Sala katika Msahafu

Egypt's Dar Al-Ifta

Sala katika Msahafu

Question

Nini Hukumu ya kusoma Quraani kwa kutumia Msahafu ndani ya Sala?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W. watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo.

          Miongoni mwa mambo bora ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna njema ni mwanadamu kukusanya mambo mawili mema kwa wakati mmoja; Sala na kusoma Quraani, basi anafanya hima kuhitimisha Quraani tukufu katika Sala yake. Kwa kuwa si jambo jepesi kwa kila mtu kuhifadhi Quraani, basi wanachuoni wamezungumzia uwezekano wa kusoma Quraani kwa Msahafu wakati wa Sala; na kufanya hivyo iwe kwa kuuchukua msahafu mkononi au kuuweka sehemu ambayo itamwezesha kuusoma.

          Na madhehebu ya Shaafiy na fatwa katika madhehebu ya Hanbaliy yanasema hivi: Inajuzu kusoma Quraani kwa kutumia Msahafu katika Sala, iwe Imamu anasalisha au mtu anasali peke yake, na hakuna tofauti kati ya Sala ya Faradhi na Sunna, na hii pia ni rai ya Imamu Ibn Qudamah aliyenukuu haya katika kitabu cha [Al Mughniy, 1/336] kutoka kwa Ataa na Yahya Al Ansaariy, mwanachuoni wa Salaf.

          Na katika Sahihi ya Buhkariy, -Ibn Abi Shaibah katika kitabu cha [Al Musanaf, 2/235], na Al Baihaiqiy katika kitabu cha [Al Sunnan Al Kubra, 2/253]- kutoka kwa Aisha mama wa waumini R.A. kwamba alikuwa akisali nyuma ya mtumwa wake anayeitwa Zakawaan na alikuwa akisoma kwa Msahafu.

          Na Imamu Al Zahriy aliulizwa kuhusu mtu anayesali kwa kusoma Msahafu katika Ramadhani, na akasema: "Wakuu wetu walikuwa wakisoma katika Misahafu". [Al Mudawanah Al Kubra, 1/288-189. Na Al Mughniy kwa Ibn Qudamah, 1/335].

          Na kwa kuwa kusoma Quraani ni ibada, basi kutazama katika Msahafu ni ibada pia, na huwezi kuzuia ibada kuingiliana na ibada nyingine, bali thawabu zinaongezeka, kwani unaongeza amali kwa kutazama Msahafu.

          Hujjatul Islamu Imamu Ghazaliy amesema katika kitabu cha [Ihiyaa Uluum Al Deen, 1/229]: "Inaelezwa kwamba kuisoma Quraani yote kwa Msahafu ni kama kuisoma yote mara saba; kwani kutazama katika Msahafu ni ibada pia.

          Na kanuni ya kisheria inasema: “njia zinachukua hukumu ya makusudio”, na kwa kuwa makusudio hapa ni kusoma, basi makusudio yakipatikana kwa njia ya kutazama katika maandishi kama Msahafu, basi inakuwa inajuzu.

          Imamu Al Nawawiy amesema katika kitabu cha [Al Majmu'i, 4/27]; "Mtu akisoma Quraani kwa Msahafu basi Sala yake haibatiliki, awe amehifadhi Quraani au la, bali analazimika kusoma

          kwa Msahafu kama hajahifadhi Surat Al FATIHAH, na kama atageuza karatasi za Msahafu katika Sala yake basi haibatiliki.

          Na mwanachuoni Mansuur Al Bahwatiy wa Hanbaliy amesema katika kitabu cha [Kashaaf Al Qinaai, 1/384]: "Inajuzu kwa mtu anayesali kusoma Quraani kwa Msahafu hata kama amehifadhi, iwe Sala ya Faradhi au Sunna. Ibn Hamed alisema hayo”.

          Lakini wanachuoni wa Hanafiy wanaona kuwa kusoma kwa Msahafu katika Sala huibatilisha, na haya ni madhehebu ya Ibn Hazm wa Dhaahriyya, na dalili zao ni kama ifuatavyo:

          Ibn Abi Dawud amepokea katika kitabu cha [Kitab Al Masahef, 655] kutoka kwa Ibn Abbas R.A., amesema “Amiri wa

waumini Omar R.A. ametukataza watu kusalisha kwa kutumia Msahafu, na ametukataza kutusalisha mtu isipokuwa aliyebaleghe”.

          Na hiyo ni athari haikuthibiti, kwani katika Isnadi yake yupo Nashal Bin Saiyd Al Naisaboriy, ambaye ni mwongo anayeachwa,

          Imamu Al Bukhariy amemzungumzia katika kitabu cha [Al Tareekh Al Kabeer, 8/115] kwa kusema: "Hadithi zake ni Munkari", na Al Nassaiy amesema katika kitabu cha [Tahdheeb AlTahdheeb, 10/427]: "Yeye si mwaminifu na hadithi zake haziandikwi

          Na miongoni mwa dalili zao: Kukamata Msahafu, kutazamia na kugeuza karatasi zake ni kazi nyingi.

          Na jawabu ni: Ikiwa sababu ya kuzuia kukamata Msahafu na kugeuza karatasi zake ni kazi nyingi zinazobatilisha Sala, basi Mtume S.A.W. alisali hali ya kuwa amembeba Umamah Binti Abi Al Aas juu ya mabega yake, na anaposujudu anamuweka, na anaposimama anambeba. Ama kuhusu kugeuza karatasi za Msahafu, basi baadhi ya hadithi zinaashiria uhalali wa kazi nyepesi ndani ya Sala, na kugeuza ni kati ya kazi nyepesi zinazosamehewa.

          Na kusoma Quraani kwa Msahafu katika Sala si kazi kubwa, kwani kugeuza karatasi za Msahafu ni kitendo cha sekunde chache kabisa; kutoka ukurasa hadi ukurasa, kwahivyo kugeuza kwenyewe ni kazi nyepesi sana. Na unaweza kutumia Msahafu wenye herufi kubwa na ukauweka juu ya kitu kilichoinuka mbele ya anayesali ili asome ukurasa mmoja na kurasa mbili, na hahitaji sana kugeuza karatasi.

          Wanachuoni wawili wa Hanafiy Abu Yusuf Al Qadhi na Muhamad Bin Al Hassan Al Shaibaniy wanasema kusoma kwa Msahafu katika Sala ni Makruhu, iwe katika Sala ya Faradhi au Sunna, lakini kusoma huko hakubatilishi Sala, kwani kusoma ni ibada iliyoongezeka katika ibaada nyingine. Na ni Makruhu kwa sababu kunafanana na kazi ya watu wa kitabu.

          Na kupata kitu kinachofanana na kazi ya watu wa Kitabu ni marufuku kama mtendaji anakusudia kupata kitu kinachofanana na chao, kwani kujifananisha ni kufanya. Na kifungu hiki kinajulisha kuwa kutia nia na kukusudia kitendo ni miongoni mwa misingi ya kisheria yanayofungamana na mwenye jukumu la kisheria.

          Imamu Muslim amepokea kutoka kwa Jabir Bin Abdullah R.A., amesema: Mtume S.A.W. alikuwa mgonjwa, na sisi tulisali nyuma yake na yeye alikuwa amekaa, basi akatugeukia, na akatuona tumesimama basi alituashiria ili tukae, na alipotoa salamu alisema:

          "Nyinyi mnakaribia kufanya kitendo kama cha Waajemi na Warumi, wanawasimamia wafalme wao hali ya kuwa wafalme wamekaa, basi msifanye hayo, wafuateni maimamu wenu, Imamu akisali huku amesimama basi salini mmesimama, na akisali amekaa basi salini mmekaa.”

          Na neno la (mnakaribia) linaashiria kukaribia jambo pamoja na kukanusha kutokea kwake. Kwahiyo masahaba walipokuwa hawakusudii kujifananisha na watu wa kitabu basi sifa hiyo iko mbali nayo kisheria, na anayesali ambaye anasoma katika Msahafu hakusudii kujifananisha na watu wa Kitabu, na kusudio lake ni jema.

          Mwanachuoni Ibn Najem Al Hanafiy amesema katika kitabu cha [Al Bahr Al Raiq, 2/11]: "Jua kwamba kujifananisha na watu wa kitabu si Makruhu katika kila jambo, kwani sisi tunakula na tunakunywa kama wanavyofanya, lakini ni haramu kujifananisha nao katika mambo mabaya tu na kukusudia kujifananisha katika mambo hayo. Hivyo basi, kama hajakusudia kujifananisha si Makruhu kwa wanachuoni wawili hao.

          Ama wanachuoni wa Malikiy wanatafautisha baina ya Sala ya faradhi na Sunna. Wanaona ni Makruhu kwa anayesali kusoma kwa Msahafu katika Sala ya faradhi, iwe kusoma mwanzoni mwa Sala au katikati ya Sala. Na pia ni Makruhu katika Sala ya Sunna ikiwa katikati ya Sala, kwa kuwa mara nyingi anajishughulisha. Lakini inajuzu katika Sala ya Sunna kama alianza Sala kwa kusoma katika Msahafu, na si Makruhu, kwani yanasamehewa katika Sunna yasiyosamehewa katika faradhi, [Manhi Al Jaleel Sharh Mukhtasar Khalil, 1/345.

          Na inawezekana kujibu hivi: Makruhu inakuja ikiwa kitendo ni upuuzi mtupu na hakina faida yoyote. Ni Makruhu kwa anayesali kufanya kitendo kinachomshughulisha kwa kuwa kinaondosha unyenyekevu ndani ya sala, ama kusoma

katika Msahafu ndani ya Sala si miongoni mwa hayo, bali ni kazi nyepesi sana anayesali anaifanya anapokuwa na shida. Mtume S.A.W. alivua viatu vyake katika Sala alipopewa Wahyi kwa kuwa vina uchafu. Aidha ameipokea Imamu Ahmad katika kitabu chake [Musnad, 3/92], na Abu Dawud katika Sunna zake (650) kutoka kwa Abi Saiyd Al Khodriy R.A.

          Na kutokana na yaliyotangulia, yanathibiti yafuatayo: Kusoma Quraani kwa kutumia Msahafu ndani ya Sala ya Faradhi na Sala ya Sunna ni sahihi na inajuzu kisheria, na wala si Makruhu, na kusoma huku hakubatilishi Sala.

Tanbihi: Kwa kuwa jambo hili lina hitilafu basi mlango ni mpana, hakuna kukanusha katika maswala yenye hitilafu, na haifai kutumia maswala yenye hitilafu katika kuleta fitina na kuwagombanisha waislamu.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas