Kukufuru sio sababu ya kuua
Question
Je, kutojiunga na Uislamu huweza kuwa sababu ya kutosha ya kuhalalisha damu na kuzimwaga?
Answer
Wengi wa wanavyuoni wamekubaliana kuwa kukufuru si sababu ya kuruhusu mauaji kwa mujibu wa Sharia ya kiislamu, wala haiwezi kuwa kisingizio cha kumwaga damu, isipokuwa katika hali maalumu ya kutokea uadui, kwani Uislamu ulikuja kwa ajili ya kupitisha amani na usalama kwa wanadamu wote si Waislamu peke yao, kwa hiyo Waislamu ni umma wa imani na mwitiko, lakini wengine ni umma wa daawa na ufafanuzi, Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote" [Al-Anbiyaa: 107], pia Mwenyezi Mungu Alikiri tabia ya kutofautiana kwa watu ambapo Alisema: "Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana* Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba" [Hud: 118-119], Alisema pia: "Angeli taka Mola wako Mlezi wangeli amini wote waliomo katika ardhi" [Yunus: 99], Mtume (S.A.W.) amesema: "Yeyote anayeomba amani kutoka kwa mwenzake kisha akaja mwenzake huyo akamuua basi muuaji mimi si mdhamini wa muuaji hata akiwa aliyeuawa kafiri" (Imesimuliwa na: Tayalisiy na Bayhaqy), na katika tamko jingine: "basi aliyeua hastahiki dhamana ya Mwenyezi Mungu" hivyo, kukana dhamana kwa aliyeua kafiri ni dalili ya kuwa kukufuru si sababu ya kuhalalisha damu.