Tofauti ya Thawabu katika Saumu kut...

Egypt's Dar Al-Ifta

Tofauti ya Thawabu katika Saumu kutokana na kiwango cha Taabu (Shida)

Question

Tumepokea swali likisema: Hisia za watu kuhusu shida (taabu/mashaka) katika Saumu hutofautiana, nami nimesikia: “Kwamba thawabu ni kwa kadri ya shida.” Je, kauli hiyo ina ukweli gani? Na je, kila shida inavyoongezeka ndivyo thawabu inavyoongezeka?

Answer

Thawabu hutofautiana katika ibada ya Saumu kutokana na urefu wa mchana, au ukali wa joto ndani yake, au kufanya kazi yenye taabu inayozidi kazi nyingine, kama vile wenye kazi ngumu na mfano wao. Hata hivyo, hilo linafungamana na ikhlas (nia safi) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Mola Mwenye Nguvu) katika ibada, na bila kukusudia kutafuta shida yenyewe (taabu) moja kwa moja.

Maelezo:

Saumu ni moja ya ibada tukufu ambazo kwayo mja hujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ni miongoni mwa sababu kuu za kusamehewa dhambi na kufutiwa makosa, iwe Saumu ni ya faradhi au Sunna. Imepolelewa kutoka kwa Abu Hurairah (R.A), alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: ((Mwenye kufunga Ramadhani kwa imani na kutarajia malipo, husamehewa dhambi zake zilizotangulia)) Imekubaliwa na wote (Al-Bukhari na Muslim).

Imepolelewa kutoka kwa Abu Sa’id Al-Khudriy (R.A), alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akisema: ((Mwenye kufunga siku moja kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atauweka mbali uso wake na Moto umbali wa miaka sabini)) Imekubaliwa na wote.

Basi ikiwa Saumu inaambatana na shida ya lazima, kiasi kwamba haiwezekani kuitimiza ila kwa kuvumilia shida hiyo, kama vile joto kali, au mchana mrefu, au kufanya kazi, basi thawabu na ujira huwa mkubwa zaidi na bora wakati huo. Kwa kule ambako imepolelewa kutoka kwa Mama wa Waumini, Aisha (R.A), kwamba Mtume (S.A.W) alimwambia katika Umra yake: ((Hakika wewe unapata thawabu kadri ya taabu yako na matumizi yako)) Imepolelewa kutoka kwa Al-Daraqutni katika Sunan na Al-Hakim katika Al-Mustadrak naye akaisahihisha. Inachukuliwa kutokana na Hadithi: Kwamba thawabu na fadhila katika ibada huongezeka kwa kuongezeka kwa taabu na matumizi.

Kwa sababu hii, Wanachuoni wa Usuul (misingi) na Fiqhi (Shria) walikadiria kwamba "Thawabu ni kwa kadri ya shida (mashaka)," yaani: Kadri kazi inavyozidi na kuwa ngumu, inakuwa bora kuliko ile isiyo hivyo. Kinachokusudiwa kwa shida hapa ni: Shida ambayo haiachani na ibada, na ndiyo ambayo Sharia imepanga juu yake ujira mkuu na thawabu tele, tofauti na ibada nyingine ambazo hazina shida. Kwa sababu shida haikusudiwi kisharia yenyewe, bali inapotokea kwa kufuata hitaji la kisharia, mwanadamu hulipwa juu yake. Na ikiwa mwanadamu anakusudia kujiletea shida yeye mwenyewe, hili ni jambo ambalo Sharia safi imelikataza, na anayefanya hivyo anaelezewa kama mwenye  kuvuka mipaka. Amesema Mtume (S.A.W): ((Wameangamia wenye kuvuka mipaka)) Alisema haya mara tatu. Imepolelewa kutoka kwa Muslim katika Sahihi yake, yaani: Wenye kwenda kina kirefu, wenye kuzidisha, na wenye kuvuka mipaka katika matendo na kauli zao.

Kusudio la Muwekaji Sharia ni maslahi ya waja katika dini yao na dunia yao.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia;

Saumu ni moja ya ibada tukufu ambazo kwayo mja hujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Thawabu na ujira hutofautiana katika ibada ya Saumu kutokana na urefu wa mchana, au ukali wa joto ndani yake, au kufanya kazi yenye taabu inayozidi kazi nyingine, kama vile wenye kazi ngumu na mfano wake.

Matendo yote yanafungamana na ikhlas (nia safi) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katika ibada, na bila kukusudia kutafuta shida yenyewe moja kwa moja.

Share this:

Related Fatwas