Kuswali ndani ya vyombo vya usafiri...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuswali ndani ya vyombo vya usafiri

Question

Ni ipi hukumu ya kuswali ndani ya vyombo vya usafiri?

Answer

Wanazuoni wamekubaliana juu ya uhalali wa kuswali swala za sunnah ndani ya vyombo vya usafiri bila kulazimika kuelekea Qibla, pamoja na kuruhusiwa kuacha baadhi ya nguzo kama kusimama, kurukuu na kusujudu; Mwenyezi Mungu anasema: “Na ni za Mwenyezi Mungu Mashariki na Magharibi; basi popote mtakapoelekea, huko ndiko aliko Mwenyezi Mungu.” [Al-Baqara: 115]. Ibn Umar (R.A) amesema: “Aya hii iliteremshwa kuhusu swala ya sunnah pekee.”

Ama Swala ya faradhi ndani ya vyombo vya usafiri, ina hali mbili:

Ya kwanza: Mtu kuswali Swala ya faradhi ndani ya chombo cha usafiri –gari au ndege au treni, meli au kinginecho - akiwa ametimiza nguzo na masharti, na ameelekea Qibla; basi Swala hiyo ni sahihi.

Ya pili: Mtu ashindwe kutimiza nguzo na masharti ya Swala ya faradhi, na asiweze kuelekea Qibla; basi hairuhusiwi kuswali ndani ya chombo cha usafiri isipokuwa kwa udhuru, kama kuogopa kuibiwa au kuuawa wakati wa kusimama njiani safarini, au kuathiriwa na mvua na mfano wa hayo, pamoja na hofu ya kupitwa na wakati wa swala. Hapo inajuzu kwake kuswali kwa namna anavyoweza, na inapendekezwa kuilipa swala hiyo baadaye.

Maelezo

Katika mambo yaliyothibiti kisharia kuwa Swala ni faradhi kwa kila Mwislamu aliyebaleghe na mwenye akili; ni nguzo ya dini na miongoni mwa nguzo tano za Uislamu, ikiwa ni nguzo ya pili baada ya shahada mbili. Mwenyezi Mungu anasema: “Na simamisheni swala na toeni zaka na rukuni pamoja na wanaorukuu.” [Al-Baqara: 43]. Na anasema: “Hakika swala imefaradhishwa kwa Waumini kwa nyakati maalumu.” [An-Nisaa: 103]. Na kutoka kwa Abdullah bin Umar (R.A) amesema: Mtume (S.A.W)  amesema: “Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: Kushuhudia kuwa hapana mungu ila Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kusimamisha swala, kutoa zaka, kuhiji, na kufunga Ramadhani.”[1]

Na miongoni mwa mambo ambayo wanazuoni wamekubaliana juu ya uhalali wa kuswali sunnah ndani ya vyombo vya usafiri bila kushikamana na mwelekeo wa Qibla, pamoja na kuruhusiwa kuacha baadhi ya nguzo kama kusimama, kurukuu na kusujudu, na kutumia ishara badala yake. Mwenyezi Mungu anasema: “Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo.}.” [Al-Baqara: 115]. Ibn Umar (R.A) amesema: “Aya hii iliteremshwa kuhusu swala ya sunnah pekee, wakati ukiwa umeelekea upande wowote anaouelekea mnyama[2] wako[3].” Na ngamia wakati huo ndio alikuwa ni chombo cha safari na usafiri.

Ama Swala ya faradhi ndani ya vyombo vya usafiri ina hali mbili:

Ya kwanza: Mtu atimize wajibu wa kuswali Swala ya faradhi ndani ya chombo cha usafiri – gari au ndege au treni au meli au kinginecho - akiwa ametimiza nguzo na masharti na kuelekea Qibla; basi swala hiyo huwa ni sahihi. Imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Abbas R.A amesema: Mtume (S.A.W) alipomtuma Ja‘far bin Abi Talib R.A kwenda Uhabeshi, Ja‘far alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nitaswalije ndani ya meli?” Mtume akasema: “Swali humo ukiwa umesimama isipokuwa kama utaogopa kuzama.”

Ya pili: Mtu kushindwa kutimiza nguzo na masharti ya Swala ya faradhi na asiweze kuelekea Qibla; basi hairuhusiwi kuswali ndani ya vyombo vya usafiri isipokuwa kwa udhuru, kama kuogopa kuibiwa au kuuawa wakati wa kusimama njiani safarini, au kuathiriwa na mvua na mfano wa hayo, pamoja na hofu ya kupitwa na wakati wa swala. Hapo inajuzu kwake kuswali kwa namna anavyoweza[4], na inapendekezwa kuilipa swala hiyo baadaye. Imepokewa kutoka kwa Imran bin Husayn R.A amesema: “Nilikuwa na maradhi ya bawasiri, nikamuuliza Mtume (S.A.W) kuhusu swala; akasema: ‘Swali ukiwa umesimama; usipoweza, basi ukiwa umekaa; usipoweza, basi kwa ubavu."[5].

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Swala tano ni faradhi kwa kila Mwislamu aliyebaleghe na mwenye akili; hairuhusiwi kuacha swala ya faradhi kwa sababu yoyote ile, kwani ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu.

2- Inajuzu kwa msafiri kuswali suna akiwa ndani ya chombo cha usafiri bila ya shida yoyote, bila kushikamana na Qibla, pamoja na kuruhusiwa kuacha baadhi ya nguzo kama kusimama, kurukuu na kusujudu, na kutumia ishara badala yake.

Kuswali faradhi ndani ya chombo cha usafiri wakati kimesimama, kwa uwezo wa kutimiza nguzo na masharti zote na kuelekea Qibla, ni jambo linaloruhusiwa kisharia na halina ubaya.

Ikiwa mwenye kuswali atashindwa kurukuu au kusujudu, au kubaini upande wa Qibla ndani ya chombo cha usafiri, basi asubiri mpaka ashuke ikiwa bado kuna muda wa kutosha, au atumie ruksa ya kuunganisha swala ikiwa inawezekana.

Ikiwa mtu atakuwa na yakini kwamba wakati wa swala ya faradhi utapita akiwa ndani ya chombo cha usafiri, basi inajuzu kwake kuiswali kwa namna anavyoweza, na inapendekezwa kuilipa swala hiyo baadaye.

 

[1] Imepokewa na Imam Bukhari.

[2] "Albaeer" ni ngamia, ambae zamani ilikuwa ni mojawapo ya vyombo vya usafirishaji vinavyotumika na watu.

[3] Imepokelewa na Dar qutny katika kitabu  sunnan 2/6.

[4] “Al-Majmu’” cha An-Nawawi (3/222).

[5] Imepokewana Imam Bukhari.

Share this:

Related Fatwas