Kusilimu Mke na Kubakia Mume wake k...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusilimu Mke na Kubakia Mume wake katika Dini isiyokuwa ya Kiislamu

Question

Kama mke alisilimu bila ya mume kusilimu, Je, ndoa yake inaendelea baada ya kusilimu kwake, au utengano unatokea baina yake na mume wake mara tu baada ya kusilimu kwake?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Kama mke na mume walisilimu pamoja, na mke hakuwa miongoni mwa maharimu wa mume -kama mwanamke aliyeharimishwa kwa nasaba au kunyonya- basi mume na mke hawa wataendelea katika ndoa yao sawa iwe kabla au baada ya kuingiliana, kwani sheria imekubali ndoa ya makafiri, kwahiyo wanabakia katika ndoa wakisilimu au ikiwa waliomba hukumu kwa waislamu, bila ya kuangalia sifa ya mkataba wao na mfumo wake, ndoa yao haizingatiwa kwa masharti ya ndoa ya waislamu kama vile walii, mashahidi wawili na tamko la kuitika na kukubali. Katika enzi ya Mtume S.A.W waume na wake zao walisilimu basi waliendelea katika ndoa zao, na Mtume S.A.W hakuwauliza masharti ya ndoa na namna yake. Na jambo hili linajulikana na wanachuoni wameliwafiki [Al Mughniy Libn Qudama, 7/116, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy, na Al Tamheed, 12/23, Ch. Wizara ya Mambo ya Wakfu ya Moroco].

 Na kama mume alisilimu peke yake, na mke wake ni miongoni mwa watu wa kitabu na mke huyo hakuwa miongoni mwa maharimu wake basi wanabakia katika ndoa yao ya kwanza sawa iwe kabla au baada ya kuingiliana, kwani ndoa ya wanawake wa kitabu ni Mubah kwa mwislamu; kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu. na chakula chenu na halali kwao. Na (mmehalalishwa kuwaoa) wanawake wema wa Kiislamu na wanawake wema katika wale waliopewa Kitabu kabla yenu. (Ni halali kwenu kuwaoa), mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila kufanya uzinizi (kwa mwanamke huyu na huyu), wala kuwaweka (wanawake wa) kinyumba.} [Al MAIDAH 5]. Basi mwanamke wa kitabu ni halali kwa mwislamu kabla ya kusilimu basi ni halali baada yake.

Lakini kama mke alisilimu, na mume wake alibakia katika dini yake, basi fatwa iliyochaguliwa ni:

Ikiwa mke kasilimu kabla ya kuingiliwa basi lazima utengano baina yao wawili uharakishwe; kwani jambo hilo ni la kiasili, na hapana masilahi hapa yanayotupelekea kukubali ndoa hiyo. Na ikiwa mke akasilimu baada ya kuingiliwa, na mume wake akasilimu kabla ya kwisha eda yake basi wataendelea katika ndoa yao, lakini kama eda yake ilitimia na mume wake hakusilimu basi mke huyu atakuwa na uhuru wa kuchagua; kama atachagua kuolewa na amtakaye basi ana haki hiyo, lakini lazima aende kwa kadhi ili autengue mkataba wa ndoa, na kama atachagua kumngojea mume wake asilimu hata kama muda utarefuka basi ni haki yake, na katika hali hiyo ndoa inazingatiwa imesimamishwa, na kama mume wake atasilimu basi wanabakia katika ndoa yao ya kwanza bila ya kuhitaji kufunga tena ndoa, pamoja na kuzingatia kutokea utengano wa kihisia na kusimama kwa tendo la ndoa baina yao tangu mwanzo wa kusilimu kwa mke. Rai hii ameisema Ibn Taimia na Ibn Al Qaim, na ameichagua Al Sana'aniy, na Al Shaukaniy ameiridhia. [Majmu'u Al Fatawi, 322/209, Ch. Dar Al Wafaa, na Ahkaam Ahlu Al Dhima, 2/692, Ch. Dar Ibn Hazm, na Subil Al Salaam, 1/148, Ch. Dar Al Hadeeth, na Nailu Al Awttaar, 6/215, Ch. Dar Al Hadeeth].

Na kuna dalili nyingi kuhusu fatwa tuliyoichagua:

Kwanza: Imethibiti kwamba Mtume S.A.W alimrudisha binti yake Zainab kwa Abi Al Aas kwa ndoa ya kwanza. Kutoka kwa Ibn Abaas R.A. amesema: "Mtume S.A.W alimrudisha Zainab binti yake kwa mume wake Abi Al Aas Bin Al Rabii' kwa ndoa ya kwanza na hakijatokea kitu". [Imepokelewa na Ahmad, Abu Dawud na Al Haakem].

Na katika tamko: "Hakukuwa na mahari" [Imepokelewa na Ahmad na Al Haakem].

Na katika tamko lingine: "Hakukuwa na ushahidi wala mahari" [Imepokelewa na Ahmad].

Na katika tamko: "Haijafungwa upya ndoa" [Imepokelewa na Al Tarmiziy].

Na katika riwaya: "Baada ya miaka sita" [Imepokelewa na Abu Dawud, Al Haakem na Al Bihaiqiy katika Al Kubra].

Na katika riwaya: "Baada ya miaka miwili" [Imepokelewa na Ahmad, Abu Dawud na Al Haakem].

Kitendo cha Mtume S.A.W kumrudisha mwanamke kwa mume wake baada ya kusilimu mume kinajulisha kwamba hakuna haja ya kufunga upya ndoa hata kama muda utarefuka na eda itamalizika.

Ama yaliyopokelewa katika hadithi ya Amru Bin Shuaib kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kwamba Mtume S.A.W alimrudisha binti yake kwa ndoa mpya, yamekuja kwa lafdhi mbili:

Lafdhi ya Kwanza: "Mtume S.A.W alimrudisha binti yake kwa Abi Al Aas kwa mahari mpya na ndoa mpya" [Imepokelewa na Ahmad, Al Tarmiziy na Ibn Majah].

Lafdhi ya pili: "Zainab binti ya Mtume S.A.W alisilimu kabla ya mume wake Abi Al Aas kwa mwaka mmoja kisha mume wake alisilimu basi Mtume S.A.W alimrudisha kwa ndoa mpya". [Imepokelewa na Al Haakem]

Hadithi hii kwa lafdhi zake mbili inarejea kwa Al Hajaaj Bin Artta'ah, ambaye amezipokea kutoka kwa Amru Bin Shuaib, na alikuwa mdanganyifu mkubwa, anawadanganya watu. Ahmad aliseme: "Hii Hadithi dhaifu, au alisema hadithi mbaya, na Al Hajaaj hakuisikia kutoka kwa Amru Bin Shuaib lakini aliisikia kutoka kwa Muhamad Bin Ubaid Illahi Al Arzemiy, na Al Arzemiy hadithi yake si lolote si chochote. Bali hadithi sahihi aliyoipokea, inasema Mtume S.A.W aliwakubalia kwa ndoa ya kwanza" [Musnad Ahmad, 2/207, Ch. Muasasat Qurtubah].

Hadithi hiyo pia ameidhaifisha Al Tarmiziy, na akasema: "Katika Isnadi yake makala", na Al Darqattniy alisema: " Hadithi hii haithibiti, na Al Hajaaj haitolei hoja, na sahihi ni hadithi ya Ibn Abaas: "Mtume S.A.W. alimrudisha binti yake kwa ndoa ya kwanza" [Sunnan Al Darqattniy, 3/253, Ch. Dar Al Maarifa].

Na Dalili ya Pili: Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abaas alisema: "Mwanamke mmoja alisilimu katika zama ya Mtume S.A.W basi akaolewa. Mume wake wa kwanza alikuja kwa Mtume S.A.W na akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi nilikuwa nimesilimu na mke wangu alijua kusilimu kwangu, basi Mtume S.A.W akamng'oa kutoka mume wake wa pili na akamrudisha kwa mume wake wa kwanza".

Na katika lafdhi: " Mwanamume alikuja hali ya kuwa ni mwislamu katika zama ya Mtume S.A.W kisha mke wake akaja hali ya kuwa ni mwislamu, basi mwanamume akasema: "Ewe Mtume wa Allah! Mke wangu alikuwa amesilimu nami basi mrudishe kwangu, Mtume S.A.W akamrudisha kwake". [Imepokelewa na Ahmad, Abu Dawud, Al Tarmiziy na Al Haakem].

Na ushahidi: kutouliza Mtume S.A.W je, mke wake alijua kusilimu kwake kabla ya kumalizika eda yake au la? Hii ni dalili kwamba eda haizingatiwi, na hayo kutokana na kutouliza katika hali hiyo, licha ya kuwepo uwezekano wa kuuliza, [Al Bahr Al Muheett, 4/201, Ch. Dar Al Kutubiy], na uwezekano hapa upo, je, mke alijua kusilimu mume wake kabla ya kumalizika eda au baada yake?, pamoja na hayo Mtume S.A.W hakumwuliza, basi hiyo inaashiria ujumla wa hukumu ya hali mbili, na kuwa hakuna tofauti kati ya kurudisha mke kabla ya kutimia eda au baada yake.

Tatu: Kutoka kwa Ibn Abaas R.A alisema: "Washirikina walikuwa katika nafasi mbili kwa Mtume S.A.W na waumini; walikuwa washirikina wa watu wa vita wanapigana na Mtume S.A.W na anapigana nao, na washirikina wa watu wa ahadi hapigani nao wala hawapigani naye, na ilikuwa mwanamke wa watu wa vita anapohama haposwi hadi apate hedhi na ajitoharishe, basi akitoharika ndoa ni halali kwake, na kama mume wake alihama kabla ya mke wake kuolewa basi atarudishwa kwake, na kama mtumwa au kijakazi wao alihama basi wako huru, na wana haki kama haki ya Muhajirina" [Imepokelewa na Al Bukhariy].

Na maana ya hayo: ndoa yake ya kwanza inaendelea lakini inasimamishwa -kwa maana kutojamiiana- hata kama aliolewa na mwingine basi ndoa ya kwanza itakuwa imevunjika, na kama mume wake alisilimu kabla ya kuolewa na mwingine basi atarejeshewa.

Na Dalili ya Nne: Mwanamke akisilimu kisha mume wake akasilimu baada yake basi ndoa inaendelea katika hali yake, kama vile Ummu Al Fadhl mke wa Al Abaas Bin Abdulmuttalib aliyesilimu kabla ya Al Abaas kwa muda, Abdulahi Bin Abaas alisema: "Mimi na mama yangu tulikuwa miongoni mwa waliopewa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kauli yake: {Isipokuwa wale waliokuwa madhaifu kweli katika wanaume na wanawake na watoto} [AN NISAA 98] [Imepokelewa na Al Bukhariy].

Na siri ya swala hili ni kama anavyoona Ibn Al Qaim kuwa mkataba katika muda huu unajuzu lakini sio lazima, na wala haukatazwi na wala hakuna madhara kwa mke, na haupingani na misingi ya sheria. Ama mwanamume akisilimu na chini yake kuna mke kafiri –inakusudiwa mwanamke asiyekuwa wa watu wa kitabu- na akakataa Uislamu basi mume kumshikilia mke kuna madhara na hakuna masilahi kwa mke huyo katika hali hiyo, kwani kama hakumtendea haki yake basi aanakuwa dhalimu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu} [AL MUMTAHINAH 10], Allah S.W. amewakataza wanaume kudumu katika ndoa ya mwanamke asiyekuwa wa watu wa kitabu-, [Ahkaam Ahlu Al Dhima kwa Ibn Al Qaim, 2/662-663].

Na fatwa tuliyoichagua inapingana na rai ya wanachuoni wa madhehebu manne, ambapo madhehebu ya Maalik, Shaafi na Hanbali yanaona kuwa eda ikimalizika na mume hakusilimu basi utengano unatokea baina yao wawili, [Al Fawakeh Al Dawani, 2/26, Ch. Dar Al Fikr, na Nihayat Al Muhtaaj , 6/292, Ch. Dar Al Fikr, na Kashaaf Al Qinai, 2/119, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya]. Na dalili yao ni yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn Shobromah kwamba alisema: "Watu katika enzi ya Mtume S.A.W mwanamume alikuwa anasilimu kabla ya mwanamke, na mwanamke anasilimu kabla ya mwanamume basi yeyote kati yao anasilimu kabla ya kumalizika eda basi ni mke wake, na kama alisilimu baada ya kumalizika eda basi hakuna ndoa baina yao". Na yaliyopokelewa kutoka kwa Al Zahriy: "Hatukuambiwa kwamba mwanamke alihama hali ya kuwa mume wake anaishi katika nchi ya kikafiri ila kuhama kwake kunatenganisha baina yake na baina ya mume wake, isipokuwa kwamba mume wake akiwa muhajiri kabla ya kutimia eda ya mtalaka wake" [Al Mudawanah, 2/214, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya, na Zad Al Miaad, 5/122, Ch, Muasasat Al Resalah, na Kashaaf Al Qinai, 5/120].

Lakini dalili hizo hazisalimiki, kwani yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn Shobromah ni isnadi Muudhwalu; kwani Ibn Shobromah mapokezi yake mengi ni kutoka kwa Taabiyna [Rejea: Araa Al Ghaleel katika Takhreej Ahadiyth Manaar Al Sabiyl lil Al Albaniy, 6/338-339, hadithi nambari 1920, Ch, Al Maktab Al Islamiy]. Na kauli ya Ibn Shehaab Al Zahriy ameitoa Malik katika Al Muwatta, Al Bayhaqiy katika Al Kubra, na Al Tahawiy alisema: "Ni hadithi iliyokatika haisihi kuitolea hoja". [Mukhtasar Ikhtelaaf Al Ulamaa, 2/235, Ch. Dar Al Bashair Al Islamiya].

Na kauli madhubuti ni hadithi tuliyoitaja; "Kwamba Mtume S.A.W. alimrudisha binti yake Zainabu kwa mume wake kwa ndoa ya kwanza".

Na wanachuoni wa Hanafiy wanaona kwamba utengano ni baina ya nyumba ya Uislamu na nyumba ya vita; basi katika nyumba ya Uislamu: kama mke alisilimu na mume wake ni miongoni mwa watu wa kitabu au si katika watu wa kitabu, katika hali hiyo anaelezewa Uislamu, basi akisilimu ndoa yao inaendelea, laa si hivyo kadhi anawatenganisha, na hakuna tofauti baina ya mke aliyeingiliwa au asiyeingiliwa. Na ikiwa amesilimu katika nyumba ya vita basi utengano baina yao unasita mpaka zimalizike hedhi tatu kama ni miongoni mwa wenye hedhi au ipite miezi mitatu, na kama mume alisilimu ndani ya muda huu basi ndoa inaendelea laa si hivyo utengano unatokea, na muda huu sio eda; kwa kuwa humjumuisha mwanamke ambaye hajaingiliwa. Na kama mke na mume walikuwa ni miongoni mwa watu wa nyumba ya vita, na mmoja wao alisilimu, na akaenda nyumba ya Uislamu utengano unatokea kwa sababu ya hitilafu ya nyumba mbili, [Badaai' Al Sanaai', 2/338, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya].

Hali ya kwanza: wameitolea dalili ifuatayo: Mwanamume mmoja kutoka Bani Taghleb, mke wake alisilimu, basi Omar R.A alimuelezea Uislamu, mwanamume huyo akakataa, basi Omar R.A akawatenganisha baina yao. Na tukio hili wamelishuhudia masahaba R.A, na lau utengano ungetokea katika Uislamu wenyewe basi kusengekuwa na haja ya kuwatenganisha. Pia Uislamu haijuzu kuwa ni wenye kubatilisha ndoa, kwani Uislamu unajulikana kwa kuhifadhi miliki, sasa unakuaje ni wenye kubatilisha! pia haijuzu kuibatilisha kwa ukafiri, kwa sababu ukafiri walikuwa nao, na haukupinga kuanzisha ndoa, kwa hiyo kutokuzuia ni bora na rahisi zaidi, na aidha hitilafu ya dini, sio sababu ya kubatilisha ndoa, mfano mume ni mwislamu na mke ni katika watu wa kitabu, na kama ndoa tutaiacha iendelee baina yao basi makusudio hayapatikani; kwani makusudio ya ndoa hayapatikani isipokuwa kwa jimai, na kafiri hayumkini kujamiiana na mwanamke mwislamu, na mwanamume mwislamu si halali kujamiiana na mwanamke mshirikina au majusi kutokana na uchafu wao, kwa hivyo hakuna faida kubakia ndoa hii. Basi kadhi atawatenganisha baina yao katika hali ya kuukataa Uislamu, na hii ndio sababu inayolazimisha utengano. [Al Mabsuutt, 2/45, Ch. Dar Al Maarifa, Badaai' Al Sanaai', 2/336]

Hali ya pili: wameitolea dalili ifuatayo: Kusilimu mmoja wao hakulazimishi utengano, wala ukafiri kwa aliyeshikilia ukafiri, na wala hitilafu ya dini kama ilivyotajwa hapo juu, lakini katika nyumba ya Uislamu inawezekana kuidhinisha sababu ya utengano kwa kadhi kumuelezea mmoja wao Uislamu, kama akikataa anawatenganisha. Na katika nyumba ya vita haitokei hiyo kwa kukosekana walii ambaye anamwita aingie katika Uislamu, basi hedhi tatu zitachukua nafasi ya miito mitatu ya kadhi katika Uislamu kwa ajili ya kuainisha sababu ya utengano, [Al Mabsuut, 5/56, na Badaai' Al Sanaai', 2/338].

Hali ya tatu: wameitolea dalili ifuatayo: Allah S.W. amesema: {Mkiona kuwa wao ni Waislamu kweli basi msiwarudishe (kwao Makka) kwa makafiri. (wanawake) hawa si halali kwa hao (wanaume makafiri)}, Aya [AL MUMTAHINAH 10], Abu Bakr Al Jasas alisema: "Katika aya hii kuna dalali nyingi za kutokea utengano kwa hitilafu ya nyumba mbili baina ya mke na mume katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi msiwarudishe (kwao Makka) kwa makafiri}, na laiti kama ndoa inabaki basi mume ana haki zaidi ya kuwa na mke. Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {(Wanawake) hawa si halali kwa hao (wanaume makafiri) wala wao (wanaume makafiri) si halali kwao}, na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na warudisheni (waume zao) mali zao (mahari) walizotoa}, kwa sababu amemwamrisha mke kurejesha mahari ya mume, na laiti kama ndoa inabaki basi mume hakustahiki kurudishwa mahari; kwani haijuzu kustahiki tendo la ndoa na badala yake, na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala kwenu si hatia kuwaoa, ikiwa mtawapa mahari yao}. Na kama ndoa ya kwanza inabaki basi haijuzu kuolewa, na dalili ya hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu}. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukataza kujizuia kumwoa kwa ajili ya mume wake wa kivita. [Ahkaamu Al Quraani kkwa Al Jasas, 3/355-356],

Na pia wameleta dalili ya kisa cha wanawake waliotekwa wa Auttaas. Kutoka kwa Abi Said Alkhudriy: "Kwamba Mtume S.A.W siku ya Hunain alituma jeshi kwa Auttaas, basi walikutana na maadui, basi walipigana nao, waislamu walishinda na wakateka wanawake, basi baadhi ya masahaba wa Mtume S.A.W walijihisi kuwa na aibu kutokana na uasherati wa wanawake hao pamoja na wanaume wao miongoni mwa washirikina, basi Allah S.W. akateremsha aya katika hali hiyo {Na pia (mmeharimishwa) wanawake wenye (waume zao) isipokuwa wale iliyowamiliki mikono yenu ya kiume}, [AN NISAA 24], yaani wao ni halali kwenu ikimalizika eda yao". [Imepokelewa na Muslim].

Na wanachuoni waliafikiana kuwa inajuzu kumuingilia mwanawake mateka baada ya kutoharika hedhi au kutimia eda, na kama alikuwa na mume katika nyumba ya vita kama mume wake hakutekwa naye, basi kutokea utengano unaungana na kusilimu kwake au kwa hitilafu ya nyumba mbili au kwa kutokea kumiliki juu yake, na wote waliafikiana kuwa kusilimu kwake hakulazimishi utengano hapo hapo, na imethibiti pia kwamba kutokea umiliki hakuondoi ndoa kwa dalili kuwa kijakazi ambaye ana mume kama ameunga mkono basi utengano hautokei, na pia kama mtu kafa ilhali kijakazi ana mume basi kuhama umiliki kwa mrithi inaondoa ndoa. Kwa hivyo hakuna sababu ya kutokea utengano isipokuwa hitilafu ya nyumba mbili, na maana ya hitiliafu ya nyumba mbili ni mmoja wao awe ni kutoka watu wa nyumba ya Uislamu kwa Uislamu au Dhima, na mwengine awe ni kutoka watu wa nyumba ya vita, basi anakuwa ni mpiganaji kafiri, Na kama wawili hawa ni waislamu basi wao ni kutoka nyumba moja hata kama mmoja anaishi katika nyumba ya vita na mwengine katika nyumba ya Uislamu

Na anazijibu dalili za waliosema utengano katika nyumba ya Uislamu unatokea kwa kutenganishwa na kadhi endapo mume atakataa kama ifuatavyo:

Kwanza: kisa cha mwanamume wa Taghalabiy ni kisa dhaifu, kwani wapokezi wake hawajulikani, na hakilingani na kisa kingine kilichopokelewa kutoka kwa Omar Bin Al Khataab R.A ambacho tulikitaja katika orodha ya dalili zetu. Na taarifa ya hayo : kisa hiki amekitoa Ibn Abi Shaibah katika kitabu cha [Al Musanaf, 4/105, Ch. Dar Al Rushd], na Al Bukhariy katika kitabu cha [Al Tareekh Al Kabeer, 4/212, Ch. Dar Al Fikr], kwa njia ya Aliy Bin Musher, pia amekitoa Altahawiy katika kitabu cha [Sharh Maani Al Athaar, 3/159, Ch. Dar Al Maairifa] kwa njia ya Muawia Al Dharir, kisha kwa njia ya Abi Yusuf Al Kadhi na wote watatu -Aliy, Muawia na Abi Yusuf- kutoka kwa Abi Is-haaq Al Shaibaniy kutoka kwa Al Safaah Bin Mattar kutoka kwa Dawud Bin Kardus, na isnadi yake ni dhaifu, kwani hali ya Dawud Bin Kardus haijulikani, pia Al Dhahabiy amesema katika kitabu cha [Al Mizaan, 2/19, Ch. Dar Al Maarifa], hakupokea kutoka kwake isipokuwa Al Safaah Bin Mattar na yeye hali yake pia haijulikani, hajulikana kwa elimu wala mapokezi, na hakupokea kutoka kwake isipokuwa watu wawili: Abu Is-haaq Al Shaibaniy na Al Awaam Bin Haushab, na wawili hawa ni waaminifu. Na mwenye sifa hii katika mapokezi basi haichukuliwi hoja kutoka kwake, lakini hadithi yake inafaa katika ufuatiliaji na ushahidi.

Na alikipokea Ibn Abi Shaibah katika kitabu cha [Al Musanaf, 4/105] kutoka kwa Ebaad Bin Al Awaam, na Al Bukhariy katika kitabu cha [ Al Tareekh Al Kabeer, 4/212] kutoka kwa Shua'bah Bin Al Hajaj, na wote kutoka kwa Al Shaibaniy kutoka kwa Yazeed Bin Alqamah.

Na Abdulrazaaq alipokea katika kitabu cha [Al Musanaf, 6/89, Ch. Al Maktab Al Islamiy] kutoka kwa Safiaa Al Thawriy kutoka kwa Al Shaibaniy, alisema aliniambia mwana wa mwanamke ambaye Omar aliwatengansha alipomfahamisha Uislamu akakataa ........ mpaka mwisho.

Na asiyejulikana katika riwaya ya Sufiyaan anashukiwa kuwa ni Yazeed Bin Alqamah mwenyewe, lakini hali ya Yazeed Bin Alqamah haijulikani zaidi kuliko Al Safaah, kwani Al Shaibaniy peke yake alipokea kutoka kwake, na wala hajulikani hata kidogo, na je aliwahi enzi ya Omar? Kuhusu hili kuna rai nyingi, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi. [Rejea: Islaamu Al-mar-at Wabaqaau Zawjihaa Alaa Diynihi. Dr. Abdullah Al Judaii, Uk. 106], ambao ni utafiti kati ya tafiti za Jarida la Baraza la Kutoa Fatwa la Ulaya, toleo la pili, Januari 2003 / Dhul-qaada 14323 H.

Pili: Uislamu haufai kuwa ni chanzo cha kubatilisha ndoa na kadhalika ukafiri kama walivyosema, lakini haulazimishi kutokuwa ndoa ni batili kuwa ni lazima, kwa sababu katika Uislamu ndoa inakuwa inajuzu baada ya kuwa ni lazima, basi inajuzu kwa kadhi kuharakisha utengano madamu mwanamke ndiye aliyechagua hayo na amewasilisha jambo hilo kwa kadhi. Aidha inajuzu kwa mke kungojea mpaka kusilimu kwa mume wake madamu yeye ndiye aliyechagua hayo. Ndoa ina hali tatu: Lazima, Kuharamisha na kuvunja mkataba, kwa mfano mtu alisilimu ana mke haijuzu kufunga nae ndoa, na hali ya kujuzu na kusimamisha ndoa, na nafasi yake ni baina ya nafasi mbili haihukumiwi kwa kulazimisha ndoa wala kwa kuikatisha kiujumla, na katika hali hiyo mke atakuwa ameachika talaka baaina. Na hii ndio hali ya kisa cha Bi Zainab na Abi Al Aas kama ilivyotangulia.

Na ndoa katika muda huo ambao mwanamke anachagua haihukumiwi kwa kubatilika wala kulazimika na kubakia kutoka kila upande, na ndio maana Amiri wa waumini Omar alimpa uhuru wa kuchagua mwanamke wa watu wa Hira ambaye alisilimu na mume wake hakusilimu kama ilivyotangulia katika orodha ya dalili zetu. Ama kauli ya kwamba hakuna faida katika kubakia ndoa kwa kutopatikana makusudio yake basi rai hiyo haikubaliki, kwani kubakia inajuzu na si lazima bila ya uwezekano wa tendo la ndoa. Hayo ni manufaa kwa mke na mume duniani na akhera bila ya ufisadi, [Ahkamu Ahlu Al Dhima. kwa Ibn Al Qaim, 2/695].

Na wanaosema utengano unatokea katika nyumba ya vita dalili yao ni kumalizika kwa hedhi tatu kunakaa nafasi tatu za kadhi kufahamisha Uislamu kabla ya kutenganisha kwa sababu walii amekosekana, kwani katika nyumba ya Uislamu inawezekana kupitisha utengano pale kadhi anapomwelezea Uislamu mmoja kati ya wawili, akikataa basi anawatenganisha, na katika nyumba ya vita haiji hivi, basi jibu lake: Hii ni kauli tu iliyokosa dalili, lakini kauli thabiti ni kinyume ya hayo, kama inavyobainika katika kisa cha Bibi Zainab kutoka riwaya ya Ibn Abaas R.A.

Na dalili za waliosema utengano unatokea kama mume na mke ni kutoka watu wa vita, kisha mmoja wao akasilimu na akaelekea katika nyumba ya Uislamu kwa hitilafu ya nyumba mbili zinajibiwa kama ifuatayo:

Ya Kwanza: Katika aya ya Suratu AL MUMTAHINAH hakuna kinachothibitisha hoja yao. Kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mkiona kuwa wao ni waislamu kweli basi msiwarudishe (kwao Makka) kwa makafiri], inaashiria kukataza kuwarejesha wanawake wahamao kwa ajili ya Allah S.W na Mtume wake kuwarejesha kwa makafiri kwa kuchelea kufitinishwa katika dini yao. Sasa katika hayo iko wapi hoja inayopelekea kutokea utengano ilhali mke anamngojea mume wake awe mwislamu anayehama kwa ajili ya Allah S.W. na Mtume wake kisha anarudi kwake? Na aidha kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wao si (wake) halali kwao (hao makafiri), na wala wao si (waume) halali kwao.}, Hii ni dalili ya kuharamisha ndoa baina ya waislamu na makafiri, na kwamba mmoja wao si halali kwa mwingine, na hakuna sababu inayopelekea kutokea utengano, na mmoja wao anasubiri mpaka mwenzake anasilimu, na anakuwa halali yake akisilimu. Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na warudishieni (waume wao) mali zao (mahari) walizotoa} pia haina dalili ya kutokea utengano, kwani kumpa mume mali alizotoa ni kupendezesha mawazo yake, na mke ni haki yake kumsubiri mume mpaka asilimu, na endapo atasilimu anarejea kwake kwa ndoa ya kwanza, pia kuna hitilafu katika kuwapa mahari waume; je, ni Wajibu au Sunna? Na je, ni kwa wenye ahadi tu au kwa wenye ahadi na wapiganaji vita?

Ama kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala kwenu si hatia kuwaoa, ikiwa mtawapa mahari yao}, basi hiyo ni risala kwa waislamu inaungana na yaliyopita, lengo lake ni kuondoa uzito juu yao kwa kuwaoa wanawake waumini wahamao kama walitalakiwa na mume wao na kuachwa, na hiyo ni baada ya kumalizika eda ya mwanamke na kuchagua kwake kwa nafsi yake, na bila shaka mwanamke kama eda yake ilitimia ana haki ya kuchagua kati ya kuolewa na amtakaye au kukaa hadi mume wake asilimu na arudi kwake, na ama kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu}, inakataza kudumu kwa ndoa ya mwanamke kafiri na kuendelea naye hali ya kuwa amebakia katika ushirikina na ukafiri wake, na hakuna ndani yake katazo la kungojea hadi mwanamke huyo asilimu.

Ya Pili: Uhakika katika kisa cha wanawake wanaotekwa katika Auttaas kwamba kilichobatilisha mkataba wa ndoa ni umiliki wa kutekwa na siyo hitilafu ya nyumba, Imamu Al Nawawiy alisema anapoielezea hadithi hiyo: "Na muradi wa wanawake wenye waume wao hapo ni wanawake walioolewa. Na maana yake: wanawake walioolewa ni haramu kwa wasiokuwa wa waume zao isipokuwa mliomiliki miongoni mwa wanawake watekwao, basi mkataba wa ndoa wake pamoja na kafiri unavunjwa na atakuwa halali kwenu kama eda au tohara yake atatimia", [Sharh Sahihi Muslim Lil Imamu Al Nawawiy, 10/35, Ch. Dar Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy], na vitabu vya sababu za kuteremsha vilieleza hayo pia, [Lubab Al Nuquul katika Asbaab Al Nuzuul Lil Al Suyuuttiy, Uk. 64, Ch. Dar Ihiyaa Al Auluum fiy Bairut]. Kwa hivyo kiliyobatilisha mkataba wa ndoa katika hali hiyo ni umiliki wa kutekwa na siyo kila umiliki.

Imamu Al Mawardiy anasema katika kitabu cha [Al Haawiy Al Kabeer, 9/260, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiya]: "Na dalili ya kuwa hitilafu ya nyumba mbili haipasi kutokea utengano kwa kusilimu kwa mmoja mke au mume ni yale yaliyopokelewa kwamba Aba Sufyaan Bin Harb na Hakeem walisilimu katika mkoa wa Mar Al Dhahraan -mkoa huo ulikuwa nyumba ya Uislamu baada ya Mtume S.A.W kuingia na kuutawala, na wake zao wapo katika ukafiri mjini Makka -wakati huo ulikuwa nyumba ya vita - kisha wake hao wawili wakasilimu baada ya kufunguliwa Makka, basi Mtume S.A.W. aliwabakisha katika ndoa. Na kama ilisemwa Mar Al Dhahraan ni miongoni mwa ardhi ya Makka, inafuata hukumu ya nyumba Uislamu na kusilimu kwake hakukuwa ila katika nyumba moja, basi kuna majibu mawili:

Kwanza: Mar Al Dhahraan ni nyumba ya Khuza'ah iliyo mbali na utawala wa Makka; kwani Khuza'ah ilikuwa katika ahadi ya Mtume S.A.W. na Banu Bakr katika ahadi ya Makureysh, na kwa nusura ya Mtume S.A.W. Khuza'ah ikawa kwa Makureysh wa Makka.

Pili: Mar Al Dhahraan kama ilikuwa ni sehemu ya ardhi ya Makka basi inajuzu kuitawala kwa kuingia Uislamu, kama vile waislamu wakiifungua ardhi ya nchi ya nyumba ya vita, ardhi hiyo inakuwa nyumba ya Uislamu hata kama nchi hiyo ilikuwa nyumba ya vita. Dalili ya hayo ni yaliyopokelewa kuwa Mtume S.A.W alipoingia Makka mwaka wa kuiokomboa, Safwaan Bin Umaia alikimbilia Twaifu, na Ekrema Bin Abi Jahl alikimbia mpaka pwani ya bahari na wawili hawa ni makafiri, basi wake zao walisilimu katika Makka na mke wa Safwaan ilikuwa ni Barzah Bint Masu'ud Bin Amro Al Thaqabiy na mke wa Ekremah ni Umm Hakeem Bint Al Haarith Bin Heshaam Bin Al Mughirah, na walichukua amani kutoka kwa Mtume S.A.W kwa waume zao basi Safwaan aliingia Makka kwa amani hiyo na alikaa na ukafiri wake hadi alishuhudia Hunain pamoja na Mtume S.A.W na alimwazima silaha kisha alisilimu, na Ekremah alirudi Makka basi akasilimu, na Mtume S.A.W aliwarudishia wake wao licha ya hitilafu ya nyumba mbili baina yao, kwani Makka ilikuwa ni nyumba ya Uislamu kutokana na ukombozi, ama Twaifu na pwani zilikuwa nyumba ya vita. Ikisemwa : sehemu mbili hizi ni ardhi ya Makka na zipo katika utawala wake basi jawabu yake imetangulia.

Ama hadithi ya Ibn Abaas katika kumrudisha Mtume S.A.W binti yake kwa Abi Al Aas, basi wanachuoni wa Hanafiy waliijibu kuwa madhehebu ya Ibn Abaas yanasema kuwa utengano unatokea kwa Uislamu, kwa dalili aliyoipokea Khaled kutoka kwa Ekremah kutoka kwa Ibn Abaas kuhusu mwanamke myahudi alisilimu kabla ya mume wake: kwamba yeye ni mmiliki wa nafsi yake mwenyewe, na haikubaliki Ibn Abaas ahitalafiane na Mtume S.A.W ilhali yeye ameipokelea kutoka kwa Mtume S.A.W mwenyewe, lakini waliyoyataja hayakubaliki; kwani kauli yake: "yeye ni mmiliki wa nafsi yake" inajulisha kuwa mkataba unabatilisha kwa uteuzi wa mwanamke siyo kwa Uislamu wake.

Hitimisho: Mke akisilimu na mume wake akabakia na dini yake – sawa iwe katika nyumba za waislamu au nyumba za wasio waislamu- basi ni haramu kufanya tendo la ndoa baina ya mke na mume. Na mke mwenyewe amwelezea Uislamu au amwakilishe mtu yeyote afanye hayo, endapo mume atasilimu basi wanaendelea na ndoa yao, na kama mume atabakia katika dini yake mpaka eda kumalizika, basi mke ana hiari baina ya kuomba kubatilisha mkataba wa ndoa kwa kuafikiana pamoja na mume wake au kuyafikisha hayo kwa kadhi ili abatilishe ndoa yao, au anangojea kusilimu mume wake, na anaposilimu wanaendelea katika ndoa yao. Na jambo hili ni jepesi katika nyumba za waislamu, kwani mke hakai pamoja na mume wake katika nyumba moja, na akiliwasilisha tu jambo hilo kwa kadhi anawatalakisha. Ama katika nyumba za wasio waislamu ni ngumu, ikiwa mke anaweza kutokaa pamoja na mume wake katika nyumba moja basi afanye hivyo, na kama hawezi katika hali hiyo inajuzu kukaa na mume wake katika nyumba moja lakini lazima asijidhihirishe mbele ya mume, na huwenda kubatilisha mkataba kukachelewa kwa miaka mingi lakini lazima asubiri na asiolewe na mwingine hadi mkataba wa ndoa ubatilike rasmi, ili asikabiliwe na matatizo mengi.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas