Ni nini maana ya "Usufi"?

Egypt's Dar Al-Ifta

Ni nini maana ya "Usufi"?

Question

Nini maana ya neno "Sufiyya" (Usufi)?

Answer

Neno Tasawwuf (Usufi) linamaanisha kuitakasa nafsi na kujishughulisha na kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Akhera badala ya mambo ya dunia. Asili ya Masufi ni kundi la wema waliotangulia walioshughulika na kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiweka mbali na kila kinachowashughulisha na mambo ya dunia, na wakashikamana katika mfumo wao na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake (S.A.W).

Mfumo wa Kisufi ni kushikamana na Qur'ani Tukufu na Sunna, na kujihisi usimamizi wa Mwenyezi Mungu (muraqaba) katika kila neno na kitendo, mpaka mja afikie daraja ya Ihsan.

Ama kuhusu Sheikh wa Kisufi, yeye kiuhalisia ni yule anayewalea wanafunzi wake na wafuasi wake katika njia ya haki na kutakasa nafsi na nyoyo kutokana na kila kinachoshughulisha mbali na kumdhukuru Mwenyezi Mungu.

Maelezo

Imethibitishwa kisharia kuwa kuitakasa nafsi na kusafisha nyoyo kutokana na kila kinachoshughulisha na kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu ni jambo la lazima kwa kila Muislamu, na watu katika hilo wapo katika daraja tofauti; kila mja anapojishughulisha na ibada na kuongeza utiifu na kujiweka mbali na maasi, anazidi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.} [Al-Anfal: 2].

Na kundi miongoni mwa Waislamu lililoitwa "As-Sufiyya" (Masufi) limekuwa maarufu kwa wingi wa ibada, kuitakasa nafsi, na kujishughulisha na kumdhukuru Mwenyezi Mungu mbali na mengineyo.

Wanazuoni wametofautiana kuhusu asili ya neno "Sufiyya" kwa maoni kadhaa; lakini yote yanazunguka kwenye maana ya usafi (safaa) na kuitakasa (tazkiya), yaani kusafisha nafsi kutokana na sifa mbaya na kutokana na kushughulika na dunia, na kuipamba kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujishughulisha na Akhera. Masufi kauli mbiu yao ni kujishughulisha na kumdhukuru Mwenyezi Mungu mbali na mambo ya dunia mpaka mja apate utulivu na amani, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!} [Ar-Ra'd: 28].

Asili ya mfumo wa Kisufi kama walivyosema wanazuoni wa Tasawwuf ipo katika Qur'ani Tukufu na Sunna, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi.} [Al-Imran: 164].

Miongoni mwa majukumu ya Mtume (S.A.W) aliyopewa na Mola wake ni kuitakasa nafsi ya waumini, kuikuza na kuilea, na kubadilisha sifa mbaya kwa sifa njema, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alitekeleza utakaso huu kwa ukamilifu.

Tasawwuf ni elimu na matendo yanayosimama juu ya kushikamana na Qur'ani Tukufu na Sunna iliyotakasika; mpaka imfikishe mwanadamu kwenye daraja ya Ihsan. Imepokelewa kutoka kwa Abdullah Ibn Umar (R.A), amesema: Alinihadithia baba yangu Umar Ibn Al-Khattab (R.A) akasema: ((Siku moja tukiwa tumeketi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), mara alitokea mtu mwenye nguo nyeupe sana, mwenye nywele nyeusi sana, hakuonekana kuwa na athari ya safari, na hakuna yeyote miongoni mwetu aliyemtambua, mpaka akaketi kwa Mtume (S.A.W), akaegemeza magoti yake kwenye magoti yake, na akaweka viganja vyake kwenye mapaja yake, akasema: Ewe Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akasema:

Uislamu ni kushuhudia kuwa hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani, na kuhiji Nyumba kwa mwenye kuwa na uwezo, akasema: Umesema kweli, (Umar) akasema: Tukamstaajabia, anamuuliza na anamsadikisha, akasema: Nieleze kuhusu Imani, akasema: Ni kumuamini Mwenyezi Mungu, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, Siku ya Mwisho, na kuamini kadari kheri yake na shari yake, akasema: Umesema kweli, akasema: Nieleze kuhusu Ihsan, akasema: Ni kumuabudu Mwenyezi Mungu kana kwamba unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye anakuona... kisha akaniambia: Ewe Umar, unamjua ni nani muulizaji? Nikasema: Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi, akasema: Huyo ni Jibril, amewajia kuwafundisha dini yenu)) [1].

Hadithi hii inaonesha kuwa Waislamu hawapo katika daraja moja katika ukaribu na Mwenyezi Mungu, bali kila mja anapozidisha matendo ya utiifu na ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu na kujishughulisha na kumdhukuru Yeye mbali na mengineyo, anakuwa amefikia daraja ya Ihsan, na huu ndio hasa Usufi uliokuwa kwa Mabwana wa Kisufi na wafuasi wao miongoni mwa wema waliotangulia.

Kwa hiyo, Wanazuoni wa Kiislamu walitenga vitabu vinavyoelezea daraja ya Ihsan na ikaitwa katika turathi za Waislamu kwa jina la Elimu ya Tasawwuf.

Ama kwa anayedai kuwa Tasawwuf ni uzushi na upotofu na haina asili katika Uislamu; hii ni kauli isiyo sahihi; kwa sababu inapingana na yale waliyopo Wanazuoni wa Kiislamu kwamba asili ya Tasawwuf imejengwa juu ya Kitabu na Sunna na kushikamana na Sharia tukufu. Imamu Al-Junayd – Imamu wa Masufi – (R.H) amesema: "Njia zote zimefungwa kwa viumbe isipokuwa kwa aliyefuata nyayo za Mtume", na akasema: "Asiyehifadhi Qur'ani, na wala hakuandika Hadithi, hafuatwi katika jambo hili; kwa sababu elimu yetu hii imefungwa na Kitabu na Sunna"[2].

Ama kuhusu Sheikh wa Kisufi: Yeye ndiye anayewafundisha wanafunzi wake wafuasi elimu ya kisharia, na anawalea juu ya kuhisi usimamizi wa Mwenyezi Mungu katika matendo yao yote na maisha yao, na anawaonyesha urithi wa Utume, na anawaongoza kwenye kuigeuza nafsi kutoka kwanye kasoro, na kuponya moyo kutokana na maradhi, yote hayo katika kushikamana kikamilifu na Sharia; mpaka afike nao kwenye kuitakasa nafsi zao.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Neno Tasawwuf linamaanisha kuitakasa nafsi na kujishughulisha na kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Akhera mbali na mambo ya dunia.

Asili ya Masufi ni kundi la wema waliotangulia waliogharimika kumdhukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiweka mbali na kila kinachowashughulisha na mambo ya dunia, na wakashikamana katika mfumo wao na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah za Mtume Wake (S.A.W).

Mfumo wa Kisufi ni kushikamana na Qur'ani Tukufu na Sunna, na kumhisi Mwenyezi Mungu katika kila neno na kitendo, mpaka mja afikie daraja ya Ihsan.

Sheikh wa Kisufi ni yule anayewalea wanafunzi wake na wafuasi wake kuelekea njia ya haki na kutakasa nafsi na nyoyo na kila kinachowaeka mbali na kumdhukuru Mwenyezi Mungu.

 

[1] imepokelewa na Muslim.

[2] "Awarif al-Ma'arif" cha As-Suhrawardi.

Share this:

Related Fatwas