Mipaka ya Mazungumzo Kati ya Walioc...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mipaka ya Mazungumzo Kati ya Waliochumbiana

Question

Ni ipi mipaka ya mazungumzo kati ya wachumba?

Answer

Ni lazima tuelewe kuwa uchumba ni miongoni mwa utangulizi wa mkataba wa ndoa, hivyo ni ahadi tu ya kuoana ambayo mmoja wa pande mbili anaweza kuivunja wakati wowote atakapo, hata mchumba wa kiume ana haki ya kurejeshewa Shabka kutoka kwa mchumba wake wa kike akitaka hata kama kuvunja huko kumetoka upande wake; kwa sababu ni sehemu ya mahari ambayo mwanamke anastahili nusu yake kwa kufunga mkataba na anastahili yote kwa kuingiliana.

Mchumba wa kiume bado ni mgeni— yaani si mume — kwa mchumba wa kike; hivyo asikae naye isipokuwa kukiwa na maharimu wake, naye mwanamke akiwa katika hijabu yake, na hilo ni kwa ajili ya maslahi ya kujuana naye, na asitazame kwake isipokuwa uso na vitanga vya mikono pekee, na hivi ndivyo walivyoamua Maimamu wanne. Inaruhusiwa kuzungumza naye kwa kuzingatia vigezo vya kisharia na adabu za Kiislamu ambazo Sharia tukufu imemwamuru mwanamke.

Maelezo

Mwenyezi Mungu  ameweka ndoa kwa ajili ya malengo matukufu na shabaha za juu, miongoni mwake ni kujistiri, usafi, kuinamisha macho, kuhifadhi kizazi kwa kupata watoto, utulivu, rehema na mapenzi kati ya wanandoa; Mwenyezi Mungu anasema: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.} [An-Nisa: 1]. Na kutoka kwa Abdillah bin Mas'ud (R.A), kwamba Mtume  alisema: «Enyi mkusanyiko wa vijana! Atakayeweza miongoni mwenu kuoa [1] basi aoe, kwani hilo ni lenye kuinamisha zaidi macho, na lenye kuhifadhi zaidi tupu, na asiyeweza basi naafunge saumu, kwani hiyo kwake ni kinga[2]» (Imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim).

Sharia tukufu imewahalalishia waliooana aina zote za muingiliano na mazungumzo bila mipaka na muingiliano kati yao, kwa sababu mkataba wa ndoa unamhalalishia kila mmoja kati ya mume na mke kufurahia upande mwingine; Mwenyezi Mungu anasema: {Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao.} [Al-Baqarah: 187].

Ama kuhusu uchumba[3]: Sharia tukufu imeuweka ili kila mmoja kati ya mwanaume na mwanamke amjue upande mwingine ambaye atakuwa mshirika wake katika maisha yake baada ya mkataba wa ndoa; kwa hiyo, muingiliano kati ya wachumba Sharia tukufu imeuwekea mipaka na vigezo ambavyo ni lazima kushikamana navyo, miongoni mwake ni:

Kwanza: Ni lazima wachumba wote wawili wajue kuwa uchumba ni kipindi cha kujuana kati yao, ili mwanamume ajue umbo na tabia ya mwanamke anayetaka kumuoa, kadhalika mwanamke amjue umbo na tabia ya mwanaume atakayekuwa mumewe.

Pili: Uchumba ni ahadi tu ya kuoana, hivyo kila upande una haki ya kuuvunja; kwa hiyo mchumba wa kiume haruhusiwi kuona kwa mchumba wake isipokuwa uso na vitanga vya mikono kama walivyosema jamhuri ya mafakihi[4]; kwa sababu bado ni mgeni[5] kwa mchumba wake.

Tatu: Mchumba wa kiume haruhusiwi kuwa faragha (kukaa peke yao) na mchumba wake katika kipindi cha uchumba; kwa sababu si miongoni mwa maharimu wake. Kutoka kwa Abdillah bin Abbas, kutoka kwa Mtume  amesema: ((Asikae faragha mwanaume na mwanamke isipokuwa akiwa na maharimu)) Bukhari na Muslim).

Nne: Mazungumzo na maneno kati ya wachumba yanajuzu kisheria katika mipaka ya kujuana na kila upande kujua tabia ya mwenzake, hivyo haijuzu kisharia mazungumzo kati ya wachumba yawe katika yale yanayochochea silika na matamanio; jambo ambalo linapelekea kutumbukia katika fitna na haramu.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Uchumba ni ahadi tu ya ndoa, hivyo kila mwanaume na mwanamke ana haki ya kuuvunja.

Uchumba umewekwa ili mwanamume ajue umbo na tabia ya mwanamke anayetaka kumuoa, na vivyo hivyo kwa mwanamke ili kumjua mwanaume anayetaka kuolewa naye.

Mchumba wa kiume haruhusiwi kuona isipokuwa uso na vitanga vya mikono kwa mchumba wake; kwa sababu bado ni mgeni kwake.

Muingiliano na mazungumzo kati ya wachumba yanajuzu kisharia katika mipaka ya kujuana.

 

Haijuzu kisharia mazungumzo kati ya wachumba yawe katika yale yanayochochea hisia na silika; kwa sababu hiyo hupelekea katika fitna na haramu.

 

[1] «Ba'a»: Uwezo wa kimwili na mali wa kuoa.

[2] «Kinga (Wijaa)»: Ujasiri na kinga kwa mtu asitumbukie katika uzina.

[3] «Uchumba (Khitba)»: Ahadi ya ndoa ambayo upande wowote unaweza kuivunja.

[4] Tafsir al-Tabari.

[5] «Ajnabi (Mgeni)»: Mtu ambaye si mume wala maharimu wa mwanamke, nao ni kila ambaye haruhusiwi kumuoa mwanamke milele kama kaka na mjomba.

Share this:

Related Fatwas