Mwenye Janaba kula na kunywa kabla ya kuoga
Question
Je, inajuzu kwa mtu mwenye janaba kula chakula au kunywa kinywaji kabla ya kuoga janaba?
Answer
Inajuzu kwa mwenye janaba kula na kunywa kabla ya kuoga janaba, lakini inapendekezwa kisharia (Mustahabb) kutawadha kwanza kabla ya kufanya hivyo. Pia, inajuzu kwake kuchanganyika na watu na kufanya nao miamala, kwani yeye si najisi; muumini ni twahara na hanajisiwi na chochote.
Vilevile, inajuzu kwa mwenye janaba kuchelewesha kuoga janaba, lakini kwa sharti kwamba asipitwe na wakati wa Swala ya faradhi. Ikiwa ana yakini kuwa wakati wa Swala unakaribia kutoka, ni wajibu kwake kuoga haraka.
Pia, si kweli yale yanayosambazwa kwa watu kwamba mwenye janaba akila au kunywa kabla ya kuoga huleta ufukara; Badala yake, inapendekezwa mtu mwenye janaba afanye haraka kuoga ili apate baraka na rehema zinazoshushwa na Malaika wa rehema.
Maelezo
Ni jambo lililothibiti kisharia kuwa miongoni mwa masharti ya kusihi kwa baadhi ya ibada - kama Swala, Tawafu, na kushika Msahafu Mtukufu - ni kutwaharika na hadathi ndogo (kutawadha) na hadathi kubwa (kuoga janaba).
Ushahidi wa sharti la twahara katika Swala ni mwigi, ikiwemo kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni... na mkiwa na janaba, basi jitakaseni (ogeni)" [Al-Ma'idah: 6]. Na Mtume (S.A.W). amesema: "Mwenyezi Mungu hakubali Swala ya mmoja wenu anapokuwa na hadathi [[1]] mpaka atawadhe" (Imepokelewa na Bukhari).
Vilevile, amri hiyo inahusu Tawafu ya Al-Kaaba; Mtume (S.A.W). amesema: "Tawafu ya kuizunguka Nyumba (Al-Kaaba) ni kama Swala, isipokuwa nyinyi mnazungumza ndani yake..." (Imepokelewa na Tirmidhi). Hadithi hii inafundisha kuwa Tawafu inashurutisha twahara kama Swala. Kadhalika katika kushika Msahafu; Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika hiyo ni Qur`ani tukufu, katika Kitabu kilichohifadhiwa, hawaigusi isipokuwa waliotakasika" [Al-Waqi'ah: 77-79]. Aya hii tukufu ni ushahidi wa kwamba sharti la kushika Msahafu ni Kutwaharika na Hadathi mbili, kubwa (Janada) na ndogo (Kukosa Udhu).
Ni jambo lililothibiti kisharia kwa makubaliano ya Wanachuoni kuwa twahara kutokana na hadathi mbili (ndogo na kubwa) wakati maji yanapopatikana inakuwa kama ifuatavyo:
Kwanza: Kutwaharika na Hadathi Ndogo [[2]]
Hii hufanyika kwa Udhu, ambao ni kuosha baadhi ya viungo vya mwili kwa maji kama ilivyotajwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpakaeni vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni" [Al-Ma'idah: 6].
Namna ya kutawadha imepokelewa kutoka kwa Sayyidina Uthman bin Affan (R.A) ambapo: "Aliomba maji ya udhu, akatawadha kwa kuosha viganja vyake mara tatu, kisha akasukutua na kupandisha maji puani na kuyatoa, kisha akaosha uso wake mara tatu, kisha akaosha mkono wake wa kulia mpaka kwenye kifundo cha mkono (el-mirafaq) mara tatu, kisha mkono wa kushoto vivyo hivyo, kisha akapaka kichwa chake, kisha akaosha mguu wake wa kulia mpaka kwenye fundo za miguu mara tatu, kisha wa kushoto vivyo hivyo. Kisha akasema: 'Nilimwona Mtume (S.A.W). akitawadha kama hivi udhu wangu huu...'" (Imepokelewa na Muslim).
Pili: kutwaharika na Hadathi kubwa [[3]]
Hii hufanyika kwa Kuoga, ambako ni kuosha viungo vyote vya mwili na kueneza maji mwili mzima; Mwenyezi Mungu anasema: "Wala (msikaribie Swala) mkiwa na janaba — isipokuwa mmo njiani — mpaka muoge" [An-Nisa: 43]. Pia imepokelewa kutoka kwa Umm Salama (R.A.) kuwa Umm Sulaim alikuja kwa Mtume (S.A.W.) na kusema: "Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kwa jambo la haki; je, mwanamke anapaswa kuoga atakapoota?" Mtume (S.A.W). akasema: "Ndiyo, akiona maji (manii)" Imepokelewa na Bukhari.
Kuhusu suala la mwenye janaba kula chakula au kunywa kabla ya kuoga, hukumu yake kama ifuatavyo:
Kwanza: Inapendekezwa (Mustahabb) kwa mwenye janaba kutawadha na kuosha tupu yake ikiwa anataka kula, kunywa, kulala, au kurudia tendo la ndoa [[4]]. Kutoka kwa Aisha (R.A) amesema: "Alikuwa Mtume (S.A.W). anapokuwa na janaba, akitaka kula au kulala, hutawadha udhu wake kama wa Swala" (Imepokelewa na Muslim).
Pili: Kuoga janaba ni wajibu ambao unaweza kucheleweshwa (Ala Al-Tarakhi) na si lazima kufanyika kwa haraka. Hata hivyo, inapendekezwa kutoichelewesha kwa hofu ya kupitwa na nyakati za Swala kwa mfano. Ikiwa mtu ana yakini kuwa kuchelewesha kwake kuoga kutasababisha kukosa wakati wa Swala ya faradhi, basi wakati huo kuoga kunakuwa ni wajibu wa haraka ili kuwahi Swala katika wakati wake.
Tatu: Yale yanayoenea miongoni mwa baadhi ya watu kuwa mtu mwenye janaba hakaribiwi na malaika kwa sababu yeye ni najisi, au kwamba mwenye janaba akila na kunywa hupata ufukara, yote hayo si maneno sahihi na hayana dalili. Mwenye janaba si mtu najisi, bali jambo la msingi ni kuwa inapendekezwa ajitakase kwa kuondoa hadathi kubwa; kwani malaika wa rehema hawamkaribii mwenye janaba ambaye ana uwezo wa kupata maji mpaka aoge. Kutoka kwa Ammar bin Yasir (R.A). Mtume (S.A.W). amesema: "Hakika Malaika hawahudhurii jeneza la kafiri, wala mwanamume aliyejipaka zafarani [[5]] (manukato ya kike), wala mwenye janaba." Na aliruhusu kwa mwenye janaba anapotaka kulala, kula au kunywa, atawadhe (Imepokelewa na Ahmad).
Nne: Inapendeza kwa mwenye janaba kuharakisha kujitakasa ikiwa anaweza. Pia, inajuzu kisharia kwake kutoka akiwa na janaba kwenda kutimiza mahitaji yake, kusimamia mambo yake na kuchanganyika na watu. Kutoka kwa Abu Hurairah (R.A). amesema: "Mtume (S.A.W). alinikuta nikiwa na janaba, akashika mkono wangu, nikatembea naye mpaka akaketi. Kisha nikaondoka kwa siri nikaenda nyumbani, nikaoga, kisha nikarudi naye bado ameketi. Akasema: 'Ulikuwa wapi ewe Aba Hirr?' Nikamueleza, akasema: 'Subhan Allah Mungu! Ewe Aba Hirr, hakika Muumini hanajisiki'" (Imepokelewa na Al-Bukhari).
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Inajuzu kwa mwenye janaba kula chakula na kunywa kinywaji kabla ya kuoga janaba, lakini inapendekezwa kisharia (Mustahabb) kutawadha kwanza kabla ya kufanya hivyo.
Inajuzu kwa mwenye janaba kuchanganyika na watu na kufanya nao miamala kwani yeye si najisi; hakika Muumini ni twahara na hanajisiwi na kitu chochote.
Inajuzu kwa mwenye janaba kuchelewesha kuoga janaba, lakini kwa sharti kwamba asipitwe na wakati wa Swala ya faradhi. Ikiwa ana yakini kuwa wakati wa sala unakaribia kutoka, basi kuoga kunakuwa ni wajibu kwake kuoga haraka.
Sio sahihi yale yanayosemwa na watu kuwa kitendo cha mwenye janaba kula au kunywa kabla ya kuoga husababisha ufukara. Badala yake, inapendekezwa kisharia kwa mtu kuharakisha kuoga ili apate baraka na rehema zinazoshushwa na malaika wa rehema.
[1] Hadathi (Ahadatha): Ni pale udhu wa mtu unapotenguka
[2] Hadathi Ndogo: Ni hali inayohitaji udhu baada ya kukojoa, kupata haja kubwa, au kutoa upepo (ushuzi).
[3] Hadathi Kubwa: Ni kuoga baada ya tendo la ndoa au kuota na kutokwa na manii.
[4] Al-Majmu' cha An-Nawawi (2/156).
[5] Mwanamume aliyepaka manukato ya kike ili kujifananisha na wanawake.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
