Je, Kuoga kunatosheleza Udhu?
Question
Je, kuoga kunatosheleza udhu?
Answer
Miongoni mwa sharti za usahihi wa baadhi ya ibada -kama Swala, Tawafu, na kushika Msahafu mtukufu- ni mtu kuwa twahara kutokana na hadathi mbili: ndogo na kubwa. Twahara ya hadathi kubwa huwa kwa kukoga, na ya hadathi ndogo huwa kwa udhu.
Inajuzu kisharia kutosheka na kuoga badala ya udhu ikiwa ni kwa nia ya kuondosha hadathi kubwa; kwa sababu kunajumuisha kuosha viungo vya udhu.
ili kutosheka na udhu katika hali ya kuoga kwa ajili ya siku ya Ijumaa au kwa usafi wa mwili na mfano wa hayo: ni kwamba anayekoga anuie kuondosha hadathi ndogo.
Maelezo
Imethibitishwa kisharia kwamba miongoni mwa sharti za usahihi wa baadhi ya ibada -kama Swala, Tawafu, na kushika Msahafu mtukufu- ni mtu kuwa twahara kutokana na hadathi ndogo na kubwa. Dalili za kushartiwa twahara kwa ajili ya Swala ni nyingi, miongoni mwazo ni: kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni.} [Al-Ma'idah: 6], na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: ((Mwenyezi Mungu hakubali Swala ya mmoja wenu anapopatwa na hadathi[1] mpaka atawadhe))[2]
Hali kadhalika kwa upande wa Tawafu kuzunguka Al-Kaaba; imepokelewa kutoka kwa Abdullah Ibn Abbas (R.A), kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((Tawafu kuzunguka Nyumba (Al-Kaaba) ni kama swala, isipokuwa nyinyi mnazungumza ndani yake, basi anayezungumza ndani yake asizungumze isipokuwa kheri[3])
Hadithi hii ni ushahidi kuwa Tawafu inashartiwa yale yanayoshartiwa kwa ajili ya usahihi wa Swala kama kutwaharika na hadathi ndogo na kubwa.
Pia hukumu ni hiyohiyo wakati wa kushika Msahafu; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu,(77), Katika Kitabu kilicho hifadhiwa, Hapana akigusaye ila walio takaswa} [Al-Waqi'ah: 77-79]. Aya hii tukufu ni ushahidi kuwa ili kushika Msahafu shrti uwe kuwa twahara na hadathi ndogo na kubwa.
Imethibitishwa kisharia kwa makubaliano ya Wanazuoni kwamba Twahara ya hadathi ndogo na kubwa wakati maji yanapopatikana huwa kama ifuatavyo:
Kwanza: Kuondoa hadathi ndogo[4]: Nayo huwa kwa udhu ambao ni kuosha baadhi ya viungo vya mwili kwa maji, kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni.} [Al-Ma'idah: 6].
Imepokelewa kutoka kwa Sayyidna Uthman Ibn Affan (R.A) namna ya kutawadha, ikapokelewa kutoka kwake: «Kwamba yeye aliomba maji ya udhu akatawadha, akaosha viganja vyake mara tatu, kisha akasukutua na kupandisha maji puani, kisha akaosha uso wake mara tatu, kisha akaosha mkono wake wa kulia mpaka kiwikoni mara tatu, kisha akaosha mkono wake wa kushoto mfano wa hivyo, kisha akapaka kichwa chake, kisha akaosha mguu wake wa kulia mpaka vifundo viwili mara tatu, kisha akaosha wa kushoto mfano wa hivyo. Kisha akasema: Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akitawadha kama udhu wangu huu, kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Mwenye kutawadha kama udhu wangu huu kisha akasimama akaswali rakaa mbili ambazo hazungumzi na nafsi yake ndani yake, husamehewa yaliyotangulia katika madhambi yake»[5].
Pili: Kuondoa hadathi kubwa[6]: Nayo huwa kwa kukoga (ghusl), ambapo ni kuosha viungo vyote vya mwili na kuyaeneza maji mwili mzima; Mwenyezi Mungu anasema: {Enyi mlio amini! Msikaribie Swala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini - mpaka mkoge.} [An-Nisa: 43]. Na imepokelewa kutoka kwa Ummu Salama (R.A) kwamba alisema: «Ummu Sulaym alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kwa haki, je, ni juu ya mwanamke kukoga atakapoota (akipatwa na janaba usingizini)? Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema: Ndio, akiyaona maji (manii)[7]». Yaani: yakitoka manii basi ni wajibu kwake wakati huo kukoga.
Ama kuhusu suala la mtu kutosheka na kukoga -yaani: kuoga- badala ya udhu katika kuondosha hadathi ndogo, hukumu yake ni hivi:
Kwanza: Wakati wa kukoga kwa nia ya kuondosha hadathi kubwa, inamlazimu aoshe viungo vyote vya mwili na kuyaeneza maji mwili mzima ikiwemo viungo vya udhu; na hiyo ni kwa sababu ya yale yaliyothibitishwa kwa wanazuoni kuwa kuondosha hadathi kubwa kunajumuisha kuondosha hadathi ndogo, na kwa hivyo kukoga -yaani: kuoga- kunatosheleza udhu.
Pili: Ikiwa kuoga kwa mtu ni kwa nia ya kuoga Ijumaa au usafi wa mwili na mfano wa hayo, basi inamlazimu wakati wa kuoga -yaani: - anuie kuondosha hadathi ndogo ili udhu uwe sahihi.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Miongoni mwa sharti za kusihi wa baadhi ya ibada -kama Swala, tawafu, na kushika Msahafu mtukufu- ni kutwaharika na hadathi ndogo na kubwa.
Twahara ya hadathi kubwa huwa kwa kukoga.
Twahara ya hadathi ndogo huwa kwa udhu.
Inajuzu kisharia kutosheka na udhu kwa kuoga ikiwa ni kwa nia ya kuondosha hadathi kubwa; kwa sababu kunajumuisha kuosha viungo vya udhu.
Ili kutosheka na udhu katika hali ya kukoga kwa ajili ya siku ya Ijumaa au kwa usafi wa mwili na mfano wa hayo ni sharti kwamba anayeoga anuie kuondosha hadathi ndogo.
[1] ((anapopatwa na hadathi)): Maana yake ni kuwa udhu wake umetenguka.
[2] Imepokelewa na Al-Bukhari.
[3] Imepokelewa na At-Tirmidhi
[4] "Kuondoa hadathi ndogo": Ni kutawadha baada ya kukojoa, au kupata haja kubwa, au kutokwa na upepo (ushuzi).
[5] Imepokelewa kutoka kwa Muslim.
[6] "Kuondoa hadathi kubwa": Ni kuoga (janaba) baada ya kujimai au kuota ndoto (ya kutoa manii).
[7] Imepokelewa na AL Bukhary.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
