Kufariki katika Ramadhani

Egypt's Dar Al-Ifta

Kufariki katika Ramadhani

Question

 Mmoja wa ndugu zangu alifariki katika mwezi wa Ramadhani akiwa amefunga. Wakati wa kumzika, mmoja wa watu aliwaambia wanawe kwa nia ya kuwafariji: “Hakika mwenye kufa katika mwezi wa Ramadhani ataingia Peponi bila ya hisabu (kuhesabiwa),” lakini mmoja wa waliohudhuria alikanusha kauli hiyo, kwa madai kuwa kauli hiyo ni kinyume na Sunna; kwa sababu hakuna matini iliyopokewa kwayo. Je, hukumu ya Sharia kuhusu hilo ni ipi?

Answer

Mja Muumini anapofariki akiwa amefunga katika mwezi wa Ramadhani, basi anatarajiwa kuingia Peponi kama ambavyo Hadithi za Mtume zilivyoeleza. Ama kuhusu kauli wanayosema baadhi ya watu kwamba mwenye kufa katika mwezi wa Ramadhani ataingia Peponi bila ya hisabu, kauli hiyo hubebwa kwa maana ya matarajio na kudhani mema juu ya kufika kwa Mwenyezi Mungu, hasa ikizingatiwa kwamba amechaguliwa marehemu nyakati zinazolingana na ahadi njema ya Kinabii iliyotajwa katika Hadithi, kwani Pepo imefunguliwa na kupambwa kwa ajili ya anayekufa katika mwezi wa Ramadhani.

Maelezo:

Mwenyezi Mungu Mtukufu Ameneemesha Umma huu kwa mwezi wa Ramadhani mtukufu. Hakuna Muislamu anayejitolea kwa Mola wake katika mwezi huu kwa Saumu, kisimamo (kuswali), sadaka, kusoma Qur'ani Tukufu, na aina nyinginezo za utiifu isipokuwa atapata thawabu tele na ujira mkubwa. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: ((Inapokuwa usiku wa kwanza wa Ramadhani, mashetani na waovu wa majini hufungwa minyororo, na milango ya Moto hufungwa na hakuna mlango wowote unaofunguliwa, na milango ya Peponi hufunguliwa na hakuna mlango unaofungwa, na mtangazaji hutangaza: Ewe mwenye kutaka kheri, kubali, na Ewe mwenye kutaka shari, acha, na Mwenyezi Mungu ana watu wanaoachwa huru kutoka Motoni, na hayo hufanyika kila usiku)) Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah katika Sunan yake.

Na imekuja katika Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W)  Hadithi zinazosisitiza kwamba Muislamu anaponyoosha nia yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katika Saumu ya mwezi wa Ramadhani, hilo litakuwa sababu ya kusamehewa dhambi zake. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A) alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: ((Mwenye kufunga Ramadhani kwa Imani na kutarajia thawabu, husamehewa dhambi zake zilizotangulia)) Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari.

Na inajulikana kwamba kusamehewa dhambi na kufa katika utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni sababu ya kupata mwisho mwema na kuingia kwa mja Muumini Peponi. Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (R.A) alisema: Nilimuegemeza Mtume (S.A.W) kifuani mwangu, naye akasema: ((Mwenye kusema: Laa ilaaha illa Llaahu (hapana mungu ila Mwenyezi Mungu), kwa kufanya matendo mema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, maisha yake yakaishia kwayo, ataingia Peponi, na mwenye kufunga siku moja kwa ajili ya  Mwenyezi Mungu, maisha yake yakaishia kwayo, ataingia Peponi, na mwenye kutoa sadaka kwa ajili ya  Mwenyezi Mungu, na maisha yake yakaishia kwayo, ataingia Peponi)) Imepokelewa kutoka kwa Maimamu: Ahmad katika Al-Musnad, na Al-Bayhaqi katika Al-Asmaa wal Sifaat, na akaitaja Imamu Al-Suyuti katika Sharh al-Suduur bi-Sharh Haal al-Mawtaa wal Qubuur chini ya mlango wa "Nyakati Bora za Kifo".

Na huenda kufunguliwa kwa milango ya Peponi hapa ni ishara (kinaya) ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anawafungulia waja wake miongoni mwa matendo ya utiifu yaliyowekwa kisharia katika mwezi huu ambayo hayapatikani katika miezi mingine, kama Saumu, kisimamo, na kufanya mema, na kwamba hayo ni sababu za kuingia Peponi na ni milango yake. Kadhalika na kufungwa kwa milango ya Moto.

Ama kuhusu yale yanayozungumzwa na baadhi ya watu: kwamba mwenye kufa katika mwezi wa Ramadhani ataingia Peponi bila ya hisabu, kauli hii, japo haikupokewa na nukuu (ya moja kwa moja), lakini inaafikiana kimaana na Hadithi tulizozitaja za kwamba Saumu ya mwezi wa Ramadhani ni sababu ya kusamehewa dhambi, na kwamba mja anapofariki akiwa amefunga, ataingia Peponi.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia;

Mja Muumini anapofariki akiwa amefunga katika mwezi wa Ramadhani, basi anatarajiwa kuingia Peponi.

Kauli wanayosema baadhi ya watu kwamba mwenye kufa katika mwezi wa Ramadhani ataingia Peponi bila ya hisabu, hubebwa kwa maana ya matarajio na kudhani mema juu ya kufika kwa Mwenyezi Mungu, kwani Pepo imefunguliwa na kupambwa kwa ajili ya anayekufa katika mwezi wa Ramadhani.

Share this:

Related Fatwas