Hukumu ya mume kumdhalilisha mkewe

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya mume kumdhalilisha mkewe

Question

Ni ipi hukumu ya kisharia (Sharia ya Kiislamu) kuhusu mume kumdhalilisha mkewe?

Answer

Ni haramu kwa mume kumdhalilisha mkewe au kushusha thamani na hadhi yake. Mtume (S.A.W.) ametuusia kuwafanyia wanawake wema, imepokewa Hadithi kutoka kwa Abou Hurayra R.A ameema: kutoka kwa Mtume (S.A.W.) amesema: ((...na wausieni wanawake kheri, kwani wameumbwa kutokana na ubavu, na sehemu iliyopinda zaidi katika ubavu ni juu yake, ukijaribu kuunyoosha utauvunja, na ukiuacha utabaki umepinda, basi wausieni wanawake kheri)).

Ama kuhusu uongozi wa mume (Qawamah), maana yake ni jukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mwanamume kusimamia mambo ya mkewe na watoto wake kwa kuwalea na kuwahudumia, pia inamaanisha mume kushauriana na watu wa nyumbani kwake katika kufanya maamuzi yenye masilahi kwa familia. Qawamah haimaanishi mwanamume kuwa na haki ya kumtesa au kumdhalilisha mkewe na watu wa nyumbani kwake.

Maelezo

1. Uislamu ni Dini ya Rehema na Ihsani

Uislamu ni dini ya rehema na kuwatendea wema viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu amemuelezea Mtume Wake Muhammad (S.A.W.) kuwa ni rehema kwa walimwengu wote: {Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote}[Al-Anbiyaa:107]. Mke ni miongoni mwa watu wenye haki zaidi ya kufanyiwa rehema, ihsani, na kutendewa wema.Sheria tukufu imemuusia mwanamume kumkirimu mkewe na kumfanyia wema, na imejenga maisha ya wanandoa juu ya mapenzi na huruma.Mwenyezi Mungu Amesema: {Na kaeni nao kwa wema. Na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkachukia kitu, na Mwenyezi Mungu akajaalia ndani yake kheri nyingi}. [Al Nisaa: 19]. Mwenyezi Mungu amefanya mahusiano kati ya wanandoa kuwa ni ya kuheshimiana, mapenzi na kutodharauliana, pia sheria imeamuru kutengana au talaka iwe kwa njia nzuri bila kumdhalilisha mwenzako ikiwa kumeshindikana kuishi pamoja; Mwenyezi Mungu Mtukufu Aanasema: {Basi ni kukaa kwa wema, au kuachana kwa ihsani} [Al Baqara:229].

Kuhusu mume anayemdhalilisha mkewe na kushusha hadhi yake kwa kisingizio kuwa ana uongozi (Qawamah), hukumu yake na maelezo ya hali yake kulingana na misingi ya kisheria ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Kitendo cha mume huyu kinachukuliwa kuwa ni haramu kisharia na ni kinyume na yale yaliyoamrishwa na Sharia katika kumkirimu mke na kumfanyia wema. Mtume (S.A.W). amemshutumu anayemdhalilisha mkewe kwa kusema: ((...Hawakirimu wanawake ila mtu mkarimu, na hawadhalilishi wanawake ila mtu duni/mnyonge wa tabia))[1].

Pili: Sharia imehimiza kutomdhulumu mwanamke. Imepokewa Hadithi kutoka kwa Abu Hurayra (R.A). amesema: Mtume (S.A.W). amesema: ((Ewe Mwenyezi Mungu, mimi ninasisitiza haki za watu wawili walio dhaifu mno: Yatima na mwanamke)). Imepokewa na Ibnu Majah.

Tatu: Imethibiti kisharia kuwa ndoa imejengwa juu ya utulivu, mapenzi, na rehema. Mwenyezi Mungu amesema: {Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao, na amejalia kati yenu mapenzi na rehema...}.

Nne:  Sharia tukufu imeweka usimamizi (Qawamah) ni jukumu kubwa na amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mwanamume kusimamia familia kwa kutoa huduma, ulinzi, na malezi, haimanishi kumtesa mke, kumdhalilisha, au mume kuwa dikteta wa maoni yake, bali Mwenyezi Mungu ameamuru mume kushauriana na familia yake katika mambo ya kimaisha, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Nao wanawake wanayo haki kwa Sharia kama ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao} [Al Baqara:228]. Na kauli yake ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: { Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa.}[Al Nisaa:34]. Usimamizi ni mwanamume kushauriana na watu wa nyumbani kwake katika kufikia masilahi yake na familia yake.

Tano: Sharia imehimiza upole katika mambo yote, na mke na familia ndio wanastahiki zaidi upole huo. Imepokewa kutoka kwa Aisha (R.A). Mtume (S.A.W.) amesema: (Hakika upole haukuwa katika kitu chochote ila hukipamba, na haukuondolewa katika kitu ila hukiharibu) Imepokelewa na Muslim.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia::

Ni haramu kwa mume kumdhalilisha mkewe au kushusha hadhi yake, Mtume (S.A.W). ametuusia kuwafanyia wanawake wema, imepokewa Hadithi kutoka kwa Abou Hurayra (R.A ) amesema: kutoka kwa Mtume (S.A.W.) amesema: ((...na wausieni wanawake kheri, kwani wameumbwa kutokana na ubavu, na sehemu iliyopinda zaidi katika ubavu ni juu yake, ukijaribu kuunyoosha utauvunja, na ukiuacha utabaki umepinda, basi wausieni wanawake kheri)). Imepokelewa na Al Bukhary.

Ama kuhusu uongozi wa mume (Qawamah), maana yake ni jukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mwanamume kusimamia mambo ya mkewe na watoto wake kwa kuwalea na kuwahudumia, pia inamaanisha mume kushauriana na watu wa nyumbani kwake katika kufanya maamuzi yenye masilahi kwa familia. Qawamah haimaanishi mwanamume kuwa na haki ya kumtesa au kumdhalilisha mkewe na watu wa nyumbani kwake.

 

[1] Imepokelewa na Ibnu Asakir katika Taareekh Dimishq.

Share this:

Related Fatwas