Madaraka ya kiongozi katika kuweka ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Madaraka ya kiongozi katika kuweka kikomo cha halali

Question

Ni maarufu katika masomo ya kifiqhi kutumia dalili ya msingi wa “Kiongozi ana haki ya kuweka kikomo cha halali”. Nini maana ya msingi huu? Na inawezekana kutumiwa kwa uwazi wake?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Miongoni mwa misingi asili ya kifiqhi ni mwenendo wa kiongozi kwa watu wake unafungamana na masilahi. Muradi wa masilahi ni yale ya kisheria na ya asili, au masilahi ya uwazi pamoja na masharti yake na si yaliyobatilishwa. Na masilahi yanatolewa kwa wote, na si kwa mtu binafsi. Kwa hiyo, mwenye madaraka na makamu wake wanalazimika kuyatumikia masilahi ya waislamu wote, na kutanguliza masilahi ya akhera kuliko ya dunia. Kiongozi ana haki ya kuandaa mambo mengi ya kujitahidi, kutokana na jitihada yake mwenyewe, baada ya kuangalia kwa makini, utafiti, uchunguzi, na kushauriana na wenye elimu na wenye uzoefu waaminifu, na kwa kuchunga kipimo cha msingi, nacho ni masilahi. Kwa hiyo, ana haki ya kufanya masuala mapya kadiri ya matatizo yanavyoonekana. Kupatikana kwa masilahi ya umma yenye masharti yake, mwenendo wa kiongozi kwa mujibu wa hayo ni wa kisheria na sahihi, na ni wajibu kuutekeleza na kuufanyia kazi, hivyo haijuzu kufanya hila kwa ajili ya kuuacha, kama ni wajibu wa wananchi wasikilize na watii. Ikiwa mwenendo wa kiongozi sio wa kisheria, hapo hakuna usikivu wala utiifu, kwa mujibu wa kauli yake Mtume S.A.W.: “Hakuna utiifu katika kumuasi Mwenyezi Mungu, lakini utiifu upo katika wema”. [Imepokelewa na Maimamu wawili]. Pia Imamu Muslim ameipokea, kutoka kwa Ibn Omar R.A., kutoka kwa Mtume S.A.W. amesema: “Mtu mwislamu lazima asikilize na kutii katika kila alilopenda na kila alilochukia, lakini akiamrishwa kuyafanya maasi, basi hapana usikivu wala utiifu”. Kwa hiyo, maoni ya asili ya watu wa Sunna kuwa: haijuzu kupambana na kiongozi mwislamu, hata akiwa dhalimu. Lakini inajuzu kupambana naye akidhihirisha kufuru kwa uwzi, wakati sisi tuna uthibitisho wa kweli kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Al-Khadimiy katika kitabu chake (Bariqat Mahmudiyah) anasema:
“Wote wameamrishwa kumtii mwenye madaraka, sharti afuate Sheria, lakini asipofuata Sheria na kumuasi kutasababisha upotovu mkubwa, pia wamtii, kwa sababu kufanya madhara madogo ni afadhali kuliko madhara makubwa. Na inafahamika katika Fiqhi kuwa: kila jambo la halali limeamriwa na kiongozi kwa ajili ya masilahi maalum, wananchi wanalazimika kulitekeleza” [1/62, Ch.ya Mustafa Alhalabiy].

Ibn Hajar katika kitabu chake Altuhfah anasema: “Inaonekana kuwa amri ya mwenye madaraka isiyokuwa na masilahi ya umma haiwajibiki kutekelezwa ila kwa nje tu, kwa ajili ya kujiepusha na madhara, kinyume cha iliyokuwa na masilahi, hapo inalazimika kutekelezwa kwa nje na ndani”. [3/71, Ch. ya Dar Ihyaa’ Alturaath Alarabiy]. Ibara hii ya “kiongozi ana haki ya kuweka kikomo cha halali” haitajwi katika vitabu vya misingi na vipimo vya Fiqhi, nayo ni miongoni mwa maana yanayotolewa na kipimo cha msingi, nacho ni masilahi.

Istilahi ya Mubaha (halali) maana yake: ni ile ambayo inalingana kati ya kuifanya au kuiacha, ambapo hakuna thawabu katika kuifanya wala adhabu katika kuiacha. Kwa mujibu wa hayo, kiongozi ana haki ya kuweka vikomo vya halali, wakati anapoona kuwa tendo hili linaleta masilahi ya umma. Pia ana haki ya kutoa amri ya kutekelezwa, na hayo yote ni miongoni mwa madaraka anayopewa kiongozi. Kiongozi kuweka kikomo cha halali kunahusisha mambo yanayoingia kimsingi katika madaraka yake, na kuwa na haki ya kuyatekeleza kwa kutumia siasa na jitihada zake, kama vile: mambo makuu ya dola yanayohusu jeshi, kuandaa taasisi na mali ya umma, uainisho wa mbinu na njia maalum kwa ajili ya utekelezaji wa kazi. Kwa hiyo, kiongozi hana haki ya kulazimisha watu wale chakula fulani wala kunywa kitu maalumu.

Kadhalika hana haki ya kuweka kanuni zinazoeleza sifa za mwanamke ambaye ana haki ya kuolewa; kama vile anakataza mwanamke mtaalamu aolewe na asiye mtaalamu, au kuwalazimisha watu wauziane kwa kutumia sarafu maalumu, au mengineyo yasiyokuwa na masilahi. Kinyume cha mambo yenye masilahi, kama vile kuzuia msichana asiolewe kabla ya kubaleghe, au kuainisha bei za vitu wakati wa mauziano kwa ajili ya kudhibiti soko ikitokea misukosuko, na mambo ya siasa ya kisheria, ambapo masilahi ya umma yanayotangulia masilahi binafsi.

Kiongozi hana haki ya kuzuia kitu miongoni mwa Mubaha (halali) kwa njia kamili. Kama vile kuzuia kula mlo kamili au kunywa kikamilifu, au kuzuia ndoa ya mitala. Kama kiongozi ataweka kanuni ya kuzuia mitala, basi haikubaliki, hata akidai kuwa ameiweka kwa ajili ya masilahi ya umma n.k. isipokuwa kuzuia huku kunafungamana na hali ya dharura na ya muda, na yeye anaona kuwa ni bora na kunafaa zaidi, ambapo haigongani na Sheria.

Dalili ya hayo, ni pale Mtume S.A.W. alipowalaumu baadhi ya masahaba wake, wakati walipotaka kutokula nyama, kutolala kitandani, kutooa wanawake, kama ilivyokuja katika Sahihi ya Muslim, kutoka kwa Anas kuwa: baadhi ya masahaba wa Mtume S.A.W. waliwauliza wake wa Mtume S.A.W. kuhusu kazi yake ya kisiri, na baadhi yao walisema: mimi sitaoa wanawake, na wengine wakasema: na mimi sitakula nyama, na wengine wakasema: na mimi sitalala kitandani, Mtume alimshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu, akasema: “Vipi watu hau wanasema hivyo? Ama mimi nasali na kulala, nafunga na kula, naoa wanawake, basi yeyote atakayeuacha mwenendo wangu atakuwa si katika wafuasi wangu”. Kwa hivyo, zuio huwa linakuwa kwa baadhi ya watu na si watu wote kwa ujumla. Na kumzuia mtu mmoja mmoja hunabadilika kutokana na masilahi. Ibn Taimiyah, katika maneno yake akizungumzia uwekaji bei anasema: “miongoni mwake huwa kuna dhulma na haijuzu, na miongoni mwake huwa kuna uadilifu na inajuzu. Ikiwa kuweka bei huko kuna kuwadhulumu watu na kuwalazimisha wauziane kwa bei ambayo hawaikubali, au kuwazuia kitu lilichohalalishwa na Mwenyezi Mungu, basi ni haramu. Lakini ikiwa uwekaji bei huo unaleta uadilifu kati ya watu kwa mfano kwa kuwalazimisha wauziane kwa bei nafuu na kuwazuia kupata faida zaidi waliyoharamishiwa na Mwenyezi Mungu, basi ni inajuzu, na ni wajibu”. [Majmuu’ Alfatawa, 28/76, Ch.ya Majma’ Al-Malik Fahd].

Huenda kiongozi akaweka kikomo katika mambo fulani si kwa njia ya kulazimisha, bali kwa kuchagua kilicho bora, na hii haiingii katika kikomo cha katazo, mfano wake ulivyokuja kutoka kwa Omar Ibn Al-Khattab R.A. wakati alipoweka kikomo cha hukumu ya uhalali wa kuoa wanawake wa watu wa kitabu (wanawake wasio waislamu), ambapo aliwazuia masahaba wakubwa kufanya hivi, ili waislamu wasiwafuate katika jambo hili, na hii husababisha masilahi ya wanawake wa watu wa kitabu (wasio waislamu) na madhara ya wanawake kiislamu. Pia wanawake wengi wa watu wa kitabu hawajiepushi na zinaa, huenda hali hii ikapelekea kuoa kahaba.

Kwa hiyo, Omar alipoweka kikomo cha jambo hili hakutaka kulizuia wala kuliharimisha, bali alijali maslahi ya waislamu na kuyatanguliza mbele. Na iwapo mmoja wa masahaba wakuu atakwenda kinyume na hayo, basi hatamuadhibu kwa kufanya hivyo. Na wakati huo huo, hukumu hii si kwa wote, bali inalihusu kundi la watu maalumu. Al-Baihaqiy na Al-Tabariy wamepokea kutoka kwa Shaqiq amesema: Hudhaifah alimuoa mwanamke wa kiyahudi, Omar akamwandikia: mwache, akamjibu: unaona kuwa haramu hata nikamwacha, Umar akajibu: sioni kuwa haramu, lakini ninaogopa kuwaoa makahaba miongoni mwao. Ibn Jarir alieleza hivyo akisema: “Omar alichukia kuona Talhah na Hudhaifah, Mungu awarehemu, wanaoe wanawake wa kiyahudi au kikristo kwa kuogopa watu watawafuata na hii husababisa kuwacha wanawake waislamu, au kwa sababu nyingine. Kwa hiyo, Omar akawaamrisha kuwaacha”. [Jamii’ Albayan 4/716, Ch. ya Dar Hajar].

Kwa mujibu wa yaliyotangulia: inatambulika kuwa ibara ya “Kiongozi ana haki ya kuweka kikomo cha halali” ingawa haikuja katika vitabu vya misingi, lakini maana yake ni sahihi, na inapatana na ilivyotajwa katika masuala ya kifiqhi na hukumu za Sheria ya Kiislamu. Na suala hili halitekelezwi kwa uwazi wake, lakini kiongozi ana haki ya kuweka kikomo cha halali kwa mujibu wa madaraka yake katika ulezi wa masilahi ya umma.
Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yote.
 

Share this:

Related Fatwas