Kutumia dawa za kupunguza hamu ya k...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kutumia dawa za kupunguza hamu ya kula wakati wa daku

Question

Ninapata ugumu mkubwa kufunga, kiasi kwamba inanizuia kufanya kazi zangu za kila siku, kwa sababu ninahisi njaa haraka sana. Je, inajuzu kutumia dawa za kupunguza hamu ya kula wakati wa daku, ili niweze kuvumilia saumu ya siku nzima?

Answer

Ndiyo, inajuzu kwa mtu anayechoka sana kutokana na kufunga, kuchukua dawa au kitu kingine chochote kinachopunguza hamu ya kula wakati wa daku, mradi tu: Kitu hicho ni halali kisharia, na hakina madhara kiafya, kwa mujibu wa ushauri wa daktari bingwa.

Maelezo

Imethibitishwa kisharia kwamba saumu hupatikana kwa kujizuia na vitu vinavyofunguza kwa namna maalumu, nayo ni kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na anayefunga awe mtu maalumu naye ni Muislamu, kwa sifa maalumu nayo ni kutokua katika hedhi au nifasi, katika wakati maalumu nao ni weupe wa mchana kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri ya pili hadi kuchwa kwa jua.

Na Mtume (S.A.W) alifanya daku kuwa ni Sunna, nayo ni jina la chakula kinacholiwa wakati wa usiku wa manane, ambao ni sehemu ya sita ya mwisho ya usiku.

 Na aliisunnisha kwa hekima, miongoni mwazo ni kupata nguvu kwa ajili ya kufunga mchana, kwa kuwa inaleta nguvu na uchangamfu zaidi. Imepokewa kutoka kwa Ibn ‘Abbas (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) alisema: “Tafuteni msaada kwa chakula cha daku kwa ajili ya kufunga mchana, na kwa kulala mchana kwa ajili ya kusimama usiku.” Imepokewa na Ibn Majah katika as-Sunan.

Imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) alisema: “Kuleni daku, kwani hakika katika daku kuna baraka.” Bukhari na Muslim.

Na imewekwa kisheria kwa yule anayechoshwa na saumu kula katika daku kile kinachoziba hamu yake, kiwe ni dawa, kinywaji au chakula, mradi tu kiwe halali katika asili yake, yaani kiwe safi na hakikuharamishwa kwa dalili ya jumla au maalumu; kwani asili ya mambo ni uhalali wake kama ilivyothibitishwa kisheria. Na ushahidi wa msingi huu ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Yeye ndiye aliyewaumbia vyote vilivyomo duniani kwa ajili yenu} [Al-Baqara:29]

Na katika Hadithi ya Salman Al-Farisi (R.A) kwamba alisema: Aliulizwa Mtume (S.A.W) kuhusu samli, jibini, na ngozi za wanyama, akasema: “Halali ni kile alichohalalisha Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake, na haramu ni kile alichokiharamisha Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake, na alichonyamaza juu yake basi ni katika yale aliyosamehe.”  Imepokewa na At-Tirmidhi na Ibn Majah katika as-Sunan.

Hata hivyo, uhalali huu umewekewa sharti la kutokupatikana madhara kwa anayekitumia; kwani imekwishathibitishwa kisharia kwamba: “Hakuna kujidhuru, wala kudhuru wengine,” nayo ni kanuni ya kifiqhi miongoni mwa kanuni tano kuu ambazo hukumu nyingi za Fiqhi huzunguka juu yake. Asili ya kanuni hii ni hadithi iliyopokewa kutoka kwa ‘Ubadah bin aṣ-Ṣamit (R.A) kwamba Mtume (S.A.W) “Alihukumu kuwa hakuna kujidhuru wala kudhuru mwengine.” Imepokewa na Ibn Majah katika Sunan yake.

Nayo ni kanuni ambayo kuizingatia kwake humzuia mwanadamu na kila kitu kinachoweza kumsababishia madhara, iwe kwa kiwango cha mtu binafsi au kwa jamii.

Na kwa mujibu wa hilo, ni lazima utumiaji wa dawa hizi uzingatie ruhusa ya wataalamu wa fani – madaktari waaminifu – ambao watathibitisha kwamba matumizi yake yataleta manufaa kwa mtumiaji na hayatasababisha madhara kwake.

Tunapata faida kutokana na yaliyopita:

Saumu ni kujizuia na vitu vinavyofuturu kwa Nia ya ibada katika muda maalumu.

Inajuzu kwa yule anayechoshwa na saumu kula katika daku kile kinachoziba hamu yake, kiwe ni dawa, kinywaji, au chakula.

Share this:

Related Fatwas