Kukata mfululizo wa Saumu ya kafara...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kukata mfululizo wa Saumu ya kafara kwa sababu ya kufunga mwezi wa Ramadhani na Sikukuu

Question

Mwanamume alilazimika kufunga kafara ya miezi miwili mfululizo kwa sababu ya mauaji ya kimakosa. Alifunga mwezi wa Shabani, kisha Ramadhani na Shawwal, na hakufuturu isipokuwa siku ya Idd El-Fitr. Je, kufunga Ramadhani na kufuturu siku ya Idd kunakatiza mfululizo wa Saumu ya kafara yake, kiasi kwamba lazima aanze tena kufunga miezi miwili mfululizo? Ikumbukwe kwamba alilipa (alifunga) siku ya Idd aliyofuturu katika siku ya kwanza ya Dhul-Qa'dah.

Answer

Mwenye kulazimika kafara ya kufunga miezi miwili mfululizo kwa sababu ya mauaji ya kimakosa, akaanza kufunga kuanzia mwanzo wa mwezi wa Shabani, kisha Saumu yake ikakatizwa na Saumu ya mwezi wa Ramadhani na kufuturu siku ya Idd El-Fitr; hakika hili halikatizi mfululizo wa Saumu yake maadamu alilipa (alifunga) siku ya Idd aliyofuturu bila ya kutenganisha kati yake na saumu ya miezi miwili. Hivyo basi, halazimiki kuanza tena kufunga kafara mara nyingine, na wala hakuna ubaya kwake.

Maelezo

Wanazuoni wamekubaliana kwa kauli moja kwamba muuaji wa kimakosa lazima atoe kafara tofauti na diyya (fidia ya damu), hakuna tofauti kati ya kuua kimakosa mdogo au mkubwa, mwanamume au mwanamke. [1]

Kafara hii ni kuacha huru mtumwa, na kwa kuwa utumwa haupo tena, na hivyo basi amri ya kuacha huru mtumwa haina mahali pa kutekelezwa, wajibu wa kafara kiasili umekuwa: kufunga miezi miwili mfululizo; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.} [An-Nisā’: 92].

Wanazuoni wamekubaliana kwa kauli moja kwamba sharti katika kafara ya kufunga miezi miwili ni: kufuatana; yaani: kufunga siku mfululizo bila ya kutenganisha kati yao. Asili ya hili ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

{basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu.}[An-Nisā’: 92] [2]  

Iwapo mwenye wajibu wa kutoa kafara akianza kufunga miezi miwili, kisha akafungua Saumu yake kabla ya kuimaliza na akakatisha mwendelezo wa Saumu yake bila ya udhuru wa halali, basi Wanachuoni wameafikiana kwamba aanze tena Saumu yake na asijenge katika siku alizofunga, kwa sababu alikatiza mwendelezo uliowekwa kwao.

Ikiwa mtu akianza kufunga miezi miwili, na kati yake ikaja kufunga kwa Ramadhani, au siku ambayo wajibu kufuturu kama vile Idi mbili; basi Wanavyuoni wametofautiana kuhusu kukata mfuatano wa kafara yake au kutokukata kwa maoni mawili:

Kauli ya Kwanza: Kwamba anayelazimika kufunga miezi miwili mfululizo, kisha Saumu yake ikakatizwa na Saumu ya Ramadhani au siku ambayo wajibu kufuturu, basi kufuatana kwa Saumu yake kumeisha, na lazima aanze tena kufunga upya; kwa sababu anaweza kujiepusha kufunga kafara yake katika Ramadhani, na kadhalika wakati wowote ambao kukifunga kumezuiliwa. Maana yake: Anapata wakati katika mwaka ambao unatosha kufunga miezi miwili mfululizo bila ya kukatizwa na saumu ya wajibu au wakati ambao kukifunga kumezuiliwa. Haya ni  Madhehebu ya Imamu Hanafi na Shafi. [3]

Kauli ya Pili: Kwamba anayelazimika kufunga miezi miwili mfululizo, kisha Saumu yake ikakatizwa na Saumu ya Ramadhani au Idd El-Fitr, basi kufuatana kwa saumu yake hakukatizwi; kwa sababu kufunga mwezi wa Ramadhani ni wajibu, na Sharia Tukufu imekataza kufunga isiyokuwa hiyo ndani yake, na Idd ni wakati ambao haramu kufunga mwanzo wake. Hivyo basi, kwa kuwa Sharia ndiyo iliyoweka mipaka ya wakati huu kwa wajibu wa kufunga au wajibu wa kufuturu, kukatizwa kwake hakukatizi saumu ya miezi miwili mfululizo; kwa sababu ni udhuru wa kisharia unaokubalika ambao haukatizi kufuatana kwa saumu ya kafara, na haya ni Madhehebu ya Imamu Hanbali, na Imamu Ibn Habib miongoni mwa Imamu Maliki. [4]

Kauli hii ndiyo iliyochaguliwa kwa ajili ya Fatwa; kwa sababu ina wepesi kwa walioamrishwa, na kuondoa uzito na kuondoa shida na kupunguza mzigo kwao; kwa rehema kwao, na kuzingatia hali zao, na kwa sababu hali za watu hutofautiana katika uwezekano wa kufunga miezi miwili katika mwaka; kutokana na aina tofauti ya misimu ya kazi zao na mfano wa hayo, na kuamrisha katika Sharia ya Kiislamu ni kwa kadiri ya uwezo na nguvu unaofaa hali na tabia za watu na uwezo wao; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

{Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo.}

[Al-Baqarah: 286]. Na imethibitishwa katika kanuni za Sharia kwamba: “Mwenye kupewa mtihani kwa jambo ambalo linakhitalifiana ndani yake, amfuate aliyeliruhusu”, na kwamba “Shida huleta wepesi” na “Jambo likibanana, hutanuka”.

Na hali ya tofauti hii iliyopo kati ya Wanavyuoni wa Fiqhi ni kabla ya kutenda kitendo, lakini kitendo kikitokea na kufanywa na aliyeamrishwa – kama ilivyo katika swali letu – basi “Wakati wowote kitendo cha mtu wa kawaida kinapokubaliana na Madhehebu ya Mujtahidi yeyote… inamtosha, na hana dhambi kwa makubaliano”.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia;

Kwamba anayelazimika kufunga miezi miwili mfululizo, kisha Saumu yake ikakatizwa na Saumu ya Ramadhani au Idd El-Fitr, basi kufuatana kwa Saumu yake hakukatizwi, na halazimiki kuanza tena kufunga kafara mara nyingine, na wala hakuna ubaya kwake.

 

[1] “Al-Mughni” cha Imam Ibn Qudamah (8/512, chapa ya Maktaba ya Kairo).

[2] “Ash-Sharhul Kabiir” cha Shams al-Din Ibn Qudamah (aliyefariki 682 AH) (8/603, chapa ya Dar al-Kitab al-Arabi).

[3] “Bada’i’ Al-Sana’i’” (5/111, chapa ya Dar Al-Kotob Al-Ilmiyyah), “Rawdat Al-Talibin” (8/303, toleo la Ofisi ya Kiislamu).

[4] “Al-Insaf” (Chapa ya 9/224 ya Dar Ihya’ Al-Turath), “Al-Taj Wal-Iklil” (5/449, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyyah).

Share this:

Related Fatwas