Kuzuru Makaburi ya watu wema

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuzuru Makaburi ya watu wema

Question

Ni ipi hukumu ya kisharia kuhusu kuzuru makaburi ya Ahlu Al-Bayt (familia ya Mtume) na watu wema? Na ipi hukumu ya anayedai kuwa kuzuru (makaburi)  ni uzushi (bid'ah) na ushirikina?

Answer

 Inapendekezwa kisharia kuzuru makaburi ya watu wema, bali ni miongoni mwa matendo makuu ya kujikurubisha na utiifu unaotarajiwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hakika kuomba dua kwenye makaburi ya watu wema kunatarajiwa zaidi kujibiwa na kukubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani ni sehemu za baraka, rehema, na ni bustani miongoni mwa bustani za Peponi. Ama kauli inayosema kuwa kuzuru makaburi ya watu wema ni uzushi na ushirikina, ni kauli batili isiyo na dalili. Hakika vitendo vya Maswahaba, wema waliotangulia (Salaf), na Wanazuoni wa Umma vinaonesha kujuzu kwa kuzuru makaburi ya watu wema na kuomba dua hapo.

Maelezo

Ni jambo lililothibitishwa kuwa kuzuru makaburi ni jambo linalopendekeza kisharia; kutoka kwa Buraydah Al-Aslami (R.A) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) Amesema: ((Nilikuwa nimewakataza kuzuru makaburi, basi zuruni kwani katika kuyazuru kuna ukumbusho wa kifo))[1]

     Na makaburi yenye haki zaidi ya kufanyiwa ziara baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) ni makaburi ya Ahlu Al-Bayt watukufu. Katika kuwazuru na kuwapenda kuna wema na kiunganishi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika kujikurubisha.} [Ash-Shura: 23]. Uhusiano haukatiki kwa kifo, bali kuzuru makaburi yao ni sehemu ya uhusiano uliosisitizwa na Sharia tukufu.

Ama madai ya anayesema: "Kuzuru makaburi ya watu wema na kutafuta baraka kwayo ni uzushi na aina miongoni mwa aina za ushirikina," akitolea dalili Hadithi ya Aisha (R.A), kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: ((Mwenyezi Mungu amewalaani Mayahudi na Manasara, waligeuza makaburi ya Mitume wao kuwa misikiti))[2]

Ili kujibu madai hayo tunasema: Maana ya kufanya makaburi kuwa misikiti ni kuyasujudu kwa ajili ya kuyaadhimisha na kuyaabudu kama washirikina wanavyosujudia masanamu ya maumbo ya watu na wanyama, na hakuna ndani yake kizuizi cha kuzuru makaburi ya watu wema na kuomba dua makaburini hapo.

Sharia tukufu imeweka fadhila nyingi na kuu kwa ajili ya kuzuru makaburi ya Ahlu Al-Bayt na Mawalii, miongoni mwazo ni hizi zifuatazo: 1- Hakika marehemu anarudisha salamu kwa anayemzuru na kumsalimia; kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) amesema: «Mtu akipita kwenye kaburi la anayemjua akamsalimia, humrudishia salamu na kumtambua, na akipita kwenye kaburi asilolijua akamsalimia, humrudishia salamu»[3].

2- Makaburi ya watu wema ni sehemu zenye baraka ambazo dua hujibiwa hapo; kwani ni bustani miongoni mwa bustani za Peponi; kutoka kwa Abu Said Al-Khudri (R.A), kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: ((Hakika kaburi ni bustani miongoni mwa bustani za Peponi au shimo miongoni mwa mashimo ya Motoni[4]))

3- Kuzuru makaburi ya watu wema ni jambo linalopendekeza kishria; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao.} [Al-Kahf: 21]; Aya hii imejalia kujenga msikiti juu ya makaburi ya watu wema kwa ajili ya kutafuta baraka zao na athari za ibada zao kuwa ni jambo la halali na linalopendekezaa.

4- Kuzuru makaburi ya watu wema kuna kufuata mfano wa vitendo vya Maswahaba (R.A) wote, na Sharia imetuamuru tuwaige na kufuata mifano yao katika kila matendo ya kheri; kutoka kwa Hussein Ibn Ali (R.A): «Kwamba Fatimah (R.A) binti wa Mtume (S.A.W) alikuwa akizuru kaburi la ami yake Hamza (R.A) kila Ijumaa, akiswali na kulia hapo»[5]. Na kutoka kwa Abdullah Ibn Umar Ibn al-Khattab (R.A) alikuwa anapokuja kutoka safarini hufika kwenye kaburi la Mtume (S.A.W) na kusema: «Amani iwe juu yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, amani iwe juu yako ewe Abu Bakr, amani iwe juu yako ewe baba yangu»[6].

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kupendekezaa kuzuru makaburi ya watu wema, bali ni miongoni mwa matendo makuu ya kujikurubisha na utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Dua kwenye makaburi ya watu wema inatarajiwa zaidi kujibiwa na kukubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani ni sehemu za baraka, rehema, na ni bustani miongoni mwa bustani za Peponi.

Kauli kwamba kuzuru makaburi ya watu wema ni uzushi na ushirikina ni kauli batili isiyo na dalili, kwani vitendo vya Maswahaba, Salaf, na wanazuoni wa Umma vinaonesha kujuzu kwa kuzuru makaburi ya watu wema na kuomba dua hapo.

 

[1] Imepokelewa na Abou Dawoud.

[2] Imepokelewa na Abou Al Bukhary.

[3] Imepokelewa na Al-Bayhaqi katika "Shu'ab al-Iman" (11/473)

[4] Imepokelewa na At-Tirmidhi

[5] Imepokelewa na Al-Bayhaqi katika "Al-Sunan Al-Kubra" (4/ 131)

[6] Imepokelewa na 'Abd al-Razzaq katika "Al-Musannaf" (3/ 576)

Share this:

Related Fatwas