Hukumu ya kujenga Makanisa

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kujenga Makanisa

Question

Ni ipi hukumu ya Sharia kuhusu kujenga Makanisa?

Answer

Dini ya Kiislamu ni dini ya Rehema na Hisani kwa viumbe wote. Hakuna kulazimishwa kwa mtu yeyote kuingia katika Uislamu. Sharia takatifu imewahimiza Waislamu kuhifadhi maeneo yote ya ibada, na imeharamisha kuyashambulia au kuyaharibu.

Na kuna makubaliano baina ya Wanazuoni wa Kiislamu kwamba inaruhusiwa kwa Watu wa Kitabu, hasa Wakristo, kujenga makanisa katika nchi za Kiislamu ikiwa wanahitaji hayo; ili waweze kutekeleza ibada zao na shughuli zao za kidini humo. Hii inahesabiwa kuwa sehemu ya wema na haki ambayo Sharia imeamrisha.

Na kukubali Uislamu kwa Watu wa Kitabu kuendelea na dini zao na kutekeleza shughuli zao za kidini, kunahitaji kuruhusu kujenga upya makanisa yaliyoanguka au kuyaruhusu kujengwa; kwa hivyo inaruhusiwa kishaia kujenga makanisa katika nchi za Kiislamu, kwa mujibu wa Sharia na kanuni zinazodhibiti hilo.

Maelezo

Uislamu umetuamrisha kuhifadhi nyumba za ibada za Watu wa Kitabu[1], uliwadhaminia usalama wake, na ukaharamisha aina zote za mashambulizi dhidi yake. Umeifanya jihadi ya Waislamu katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa sababu ya kuzilinda dhidi ya kubomolewa na dhamana ya usalama kwa wafanya ibada waliomo ndani yake. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema: {Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka zingelibomolewa nyumba za watawa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi} [Al-Hajj: 40]. Katika Aya hii tukufu, kuna amri ya kuhifadhi nyumba zote za ibada, kwa sababu ndani ya zote hizo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anatajwa[2].

Hakika Wanazuoni wametaja kuwa Mtume (S.A.W.) walipomjia Wakristo wa Najran mjini Madina na wakati wao wa kusali ukaingia, aliwaruhusu kutekeleza sala yao ndani ya msikiti wake (S.A.W.)[3].

Ama kuhusu suala la kuwaruhusu Watu wa Kitabu miongoni mwa Wakristo wanaoishi katika nchi za Kiislamu kujenga makanisa katika nchi hizo, hukumu yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Imethibiti katika Sharia ya Kiislamu yenye usamehevu kuwa haijuzu kisharia kumlazimisha yeyote kuingia katika Uislamu; bali dini ya Kiislamu imewatambua watu katika dini zao na yale wanayoyaamini, na ikawaruhusu kutekeleza ibada zao. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema: {Hapana kulazimisha katika dini} [Al-Baqarah: 256], na Akasema: {Na sema: Hii ni haki itokayo kwa Mola wenu. Basi anayetaka, na aamini; na anayetaka, na akufuru} [Al-Kahf: 29].

Aya hizi za Qur`ani Tukufu zinaonesha kuwa Uislamu umewaruhusu Watu wa Kitabu kutekeleza ibada zao na taratibu zao maalumu ndani ya mahekalu na makanisa yao. Jambo hili linapelekea kuruhusiwa kujenga upya yale yaliyobomoka katika mahekalu na makanisa hayo, na kuwaruhusu kuyajenga pindi wanapoyahitaji.

Pili: Utendaji wa Waislamu kupitia historia na Ustaarabu wao tangu karne za mwanzo umekuwa ni kuwaruhusu Watu wa Kitabu kujenga makanisa yao wanayoyahitaji kwa ajili ya kutekeleza ibada na taratibu zao za kidini. Abu Umar al-Kindi alitaja kuwa Musa bin Isa alipotawala Misri katika zama za Amirul-Mu’minin Harun Al-Rashid, aliwaruhusu Wakristo kujenga makanisa yaliyobomolewa na Ali bin Suleiman. Makanisa hayo yalijengwa kwa ushauri wa Wanazuoni wa Kiislamu; miongoni mwao akiwa Layth bin Saad na Abdullah bin Lahi’ah. Hoja yao katika kujuzu kwa ujenzi wa makanisa ilitegemea sababu kadhaa:

1- Kwamba ujenzi wa makanisa hayo unazingatiwa kuwa ni sehemu ya ujenzi wa dunia (uimarishaji wa ardhi) ambao Uislamu umeuhimiza.

2- Kwamba mengi ya makanisa hayo yaliyoko Misri hayakujengwa ila baada ya kuingia kwa Uislamu nchini Misri, na hiyo ilikuwa katika zama za Maswahaba (R.A.) na Tabiina, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyepinga ujenzi wa makanisa wakati huo[4].

Tatu: Yale yaliyopokelewa katika baadhi ya vitabu vya Fiqhi vilivyorithiwa miongoni mwa kauli za baadhi ya Wanazuoni zinazoamua kuzuia ujenzi wa makanisa katika nchi za Waislamu, ilikuwa ni kwa sababu ya baadhi ya mazingira ya kihistoria na kijamii ya nyakati hizo, na tunataja miongoni mwa mazingira hayo yafuatayo:

1- Baadhi ya nchi za Kiislamu kukabiliwa na vita vya msalaba vilivyochukua sura ya kidini iliyokuwa ikichochewa na kundi la watu waliojinasibisha na kanisa wakati huo, jambo lililowapelekea Wanachuoni wa Fiqhi wa Kiislamu kufuata kauli zinazosaidia kuleta utulivu wa dola ya Kiislamu na mfumo mkuu kwa upande mmoja, na kuzuia uchokozi dhidi ya itikadi za Waislamu na Misikiti yao kwa upande mwingine.

2- Kuingia kwa idadi kubwa ya Watu wa Kitabu katika dini ya Uislamu, jambo lililopelekea kutelekezwa kwa makanisa mengi kwa kukosa watu wa kwenda, hali iliyoyafanya baadhi ya wakati kuwa sehemu za kujificha wahalifu na wakimbizi wa Sharia na mfano wa hayo.

Nne: Imethibiti kisharia kuwa kubadilika kwa uhalisia kunapelekea kubadilika kwa Fatwa iliyojengwa juu ya uhalisia huo. Na Uislamu umetuamrisha kuonesha wema, rehema, na uadilifu katika kushirikiana na wanaotofautiana nasi katika itikadi, hususan Watu wa Kitabu. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema: {Mwenyezi Mungu hakuwakatazeni kuwatendea wema na uadilifu wale ambao hawajakupigeni katika dini, wala hawajakutoeni katika majumba yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao uadilifu} [Al-Mumtahina: 8]. Hivyo basi, hakuna kizuizi kisharia kwa wao kujenga kanisa pindi wanapolihitaji kwa ajili ya kutekeleza ibada zao, kwani jambo hilo linahesabika kuwa ni katika mlango wa wema na uadilifu.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

1- Dini ya Kiislamu ni dini ya rehema na ihsani kwa viumbe wote, na haijuzu kumlazimisha yeyote kuingia katika Uislamu.

2- Uislamu umewaamrisha wafuasi wake kuhifadhi sehemu zote za ibada, na ukaharamisha kuzishambulia.

3- Ni jambo lililokubaliwa na Wanazuoni wa Kiislamu kuwa inajuzu kwa Watu wa Kitabu miongoni mwa Wakristo kujenga makanisa katika nchi za Waislamu madamu wanayahitaji; na hiyo ni kwa ajili ya kutekeleza ibada na taratibu zao za kidini humo; kwani jambo hili linahesabika kuwa ni katika mlango wa wema na uadilifu ulioamrishwa kisheria.

4- Hatua ya Uislamu kuwatambua Watu wa Kitabu katika dini zao na utekelezaji wa ibada zao inapelekea kuruhusiwa kuzijenga upya pindi zinapobomoka, na kuruhusu ujenzi wake; kwa sababu hiyo, inajuzu kisharia kujenga makanisa katika nchi za Waislamu, kwa mujibu wa Sharia zinazosimamia jambo hilo.

 

[1] "Watu wa Kitabu": Mayahudi na Wakristo.

[2] "Tafsir Muqatil" (3/129).

[3] "Tafsir Ibn Kathir" (2/42), na "Ahkam Ahl Al-Dhimma" cha Ibn Qayyim Al-Jawziyya (1/397).

[4] "Al-Wulah wal-Qudah" (uk. 100).

Share this:

Related Fatwas