Je, Bidaa (uzushi) Inafungamana na Ibada Tu?
Question
Je, bidaa inafungamana na ibada tu, ama inaingia katika Mila na Miamala?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Neno bidaa katika lugha ya Kiarabu limenyambulika kutoka kitenzi bada'a; maana yake ni ameanzisha au amezusha kitu fulani. Na pia ina maana ya kitu cha kwanza au mtu wa mwanzo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Sema: Mimi si kiroja (mpya) katika mitume} [AL AHQAF 9]: Maana; mimi sikuwa Mtume wa mwanzo ambaye Mweyezi Mungu alimtuma kwa watu, bali aliwatuma Mitume wengine zamani. Basi, kwa sababu gani mnanikanusha ilhali mimi ni kama Mitume waliotangulia?. Na katika kamusi ya Lisaan Al-'Arab: Almubtadi'; maana yake ni mvumbuzi, ni mtu aliyeleta kitu ambacho hakijakuwepo, bali yeye ndiye aliyekianzisha. Na miongoni mwa mnyambuliko wa neno bada'a ni ibtada'a ambalo lina maana: mtu aliyefanya bidaa kama katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na uruhubani (Utawa: Wanaume kutooa na Wanawake kutoolewa) wameubuni (wenyewe) Sisi hatukuwaandikia hayo. (Wenyewe walifanya haya) ili kuitaka radhi ya Mwenyezi Mungu} [AL HADYD27], na kati ya mnyambuliko wa neno bada'a ni albadii' ambalo ni miongoni mwa majina ya Allah S.W, na maana yake ni: Muumba kila kitu pasina ruwaza. [Lisaan Al-'Arab 8/6, Ch. Dar Sadir].
Ama neno bidaa katika istilahi maana yake ni: Kuzusha jambo jipya ambalo halikuwapo zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.. Na bidaa imegawanyika sehemu mbili: bidaa nzuri na bidaa mbaya [Tahdhiib Al Asmaa wa Al Lughaat na Al Nawawiy:1/22, Ch. Al Muniriyah].
Sheikh Izz Al Deen Ibn Abdulsalaam anasema: “Bidaa maana yake ni kutenda tendo ambalo halikuwepo katika zama za Mtume wa Mweyezi Mungu S.A.W..” [Kawa'id Al Ahkam na Izz Al Deen Ibn Abdussalam: 2/172, Ch. Al Istikamah].
Maana hii inaingiza Bidaa katika mila na miamala. Sheikh Izz Al Deen Ibn Abdulsalaam anasema: "kwa kuwa bidaa inaingia katika ibada, miamala, aina nyingine za maisha n.k basi inagawanyika katika sehemu tano, nazo ni: Haramu, Wajibu Sunna, Makruhu (yenye karaha), na Mubaha (halali)". Na kwa ajili ya kuelewa kila aina lazima tuihusishe na misingi ya sheria ya kiislamu. Iwapo bidaa itaingia katika misingi ya kuwajibika basi bidaa hii ni wajibu, na ikiingia katika misingi ya haramu basi hii itakuwa haramu, na ikiingia katika misingi ya kupendeza basi itakuwa Sunna, na ikiingia katika misingi ya kuchukiza basi itakuwa Makruhu (yenye karaha), na ikiingia katika misingi ya ruhusa basi itakuwa Mubaha (halali). Na bidaa ya wajibu ina mifano, na moja ya mifano hii ni kusoma elimu ya sarufi ya lugha ya Kiarabu ambayo kwayo yanafahamika maneno ya Mwenyezi Mungu na maneno ya Mtume S.A.W., na hii ni wajibu. Kwani kuhifadhi sheria ya Kiislamu ni wajibu, na haiwezekani kufanya hivyo isipokuwa kwa kujua elimu ya sarufi ya lugha ya Kiarabu, na jambo lolote la wajibu haliwezi kufanyika isipokuwa kwa jambo jingine basi jambo hilo jingine huzingatiwa kuwa ni wajibu. Na bidaa ya haramu ina mifano, na kati ya mifano hii ni madhehebu ya Al Qadriyya, Al Jabriyya, Al Murjia, Al Mujassima. Na kuwajibu hawa kwa njia njema ni bidaa ya wajibu. Na bidaa ya Sunna ina mifano kama kuanzisha ngome kwa ajili kujihami dhidi ya maadui, kuanzisha shule, na kujenga mahodhi kwa ajili kuweka akiba maji. Na pia kila jambo jema ambalo halikuwepo katika zama za mwanzo za Kiislamu kama sala ya Tarawehe, maneno mazuri ya Al Tasawuf, na maneno yanayohusu mjadala katika mikusanyiko kwa ajili ya kutoa dalili zinazohusu masuala mbalimbali iwapo kufanya hivyo kutakusudiwa Mwenyezi Mungu. Na bidaa inayochukiza mifano yake ni kama ifuatavyo: kuremba misikiti, kupamba misahafu, kutia sauti nzuri Quraani kwa namna ambayo inabadilisha maneno ya Quraani kutoka hali yake ya Kiarabu kwani kilicho sahihi ni kwamba bidaa hii ni haramu. Na bidaa ambayo ni Mubaha mifano yake ni kama ifuatavyo: kupeana mikono nyakati za asubuhi na alaasiri, kula vyakula vinono na vinywaji vizuri, kuwa na mavazi na makazi mazuri, kuvaa mavazi ya watu wa dini na kupanua mikono ya mavazi kama vile kanzu. Baadhi ya watu wanaweza kutofautiana kuhusu hayo na wakayafanya bidaa inayochukiza, na wanachuoni wengine wakayafanya ni sunna ambazo zilifanywa wakati wa Mtume S.A.W. na baada yake kama vile kusema (Audhu billahi mina alshaytani alrajiim) na (Bismillah) katika Sala” [Kawaid Al Ahkam na Izz Al Diin Ibn Abdulsalaam, 4/202-205, Ch. Aalam Al Kutub]. Na Alqirqfiy alimfuata katika mgawanyiko huu katika kitabu chake kilichoitwa “Alfuruq”.
Ibn Abdeen katika maelezo yake anagawanya bidaa katika aina tano ambazo zinahusu ibada na mila, anasema: “Bidaa ni aina tano: Haramu, Wajibu kama vile kuweka dalili ili kuwajibu watu wa makundi yaliyopotea, na kujifunza sarufi ya lugha ili kufahamu kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume S.A.W.. Na bidaa ya Sunna (inayopendeza) ni kama kuanzisha ngome kwa ajili ya kujihami dhidi ya maadui, kuanzisha shule, na kila jambo zuri ambalo halikuwepo katika zama za mwanzo za Mtume Muhammad S.A.W.. Na bidaa inayochukiza kama vile kupamba misikiti. Na bidaa ya mubaha (inayoruhusiwa) ni kama ulaji wa vyakula vinono, vinywaji, na mavazi” [Rad Al Muhtaar, 1/560, Ch. Dar Alfikr].
Na Al Manawi katika kitabu chake “Faid Alkadiir” amegawanya bidaa aina mbili: bidaa nzuri na bidaa mbaya, akasema: “Bidaa kama ilivyosemwa katika kamusi: ni kitu kilichozushwa katika dini baada ya dini kukamilika, na kile kilichozushwa baada ya Mtume S.A.W. miongoni mwa mambo ya matamanio. Na wengine wanasema bidaa ni jina la kitu kilichozushwa, kisha baada ya hapo kitu hicho kikawa kinatumika zaidi katika masuala ya kisheria ya Kiislamu na kinakwenda kinyume na misingi ya Ahlu Sunna Wa Aljamaa katika masuala ya imani, na hiyo ndiyo maana inayokusudiwa kwa neno bidaa mbaya, kwa sababu limetajawa katika mazingira ya kuonya na kuaibisha. Ama kitu kipya ambacho kinakubaliwa na akili na hakipingi misingi ya kisheria basi kinazingatiwa kwamba ni bidaa nzuri.” [Faid Al Qadeer Sharhu Al Jamii Al Sagheer, Al Manawi, 1/72, Ch. Al Maktaba Al Tujaria Al Kubra].
Naye Al Imam Al Shafiy amegawanya bidaa katika sehemu mbili kuu ambayo ndani yake imeingia ibada na mila. Al Baihakiy alipokea akasema: “Al Shafii R.A.: vilivyozushwa ni aina mbili. Aina ya kwanza ni kile kilichozushwa na kinakwenda kinyume na kitabu cha Mwenyezi Mungu Myukufu, Sunna, na yale yaliyopokelewa kutoka hadithi za Mtume, maneno ya masahaba na wafuasi wa masahaba, na yale waliyokubaliana nayo wanachuoni wote. Aina hii ni bidaa ya upotovu. Na ya pili ni kile kilichozushwa kutoka mambo mazuri. Hii inazingatiwa ni bidaa siyo mbaya. Na Omar R.A. alisema kuhusu kusali sala ya Tarawehe kwa jamaa wakati wa mwezi wa Ramadhani: “Hii ni bidaa iliyo nzuri”. Al Shafiy anamaanisha jambo hilo halikuwepo zamani [Al Madkhal Ilaa Al Sunan Al Kubra, 1/206, Ch. Dar Al Khulafaa Lilkitaab Al Islami].
Al Tartushi wa madhehebu ya Imam Malik anasema: “Asili ya neno bidaa maana yake ni kugundua, nacho ni kitu ambacho kinazuka bila kuwa na asili hapo kabla, na hakina mfano, na hakijazoeleka mfanowe. Kwa mfano tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu: {(Yeye ndiye) Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza} [Al BAQARAH 117], na kauli yake Mtukufu: {Sema: Mimi si kiroja (mpya) katika mitume} [AL AHQAF 9]: Maana; mimi sikuwa Mtume wa mwanzo ambaye Mweyezi Mungu Mtukufu alimleta kwa watu, bali aliwaleta Mitume wengine zamani. Jina hili la bidaa linaingia katika kitu kilichovumbuliwa na moyo, ulimi au viungo. [Al Hawadith wa Al bidaa na Al Tartushi, Uk.39, Ch. Dar Ibn Al Jawziy].
Naye Ibnu Al Haji wa madhehebu ya Imam Malik anasema katika kitabu chake [Al Madkhal]: “Bidaa “uzushi” wanavyuoni wameigawanya katika sehemu tano, bidaa iliyo wajibu kama vile vitabu vya elimu kwani havijakuwepo hapo zamani, kwa kuwa elimu ilikuwa katika vifua vya watu, uandishi wa msahafu na kutia nukta katika msahafu. Na bidaa ya pili ni bidaa inayopendeza, kama vile kujenga mahodhi ya kuhifadhi maji, kusafisha barabara kwa ajili ya kupita watu, kujenga madaraja, kujenga shule na vyote vinavyofanana na hali hizo. Na bidaa ya tatu ni Mubah kama vile kutumia ungo, chujio, chumvichumvi za potashi n.k. Na bidaa ya nne ni Makruhu yaani inachukiza ni kama vile kuremba misikiti na kuremba misahafu. Na bidaa ya tano ni haramu, nayo ni ile ambayo hatuwezi kuzungumzia mifano yake kwa sababu ni mingi sana” [Almadkhal, na Ibnul Haaj, 2/257, Ch. Maktabat Dar Al Turaath], Kwa kufanya mabadiliko madogo.
Na dalili ya kuwa bidaa inagawanyika katika migawanyiko hii ambayo inaingia katika masuala ya ibada na mila ni hadithi ya Omar ibn Al Khattab ambayo ilitolewa na Albukhari kutoka kwa Abdalrahman ibn Abdelqary kwamba alisema: “nilitoka nikiwa na Omar Ibn Al khattab R.A usiku wa mwezi wa Ramadan tukielekea msikitini, tukawakuta watu wakiwa wamegawanyika kila mmoja anasali peke yake, na kila mtu anasali kivyake vyake, akasema Omar mimi naona kama watu wote hawa watakusanywa kwa msomaji mmoja litakuwa jambo bora zaidi, kisha akaazimia hivyo akawakusanya kwa Ubai ibn Kaab. Kisha nilitoka naye usiku mwingine, tukamkuta msomaji anawasalisha watu, Omar akasema: “hii ni bidaa nzuri kabisa yaani huu ni uzushi mzuri, wanaoifanya ni bora kuliko wasioifanya”. Na hapa Omar anakusudia mwisho wa usiku, kwani watu walikuwa wakiamka mwanzoni mwa usiku. Hadithi hii inaonesha kwamba bidaa ni aina mbili, bidaa nzuri na bidaa mbaya. Na kama bidaa haigawanyiki basi ingekuwa ni upotovu tu. Kwa sababu hadithi aliyoipokea Abu Daud na Tirmidhiy kutoka kwa Al Arbadh ibn Sarea alisema: “Mtume S.A.W. anasema: “Nakuusieni kumcha Mwenyezi Mungu, kumsikiliza na kumtii, hata kama mtumwa wa kihabeshi atakuamrisheni hivyo , hakika atakayeishi miongoni mwenu baada yangu ataona hitilafu nyingi sana, basi nakuusieni mshikamane na Sunna yangu na mwendo wa masahaba walioongoka, shikamaneni nazo na mjitahidi, na tahadhirini na mambo yanayozushwa, kwani kila kinachozushwa ni bidaa (uzushi) na kila bidaa ni upotovu”. Hadithi ya Mtume S.A.W. imejumuisha kila bidaa ni upotovu, ikaja hadithi ya Omar ikaweka wazi kwamba kila aina ya bidaa haina msingi wa kisheria basi ni upotovu. Na kuna hadithi nyingine iliyopokelewa na Muslim kutoka kwa Jareer Al Bajli inatia nguvu maana hiyo kwamba Mtume S.A.W. amesema: “Yoyote atakayezusha jambo zuri, basi atakuwa na malipo kutokana na jambo hilo, na atakuwa na malipo ya kila anayefanya jambo hilo mpaka siku ya Kiyama, na yoyote atakayezusha jambo baya, basi atakuwa na mzigo wa dhambi, na atabeba mizigo ya dhambi ya kila anayefanya jambo hilo mpaka siku ya Kiyama”. Na Haya yanathibitshwa na yale yalipokewa na Ibn Abi Shaiba katika kitabu chake kwamba Al Hakam Ibn Al Aaraj alisema: Nilimwuliza Muhammad S.A.W. kuhusu Sala ya Dhuhaa, Je, sala hii inaweza kusaliwa kwa jamaa? Mtume alikuwa ameegemea juu ya chumba chake Akasema: Hii ni bidaa, ni bidaa nzuri sana.
Al-Nafrawey wa madhehebu ya Imam Malik alisema: “Bidaa ni jambo ambalo halikuwepo katika zama za Mtume S.A.W. hata kama sheria imehukumu ni bidaa haramu, inayochukiza, wajibu, inayopendeza, au ni bidaa inayoruhusiwa.
Kuna wanaosema kama Ibn Abdulsalaam, Al Kirafiy n.k kwamba bidaa inachukua hukumu tano za Kiislamu. Na maana hii Al Nafrawiy iko karibu sana na maana ya kilugha, yaani kila kilichofanywa pasina ruwaza”. [Al Fawakih Al Dawani Alaa Sharh Risaalat Al Qayrawaniy, 1/109, Ch. Dar Alfikr].
Na kwa mujibu wa yaliyotangulia, Hakika bidaa inaingia katika masuala ya ibada, mila, na miamala. Na inagawanyika katika aina tano za hukumu za Kiislamu.
Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.