Utungaji wa Sheria ya Kiislamu

Egypt's Dar Al-Ifta

Utungaji wa Sheria ya Kiislamu

Question

Nini kusudio la istilahi ya Utungaji wa Sheria ya Kiislamu, nini faida na masilahi yake, na upi msimamo wa wanachuoni wa Fiqhi ya Kiislamu kuhusu swala hili?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimshukie bwana wetu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na waliomfuata. Na baada ya hayo:

          Hakika Utungaji wa Sheria ya Kiislamu ni miongoni mwa masuala muhimu yanayoshughulisha uwanja wa Kiislamu tangu muda mrefu katika enzi hii ya kisasa. Kwa hiyo, tunaona wanachuoni wengi wa Fiqhi waliunga mkono wazo la Utungaji wa Sheria ya Kiislamu. Na ili tuweze kuhukumu Utungaji wa Sheria ya Kiislamu, hatuna budi kufikiria uhakika wake na kujua sifa zake.

          Utungaji wa Sheria: ni kuunda hukuma zake katika umbo la kanuni zinazotekelezwa mbele ya mahakama. Na uundaji wa hukumu katika umbo la kanuni zinazotekelezwa unamaanisha: kukusanya misingi inayohusu tawi miongoni mwa matawi ya sheria, kama mambo ya kifamilia, haki za mume na mke n.k., baada ya kupanga na kupangilia misingi hii na kuondosha utata au ugumu kisha kutolewa hukumu katika umbo la kanuni zinazowekwa na dola, ili zitumike kwa ajili ya kuhukumu baina ya watu mahakamani.

          Hapo, inaonekana kuwa Utungaji unajengeka kwa vipengele viwili:

          Kwanza: kuunda hukumu za kisheria katika ibara fupi ya kisheria iliyo wazi.

          Pili: kumlazimisha jaji kuamua kwa mujibu wa sheria hii, hata ikipingana na rai yake mwenyewe.

Utungaji hauhusishi tu kuunda upya hukumu zilizomo katika vitabu vya Fiqhi, lakini unakusanya pia kuzipangilia upya na kuzipanga katika makundi maalumu na nadharia mnasaba. Na kama kuna swala au kesi ambayo haina hukumu inayofaa katika vitabu vya zamani vya Fiqhi vilivyotungwa basi utungaji wa sheria unachukua mkondo wake katika kutoa hukumu mpyakuhusu swala hilo kwa njia ile ile iliyotumika kutoa hukumu katika vitabu vya Fiqhi vilivyotungwa zamani, na njia hii ya kutoa hukumu inafafanuliwa na Elimu ya Misingi ya Fiqhi.      

          Utungaji una sifa maalumu zinazotofautiana na njia ya kutoa hukumu katika Fiqhi ya kale. Kwa hiyo, inawezekana kuainisha sifa hizo, kama ifuatavyo:

·        Uwazi wa msingi wa kisheria, ili kurahisishwa kuurejelea ima kwa upande wa Jaji au kwa upande wa mwenye kesi mahakamani.

·        Umadhubuti wake.

·        Urahisi wa kuurejelea.

·        Kutokuwepo ukinzani kati yake na misingi inayohusika.

·        Umoja wa kisheria katika nchi moja.        

          Kwa hivyo, Utungaji kwa kuangalia sifa hizi unapelekea masilahi mengi kwa ujumla, miongoni mwake:

·        Kurahisisha utekelezaji wa hukumu ya Sheria ya Kiislamu katika madola yanayotaka kuhuisha kanuni kwa msingi wa Sheria ya kiislamu.

·        Kuunga mkono nchi ambazo zinatekeleza hukumu ya Sheria ya Kiislamu,lakini bila Utungaji, ili kwenda sambamba na mifumo ya sheria za kisasa, na kujiepusha na tuhuma ya kurejea nyuma, na kutokuwepo kwa sheria ya wazi kwa nchi hizi.

·        Kuafikiana na misingi ya mifumo ya hukumu ya kisasa kwa kumhabarisha mwananchi sheria, na pia kurahisisha kuisoma, na kuzijua sheria zinazoambatana na vitendo vyake vinavyovunja sheria za nchi.

·        Kwenda sambasamba na mfumo wa kisasa wa kimataifa kuhusu nchi kutangaza katiba na sheria zake, na yanayotokana na mikataba ya kimataifa inayokidhi maendeleo ya kisasa, ambayo hayapotoshi misingi na utambulisho wa umma wa Kiislamu.

·        Kupambana na udanganyifu unaoweza kutokea katika zama ya uharibifu wa dhamira ya baadhi ya majaji , wakati jaji anapojua kuwa kuna sheria inamlazimisha kuamua kwa haki, na kuwa kuna chombo kikubwa cha mahakama kinaangalia uamuzi wake, na kuainisha namna ya kutekeleza sheria.

          Wakati wa utungaji, kiongozi anachagua moja ya rai, kisha rai hii inakuwa uamuzi wa kisheria wa lazima, na hali hii inapatana na msingi unaosema “kiongozi ana haki ya kusema jambo fulani ni ruhusa kwa mujibu wa mtazamo wake kwa kuwa lina masilahi ya raia.

          Maudhui ya Utungaji wa Sheria ina asili katika uchunguzi wa wanachuoni wa Fiqhi, hasa katika suala la kumlazimisha jaji afuate madhehebu maalumu, lakini maudhui hii kutokana na kanuni zake na sifa zake inazingatiwa ni ya kisasa. Kwa hiyo, wanachuoni wengi wa Fiqhi wanaafiki na wanatumia sifa zake zilizotajwa na masilahi yake. Miongoni mwa wanachuoni hawa ni: Imamu Muhammad Abdu, Sheikh Muhammad Rashiid Ridha, Sheikh Ali Al Khafiif, Sheikh Hasanein Makhluuf, Sheikh. Ahmad Shakir, Sheikh Muhammad Abu Zahrah, Sheikh Ahmad Fahmy Abu Sinnah, Sheikh Ali Al Tantawiy, Sheikh Abdullahi Al Khayyat, n.k.

          Baadhi ya wanachuoni wa Fiqhi walikataa wazo la utungaji wa Sheria, wakiogopa kuwa utungaji huu utalamzimsha anayejitahidi kufuata madhehebu maalumu, na hali hii inaondosha jitihada.

          Lakini tunaweza kuyajibu hayo kuwa: Utungaji hauondoshi jitihada, kwa sababu jitihada ipo, na uwanja wake ni Fiqhi katika kiwango cha utafiti na kutoa fatwa, na itaendelea kuwepo kama ilivyo. Na utungaji wa sheria ambao wananchi wanawajibika nao katika dola, unasimamiwa na majaji, na unatekelezwa na serikali, hilo ni jambo lingine liliopo katika mfumo wa dola la kisasa, na utawala wa kutenganisha mihimili mitatu ya dola (Bunge, Mahakama, na Serikali) kwa ajili ya kulinda masilahi ya wananchi. Hilo ni jambo la utaratibu ambalo linaendesha mambo ya maisha na mpangilio wa masilahi.

          Inawezekana kuwashirikisha wanaojitahidi wawe wajumbe katika kamati za utungaji, ambapo wanazitumia jitihada zao katika kuamua rai bora za kifiqhi, kujitahidi katika masuala mapya, na kuunda maoni yanayokubaliwa na kamati za utungaji. Pia si lazima anayejitahidi ashike wadhifa wa jaji, bali hunufaisha kwa jitihada yake katika uwanja wa fatwa na utungaji wa kifiqhi.

          Kuhusu kiwango cha mambo ya ukadhi, Utungaji haumaanishi kamwe kusita jitihada ya kisheria, kwa sababu zoezi lenyewe la jitihada lazima litanguliwe na jitihada, na kufuatiwa na jitihada . Jitihada ya bidii inatangulia kwa uchunguzi katika vitabu vya kale, kama vile vitabu vya madhehebu manne na vinginevyo, na kuchagua maoni na mitazamo yanayohusisha hali ya siku hizi na matatizo yake. Na hayo hayamaliziki isipokuwa kwa kuwepo jitihada, kwa upande mmoja jitihada katika ngazi ya madhehebu maalumu ni kuchagua rai bora katika rai nyingi ndani ya madhehebu moja. Na kwa upande mwingine, jitihada katika ngazi ya madhehebu mengi ni kuchagua rai bora miongoni mwake, kwa kuitumia katika suala au kesi zinazopatikana.

          Jitihada hii ya bidii itajengeka kwa dalili za asili zinazojulikana, ambapo masharti ya jitihada yaangaliwe, kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Kiislamu.

          Utungaji ukimalizika, utahitaji jitihada pia. Kwa hiyo, wasimamizi wa zoezi la kisheria wakiona baadhi ya kanuni hazinasibiani na hali za watu na maisha yao, basi si vibaya, bali ni lazima, kutoa jitihada mpya mbele ya kamati za Utungaji kwa ajili ya kuitathmini, kukubaliwa na kupitishwa au kukataliwa.

          Kwa kuongeza, maendeleo ya kudumu yatapelekea kugundua aina za matatizo mapya, ambayo yatatolewa mbele ya Mahakama, wakati yanahitaji jitihada mpya, ambayo itafanywa na majaji na wenye kujitahidi, kwa ajili ya kuongeza kanuni mpya, au kurekebisha kanuni za zamani ambazo hazifai kuzitumia wakati wa kutoa hukumu kuhusu hali na matatizo ya siku hizi.

          Baadhi ya wanachuoni wa Fiqhi wanapinga kazi ya Utungaji, kwa kuogopa kuwa utungaji hauwezi kutatua hitilafu wakati majaji wanapohitilafiana katika tafsiri ya matini. Na suala hili linajibiwa kuwa: urahisi huushinda ugumu. Na ikiwa utungaji sheria hauzuii tofauti (zilizopo) kiukamilifu, basi unaweza kuipunguza na kuifanya iwe finyu. Na hivyo ndivyo inavyotakiwa.

          Kwa mujibu wa yaliyotangulia na kuhusu swali: Utungaji ni chombo cha matumizi ya Sheria ya Kiislamu, na vyombo huchukua hukumu za malengo. Hakika ya utungaji ni muundo wa kanuni za Kiislamu, na kuzipangilia kwa njia mpya ambayo inanasibiana na maendeleo ya zama hizi. Na hayo humrahisishia kadhi na mwenye kesi kurejea hukumu na kuzijua nje ndani, . Licha ya hayo, Utungaji huhifadhi umoja wa sheria ndani ya nchi moja. Na hivyo vyote vimeonekana katika: Majalat Alahkaam Aladliyah; (Jarida la Maamuzi ya Kisheria).

          Na kama ilivyoashiriwa hapo juu, wanachuoni wengi wa Fiqhi wameafiki na kuunga mkono fikra hii ya utungaji wa Sheria, kwa sababu huleta masilahi mengi, na ni miongoni mwa njia za kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Kiislamu katika mfumo wa Sheria na mahakama za nchi.

Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas