kama ni machimbuko yake pekee, lakini ni miongoni mwa machimbuko haya, na hii inabainika kutoka kwa sehemu za kuitabiri ndoto, kama itakavyokuja.
Na kuhusu kuitabiri ndoto kuna sehemu kadhaa: huenda asili yake ni ishara ya Qur`ani, au ya Sunna, au kutoka katika Methali mashuhuri kati ya watu, na huenda utabiri unalingana na majina, maana, kinyume cha kitu, au dhidi yake.
Kuitabiri ndoto kwa ishara ya Qur`ani: mfano wa (kamba) inayotabiriwa kwa ahadi, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu}. [AALI IMRAAN: 103].
Na jahazi (safina) linatabiriwa kuwa: uokoaji, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na tukamuokoa yeye na watu wake (katika) safina}. [AL ANKABUUT: 15].
Kuhusu utabiri kwa ishara ya Sunna, mfano wake: kunguru, anayetabiriwa kuwa: mwanamume fasiki, kwa sababu Mtume S.A.W., alimuita fasiki, na panya wa kike anatabiriwa kuwa; mwanamke fasiki, kwa sababu Mtume S.A.W., alimuita fasiki.
Kuhusu kutabiri kwa ishara ya Methali; mfano wake mtengenezaji dhahabu, anatabiriwa kwa uongo, kwa kusemwa kwao; watengenezaji wa dhahabu ni waongo kabisa; na kuchimba shimo inatabiriwa werevu, kwa kusema: aliyechimba shimo liwe mtego wa nduguye, basi mchimbaji ataanguka ndani yake.
Kuhusu kutabiri kwa ishara ya majina, kama akiona usingizini mtu huitwa Rashid, basi inatabiriwa kuwa muongozi, na kama kuitwa Salim, inatabiriwa kuwa amani. Kutoka kwa Anas Ibn Malik alisema: Mtume S.A.W., alisema: “Usiku mmoja niliona usingizini kuwa sisi kama kwamba tuko katika nyumba ya Uqbah Ibn Raafii’, na tukapata tende ya aina ya Taab (pevu), na nikaitabiri kuwa utukufu wetu duniani, na kufuzu katika Akhera, na dini yetu imekwishatimu”.
Kuhusu kutabiri kwa ishara ya kinyume cha kitu na dhidi yake, mfano wake: hofu inatabiriwa kuwa amani, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {na atawabadilishia amani baada ya hofu yao}. [AN NUUR: 55], na vile vile usalama unatabiriwa kuwa hofu.
Na huenda hukumu ya kutabiri inabadilika kwa kuongeza au kupunguza, mfano wa kauli yao kuwa mlio ni furaha, na ikiambatana na sauti na kelele nayo ni msiba; na kucheka ni huzuni, na ikiwa tabasamu basi ni heri.
Na huenda utabiri unabadilika kutokana na hali ya muonaji, mfano wake kuiona pingu usingizini ni makuruhi, lakini kwa mtu mwema ni kufunga mkono na maovu; na Ibn Siriin alikuwa akisema kuwa mtu anayehutubia juu ya membari ni hali ya kupata madaraka, na kama hakuwa katika wenye wa kupata madaraka basi atasulubiwa; na siku moja mtu akamuuliza Ibn Siriin akisema: niliona usingizini mimi kama kwamba ninaadhini, akajibu: utahiji, na mtu mwingine akamuuliza swali hilo hilo akajibu: mkono wako utakatwa kutokana na wizi.
Na Ibn Siriin alipoulizwa kuhusu tofauti ya utabiri pindi ndoto ni moja, kajibu: Nilimwona mtu wa kwanza mwenye sura nzuri, basi niliitabiri kwa ishara ya Mwenyezi Mungu: {Na (tukamwambia:) “Utangaze kwa watu habari za Hija”} [AL HAJJ: 27], na nilimuona wa pili huwa na sura mbaya, basi niliitabiri kwa ishara ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {kisha mnadi akanadi: “Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi}. [YUSUF: 70]; na huenda mtu anaona kitu usingizini kisha atapata kitu hicho chenyewe ikiwa mamlaka, Hija, kurudi msafiri, heri, janga, n.k.
Na Mtume S.A.W., aliona usingizini habari ya kufungua Makkah, ambapo ikawa hivyo hivyo, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Kwa yakini Mwenyezi Mungu amemhakikishia Mtume wake ndoto yake ya haki}. [AL FAT-H: 27].
Na huenda akaona ndoto inayohusu mtu fulani lakini inakuwa ya mtoto wake, ndugu yake, au mwenye jina lake hilo hilo, na Mtume S.A.W., aliona usingizini ahadi ya Abu Jahl naye, lakini inahakikishwa kwa mtoto wake Ikrimah, na aliposilimu Ikrimah Mtume S.A.W., alisema: “Hiyo hiyo”, na aliona pia utawala wa Makkah ni kwa Usaid Ibn Al-A’aas, lakini ulikuwa kwa mtoto wake A’attab Ibn Usaid, alipotawaliwa Makkah na Mtume S.A.W,”. [Taz. Sharh As-Sunnah; 12/219-225, kwa Muhtasari].
Imamu Ibn Al-Qayim anasema: “Walisema: hakika Mwenyezi Mungu Ametoa methali na kuigawanya kikadari na kisheria katika hali ya uamkaji na usingizi, na akawaongoza waja wake wazingatie hivyo, na wavuke kutoka kwa kitu hadi kingine, na kutoa hoja juu ya hoja, bali hii ni asili ya kuitabiri ndoto ambayo ni sehemu ya Utume na aina ya Wahyi; kwa sababu inaundwa na Qiyasi na tamathali, na kuzingatia kati ya akili na hisia, na huoni kuwa nguo, mfano wa kanzu, zinatabiriwa kuwa dini, na sifa zake miongoni mwa urefu, ufupi, usafi, uchafu, zote zinaambatana na dini, kama Mtume S.A.W., alivyoitabiri kanzu kuwa dini na elimu, na kadiri ya kushirikiana kati yake kuwa: kila moja inasitiri mhusika wake na kumpabanisha kati ya watu; kwa mfano kanzu inasitiri mwili, na elimu na dini zinasitiri roho na moyo wake na kupambakati ya watu”. [Ii’laam Al-Muwaqii’in An Rabil A’alamin: 1/146-149, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Na Imamu Malik amepokea kutoka kwa Is-haaq Ibn Abdillahi Ibn Abi Talha, kutoka kwa Zufar Ibn Saa’saa’ah Ibn Malik, kutoka kwa babake, kutoka kwa Abu Huraira kuwa “Mtume S.A.W, alikuwa anapotoka kwenye Swala ya Al-Ghadah (Alfajiri), husema: Je kuna mtu yoyote miongoni mwenu aliyeota ndoto yoyote usiku huu? Na pia akisema: hakuna linalobaki baada yangu kuhusu Unabii isipokuwa ndoto njema”.
Al-Baji anasema: “Kauli yake Mtume S.A.W, wakati akitoka kwenye Swala ya Alfajiri: “Je kuna mmoja kati yenu aliona ndoto usiku huu?” inawezekana, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa yote, kuwa Mtume anaomba kusikia ndoto yenye habari njema kwake S.A.W., na Waislamu, na anadhihirisha hivyo kutoka kwao, kuhusu mambo ambayo Wahyi haujafikisha bado, na inawezekana pia kuwa anataka kuwafundisha ibada na kuwaelekeza fadhila zake, na kwa hivyo alisema: “hakuna linalobaki baada yangu kuhusu Unabii isipokuwa ndoto njema” kuwahimiza ili wajifunze, na kupata faida na kubaki baada yake sehemu ya Unabii inayowapendeza, na kuwahimiza wafanye masilahi, na kuwazuia madhambi”. [Al-Muntaqa Sharh Al-Muwatwa’: 7/277, Ch. ya Matbaa’at As-Saa’adah].
Na kuhusu hukumu ya uwongo katika kusimulia ndoto, kutoka kwa Ibn Abbas, kutoka kwa Mtume S.A.W, kuwa alisema: “Anayesimulia ndoto wakati yeye hakuona ndoto hii, atalazimika kuunga kati ya chembe mbili za shayiri, na yeye hataweza kufanya”. [Ameipokea Imamu Bukhary].
Na kauli yake: "Anayesimulia ndoto wakati yeye hakuona ndoto hii" yaani alidai kuwa aliiona ndoto.
Na (atalazimika) yaani katika siku ya Kiyama, na hii ni aina ya adhabu, na (kuunga) yaani kuzifanya chembe hizi ziwe moja. Na (hataweza kufanya) yaani yeye hana uwezo wa kufanya, na hii ni kinaya ya kuendelea adhabu juu yake.
Na kutoka kwa Ibn Omar, kuwa Mtume S.A.W. alisema: “Miongoni mwa uwongo wa wazi kabisa, ni mtu kuyaonesha macho yake mambo asiyoyaona”. [Ameipokea Bukhariy].
Na kauli yake; (uwongo wa wazi kabisa) yaani uwongo mkubwa sana, hali ya kuwa kushangaza.
Na (anayaonesha macho) yaani anadai kuwa ameiona ndoto na hali ya kuwa hakuona kitu.
Na Imamu Al-Bukhariy ameweka mlango katika kitabu chake, anwani yake ni: (Mlango wa aliyesema uwongo katika ndoto yake); na Ibn Hajar anasema: “kauli yake: (Mlango wa aliyesema uwongo katika ndoto yake) yaani mtu huyu ni mbaya, na maneno kamili ni: Mlango wa dhambi ya aliyesema uwongo katika ndoto yake… na makusudio ni kumlazimisha ni aina ya kuadhibiwa.
Na kuhusu uwongo wa ndoto ya usingizini At-Twabariy anasema: hakika onyo lake ni kubwa kabisa hali ya kuwa uwongo wa kuwa macho huenda ni mbaya sana kuliko huo, kwa sababu unaambatana na ushahidi wa uuaji, au adhabu, au kuchukua mali, kwa sababu uwongo wa ndoto ya usingizini ni uwongo kwa Mwenyezi Mungu kuwa alimwonesha asiyoyaona , na uwongo kwa Mwenyezi Mungu ni mbaya sana kuliko uwongo kwa wanadamu , kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na mashahidi (Malaika wao) watasema: “Hao ndio waliomzulia Mola wao uwongo”}.
Na hakika uwongo wa kuota ndoto usingizini unazingatiwa kuwa ni uwongo kwa Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa Hadithi isemayo: ndoto ni sehemu moja ya Utume, na sehemu inayoambatana na Utume bila shaka inaambatana na Mwenyezi Mungu. Mwisho kwa muhtasari”. [Fat-h Al-Bariy, na Ibn Hajar: 12/428].
Na kwa mujibu wa yaliyotangulia kutajwa na maelezo yake: Kuzitabiri ndoto za usingizini ni busara, na machimbuko yake ni Qur`ani, Sunna, Methali za watu na Desturi zao, na hayo yalikuwa katika Mataifa yaliyotangulia zamani. Na haijuzu kuutumia Utabiri wa ndoto isipokuwa kwa mtaalamu wa misingi ya kutabiri.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas