Mwenye Mtaji Kuweka Masharti ya Kut...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mwenye Mtaji Kuweka Masharti ya Kutobeba Hasara Katika Mudaraba (Ushirika)

Question

Nataka kufanya mkataba wa ushirika na mtu, ambapo nitampa fedha, naye ananunua na kuuza bidhaa, kwa malipo ya asilimia 40% ya faida iwe yake, na asilimia 60% iwe yangu, na nitamuwekeaweka sharti kwamba mimi sitabeba hasara yoyote. Je, hukumu ya kufanya mkataba huu ni ipi kisharia?

Answer

kuingia mkataba wa Mudaraba (ushirika wa mtaji na kazi) huku mwenye mtaji akiweka sharti kwa mwenza anayefanya biashara na mtaji huo kwamba hatabeba hasara yoyote ya mtaji au sehemu yake, ni sharti batili (fasidi) ambalo linabatilisha mkataba kwa mujibu wa yale waliyokubaliana Wanazuoni wa Fiqhi na sheria iliyopitishwa, huku ikizingatiwa katika yote hayo sheria na kanuni zinazotumika kuhusu ushirikishwaji na uwekezaji wa fedha.

Maelezo

Asili ya hukumu za miamala ya kifedha katika Sharia ya Kiislamu ni kwamba imehalalishwa ili kutimiza maslahi ya viumbe na kukidhi mahitaji yao, na hilo linakuwa ndani ya mfumo wa amri na makatazo ya kisheria yanayohakikisha upatikanaji wa haki katika kila upande kupata manufaa yake kwa kufanya biashara na upande mwingine. Kwa hiyo, inashartiwa iepukane na: udanganyifu, utata, dhara madhara, na riba.

Katika miamala inayofanywa na watu, mwanzoni huzingatiwa kutimiza masharti ya mikataba kwa ujumla, kama vile uwezo wa wale wanaofanya mkataba, kupatikana kwa ridhaa kati yao, kutokuwepo kwa utata, na vilevile muamala kuepukana na masharti yaliyokatazwa kisharia, kama ilivyokuja katika Hadithi Tukufu kwamba Mtume (S.A.W) amesema: “Waislamu wanawajibika kutekeleza masharti yao, isipokuwa sharti ambalo linaharamisha halali au sharti ambalo linahalalisha haramu”. Imepokewa na Tirmidhi na akaisahihisha, na Daraqutni na Baihaqi katika Sunan.

Aina ya mkataba wa ushirika ambao umeulizwa hapa ambapo muulizaji anampa mwenza wake kiasi cha fedha, naye mwenza anafanyia kazi fedha hiyo kwa kununua na kuuza bidhaa, ambapo mwenza huyo anapata asilimia 40% ya faida na mwenye mtaji anapata asilimia 60%, unaingia chini ya mkataba wa Mudaraba au Qiradh (ushirika wa mtaji na kazi), ambao unaruhusiwa kisheria.

Waislamu wamefanya miamala kwa kutumia mkataba huu tangu zama za Mtume (S.A.W) hadi wakati wetu bila kupingwa, na idadi ya Maimamu wamenukuu makubaliano juu ya hilo.

 Wanazuoni wa Fiqhi wamekubaliana kwamba mkono wa Mudarib (mwenza anayefanya kazi) katika mali ya Mudaraba ni mkono wa amana. Maana yake ni kwamba mali, ingawa iko mikononi mwake, bado ni mali ya mwenye mtaji, naye amepewa amana juu yake. Ama kwa upande wa matumizi yake, yeye ni wakala wa mwenye mtaji. Akipata faida, anakuwa mshirika katika faida, na ikipoteza mali au kuharibika, hana dhamana (hapigwi faini) juu yake, isipokuwa ikiwa uharibifu wa mali hiyo au hasara iliyotokea inatokana na kukiuka kwake (kutokubaliana) au kuzembea kwake katika kuihifadhi; kwa sababu hiyo ndiyo njia ya amana.

Ama kuhusu hukumu ya kuweka sharti na mwenye mtaji kwa mshirika (Mudarib) (mwenza mfanyakazi) la kutobeba hasara yeyote, basi mwenye mtaji akitaka kuweka sharti kwa mshirika (Mudarib) katika mkataba wa  ushirika Mudaraba la kutobeba hasara yeyote—kwa kudhani inatokea-katika mali ya ushirika Mudaraba, na kwamba mshirika Mudarib ndiye anayebeba hasara hiyo peke yake moja kwa moja, hata kama hakukiuka wala kuzembea katika kuihifadhi mali-kama ilivyo katika mfumo wa suala letu- hakuna tofauti kati ya Wanazuoni wa Fiqhi kwamba sharti hili ni batili, na maana yake ni kwamba hairuhusiwi kuweka sharti hili tangu mwanzo.

Hata hivyo, Wanazuoni wa Fiqhi wametofautiana juu ya uhalali wa mkataba huu pamoja na kuwepo kwa sharti hili. Madhehebu ya Imamu Hanafi na Hanbali wameona kwamba sharti ni batili, lakini mkataba ni halali. Madhehebu ya Imamu Hanafi wameeleza hilo kama wadi'ah (upotevu), ikimaanisha uharibifu au hasara ya sehemu ya mali ya ushirika Mudaraba. Wakati huo huo, Madhehebu ya Imamu Maliki na Shafi wameona kwamba mkataba wa Qiradh au Mudaraba unakuwa batili kwa sharti hili[1].

Na kwa mfumo ule ule waliokwenda nao Madhehebu ya Imamu Malik na Shafi, ndivyo ulivyokuja msimamo wa Sheria ya Kiraia ya Misri katika Kifungu Na. (515- aya ya 1) kwamba: «Ikiwa imekubaliwa kwamba mmoja wa washirika hatachangia katika faida za kampuni au katika hasara zake, basi mkataba wa kampuni unakuwa batili». Hii inaonesha kutokuwa halali kwa sharti la mshirika kutopata hasara, na kwamba mkataba katika hali hii unabatilika, kwani "kutochangia kwa mshirika katika faida au hasara kunaondosha nia ya ushirika, na kutokana na hilo, athari yake haibaki kwa kubatilisha sharti tu, bali inabatilisha mkataba mzima kwa kuzingatia kuwa ni miongoni mwa masharti ya msingi ambayo yanachukuliwa kuwa ni sehemu isiyogawanyika, pia inafaa kwa kila mwenye masalahi kushikamana  nayo na mahakama kuhukumu kwa hukumu hiyo moja kwa moja”  kama ilivyokuja katika rufaa ya Misri kifungu nambari 1902 cha mwaka 63, kikao cha 23/2/2001."

Pamoja na hayo, ni lazima kuzingatia kwamba kutoa au kupokea fedha kwa ajili ya biashara kunapaswa kuzingatia sheria na kanuni zilizopangwa; kwa sababu kuzuia kwa kiongozi (serikali) wigo wa utekelezaji wa mkataba fulani ni miongoni mwa mambo yaliyohalalishwa kisheria. Na asili katika hilo ni kuzingatia maslahi na kuzuia uharibifu. Kizuizi hiki huondoa utata na kufanya jambo kuwa halali ndani ya mipaka ya kizuizi hiki, na utekelezaji wake wakati huo unakuwa wajibu.

Sheria ya Misri imekataza watu binafsi kukusanya fedha kutoka kwa wengine kwa ajili ya uwekezaji au uajiri wake, ambapo Kifungu cha Kwanza cha Sheria Na. 146 ya mwaka 1988 kimeeleza kwamba: «Hairuhusiwi kwa isiyokuwa kampuni ya hisa inayotoa hisa zake kwa usajili wa umma na iliyosajiliwa katika daftari liliyoandaliwa na Mamlaka kwa ajili ya hilo, na kupokea fedha kutoka kwa raia kwa sarafu yoyote, kwa njia yeyote, na chini ya jina lolote kwa ajili ya kuzitumia au kuwekezwa au ushirika, iwe lengo hili ni dhahiri au limefichwa. Pia inakatazwa kwa isiyokuwa kampuni kutoa wito kwa umma kwa njia yeyote ile ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa ajili ya usajili wa umma au kukusanya fedha hizi kwa ajili ya kuzitumia, kuwekezwa au ushirika.»

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Asili ya hukumu za miamala ya kifedha katika Sharia ya Kiislamu ni kwamba zimehalalishwa ili kutimiza maslahi ya waja na kukidhi mahitaji yao. Miamala inayofanywa kati ya watu huchungwa ndani yake kwanza, kutimiza masharti ya mikataba kwa ujumla, kutokana na uwezo wa wale wanaofanya mkataba, kupatikana kwa ridhaa kati yao, kutokuwepo kwa utata, na vilevile muamala kuepuka masharti yaliyokatazwa kisheria.

Kutoa au kupokea fedha kwa ajili ya biashara kunapaswa kuzingatia sheria na kanuni zilizopangwa; kwa sababu kiongozi kuweka vigezo katika utekelezaji wa mkataba fulani ni miongoni mwa mambo yaliyohalalishwa kisheria.

Sheria ya Misri imekataza watu binafsi kukusanya fedha kutoka kwa wengine kwa ajili ya uwekezaji au kuzifanyia kazi.

Raia wanapaswa kuzingatia umuhimu wa hatari ya watu binafsi kukusanya fedha kutoka kwa wengine kwa ajili ya uwekezaji au kuzifanyia kazi, na kuongeza uelewa wa kufanya kazi chini ya mwavuli wa taasisi na kampuni rasmi za kifedha zilizoidhinishwa, ambazo ziko chini ya usimamizi wa serikali na ulinzi unaohitajika kwa wale wanaofanya miamala katika hilo.

 

[1] “Bada’i’ al-Sana’i’” (6/80, chapa ya Dar al-Kutub al-‘Ilmiyya), “Matalib Uli al-Nuha” (3/521, toleo la Al-Maktab al-Islami), “Al-Sharh al-Kabir” (3/519-520, Daraja la al-Fikr-e-Hadition al-Fikr (7/332, chapa ya Dar al-Kutub al-‘Ilmiyya).

Share this:

Related Fatwas