Zaka kwa Kadi (kadi ya visa) ya Man...

Egypt's Dar Al-Ifta

Zaka kwa Kadi (kadi ya visa) ya Manunuzi

Question

Nina kadi ya mkopo, ambayo Benki inanipa kupitia kadi hiyo kiasi cha fedha kinachofikia takriban pauni laki moja, na huwa natumia kwa ajili ya manunuzi na hulipia kabla ya muda uliowekwa kumalizika. Je, ni lazima nitoe zaka juu ya fedha hizi? Na je, ni lazima kuziunganisha (kuongezea) fedha hizi — ikiwa hazijafikia kiwango cha Zaka — na jumla ya fedha ninazomiliki na kisha kutoa Zaka yake?

Answer

Hakuna Zaka juu ya kiasi cha fedha kinachopatikana kupitia kadi za mkopo (Credit Card); kwa sababu hakijatimiza sharti la ulazima wa Zaka ya mali, kwani umiliki kamili haujatimia.

Maelezo

Zaka ni ibada na nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu, ambayo Mwenyezi Mungu amewafaradhishia matajiri kwa lengo la kuziba mahitaji ya walengwa wanane waliotajwa katika Qur'ani Tukufu, hasa mafakiri na masikini. Kwa ajili hiyo, Mtume (S.A.W) aliwataja katika Hadithi ya Mu'adh (R.A) alipomtuma Yemen na akamwambia: "Waambie kuwa Mwenyezi Mungu amewafaradhishia sadaka katika mali zao, itakayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurejeshwa kwa masikini wao." (Bukhari na Muslim).

Kinachokusudiwa katika Kadi ya mkopo — ambayo pia hujulikana kama kadi ya malipo ya baadaye — ni kadi ya kielektroniki ya malipo inayotolewa na taasisi maalum, kama benki au shirika la kifedha (k.m. kampuni ya mikopo/ufadhili). Kadi hii ni njia ya mkopo inayomwezesha mmiliki kutumia kiasi fulani cha fedha kwa mujibu wa kikomo cha mkopo kilichowekwa, ili afanye malipo, manunuzi, au kutoa fedha taslimu, kulingana na sera ya taasisi hiyo ya kifedha.

Kutokana na hayo, kadi hizi ni aina ya bidhaa ya kifedha inayomwezesha mmiliki kutumia kiasi maalumu cha fedha kwa ajili ya manunuzi au kutoa fedha taslimu, mradi tu kuna salio la kutosha kwa ajili ya muamala. Hivyo basi, ni mali inayopatikana kwa ajili ya mwenye kadi. lakini hazihesabiwi kuwa mali yake kamili, kwani haziingii mikononi mwake isipokuwa pale anapofanya malipo, au baada ya kutoa fedha taslimu. Aidha, mara baada ya matumizi, fedha hizo huwa ni deni analodaiwa na taasisi iliyotoa kadi.

Kisharia, ni sharti la ulazima wa Zaka kutimia umiliki kamili wa mali, kama asemavyo Mwenyezi Mungu: "Chukua sadaka kutoka katika mali zao, ili uwatakase na kuwasafisha kwayo." [Tawba: 103].

Wanazuoni wa Fiqhi wamekubaliana kuwa Zaka hailazimu isipokuwa kwa mali inayomilikiwa kwa umiliki kamili, yaani mtu awe na uwezo kamili wa kuitumia mali hiyo kama apendavyo na faida zake zimfikie yeye binafsi.

Ikiwa ni hivyo, “basi inaonekana kwamba hukumu kuhusu ulazima wa kutoa Zaka kwa mali zinazopatikana kupitia kadi ya mkopo (Credit Card) inakuwa na hali mbili, kulingana na namna mmiliki wa kadi anavyotumia kadi hiyo.”

Hali ya kwanza: Ikiwa kiasi cha fedha kilichowekwa hakitumiki, au kinatumika kwa ajili ya kulipia na manunuzi tu — basi hakuna Zaka juu ya kiasi hicho, wala hakihesabiwi kama sehemu ya jumla a mali inayomilikiwa na mtu, kwa sababu umiliki kamili haujatimia, na kwa kuwa fedha bado zipo chini ya udhibiti wa taasisi iliyotoa kadi.

Hali ya pili: Ikiwa kiasi hicho kitachukuliwa kwa njia ya kutoa fedha taslimu na kikawa mikononi mwa mmiliki wa kadi, naye akaanza kukitumia apendavyo — bado hakitazamiwi kuwa mali kamili, kwa sababu umiliki ni pungufu. Hii ni kwa sababu mwenye kadi anadaiwa kurejesha fedha hizo ndani ya muda maalumu waliokubaliana, na iwapo atachelewa atalazimika kulipa gharama za ziada. Kwa hivyo, hata kama ana mali nyingine iliyofikia kiwango na imepitwa na mwaka wa Zaka (hawl), bado kiasi hicho hakiongezwi kwenye jumla ya mali hiyo. Hali ya kuwa fedha hizo ziko mikononi mwake haibadilishi chochote, kwa kuwa hali hiyo inafanana na kutokuwa na mali, kulingana na maoni ya wanazuoni wengi wa Madhehebu ya Hanafi, Maliki na Hanbali kuhusu zaka ya mali ya mwenye deni[1].

Kwa hivyo, hakuna Zaka juu ya kiasi cha fedha kinachopatikana kupitia kadi ya mkopo (Credit Card), kwa kuwa hakitimizi masharti ya ulazima wa Zaka ya mali — kwa sababu umiliki kamili haujatimia. Iwe mmiliki wa kadi ametumia kadi hiyo kufanya malipo na manunuzi — kwani kiasi (yaani, salio) hicho ni katika yale yaliyo tayari kutolewa lakini bado hakijaingia katika umiliki wake — au ameitoa kwa njia ya uondoaji wa pesa taslimu; basi katika hali zote hizo, umiliki wake wa fedha hizo ni umiliki usiokamilika, kwa kuwa dhamana ya mmiliki wa kadi inabaki imefungwa na ulazima wa kulipa kiasi kilichotolewa kwa wakati uliokubaliwa kati yake na taasisi iliyomtolea kadi hiyo.Na kwa kuwa madai ya kulipwa yanamuelekea yeye (mmiliki wa kadi), basi mali hiyo inachukuliwa kuwa kana kwamba haipo.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia;

Zaka si wajibu kwa fedha zinazopatikana kupitia kadi za mkopo, kwa sababu umiliki kamili haujatimia.

 

[1] “Al-Jawhara an-Nayyira” (Juzuu ya 1, uk. 114, toleo la Al-Matba‘a al-Khayriyya)“Manah al-Jalil” (Juzuu ya 2, uk. 45, toleo la Dar al-Fikr). “Ash-Sharh al-Kabir” (Juzuu ya 6, uk. 343, toleo la Hajr).

 

Share this:

Related Fatwas