Familia kujinasibisha na Familia Nyingine
Question
Tulipitia barua iliyopokewa kutoka kwa Mheshimiwa Sheikh/ Ali Abdel-Baqi Shehata (Katibu Mkuu wa Baraza la Utafiti wa Kiislamu) tarehe: 2/21/2013 AD, ambayo imewekwa kwenye Fatwa nambari Na. 165, mwaka 2013, kuhusu familia kujinasibisha na Familia nyingine, kwa hivyo amelipeleka swali hilo kwa Ofisi ya Fatwa ya nchini Misri kwa ajili ya mamlaka yake; Kwa kuzingatia pendekezo la Kamati ya Utafiti wa Fiqhi ya Baraza la Utafiti wa Kiislamu katika kikao chake cha nane katika kikao chake cha arubaini na tisa, kilichofanyika siku ya Jumatano, Rabi` Al-Akhir 3, mwaka wa 1434 AH, sawa na Februari 13, 2013.
Nakala ya swali lililowasilishwa ni kama ifuatavyo:
Kuna familia mbili, moja yao inataka kujiunganisha na kujinasibisha na nyingine, ilimradi iwe sehemu muhimu ya familia hiyo kinasaba kwa nasaba iliyoandikwa, na iliandikwa katika hati kwa jina la: "Hati ya kuunganisha nasaba". Je, hilo linajuzu kisheria au la?
Answer
Sifa zote njema ni za Allah pekee, na swala na salaam ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu, na pia juu ya aali zake (watu wa nyumba yake) na maswahaba zake, na juu ya wale wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.
Sheria ya Kiislamu imelipa uzito mkubwa suala la nasaba, na ikaufanya ulinzi wa nasaba kuwa mojawapo ya malengo muhimu ya kisheria, na ikaweka kanuni na mipaka ya kuihifadhi na kuilinda isichezewe na kuilinda kutokana na uwongo; Kwa hivyo, kanuni za ndoa zilitungwa, na kwa upande mwingine zinaa, tuhuma za usaliti wa ndoa za Waislamu zilikatazwa, na zikatungwa hukumu zingine.
Mwenyezi Mungu hakuwaachia viumbe wake nafasi ya kuchagua nasaba zao, bali aliiwekea uthibitisho wa ukoo kwa njia maalum; Kama vile ndoa sahihi, kukiri, ushahidi, ndoa inayoshukiwa, na kila ndoa iliyobatilishwa baada ya kuingia kwa sababu ya kuharibika kwake.
Kwa hiyo Sheria ilikataza kuasili; Nako ni kule ambako mwanamume anamnasibisha kwake mtoto wa mtu mwingine, na kilichofuatwa katika zama za kabla ya Uislamu ni kwamba kusaili kunamthibitishia mtoto anayedaiwa juu ya mwenye kuasili haki zote ambazo zinawekwa kwa ajili ya mwana halisi juu ya baba yake; Al-Nasafi alisema katika tafsiri yake [3/17, Dar Al-Kalim At-Twayyib: “Ikasemwa: “Mtu katika zama za kabla ya Uislamu, kama mtoto wa mtu akimpenda, angemshirikisha kwake, na amemwekea kama fungu la urithi la mtoto wa kiume kutoka watoto wake, na akanasibishwa kwake; inasemwa: Fulani ni mwana wa fulani.
Basi Uislamu ukaufuta mfumo huu, ukaamrisha asinasibishwe mtoto yeyote isipokuwa kwa baba yake tu, na kwamba mtoto anayedaiwa asinasibishwe kwa yule aliyemfadhili. Mwenyezi Mungu anasema: “Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayesema kweli, naye ndiye anayeongoa Njia.(4) Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu (5).” [AL AHZAAB: 4,5]; Mwanachuoni Al-Taher Ibn Ashour amesema katika “Al-Tahrir Wa At-Tanweer” [21/261, Al-Dur Al-Tunisiah Lil-Nashr]: “Jambo hili ni uthibitisho, ambao kwa hilo madai ya mwenye kuasili yanabatilika kuwa mwanawe. Maana ya kuwaitia kwa baba zao: nasaba. Na maana ya kuwaitia kwa baba zao: matokeo ya hilo; Nayo ni kuwamba wao ni watoto wa baba zao, sio watoto wa wale waliowafadhili.
Inajulikana kuwa sahaba mkubwa Zaid Ibn Haritha aliitwa (Zayd Ibn Muhammad) wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alipomfadhili. Katazo liliposhuka, jina lake lilirudishwa kama lilivyokuwa (Zayd Ibn Haritha).
Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Wathila Ibn Al-Asqaa, R.A. kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Mojawapo ya uwongo mkubwa zaidi ni kwamba mtu anajinasibisha na baba asiyekuwa wake”
Imepokelewa kutoka kwa Imam Muslim kutoka kwa Ali Ibn Abi Talib R.A. kwamba Mtume S.A.W. amesema: “Mwenye kujinasibisha na baba asiyekuwa wake, au kujihusisha Mtumwa na Bwana si wake, basi laana ya Allah, Malaika, na watu wote itakuwa juu yake, wala Allah hakubali kutoka kwake toba wala fidya siku ya Kiyama”.
Imamu Al-Nawawi amesema katika kitabu cha “Sharhu Muslim” [9/144, Dar Ihyaa At-Turathi Al-Arabi] wakati wa kutoa maoni yake juu ya Hadithi hii: “Hili liko wazi katika ukali wa uharamu wa mtu kujihusisha na mtu asiyekuwa baba yake, au kujihusisha Mtumwa kwa asiyekuwa Bwana wake, Kwa sababu ya kukufuru kwa neema, na kupoteza haki za urithi, uaminifu, akili na mengineyo, licha ya kukatwa kwa ukoo na kuasi”. Kuna mambo kadhaa muhimu yanayohusiana kwa karibu na suala la ukoo; ambapo matokeo yake ni kuruhusiwa na kutoruhusiwa:
Mojawapo ni: ndoa; Ukoo ni moja ya sababu ya kuharimisha wanawake. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: “Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada” [AN NISAA: 23], walioharimishwa kutoka nasaba ni saba; Wa kwanza wao ni: mama, hata akiwa wa daraja la juu, na mama ni: kila mwanamke ambaye ukoo wako unaishia kupitia kwake au bila yake. Na wa pili: mwana wa kike, hata akiwa chini, na mana wa kike huyo ni: kila mwanamke ambaye ukoo wake unaishia kwako kwa kuzaliwa, au kwa njia au vinginevyo. Wa tatu: dada, naye ni: yeyote aliyezaliwa na wazazi wako au mmoja wao na kisha dada yako. Na wa nne: shangazi, naye ni: kila dada wa kiume wa mwanao bila mpatanishi, hivyo shangazi yako ni halisi, au kwa mpatanishi; Kama shangazi ya baba yako. Shangazi anaweza kuwa kwa upande wa uzazi; Kama dada wa mama ya baba. Na wa tano: shangazi, naye ni: kila dada wa kike aliyekuzaa wewe na shangazi yako ni wa kweli, au kupitia mpatanishi; Kama shangazi ya mama yako, na shangazi anaweza kuwa kwa upande wa baba. Kama dada wa mama. Na wa sita na wa saba: binti wa kaka na binti wa dada wa pande zote, na binti za watoto wao, hata wakiwa chini zaidi [Angalia: Al-Iqna' cha Al-Khatib Al-Sharbiny 3/417, 418 - pamoja na Hashiyat Al-Bajirmi-, Dar Al-Fikr]. Kujua ni nani anayeruhusiwa kuoa na ni nani anayeharamishwa kunategemea kuthibitishwa kwa nasaba au kutokuwepo kwake.
Ikiwemo: Urithi; nao urithi ulikuwa mwanzoni mwa kutunga Sheria ya udugu iliyofanyika Madina, kisha Sheria ikakataza hilo, na kufanya urithi baina ya jamaa tu; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu” [AL ANFAAL: 75]. Ibn Abbas amesema: “Mtume S.A.W. alifanya udugu baina ya maswahaba zake, na wakaurithi kwa udugu huo mpaka ilipoteremka Aya hii, wakarithishwa kwa nasaba. [Zad Al-Misir fi 'ilm Al-Tafsir, kitabu cha Ibn Al-Jawzi 2/229, uk. Dar Al-Kitab Al-Arabiy]
Ikiwemo: kuunganishwa kwa jamaa, na ilipokelewa katika matini nyingi ya kisheria amri ya kuunganisha kwa jamaa, na tishio la kuwatenga; zikiwemo aya hii ya Qur'ani: Mwenyezi Mungu anasema: “Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu?” [MOHAMMAD: 22].
Imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim kutoka kwa Mama wa Waumini Aisha, R.A., kwamba Mtume, S.A.W amesema: “Tumbo la uzazi limeshikamana na arshi, linasema. “Yeyote atakayejiunga nami, basi Mwenyezi Mungu atamunganisha, na yeyote anayenitenga, basi Mwenyezi Mungu atamkatilia mbali” Ni lazima kwa mtu kuunganisha tumbo hilo la uzazi ambalo limewekwa kwa Sheria, sio lile analozua. Al-Qadi Iyadh amesema katika “Ikmaal Al-Moallem Bi’fawaid Muslim” [8/20, 21, Dar Al-Wafaa]: “Hakuna ubishi kwamba kuunganishwa kwa jamaa ni wajibu na kuwatenga ni dhambi kubwa. Hadithi katika sehemu hii zinathibitisha hivyo... Wanavyuoni wametofautiana kuhusu jamaa ambao ni wajibu kuunganishwa, baadhi yao walisema kwamba: ni kila jamaa ambao mmoja wao ni mwanamume aliyemharamishia kuolewa na mwingine, hivyo si wajibu pamoja na watoto wa baba mdogo na watoto wa wajomba na wa mashangazi. Alitaja kauli yake kuwa inakataza kuunganishwa kwa dada wawili na mwanamke na shangazi zake wa baba na mama, kuogopa kutenganisha, na hilo linajuzu kwa watoto wa baba mdogo na watoto wa mjomba. Na ikasemwa: Bali haya yanahusu kila jamaa walio na mafungamano katika urithi, ikiwa ni haramu au vinginevyo. Na ikatajwa katika athari kwamba: “Mwenyezi Mungu anauliza kuhusu jamaa, hata ikiwa ni arubaini.” Hili linathibitishwa na kauli yake, Mtume S.A.W. “Na bwana wako, kisha anayekukaribia na anayekukaribia zaidi.”
Ikiwemo: katika umiliki, imethibiti katika Fiqhi kwamba umiliki haukuwa baina ya asili na tawi, hivyo mtu hammiliki baba yake, hata akiwa ni juu katika nasaba, wala mwanawe, hata akishuka chini katika nasaba, na asili yake ni kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma.” [AL ISRAA: 24], Kuinamisha bawa la unyenyekevu hakuji na utumwa, na tawi lake ni kauli ya Mwenyezi Mungu: “Wala hahitajii Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa na mwana (92) Hapana yeyote aliomo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Arrahmani Mwingi wa Rehema kuwa ni mtumwa wake (93)” [Mariyam: 92,93] Hali hii inaashiria kukanusha kwa muungano wa uzazi na utumwa.
Baadhi ya wanavyuoni wametanua juu ya hali hiyo, wakisema kuwa mwenye tumbo la uzazi kutoka kwa maharimu basi ameachiliwa huru. Ushahidi wa yale yaliyopokelewa na wale Maimamu wanne ambao ni Ahmad katika Musnad yake kutoka kwa Samra Ibn Jundub, R.A, kwamba Mtume, S.A.W amesema: “Mwenye kumiliki tumbo la uzazi kutoka kwa maharimu basi anaachiliwa huru.”
Al-Manawi amesema katika “Al-Taysir Sharh Al-Jami’ Al-Sagheer” [2/445, Maktabat Al-Imamu Al-Shafi'i katika Riyadh]: “Mwenye kumiliki tumbo la uzazi kutoka kwa maharimu” maana yake: asiyeruhusiwa kuolewa na jamaa, “basi anaachiliwa huru” maana yake: anaachwa huru kwa kuingia katika milki yake. Imamu Abu Hanifa akaichukua kwa jumla ya rai hii, na Al-Shafi'i akasema: Asili na tawi tu zitaachwa huru.
Kutokana na hayo yaliyotangulia, inaonekana kwamba kuna hukumu nyingi zinazotokana na ujuzi wa jamaa. Bali, hii inajumuisha mzunguko mzima wa nasaba. Kwa hiyo, ujuzi wa nasaba ya kisheria ya mtu ni wajibu. Kwa sababu ni njia ya faradhi, na kila jambo ambalo wajibu hautimii isipokuwa kwalo, basi nalo hilo huwa ni wajibu.
Imepokelewa kutoka kwa Ahmad na Tirmidhiy kutoka kwa Abu Huraira R.A., kwamba Mtume amesema S.A.W.: “Jifunzeni kutokana na nasaba zenu ambazo mnaungana nazo matumboni mwenu; kuunganishwa kwa tumbo la uzazi ni kwa ajili ya kuleta upendo wa familia, kwa ajili ya kuwa na mali nyingi, na kuwa na umri mrefu.”
Na imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud Al-Tayalisi katika Musnad yake kutoka kwa Ibn Abbas R.A., kwamba mtu mmoja alimjia na kumwambia: Wewe ni nani? Akasema: na akabainisha kwamba ana tumbo la mbali pamoja naye, kwa hivyo alizungumza naye kwa upole. Akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: Jueni jamaa zenu kwa ajili ya kuwaunganisha jamaa zenu; Hakuna undugu panapokatwa tumbo hata liwe karibu kiasi gani, na hakuna undugu tena panapotokea kutengana hata kuwe kutengana huko ni wale ndugu wa mbali.
Kwa maana hii, Imamu Ibn Hazm anasema katika “Jamharat Ansaab Al-Arab” (1/2, 3 Dar Al-Kutub Al-Ilmiyya: “Ni wajibu katika nasaba mtu kumjua baba yake na mama yake, na kila atakayekutana naye kwa nasaba katika tumbo la uzazi linaloharamishwa, ili kuepukana na yale aliyoharamishiwa kuolewa nao. Na kumjua kila mtu ambaye ana uhusiano naye kwa tumbo ambao unalazimu urithi, au unahitaji kuunganishwa naye, au kutumia pesa, au mkataba au hukumu; Yeyote asiyejua haya amekosa wajibu wa dini yake”
Kwa hiyo, kuchezea nasaba kwa kuingiza isiyokuwa ndani yake; kumhusisha mtu kwa asiyekuwa baba yake ili amshirikishe jina lake lote ni Uharibifu mkubwa wa nasaba; Kwa sababu ya kuchanganya nasaba, kuvurugika kwa undugu na mafungamano asilia ya kifamilia, uvunjaji wa mirathi na mengine yanayofanana na hayo, na kuenea kwa uadui na chuki baina ya watoto na jamaa halisi na baina ya mtu wa kuasili; Kwa msongamano wake nao katika gharama na urithi na kadhalika. Mbali na uwongo ulioharamishwa unaopelekea kuvuruga mafungamano ya kijamii.
Lakini kuna maana nyingine ya kuhusiana na wengine ambayo haijakatazwa, wala haijumuishi maovu yoyote yaliyotajwa. Ni kwa mtu anayehusiana na familia fulani kwa njia inayoonesha kuwa ni wa familia hii kabisa, bila ya udanganyifu kwamba yeye ni mtoto wa mmoja wa jamaa zake halisi, kwamba sifa ya familia ziko mwishoni mwa jina lake, na hii ni sawa na uhusiano uliokuwa kati ya makabila ya Kiarabu hapo awali, na hali hii haiingii ndani ya wigo wa kuasili ambao umekatazwa na sheria; Kwa sababu kuasili ni kumnasibisha kinasaba kwa asiye na nasaba naye na kumwita mwanae katika hali ya mirathi na nasaba, na kukaa peke yake pamoja na wanawake wa familia kama maharimu wake, na mambo mengine yaliyokuwa ya kawaida katika zama za kabla ya Uislamu na katika zama za Uislamu wa mwanzo. Kisha Uislamu ukaikataza hali hiyo kuhakikisha kutochanganywa kwa nasaba - kama ilivyotajwa hapo awali -.
Mwanachuoni Al-Alusiy amesema katika “Rouh Al-Ma’ani” [21/149, uk. Al-Muneriyah [katika tafsiri ya Aya hii: “Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu” [AL AHZAAB: 5]: “Maana ya dhahiri ya Aya hii ni kukataza kumhusisha mtu kwa asiyekuwa baba yake kwa makusudi, na labda hali hiyo ni kama ilivyokuwa katika zama za Ujinga (kabla ya Uislamu), lakini ikiwa si hivyo, kama mzee anavyosema kumwambia mdogo kwa huruma: (Ewe mwanangu) - na mara nyingi usemi huu husemwa - basi inaonekana kwamba hakuna katazo lolote. Katika maelezo ya chini ya Al-Khafaji juu ya tafsiri ya Al-Baydawiy: kuasili, na ikiwa tafsiri yake ni sahihi ni kama udugu, lakini imeharamishwa kwa kufanana na makafiri. Labda hakuna ushahidi wa uharamu huu katika Aya iliyotajwa. Ni nini kinachoashiriwa na uharamu wa kudai kwa namna ilivyokuwa katika zama za kabla ya Uislamu”.
Imepokelewa kutoka kwa Mashekhe wawili kutoka kwa Anas, R.A., amesema: Mtume S.A.W. aliwaita Al-Ansar akisema: “Je, kuna yeyote asiyekuwa miongoni mwenu?” Wakasema: Hapana isipokuwa mtoto wa dada yetu, Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akasema: “Mtoto wa dada wa watu ni miongoni mwao”. Katika Hadithi hii, Mtume S.A.W., amebainisha kuwa mtoto ni wa kabila la mama yake na si miongoni mwao kiuhalisia.
Al-Manaawiy amesema katika kitabu cha “Faydh Al-Qadiir” [1/87, 88, Dar Al-Maarifa]: Kauli yake: “Mtoto wa dada wa watu ni miongoni mwao”; kwa sababu amenasibishwa kwa baadhi yao, naye ni mama yake, kwa hiyo ana uhusiano na jamaa zake katika yote anayopaswa kuhusiana nayo, kama vile msaada, ushauri, mapenzi, kufichua siri, usaidizi, uchamungu, huruma na ukarimu. Na kadhalika”
Na katika Sahih Al-Bukhari: Kwamba Hatib Ibn Balta’ah R.A., alimwambia Mtume S.A.W.: “Nilikuwa mmoja wa Makureshi, lakini sikuwa miongoni mwao.” Katika Hadith hii, Hatib, R.A., ametaja kwamba yeye ni mmoja wa kabila la Makureshi lakini si kwa maana halisi.
Al-Hafidh Ibn Hajar amesema katika Fath Al-Bari [8/634, Dar Al-Marifa]: “Kauli yake: (Nilikuwa mmoja wa Makureshi), maana yake ni: si kwa kweli, kwa sababu alisema baada ya hapo: (Nami sikuwa miongoni mwao) Kauli yake: (Nilikuwa mmoja wa Makureshi, lakini sikuwa miongoni mwao) Huu sio mgongano, bali alimaanisha kuwa yeye ni miongoni mwao kwa maana ya kuwa yeye ni mshirika wao, na hayo yamethibitishwa na Hadithi ya Mtume S.A.W. isemayo: “Mshirika wa watu ni miongoni mwao”.
Kazi ya watu wema waliotangulia na watu wa Hadithi ilifanywa bila lawama kwa uuwiano usio wa kawaida, na kama jambo hilo likiharamishwa au kulazimu kuasili ambako kumekatazwa, walikuwa wakilikanusha.
Al-Hafiz Al-Sakhawi amesema katika “Fath Al-Mughith Bi-sharh Alfiyat Al-Hadith” [3/297, Dar Al-Kutub Al-Ilmiyyah], akielezea maneno ya Al-Iraqi: “(Na wakanasibisha) baadhi ya wapokezi na mahali palipotokea tukio, au katika nchi, au kabila, au ufundi, au sifa, au mambo mengine ambayo hayaonekani mbele ya ufahamu unaokusudiwa.
Al-Hafiz Al-Suyuti anasema katika kitabu cha “Tadreeb Al-Rawi” [2/ 340, Maktaba Ar-Riyadh Al-Hadithah]: “Msimulizi anaweza kunasibishwa na nasaba: kutoka mahali, au kabila, au ufundi, siyo hali iliyodhahiri ambayo inatangulia uelewa wa nasaba hii haikukusudiwa, bali kwa sababu ya mahali pamoja, au kabila hilo, na kadhalika.
Na nasaba, ikiwa imetoka katika asili ya mtu, inaweza kuwa kwa ajili ya uhuru, hali ambayo inatokea mara nyingi, kama: Abu Al-Bakhtari Al-Ta'i'i, na jina lake ni Said Ibn Fairouz, ambaye ndiye bwana wa Tai, kwa sababu bwana wake alitoka Tai na alimwacha huru. Inawezakana ni kwa ajili ya kuwa mshirika; hali ambayo ndiyo chimbuko lake ni mkataba na mapatano ya kusaidiana, na kukubaliana, kama vile: Imamu Malik Ibn Anas Al-Asbahi Al-Tayimi, yeye ni Asbahi kwa kweli, na mshirika kwa kabila la Tayim. Hii ni kwa sababu watu wake wa "Asbah" washirika kwa Tayim wa Makureshi. Uislamu ulifuta ushirika wa utii uliokuwa katika zama za kabla ya Uislamu za ugomvi na mapigano baina ya makabila au uvamizi bila ya ushindi wa waliodhulumiwa na kuunganisha undugu. Nasaba inaweza kuwa kwa utii wa mhudumu; kukodisha au kujifunza; Kama: Miqsam, iliambiwa kuwa ni mtumwa wa Ibn Abbas kwa ajili ya usahaba wake. inaweza kuwa kwa kunyonyesha; Kama Abdullah Ibn Al-Saadi, ambaye ni mmoja wa masahaba; Baba yake aliitwa: Al-Saadi; Kwa sababu alinyonyeshwa katika Bani Saad Ibn Bakr. Inaweza kuwa kwa dini na Uislamu; Kama vile: Muhammad Ibn Ismail Al-Bukhari Al-Jaafi; Kwa sababu babu yake Al-Mughirah alikuwa mmoja wa majusi, basi alisilimu kwa sababu ya Al-Yaman Ibn Akhnas Al-Jufi, na akanasibishwa kwake. Nasaba inaweza kuwa kwa cheo fulani; kwa maana kuwa jina lake linajumuishwa katika moja ya madaraka, kwa hivyo kunasibishwa na wamiliki wa madaraka hayo. Huyu ni kama Imamu Al-Layth Ibn Saad Al-Fahmi, na alinasibishwa na Fahm; Kwa sababu jina lake lipo katika diwani ya Misri katika watumwa wa Kinana Ibn Fahm, na watu wa nyumba yake wanasema: Sisi ni Wafursi kutoka kwa watu wa Isfahan, yaani: asili yake ni kutoka Isfahan, lakini ananasibishwa na Fahm; Kwa sababu jina lake limo katika diwani ya Fahm [Rejea: Tarekh Dimishq 50/347, Dar Al-Fikr]. Nasaba kwa watu wasio wa asili katika mifano ya awali haijumuishi makatazo ya kisheria katika kuasili.
Ipasavyo, na katika suala la swali hilo: kuunganishwa kwa familia mbili au koo mbili ikiwa ni kwa njia ya kuchanganya nasaba; kwamba wote wachukue nasaba kamili kwa kubadilisha nasaba yao kwa baba zao na kuwahusisha na watu wengine wa familia nyingine, ni jambo ambalo haliruhusiwi kwa mujibu wa Sheria. Nalo ni miongoni mwa madhambi makubwa yaliyokatazwa. Na ikiwa ni kwa namna ambayo ukamilifu wa jamaa nyingine huonekana; kwamba sifa yake iko mwisho wa jina la mtu; kwa kuchukua jina la ukoo wa familia nyingine, bila ya kudanganya ukweli kwamba mmoja wa jamaa zake ni mtoto wa damu yake mwenyewe, hii inaruhusiwa, na haiingii ndani ya kuasili au kumnasibisha mtu kwa yeyote asiyekuwa baba yake ambaye amekatazwa kisheria.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi
Ofisi ya Fatwa