Wizi kati ya ndugu
Question
Je, uhusiano wa mwizi na aliyeibiwa unaweza kuathiri utekelezaji wa adhabu ya wizi?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Asili katika sheria ya Kiislamu ni kwamba kuchukua mali ya mtu mwingine pasipo haki ni haramu kisheria, maana mali ya mtu ikichukuliwa bila ya ridhaa yake si halali, kwani Mtume S.A.W. alisema: “Hakika damu ya kila Mwislamu na mali yake na heshima yake ni haramu juu yenu”. Wizi ni aina mojawapo ya kuchukua kitu bila ya haki, na hadithi nyingi za Mtume S.A.W. zimekataza wizi, kama ilivyokuja katika kauli yake Mtume S.A.W “Mwenyezi Mungu amemlaani mwizi anayeiba yai, mkono wake unakatwa”. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaja adhabu ya wizi katika kitabu chake kitukufu nayo ni kukata mkono wa mwizi ambapo amesema: {Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao} [AL MAIDAH: 38].
Dalili za kuharamisha wizi na kukata mkono wa mwizi zinajumuisha wizi kati ya ndugu na wizi baina ya watu wengine, lakini wanachuoni wametoa maelezo marefu kuhusu wizi unaojitokeza baina ya wawili. Kwa mfano mtu kamwibia baba yake au babu yake au kuna undugu (kati wa mwizi na aliyeibiwa) wa kizazi au ndoa.
Ikiwa mtu kamwibia baba yake au babu yake (au jamaa yake upande wa baba) au mama yake au bibi yake (au jamaa yake upande wa mama), na mali akaichukuwa kwa njia ya wizi ulioharamishwa, tena masharti ya wizi yakatimia nayo ni kuchukua mali kwa njia ya kuficha na kutimia kiwango basi wanachuoni wamekubaliana kwamba adhabu ya wizi haitatekelezwa juu ya mwizi huyu (mwizi ndugu) hata kama alichokichukua kimo ndani ya kiwango cha matumizi ya lazima au laa. Mwizi huyu anapata dhambi akichukua mali ya mzazi wake bila ya haja. Aidha, ikiwa mzazi kamwibia mtoto wake wa kiume au wa kike, wanachuoni wanasema adhabu ya wizi haitatekelezwa juu yake isipokuwa upande wa pili wa wanachuoni wa madhehebu ya Malikiya wanasema uhusiano wa udugu hauzuii kutekelezwa adhabu ya wizi kwa mtu huyu. Kwahiyo aliyemwibia mwanawe adhabu ya wizi itatekelezwa juu yake.
Kwanza: wanachuoni wanazitegemea dalili zinazothibitisha kwamba baba ana haki katika mali ya mtoto wake, naye anaweza kuchukua mali ya mtoto,mjukuu na kuendelea, kwani kuchukua mali zao ni kama kuchukua mali yake mwenyewe. Miongoni mwa dalili hizi ni kauli ya Mtume S.A.W.: “Hakika chakula kizuri zaidi ni kile ambacho mtu alikipata kwa chumo lake, na anachokipata mtoto kinatokana na mzazi” [imepokelewa na Abu Dawuud na Al Tirmidhi na Al Nassa’iy], na katika riwaya nyingine: “Kuleni katika chumo la watoto wenu”.
Pia uhusiano wa karibu wa baba na mtoto wake daima unakuwa mwepesi katika jambo la kuchukua mali, maana kila mmoja anakuwa katika nafasi ya mwenzake, kwa hiyo ushahidi(kwa mfano ushahidi mahakamani) wa wenyewe kwa wenyewe unakatazwa [Rejea: Bada’i Al Sana’i 7/71, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya & Fat-h Al Qadeer 5/380:381, Ch. Dar Al Fikr & Sharh Al Kharshiy Aly Khalili, 8/96, Ch. Dar Al Fikr & Minah Al Jalili, 5/419, Ch. DarAl Fikr, Hashiat Al Dusookiy juu ya Al Sharh Al Kabiir, 4/337, Ch. Dar Al Fikr & Tohfat Al Muhtaj 9/130, Ch. Ihiyaa’ Al Turath Al Arabiy & Mughniy Al Muhtaj, 5/471, Ch. Dar Al Kutoob Al Elmiya & Al Mughniy, 9/115, ch. Dar Al Fikr & Al Insaf 10/278, Ch. Ihiyaa’ Al Turath Al Arabiy).
Pili: wanachuoni wamechukua dalili kutoka kauli ya Mtume S.A.W. alipomwambia Hind bint Utba: “Chukua kwa wema (kutoka mali ya mumeo) kiasi kinachokutosheleza wewe na mtoto wako”.
Neno lake Mtume S.A.W. “Chukua” lina maana ya ruhusa kuchukua kilichozoeleka “Kwa wema” endapo mwenye jukumu (mfano mume) atajizuia kutoa matumizi au atafanya ubahili, akifanya hivi anakuwa ni dhalimu amezuia haki ya kisheria iliyo wajibu nayo ni kutoa matumizi yanayohitajika ili kukidhi mahitaji na mambo ya lazima. Matumizi ni kama deni ,haya mawili ni haki ambayo ni lazima itekelezwe. Anayedai inajuzu kwake kuchukua kiwango cha haki endapo mdaiwa hataki kulipa, hali hii haizingatiwi ni uhalifu kwa sababu anayedai amechukua haki yake.
Imam Nawawiy alisema: “Tunafahamu kutokana na hadithi ya Hind kwamba yoyote mwenye haki (mali) yake kutoka kwa mtu mwingine ambaye hataki kumpa basi inajuzu endapo ataweza kuchukua haki (mali) yake anayostahiki bila ya idhini ya huyo mtu mwingine” [Sharh Sahih Muslim, 12/7, Ch. Ihiyaa’ Al Turath Al Arabiy].
Maana ya kutothibiti kosa la wizi katika hali ya baba kumuibia mwanae au mtoto kumuibia baba yake (upande wa kuumeni kuchukua mali kutoka tawi lake, na tawi kuchukua mali kutoka upande wa kuumeni wake) linasababisha kuwepo shaka, na adhabu huwa hazitolewi kama kuna shaka yoyote.
Ama, kama kuna udugu na ujamaa kati ya mwizi na aliyeibiwa, basi wanachuoni wengi wa madhehebu ya Maaliki, Shafiy na Hanbaliy wameona kwamba wizi kati ya ndugu wa nasaba wenyewe kwa wenyewe si jambo la shaka linalozuia utekelezaji wa adhabu ya kuiba, kwa hiyo walilazimisha kukata mkono wa aliyeiba mali ya kaka yake, dada yake, ami yake, shangazi yake, ndugu za mama yake na watoto wao, mama aliyemnyonyesha na dada yake wa kunyonya, mama yake wa kambo, na baba yake wa kambo, mtoto wa mke wake au mama yake. Na hapa walibainisha sababu ya hukumu hii kwamba ushahidi (kwa mfano ushahidi mahakamani) wa wenyewe kwa wenyewe unakubalika, kwa hivyo uhusiano ulio kati yao hautakuwa na athari katika kosa la wizi.
Madhehebu ya Hanafiy yamepinga kauli hiyo kwa kusema: Ni marufuku kukata mkono wa mwizi ndugu wa damu (mwenye sifa ya Maharim ambaye ndugu ni haramu kumuoa au kuolewa naye kisheria); kwani kuingia kwao nyumbani wenyewe kwa wenyewe bila ya idhini kutakuwa ni jambo la shaka linalosababisha kuondosha adhabu, lakini ikiwa mwizi si mwenye udugu wa damu (hana sifa ya Maharim; wanaweza kuoana kisheria) basi adhabu ya wizi itatekelezwa juu yake; kwani wa aina hii wanakuwa hawana haki ya kuingia katika nyumba zao wenyewe kwa wenyewe bila ya idhini. Pia wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy wamehitalifiana baina yao katika suala la wizi wa jamaa wasio na udugu wa damu (wenye sifa za Maharim; wanaweza kuoana kisheria) kama mama na dada wa kunyonya, ambapo Abu Hanifa na Muhammad wanasema adhabu ya wizi juu ya mwizi huyo inatekelezwa, ama Abu Yusuf anasema haitekezwi adhabu kwa mwizi huyo. [Rejea: Bada’i Al Sana’i 7/75 & Fat-h Al Qadeer 5/380:381].
Ama uhusiano wa kindoa ukiwa bado upo baina ya mwizi na aliyeibiwa, kama mke akichukua kutoka mali ya mumewe kiasi cha matumizi ya lazima, basi kwa mujibu wa makubaliano ya wanachuoni halitakuwa kosa la wizi ulioharamishwa, na dalili yao ni hadithi ya Hind bint Utba “Chukua kwa wema (kutoka mali ya mumeo) kiasi kinachokutosheleza wewe na mtoto wako”.
Ama mke akichukua kutoka mali ya mumewe kiasi cha ziada cha matumizi yake, madhehebu ya Hanafiy yanaona hakuna kukata mkono wa yoyote akiwa mke au mume, na hayo ni maoni ya madhehebu ya Hanbaliy; kwani wana ndoa wawili kawaida hawana pingamizi katika mali, tena wanakuwa na haki ya kurithiana bila ya kunyimwa.
Lakini madhehebu ya Malikiy na Shafiy yamelazimisha kutekeleza adhabu ya wizi wa aina hiyo, kwa kutokuwepo jambo la shaka [Rejea: Fat-h Al Qadeer 5/382 & Sharh Al Kharshiy Aly Khalili, 8/100, Ch. Dar Al Fikr & Mughniy Al Muhtaj, 5/473 & Al Insaf 10/280 Kashf Al Kinaa’, 6/142, Ch. Dar Al Fikr].
Kwa hiyo, uhusiano wa karibu wa damu (udugu wa nasaba) na uhusiano wa kindoa unapelekea kutotekelezwa adhabu ya wizi ingawa ni kosa na ni dhambi. Ama wizi unaotokea baina ya watu wasiokuwa ndugu na hawana ujamaa basi hauathiri utekelezwaji wa adhabu ya wizi.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi.