Uislamu na Msimamo wake katika Elim...

Egypt's Dar Al-Ifta

Uislamu na Msimamo wake katika Elimu ya Kisasa (Sayansi).

Question

Elimu ya kisasa kama tuonavyo hivi sasa, inafichua siri nyingi za ulimwengu ambazo hazijawahi kumpitikia akilini mtu yoyote kati ya waliotutangulia. Sababu ya haya ni mfumo wa elimu hii unaofuatwa kikaumilifu. Je Uislamu unaafikiana na elimu hii kiroho na kimfumo? Na dalili gani ya kuafikiana huko?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
1 - Kama utaangalia kwa kina kauli ya marehemu Profesa Abulwafa Al-Ghonemy Al-Taftazaniy mmoja wa wasomi wa kileo waliobobea katika elimu ya falsafa ya Kiislamu basi utakuta kuwa sayansi ni kitu chenye thamani kubwa. Mtaalamu anapata maelezo yake kwa mujibu wa kanuni maalumu ambazo hujulikana kwa jina la “ misingi ya njia ya kisayansi”, sayansi si maelezo tu bali pia ni njia au mfumo wa kupata maelezo. Kwa hali hii, sayansi ni kitu cha thamani sana. Jamii ikiamini kuwa sayansi ndio mtindo wa maisha basi jamii hii itafanikisha maendeleo ya kitamaduni. Na kama haijaamini basi wanajamii watakuwa ni wahanga wa wa mawazo potofu na ngano za kale bila ya maendeleo ya hali na mali.
2 - Elimu ina thamani kubwa katika Uislamu, elimu ndio sababu ya kufadhilisha baina ya watu katika jamii, kwasababu elimu ndio msingi wa kila kazi yenye mafanikio au tabia njema na uchamungu -Uchamungu ni kati ya misingi ya kufadhilisha baina ya watu-. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Mwenyezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu; na waliopewa elimu watapata daraja zaidi. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda yote}. [AL MUJADAILAH :11]. Na anasema:{Sema: “Je, wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua?”} [AZ ZUMAR: 9].
3 - Uislamu unawatanabahisha watu kuwa elimu haina kiwango maalumu wala mpaka, hapo zamani watu waliitakidi kwamba elimu ina kikomo. Wataalamu wa mfumo wa utafiti wa kisasa wanathibitisha kuwa matokeo ya sayansi ni yenye kubadilika. Huu ni uthibitisho kwamba maendeleo ya sayansi yanaendelea. Allah S.W anasema: {Na sema (uombe): “Mola wangu! Nizidishie elimu.”} [TAHA: 114]. Ni wajibu kwa mwislamu kuzidisha katika kutafuta elimu siku baada ya siku, kwani elimu haina mwisho.
4 - Katika kuonesha elimu katika Uislamu imepewa umuhimu mkubwa sana ni kwamba amri ya kwanza katika Quraani kuteremshiwa Mtume S.A.W. ilikuwa ni kauli ya Allah S.W. {Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanadamu kutokana na pande la damu. Soma, na Mola wako ni mkarimu sana. Ambaye aliyefunza kwa kalamu. Amemfunza mwanadamu yale asiyoyajua.}. [AL ALAQ: 1-5]. Kutokana na umuhimu wa elimu, Mtume S.A.W. aliwataka mateka wa vita vya Badr wanaojua kusoma na kuandika, kila mmoja awafundishe watoto kumi wa Kiislamu katika mji wa Madina,kufundisha huku kuwe ni fidia ya kuachiliwa huru.
5 - Elimu katika Uislamu ni lazima iwe na manufaa. Mtume S.A.W. katika dua yake, alikuwa anajikinga kutokana na shari ya elimu isiyofaa. Alikuwa anaomba hivi; “Ewe Mola najilinda kwako kutokana na moyo usionyenyekea, na dua isiyosikilizwa, na nafsi isiotosheka na elimu isiyo na manufaa”.
Na kusudio la elimu yenye manufaa katika Uislamu ni ile anayonufaika nayo mtu na jamii. Na imepokelewa kutoka kwa Khalifa Omar bin Abdul-aziz kwamba alimuandikia Abu Bakar bin Hazm hivi; “Angalia mazungumzo ya Mtume S.A.W. na uyaandike, mimi ninachelea kutoweka kwa athari ya elimu na kupotea kwa wanachuoni. Na wanachuoni waieneze Elimu na kuifanyia kazi ipasavyo mpaka akaelimika asie na elimu. Kwani elimu huangamia kwa kufichwa”.
6 - Elimu katika Uislamu ni jambo lenye thamani kubwa sana, na makubaliano kati ya elimu na Uislamu yako wazi, na viwili hivi havipingani. Uislamu pamoja na elimu ni roho na mfumo, na Quraani inapozitaka akili kugundua maumbile ya viumbe basi bila shaka inawalingania wazi wazi katika elimu kwa maana ambayo inafahamika katika enzi zetu.
7 - Quraani tukufu inahimiza elimu katika kauli yake Allah S.W,: {Allah ambaye anatuma pepo kisha zikatimua mawingu, kisha akayatawanya mbinguni atakavyo, na akajaalia mapande mapande, basi utaona matone ya mvua yanatoka baina yake. Anapoifikisha kwayo amtakaye kati ya waja wake, mara hao wanafurahia.}. [AR RUM: 48]. Na kauli yake: {Je, huoni kwamba Allah anasukuma mawingu, kisha anayaambatisha baina yake, kisha anayafanya matabaka ya mirundi? Basi utaona matone ya mvua yanatoka katikati yake. Na anateremsha kutoka mbinguni katika majabali (ya mawingu); mvua ya mawe, akamsibisha nayo amtakaye, na akamuepushia amtakaye. Hukaribia mwako wa umeme wake kupofua macho.}. [AN NUR: 43]. Katika aya mbili hizi, Quraani tukufu inatusukuma katika mchakato wa kutafakari katika kuunganisha matukio ya kimaumbile kwa sababu zake halisia si kiupumbavu, kwani mawingu, mvua na umwesa kutokea kwake kunafungamana na vitendea kazi maalumu kama nyuzi joto, maji ya bahari n.k
9 - Aya za Quraani tukufu zinazohimiza akili ya mwenye kufikiria kufichua kanuni za maumbile zimejaa tele, pia aya hizo ni dalili tosha kwamba ulimwengu huu haukuumbwa kuwa batili au bure, bali umeumbwa kwa lengo maalumu.
10 - Quraani tukufu sio tu inawafikiana na elimu ya kisasa bali Quraani imeitangulia elimu hii. Ndani ya Quraani kuna aya nyingi sana za miujiza ya kisayansi, na wanasayansi kila uchao wanavumbua siri za miujiza yake ya kisayansi. Na watafiti wengi wamezungumzia muujiza wa Quraani kwa tafiti na mapana kwa marefu.
11- Na tunashangaa sana tunapooona mfano wa Arnest Renan aliyesema “Uislamu unapinga elimu na falsafa, kwahiyo unakwamisha maendeleo na mafanikio”. Na fikra hii potofu bado ipo katika nafsi za watu wengi.
12- Uislamu umeanza kwa elimu, na umethibitsha kwamba uumbaji wa binadamu umenza kwa elimu. Allah s.w anasema: {Na Akamfunza Adam majina ya vitu vyote}. [AL BAQARA: 31]. Na aya ya kwanza kumteremkia Mtume S.A.W. ni kauli yake Allah S.W.: {Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba}. [AL ALAQ: 1]. Na dalili kubwa inayothibitisha daraja ya elimu katika Uilsamu ni kauli yake Allah S.W: {Allah ameshuhudia kwamba hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki ila yeye; na Malaika, na wenye elimu wote wameshuhudia kwamba yeye ni mwenye kusimamisha (uumbaji Wake) kwa uadilifu. Hapana Mola ila yeye mwenye enzi ya nguvu asiyeshindika daima na mwenye hekima).}. [AALI IMRAN: 18]. Na Mwenyezi Mungu ameambatanisha shahada yake na shahada ya Malaika na shahada wa Wataalamu. Na wanashuhudia kwa kipi? Wanashuhudia upweke wake, usimamizi wake,uadilifu nk.
13 - Na miongoni mwa sifa za Quraani tukufu zilizowavutia wataalamu, wanasayansi na watafiti, ni kuisifu akili na kutaka itumike kwa lengo la kuyafikia mambo yatakayomnufaisha mwanadamu katika maisha yake. Kuna zaidi ya aya 350 ndani ya Quraani tukufu zinaashiria akili, mnyambuliko na maana zake mbalimbali. Na Quraani tukufu inapozungumzia akili katika aya zake, haimaanishi maana fupi au ya juu juu na wala haizungumzii akili tambuzi au ile yenye kuyadiriki mambo au ile yenye kazi ya uzingativu wa kweli na yenye kupitisha hukumu zilizo sahihi, isipokuwa Quraani huzungumzia na hukusanya kila kitu kinachoupanua ubongo wa binadamu katika kukizingatia kitu au wadhifa maalumu. Akili inayosemeshwa na Uislamu ni akili ambayo inalinda dhamira, inaelewa ukweli, inapambanua vitu, inasawazisha yanayopingana, inazingatia mwisho wa mambo na matokeo na inapanga na inaboresha uelewa na mtazamo. Kutokana na hali hii, wanasayansi waislamu wamezama katika elimu za maisha, ustaarabu wa kibinadamu na akili ya kivitendo, na wanasayansi hawa wanaiona dunia ni maudhui ya kudurusiwa, kufanyiwa utafiti na kufaidika nayo.
14 - Uislamu unapinga akili potofu na uzushi kuhusu matukio ya kilimwengu. Na ushahidi madhubuti juu ya hayo ni hadithi sahihi kutoka kwa Mughiyra bin Shuaba alisema: “Jua lilipatwa siku aliyokufa Ibrahim (mtoto wa Mtume S.A.W.), watu wakasema; jua limepatwa kwa sababu ya kifo cha Ibrahim. Mtume s.a.w akasema: Jua na mwezi ni dalili kati ya dalili za Allah, havipatwi viwili hivi kwa kifo cha mtu wala kwa uhai wake, mtakapoona jua na mwezi yamepatwa basi mwombeni Allah na salini mpaka hali ya kupatwa iondoke”. Ameipokea Bukhari na Muslim.
15 - Bwana wetu mkweli na mwaminifu Mtume S.A.W. ameidhinisha msingi wa kisayansi utakaobakia milele wenye kuongoza kuelekea njia ya uongofu. Wakati wa uongozi wa Omar bin Khattab kuna tukio ambalo wanahistoria wengi wamelitaja nalo ni maji ya Mto kutotiririka, enzi hizo wamisri waliitakidi kwamba maji ya Nile hayateremki isipokuwa baada ya mwanamke mzuri kutupwa ndani ya mto mpaka akazama na kufa. Kiongozi wa Misri akamwandikia barua Omar bin Khattab inayoeleza hali hiyo. Omar akajibu barua kwa kusema “Ikiwa maji ya Nile yanapita yenyewe basi hatuna haja nayo, na kama yanapita kutoka kwa Allah basi ewe Mola tubarikie”, basi maji ya Nile yakaendelea kupita, na mila ile potofu ikatoweka. Kutokana na haya, waislamu wameamua kuachana na mambo ya kizushi yasiyokuwa na dalili za kielimu wala kiakili katika maisha.
16 - Uislamu ni dini adhimu inayolingania elimu na kazi mwanzo hadi mwisho. Na ustaarabu wa kwanza kujali elimu na kuitukuza ulikuwa ni ustaarabu wa Kiislamu. Na dini ya kwanza kulingania elimu ni dini ya Kiislamu. Na hili ni jambo ambalo analifahamu vyema kila mwenye kujua baadhi ya aya za Quraani na hadithi zinazoeleza maswala ya kielimu na kisayansi.
17 - Elimu za waislamu na ustaarabu wao zimejengeka kwa misingi ya kiakili na kielimu, na kwa misingi hii ndio tunatakikana turudi na tuimiliki, na iwe chombo chetu kikuu ambacho tunakitumia katika kukabiliana na matatizo yetu na mahitaji yetu.
18 - Mfumo wa kilimwengu wa kisasa wa nchi za Magharibi katika muono wake juu ya dini ni kwamba dini ni mkusanyiko wa ngano za kale, mambo yaliyofichikana, na njozi zinazohusiana na nafsi za watu kwa ujumla. Mfumo wa kilimwengu wa nchi za Magharibi umeujenga muono wake huu katika mazingira maalumu ya kihistoria kwenye ustaarabu wa kimagharibi wa kati. Na kila walichokizungumzia wataalamu wa Magharibi wa mambo ya kijamii, kinafsi na kimaadili juu ya dini ni hali halisi iliyokuwa ikijulikana tu katika jamii ya kimagharibi kwa jina la dini. Lakini haikumaanisha kuwa ni dini ya kweli inayoridhiwa na Mwenyezi Mungu kwa viumbe vyake na namna alivyowaumba. Na lau kama ingelikuwa kama mfumo huo wa kilimwengu ujitakiavyo, kwa maana halisi ya kisayansi basi ingesimamia kwenye mipaka ya ukweli na akili, na pia ingefanya uadilifu katika ufahamu wa dini iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, na sio kwa kuutathmini mfumo wake kwa kutumia matamanio ya kibinadamu kwa lengo la kuivamia dini kwa njia yoyoe ile, iwe kwa haki au batili.
19 - Swala la kutenganisha dini na dola kama unavyotaka mfumo wa kidunia(kisekula) wa nchi za Magharibi ni swala ambalo linatokana na msuguano kwao wao kati ya dini na elimu, mfumo wa kiraia na maendeleo, na swala la kutenganisha dini na dola linatokana na mazingira ya kihistoria na ustaarabu wa fikra za kimagharibi.
20 - Dini ya Kiislamu kwa ustaarabu wake ambao hata siku moja haujapinga elimu na mfumo wa kiraia, katika dini hii swala la kutenganisha dini na dola halina kisingizio. Ndani ya Uislamu hakuna haja ya kifikra, kistaarabu, kihistoria na kimfumo ambayo inatufikisha katika matokeo ambayo yamepatikana na jaribio la kimagharibi kutokana na elimu kugongana na utamaduni wake ulioenea.
21 - Mambo yote ya kidini, kistaarabu, kifikra na kitamaduni yanaunga mkono kikamilifu elimu, yanaikumbatia, yanaihimiza na kwa kupitia elimu waja wanamuabudu Allah S.W. Sasa inakuaje sisi kama waislamu tunakaa mbali na sayansi na maendeleo ya kweli ya kielimu!
22 - Kujiweka mbali huku na elimu hakutokani na misingi ya kifikra ya dini ya Kiislamu na utamaduni wake, bali sisi wenyewe tumejitenga na misingi hiyo na hatuifanyii kazi, kwahiyo sisi wenyewe ndio wenye mapungufu. Hakika maendeleo kwetu sisi kama Umma wa Kiislamu ni kwa ufahamu sahihi, kamili na wa kina pamoja na elimu sahihi na ya kudumu ya dini ya Kiislamu kwa misingi yake na fikra zake za kielimu.
23 - Vitendo vibaya, ufahamu wenye upungufu na utendaji wenye kasoro ndio sababu kuu ya matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu katika zama hizi.
24 - Swala la elimu (sayansi) na mfumo wa kielimu katika Uislamu tumelizungumzia katika maudhui nyingi na tumefafanua sifa za kufikiria katika upande wa elimu na mfumo wake katika fikra ya Kiislamu.
MAREJEO:
- Profesa Abo-Al-Wafa Al-Ghonemiy Al-Taftazaniy (Mwalimu wa Falsafa ya Kiislamu – Chuo Kikuu cha Cairo), kitabu “Al-insanu walkawnu fil Islam”, Cairo: Daru Thaqafa linnashri watawziy, 1995, (uku 21 – 23 na 60 - 63).
- Nasrudiyn Mesbah Al-Qadhy, kitabu “Minhaj Al-Islam fiy muwaajahatu tahaddiyaat hadhaaratu muasirrah”, Cairo: Dar Al-Fekr Al-Arabiy, chapa ya 1, mwaka 1423H / 2002, (uku 220 – 248).
- Ahmad Abd Al-Reheem Al-Sayeh, kitabu “Falsafatu hadhaaratu Islaamiyya”, Cairo: Baraza kuu la Mambo ya Kiislamu, 1410 H / 1989 B.K, (ku 102 – 114).
 

Share this:

Related Fatwas