Kuafikiana Kati ya Ilivyopokelewa K...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuafikiana Kati ya Ilivyopokelewa Kuhusu Ubaya wa Dhana Mbaya na Kuzuiliwa, na Ilivyopokelewa Kuwa ni Miongoni mwa Welekevu.

Question

Mtu anaweza kuwa anazichunguza hali za watu, ambapo hali hizo zikapelekea kumfanya adhani dhana mbaya juu yao, lakini bila ya dalili ya wazi. Je, hiyo inzingatiwa Kuwa ni miongoni mwa dhana mbaya ambayo tumekatazwa Kuwa nayo? Hivyo basi vipi kuafikiana kati ya ilivyopokelewa kuhusu ubaya wa dhana mbaya pamoja na kukatazwa kwake, na ilivyopokelewa kuwa miongoni mwa welekevu? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya utangulizo huo:
Sharia Tukufu inatukataza kuwadhania watu dhana mbaya. Kuwadhania watu vibaya ni kuichukua mienendo yao kwa njia ya ubaya, bila ya alama wala dalili, kwa sababu asili ya kutendeana ni kuvumiliana na usalama, Mwenyezi Mungu anasema: {Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na (kuwadhania watu) dhana (mbaya) kwani (kuwadhania watu) dhana (mbaya) ni dhambi. Wala msipeleleze (habari za watu). Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Je! Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa? La, Hampendi; (Basi na haya msiyapende). Na Mcheni Mwenyezi Mungu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba (na) Mwingi wa kurehemu}. [AL HUJURAT; 12].
Imamu Ibn Kathiir katika Tafsiir yake [7/377, Ch. ya Dar Twiiba] anasema: “Mwenyezi Mungu anasema, akiwakataza waja wake waumini kwa mengi ya dhana, nayo ni tuhuma na kuwabebesha jamaa wa karibu, na watu wengine, kwa yasiyo haki; kwa sababu baadhi ya hayo ni dhambi halisi, kwa hiyo yaepukwe kwa tahadhari”.
Na Imamu At-Twahir bin A’ashuur anaelezea uwajibikaji wa kuzichunguza dhana, na kubainisha kusudio la dhana iliyotajwa katika Aya, na maana ya kuwa ni dhambi, akisema katika Tafsiir yake [At-Tahriir wat-Tanwiir: 26/251, Ch. ya Ad-Dar At-Tunusiyah]: “Kutokana na amri ya Aya hii inaonesha jinsi ya kujiepusha na mengi ya dhana, basi tulijua kuwa dhana zenye dhambi si chache, kwa hiyo tunapaswa kuzitambua aina za dhana, kwa kujua ipi ni batili na ipi ni ya kweli.
Na maana ya dhana hapa ni: ile inayoambatana na hali za watu, lakini mwandishi aliiondosha ibara hii ili nafsi ya msikilizaji ielekee kuwa: kila dhana inaweza kuwa na dhambi; na sentensi isemayo: {kwani (kuwadhania watu) dhana (mbaya) ni dhambi}, ni kuyarejesha maneno yaliyoachwa kwa ajili ya kubainisha; kwa sababu kauli yake: {Jiepusheni sana na (kuwadhania watu) dhana (mbaya)} inamtanabahisha msikilizaji atafute maelezo ambayo ni: Jueni kuwa baadhi ya dhana ni makosa makubwa. Na hii ni kinaya inayoonesha uwajibikaji wa kuzingatia athari ya dhana, ili maana yake ilingane matokeo ya dhana na wanavyojua miongoni mwa hukumu za Sharia, au waulizie wanazuoni kuwa maelezo haya ya kurejesha huonesha kuwahofisha juu ya kuitenda dhambi.
Na maelezo haya si kwa ajili ya kubainisha aina nyingi za dhana ambazo inaamriwa kuziepusha; kwa sababu ni aina nyingi. Kwa hiyo alitanabahi matokeo yake na kuacha ufasiri; kwa sababu kuzificha aina hizi hupelekea kupata mengi ya tahadhari.
Na maana ya kuwa ni dhambi ni kwamba: dhana hiyo inaweza kuambatana na kazi au huwa ni imani tu; na ikiwa ni kazi kama kauli au kitendo kama vile kusengenya, upelelezi, na nyiginezo, hapo mwenye kudhani anahesabia kuwa dhana yake ni uwongo, kisha akiitazama kazi yake iliyoundwa juu ya dhana hii, ataona kuwa akitendea mwenzake kwa njia ambayo haistahiki hivyo, kutokana na kumtuhumu kwa batili, hapo atapata dhambi kwa ajili ya aliyoyaficha ndani ya moyo wake juu ya mwenzake mwislamu”. [Mwisho]
Na katika Vitabu viwili vya Sunna Sahihi, kutoka kwa Abu Haraira R.A., kuwa Mtume S.A.W., anasema: “Tahadharini na dhana, hakika dhana ni uwongo mtupu, wala msichunguzane, wala msifanyiane ujasusi, wala msihusudiane, wala msikatiane, wala msichukiane, kuweni, Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, ndugu”.
Hadithi hii inatahadharisha dhana mbaya kwa waislamu, bila ya kujua wala Kuwa na hakika.
Na katika kitabu cha: [Fat-h Al-Bariy, na Ibn Hajar: 10/481, Ch. ya Dar Al-Maa’rifah. Bairut] imetajwa kuwa: kauli yake; “Tahadharini na dhana”, Al-Khatwabiy na wengineo wamesema: kusudio sio hilo la kuacha dhana ambayo inaambatana na hukumu, bali ni kuiacha dhana ambayo inamdhuru anayedhaniwa, vile vile inapokuwepo moyoni bila ya dalili, kwa sababu mwanzo wa dhana ni mawazo tu, na haiwezekani kuyaepusha, na jambo ambalo haiwezekani kuepukana nalo pia haiwezekani kulikalifishwa, kwa kutegemea Hadithi ya: Mwenyezi Mungu huachilia umma mazungumzo ya nafsi yake.
Na Al-Qurtwubiy anasema: “Muradi wa dhana hapa ni tuhuma bila ya sababu, mfano wa yule anayemtuhumu mtu kazi chafu, bila ya kuwepo sababu, kwa hiyo aliongeza kauli yake: na wala msipelelezi (habari za watu); kwa sababu kwa kawaida mtu anapopata mawazo ya tuhuma huwa anataka kuihakikisha, na kwa hiyo atafanya ujasusi, atatafuta, na kusikiliza, kwa hiyo amekatazwa kufanya hivyo. Na Hadithi hii inalingana na kauli yake Mwenyezi Mungu: {Jiepusheni sana na (kuwadhania watu) dhana (mbaya) kwani (kuwadhania watu) dhana (mbaya) ni dhambi. Wala msipeleleze (habari za watu). Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine}, na muktadha wa Aya unaonesha amri ya kuiangalia heshima ya mwislamu kwa haraka, kwa sababu ya kutangulia katazo la kuigusa dhana, na kama mwenye dhana akisema: natafuta ili nipate uhakika, basi ataambiwa; {Wala msipeleleze (habari za watu)}, na kama akisema: nilihakikisha bila ya upelelezi, basi ataambiwa: {Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine}”. {Mwisho]
Maandiko ya Sharia ni mengi sana na yanahimiza kuhusu dhana njema kwa waumini, miongoni mwake, ni kama ilivyopokelewa kuhusu tukio la uzushi (Ifki), ambalo kutokana nalo, Qur`ani imeteremshwa na kusomwa mpaka Siku ya Malipo, kwa ajili ya kumwondoshea dhana mbaya Mama wa Waumini Bibi Aisha R.A. Na mahali pa ushahidi katika Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: {Mbona mliposikia (habari) hii, wanaume Waislamu na wanawake Waislamu hawakuwadhania wenzao mema, na kusema “huu ni uzushi dhahiri”}. [AN NUR: 12].
Imamu At-Tabariy katika Tafsiir yake [19/128, Ch. ya Muassasat Ar-Risalah] anasema: “Hii ni laumu ya Mwenyezi Mungu kwa wenye imani kwake, kutokana na ilivyotokea katika nafsi zao kuhusu tetesi ya waliotangaza ouvu kwa Aisha, Mwenyezi Mungu anawaambia: Enyi watu, kwa nini mliposikia yalivyosemwa na wazushi, waumini wanaume na wanawake kati yenu wajidhanie nafsi zao mema? yaani: mlidhania mema huyu aliyefanya hivyo kati yenu, na hamkudhani kuwa yeye alifanya kazi chafu; na akasema: nafsi zao, kwa sababu Waislamu wote ni kama nafsi moja, kwani wao ni watu wa Mila moja”. [Mwisho]
Pia miongoni mwa maandiko yanayohimiza dhana njema kwa waumini, ni kama ilivyopokelewa katika Vitabu viwili vya Sunna Sahihi, kutoka kwa Mama wa Waumini Safiyah R.A, alisema: “Mtume S.A.W. alikuwa amekaa Itikafu, nikamwendea usiku kumzuru, nikazungumza naye kisha nikarejea, Mtume S.A.W. akasimama pamoja nami ili anishindikize. Wakapita watu wawili miongoni mwa Ansaar, watu wale walipomuona Mtume S.A.W. waliharakisha mwendo. Mtume S.A.W. akawaambia: “Tembeeni taratibu, huyu ni Safiyah Binti Huyayi”. Wale watu wakasema: Lo! Hatuna mawazo mabaya juu yako! Mtume S.A.W. akawaambia: “Hakika Shetani hupita ndani ya mwanadamu kama mapitio ya damu kwenye mishipa. Nami nilichelea asije akaingiza shari (au kitu) nyoyoni mwenu”.
Kwa hiyo dhana njema kwa waumini inatakiwa na inapewa kipaumbele; kwa sababu ni asili, kwa kuwa hazipo alama wala dalili kinyume na hayo.
Kuhusu ilivyopokelewa juu ya kauli ya kuwatahadharisha watu juu ya dhana mbaya, au kuwa dhana mbaya ni miongoni mwa welekevu, inawezakana kuelekezwa mielekeo kadhaa, miongoni mwake ni kama ifuatavyo:
Dhana mbaya inategemewa kwa mtu mwenye mwonekano mbaya; Imamu Al-Qurtubiy katika Tafsiir yake [Al-Jamii’ Li Ahkaam Al-Qur'aan: 16/332, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Masriyah] anasema: “wengi wa wanazuoni wanaona kuwa dhana mbaya kwa mtu mwenye mwonekano mzuri haijuzu, na hakuna kosa la dhana mbaya kwa mwenye mwonekano mbaya”. [Mwisho]
Wanazuoni wa madhehebu ya Shafiy na wengineo wanasema kuwa: dhana inagawanyika kama ifuatavyo: wajibu, inayotakiwa, haramu, na halali.
Wajibu: ni dhana njema kwa Mwenyezi Mungu; Haramu: ni dhana mbaya kwa Mwenyezi Mungu, na kila Mwislamu mwenye uadilifu wa wazi; Halali: ni dhana kwa aliyejulikana kwa Waislamu Kuwa anafanya mambo mabaya na kueneza machafu, hapo si haramu kumdhania ubaya; kwa sababu yeye amejionesha hivyo, vile vile aliyejisitiri, basi hadhaniwa ila heri, na aliyeingia njia ya ubaya atatuhumiwa, na aliyejifedhehi tutamdhania ubaya.
Na miongoni mwa dhana inayojuzu, katika makubaliano ya Waislamu, dhana ya mashahidi katika Kalenda, na fidia za jinai, kama ilivyokubaliwa kuhusu habari ya mtu mmoja katika hukumu, kwa kauli ya pamoja, na inawajibika kuitekeleza sana, na dalili zote ziwe mbele ya Mahakimu. [Taz. Hashiyat Ar-Ramliy Al-Kabiir Ala Asna Al-Matwalib; Sharh Raudh At-Twalib, na Sheikh Zakariya Al-Ansariy: 1/296, Ch. ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy; Hashiyat Al-Qalyubiy Ala Sharh Al-Jalal Al-Mahaliy Limihaj Al-Imam An-Nawawiy: 1/231, Ch. ya Al-Halabiy; Nihayat Al-Muhtaj Ila Sharh Al-Minhaj, na Ash-Shams Ar-Ramliy: 2/429, Ch. ya Al-Halabiy; Subul As-Salam, na Al-Amiir As-Sana’aniy: 2/665, Ch. ya Dar Al-Hadith].
Na miongoni mwake ni kwamba: kusudio la dhana mbaya inayosemwa kuwa ni aina ya elekezi ni: hadhari, kuangalia, na kuonya, na siyo ya maana ya kuujaza moyo dhana mbaya za watu bila ya Kuwa na hakika au dalili, hali inayopelekea mtu kwenda mbali zaidi na upelelezi na kusengenya, kwa hivyo ugomvi na uhasama unapatikana, na Imamu Ibn Al-Qayim alitaja hivyo katika kitabu chake; [Ar-Ruuh: Uk. 237-238, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah, Bairut] ambapo anasema:
“Tofauti kati ya kujihadhari na dhana mbaya kuwa: mwenye kujihadhari mfano wake mtu aliondoka na kusafiri pamoja na mali na kipando chake, na hali yake kuwa anatahadhari haraka dhidi ya jambazi na kila mahali anapotazamia shari, pamoja na kuzinduka, maandalizi na kuchukua sababu ambazo anajinusuru na hatari; kwa hiyo mwenye kujihadhari ni kama mtu mwenye silaha anayejitolea, na huku akiwa tayari kupambana na adui, akatayarisha zana, na kwa kuwa hamu yake ni kutayarisha sababu za kujinusuru na kupigana na adui, basi atakuwa amezishughulikia zaidi sababu hizi kuliko dhana mbaya kwake; na kila alipokuwa na dhana mbaya, alizidisha aina za maandalizi na mzinduko.
Lakini dhana mbaya ni: Mtu kuujaza moyo wake kwa dhana mbaya kwa watu, mpaka kukadhihirika kupitia ulimi na viungo vyake, na vyote hivyo vikaambatana naye katika sura za: ubaya wa kauli na vitendo, matusi, aibu, na bughudha; Watu wakawa wanachukiana wenyewe kwa wenyewe, wanalaaniana wenyewe kwa wenyewe, na wanaonyana wenyewe kwa wenyewe.
Wa kwanza ni: mtu mwenye kujhadhari, anawatendea kwa tahadhari; na wa pili: Ni mtu anajiepusha nao, na kujiepusha kuyapata maudhi yao; wa kwanza: anaingia kati yao kwa njia ya kutoa nasaha na wema pamoja na kujihadhari; na wa pili: anajitenga nao, na kujiweka mbali na uzushi, utapeli, na bughudha”. [Mwisho]
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: Hakika dhana mbaya kwa mtu alinayejulikana kwa uadilifu kati ya Waislamu ni haramu; na dhana iliyo halali ni kwa mtu anayejulikana kwa mabaya na kufanya machafu wazi wazi, basi dhana mbaya juu ya Mtu huyu haiharamishwi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas