Ndoa ya Muta’a, Ndoa ya Muda Mfupi...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ndoa ya Muta’a, Ndoa ya Muda Mfupi, na Ndoa kwa Nia ya Talaka.

Question

Ni nini ndoa ya muta’a? Na ni nini hukumu yake? Na je, ndoa ya muta’ani ile ile ya muda mfupi? Na pia ni ile ile ya nia ya talaka? 

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Neno muta’a katika lugha ya Kiarabu maana yake kama alivyotaja Ibn Mandhuur: “Kuoa ndoa ya muta’a wakati hutaki kuidumisha ndoa hiyo.” [Lisaan Alarab: 6/4127, Ch. ya Dar Al-Maarif].
Ndoa ya muta’a ni aina moja ya Nikahi za Al-Jahiliyyah, na ilikuwa halali mwanzoni mwa Uislamu, lakini ikaharamishwa baadaye. Na sura yake: Mtu mmoja anasema kumwambia mwanamke fulani: Nitakulipa kitu fulani, sharti nilale nawe kwa nia ya kustarehe kwa muda maalumu, kama vile mwezi mmoja, mwaka mmoja au mfano wake, na iwe muda huo unaeleweka au haueleweki.Au mtu akisema: Nitakulipa kitu kadhaa sharti nipe muta’a, yaani nistareheshe muda wa msimu wa Hija, au muda wa kukaa kwangu katika mji huu, au mpaka fulani aje. Na ukifika wakati ulioainishwa mtengano utatuka bila ya talaka.
Hukumu ya nikaha hiyo ni haramu, kwa mujibu wa madhehebu manne na mengineo. Kadhalika, haitambuliwi ndoa ya aina hii, iwe Nikahi, kwa kuthibitika kutenguliwa, na kutokuwa na masharti sahihi ya ndoa.Basi, uharamisho wake kwa wanazuoni wa madhehebu ya Sunnah unakaribia kauli ya pamoja.
Tunasema (unakaribia kauli ya pamoja) kwa kunukuliwa na Ibn Abbas RA kuwa inajuzu, pia kwa wenzi wake wengi wa Ibn Abbas kuwa inajuzu kama Attaa na Tawus, na pia Ibn Juraaij. Lakini imenukuliwa kuwa Ibn Abbas aliibadilisha rai yake hii baadaye.
Ibn Qudamah alisema: “Kuhusu kauli ya Ibn Abbas, imepokelewa kuwa aliibadilisha. Aidha, Abubakr alipokea kwa Isnaad yakena Said bin Jubair kuwa alisema: Nilimwambia Ibn Abbas: Umezungumza mengi kuhusu ndoa ya muta’a hata watu wengi wanajua hivyo, Je unasema nini? Ibn Abbas alisimama kuhutubia, akasema: Hakika ndoa ya Mutaa ni sawa na nyamafu, damu, na nyama ya nguruwe” yaani katika uharamu. [Al-Mughniy na Ibn Qudamah: 10/48, Ch. ya Dar Aalam Al-Kutub].
Inaonekana kuwa Ibn Abbas alikuwa akiona kwamba ndoa ya muta’ani haramu kama vile nyamafu na nyama ya nguruwe, kwa maana ya ikiwepo dharura basi inajuzu.Pia imenukuliwa na wanafunzi wa Ibn Abbas kuwa ni halali.
Hivyo, imenukuliwa na madhehebu manne ya kifiqhi na mengineyo kuwa ni haramu. Wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy walielekea kuwa ndoa ya muta’a ni batili. Ibn Ali Al-haddadiy Al-Abbadiy alisema: “Ndoa ya muta’a na ya muda mfupi ni batili”, na sura yake ni: Mtu mmoja anamwambia mwanamke mmoja: Chukua kiasi hiki cha fedha kwa ajili ya kunistarehesha siku kadhaa.Na hii ni batili kwa wanazuoni wote wa Fiqhi.
Na sura ya ndoa ya muda mfupi ni kufunga ndoa kwa kuwepo mashahidi wawili pamoja na kuwepo muda maalumu kama vile, siku kumi au mwezi mmoja. Zufar anaona kuwa ni sahihi, kwa sababu ndoa haibatilishwi kwa masharti yasiyo sahihi. Na tofauti kati ya aina hizi mbili kuwa tamko la kuoza limetajwa katika ndoa ya muda mfupi, lakini halitajwi katika ndoa ya muta’a. Kwa muono wa Zufar, ndoa ya muda mfupi inajuzu kwa sababu sharti la muda linabatilishwa, kwa hiyo ndoa inaendelea kudumu, kwa sababu asili ya ndoa ni kuwa kwake ya kudumu. Na kama akisema: Nakuoa sasa na baada ya siku kumi nitakuacha, ndoa inajuzu, kwa sababu sharti la muda haliathiri kuwa ndoa ni milele. [Al-Jawharah Al-Naiyyrah na Al-Abbbaadiy, 2/18, Ch. ya Al-Matba’ah Al-khairiyyah].
Al-Sarkhasiy alisema: “Kama akisema: Nakuoa muda wa mwezi mmoja, na mwanamke akakubali, basi hii ni muta’a na si ndoa sahihi kwa mujibu wa maoni yetu”. [Al-Mabsuut na Al-Sarkhasiy, 5/153, Ch. ya Dar Al-Ma’arifah].
Al-Kasaniy alisema: “Kumwambia mwanamke: Nitakupa pesa fulani, sharti nistareheshe kwa mfano muda wa siku moja, mwezi mmoja au mwaka mmoja.Na hakika, hii ni batili kwa maoni ya wanazuoni wengi”. [Badai`I Al-Sanai`i Fi Tartiib Al-Sharai`i na Al-Kasaniy 2/272, Ch. ya Dar Alkutub Al-Ilmiyyah].
Ibn Abidiin alisema: “Ndoa ya mut’a na ndoa ya muda mfupi zimebatilishwa, kama ilivyokuja katika kitabu cha (Al-Fath) kuwa Shiekh wa Uislamu alitofautisha kati ya aina hizi mbili za ndoa kwa njia ya tamko; akitaja muda basi ni ndoa ya muda mfupi, au akitaja muta’a basi ni hiyo hiyo. [Hashiyat Ibn Abidiin, 3/52, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyyah].
Wafuasi wa madhehebu ya Malik wanaona kuwa ndoa ya muta’a ni ndoa ya muda mfupi yenyewe, na walielekea kuwa batili, wakapokea kauli ya pamoja, na wakaihesabia kama ni ndoa ya mke wa tano au ndoa ya kukusanywa madada wawili. Abul-Hassan Al-Malikiy alisema: “Kadhalika haijuzu ndoa ya muta’akwa kauli ya pamoja, nayo ni ile ndoa ya muda mfupi, kwa sifa hasa pasipo na walii, mashahidi wala mahari.
Ibn Abdel-Bar na Ibn Rushdi walisema: Ni ndoa yenye mahari, mashahidi na walii, lakini imeharibika kwa sababu ya kuweka muda. Kwa hiyo, lazima ibatilishwe, si kwa njia ya talaka, mume na mke waadhibiwe si kwa daraja ya Haddu, watoto kama watazalika, wanasibishwe na baba yao. Kuhusu mke, ana Edda kamili, hana mahari ikiwa utengano ulikuwa kabla ya kuingiliana, lakini baada yake kama ikiwekwa mahari basi ni haki yake, na isipowekwa, basi ana haki ya mahari ya ndugu zake. Hivyo, ubatilisho wa aina hii ya ndoa ni kutokana na mkataba wake”. [Kifayat Al-Talib Al-Rabbaniy, Sharh Al-Risalah, 2/53, Ch. Dara Al-Fikr].
Ibn Mhanna Al-Nafrawiy alisema: “Haijuzu maana yake ni haramu; ndoa ya muta’a. Nayo ni ndoa ya muda mfupi, kwa ilivyopokelewa kuwa: Yeye (Mtume S.A.W.) aliikataza mwaka wa ufunguziwa Makkah. Na Al-maziriy alitaja kauli ya pamoja kuhusu uharamu wa ndoa hii mpaka siku ya Kiyama, kama ilivyokuja katika mapokezi; Hapo hapana hitilafu ya rai hii isipokuwa kwa baadhi ya wazushi”. [Al-Fawakih Al-dawaniy, Sharh Al-Risaalah, 2/12, Ch. ya Dar Al-Fikr].
Sheik Uleish alisema: “Kuvunja ndoa iliyo batili ambayo huvunjika milele, ni mfano wa ndoa ya tano, na ndoa ya muta’a”. [Manhu Al-jaliil, Sharh Mukhtasar Khaliil, 4/40, Ch. ya Dar Al-Fikr].
Wafuasi wa madhehebu ya Shafiy walielekea kuiharamisha. Al-shiraziy katika kitabu cha Al-Muhadhab: [2/446-447, Ch. ya Dar Al-kutub Al-Ilmiyyah]alisema: “Haijuzu ndoa ya muta’a, na sura yake ni mtu akisema: Ninakuozesha mwanangu wa kike muda wa siku moja, au mwezi mmoja; kwa ilivyopokelewa na Muhammad bin Aly R.A kuwa alimsikia baba yake Aly R.A alipokutana na Ibn Abbas na kupewa habari kuwa yeye anaruhusu ndoa ya muta’a, hivyo, Aly R.A akamwambia: Wewe mtu wa kusahau, maana Mtume S.A.W aliikataza katika siku ya Khaibar, na pia nyama ya punda wa kufugwa”. Na kwa sababu ndoa hii ni aina ya mkataba, unaojuzu kwa milele si kwa muda mfupi kama kuuziana kitu, pia aina hii ya ndoa haihusishwi na talaka, dhihari, urithi, na Eda ya kifo, hivyo ni batili kama vile aina zote za ndoa batili.
Wafuasi wa madhehebu ya Hanbal walielekea, kutokana na rai sahihi, kuwa Mutaa ni batili. Ibn Qudamah alisema: “Maana ya ndoa ya muta’a ni kuoa mwanamke kwa muda, kama vile kusema: Nimekuozesha mwanangu wa kike kwa muda wa mwezi mmoja, au mwaka mmoja au kwa kumaliza msimu huu au kurejea kwa mahujaji n.k. Na uwe muda huo unafahamika au haufahamiki. Maana ndoa hii ni batili, na imeainishwa hivyo na Ahmad, naye akasema: Ndoa ya muta’a ni haramu.
Abubakr alisema: kuna mapokezi mengine yanamaanisha kuwa Makruhi na si haramu; kwa sababu Ibn Mansuur alimwuliza Ahmad juu ya suala hili, akajibu: Afadhali mtu ajiepushe nayo. Akaongeza: Ni wazi kuwa ni makruhi na si haramu, Lakini wenzetu wengine, bila kuwamo Abubakr, wanakataza hivyo, wanasema: Suala hili lina mapokezi mamoja yaliyomaanisha kuwa ni haramu. Na hiyo ndiyo kauli ya jumla ya Masahaba na Wanazuoni wa Fiqhi”. [Al-Mughniy, na Ibn Qudamah 7/ 571, Ch. Ya Dar Al-Fikr].
Kwa hivyo, maelezo yaliyotangulia yanaonesha maoni ya Wanazuoni wa Fiqhi wa Madhehebu manne na kauli zao kuhusu aina ile ya Ndoa. Vile vile, Madhehebu ya Dhahiriyyah yanakubali kuwa Ndoa ya Muta’a ni haramu; katika kitabu cha Al-Muhallaa: “Abu Muhammad anasema: Ndoa ya Muta’a haijuzu. Nayo ni ile Ndoa inayoainishwa kwa muda mfupi, ingawa ilikuwa halali wakati wa Mtume S.A.W, kisha Mwenyezi Mungu akaifuta kwa ulimi wa Mtume wake S.A.W, mfuto halisi, mpaka siku ya Kiyama”. [Al-Muhalla na Ibn Hazm, 9/127, Ch. Ya Dar Al-Fkr].
Katika Madhehebu ya Al-Zaaidiyyah, Ahmad bin Yahya bin Al-Murtada alisema: “Imeharamishwa Ndoa ya Mut'aa, nayo ni ile Ndoa ya Muda; kwa mujibu wa kukatazwa kwake na Mtume S.A.W, na Ali (Alaihis Salaam) pia”. [Al-Bahr Al-Zakhaar na Ahmad bin Yahya Al-Murtada 4/22, Ch. Ya Dar Al-Kitaab Al-Islamiy].
Katika Madhehebu ya Ibadhiy: Ibn Issa Atfiish alisema: “Ndoa ya Muta’a ilifutwa kwa Aya ya Mirathi, nayo ni Aya ya kutaja Mirathi ya mume na mkewe, kutokana na kwamba ndoa ya Muta’a haina utaratibu wa kurithiana. Kwa hiyo, wengine walisema: Mirathi ya mume na mkewe hutokana na Ndoa, kwa hiyo, Ndoa ya Muta’a imefutwa. Na imesemekana kuwa imefutwa kwa Aya za Talaka, Mirathi na Eda, baada ya kuwa ilikuwa inajuzu hapo kabla”. [Sharhu-Niil wa Shifaaul Aliil na Muhammad bin Yusuf bin Issa Atfiish 6/318, Ch. Ya Maktabatul Irshaad].
Mafaqihi wa Ahlus-Sunna na wengineo walitoa dalili nyingi za kuharamisha ndoa ya muta’a miongoni mwake: Bukhariy, na Ali R.A, kuwa alimwambia Ibn Abbas RA, kuwa: Mtume S.A.W, alikataza ndoa ya muta’a na nyama ya punda wa kufugwa zama za Khaibar.
Ilikuja katika pokezi la Muslim kuwa Mtume S.A.W, alisema: “Enyi watu, mimi nilikuruhusuni katika ndoa ya muta’a, lakini Mwenyezi Mungu ameharamisha hivyo mpaka siku ya Kiyama, basi mwenye kuwa na yeyote miongoni mwao awaache na wala msichukue chochote katika vile mlivyowapa"
Katika hadithi ya Ibn Hibbaan, Daraqutniyna Al-Baihaqiy kutoka kwa Abi Hurairah kuwa Mtume S.A.W, aliposhuka mahala pa Thaniyyatul-Wadaa’ aliona taa, akasikia wanawake wakilia, akasema: Ni nini? Wakasema: Ewe Mtume, ni wanawake walioolewa ndoa ya muta’a, Mtume alisema: imevunjwa au imeharamishwa kwa mujibu wa ndoa, talaka, eda na mirathi”.
Hawa wanaosema kuwa inajuzu ndoa ya muta’a, ambao wafuasi wa Shia Imamiyya, wameandika hukumu zake katika vitabu vyao vya fiqhi. Ja’far bin Hassan Al-Hudhliy alisema: “Hukumu zake ni nane: kwanza: kuwepo muda na mahari, basi mkataba ni sahihi, kuwepo muda na mahari haikuwepo, basi mkataba ni batili, na kama muda tu hautakuwepo ndoa ya muta’a itabatilika na mkataba utakuwa wa kudumu.
Pili: kila sharti linaloshurutishwa lazima lifungamane na tamko la mapatano (Ijaab) na maridhiano (Qabuul), kwa hiyo, hakihesabiki kilichotajwa kabla ya mkataba wala baada yake.
Tatu: Mwanamke aliyevunja ungo na mwenye akili, ana haki ya kujioozesha mwenyewe ndoa ya Muta’a , na walii wake hana haki ya kumpinga, ni sawa sawa akiwa msichana au mwanamke.
Nne: inajuzu kuweka sharti ya kuonana kimwili mchana au usiku, au kuainisha mara kadhaa kila wanapokutana.
Tano: Inajuzu kutomwagia manii ndani (Azl), hali ya kuonana, bila ya idhini ya mwanamke, akipata mimba, basi mtoto ni wake, hata kama mume atamwaga manii nje kutokana na uwezekano wa manii hayo kuingia bila yeye kujua, na mwanamume akimkana mtoto, basi mtoto huyo atakuwa amekanwa, lakini bila ya kufanya Lia’an.
Sita: haituki talaka ila katika muda unapofikia, na vile vile, haipatikani Iilaa’ wala Lia’an wala Dhihaar.
Saba: Mkataba wa aina hii hauna mirathi kati ya mume na mke, ikiwa kwa kushurutishwa au la, kama ikishurutishwa na pande mbili au mmoja wao, inasemwa kuwa: Inalazimika kwa mujibu wa sharti, na inasemwa kwamba: Hailazimiki, kwa sababu kulazimika ni kutokana na Sheria, na hali hii ni sharti kwa asiye mrithi, mfano wake kuweka sharti kwa mgeni, lakini kulazimika ni rai iliyo mashuhuri.
Nane: Muda wake ukifika baada ya kuingiliwa, eda yake inakadiriwa kwa hedhi mbili, ingawa inasemekana kuwa ni kwa hedhi moja, lakini si rai yenye nguvu, kama mke hapati hedhi na ilhali hajafikia kukatika hedhi, basi eda yake siku arubaini na tano. Na eda huanzia baada ya kifo cha mume, kama hapakuwepo maingiliano, basi eda ni miezi minne na siku kumi, kwa mwanamke asiyekuwa na mimba na vile vile kwa mwenye mimba. Akiwa mke ni mjakazi na ilhali hana mimba, basi eda yake ni miezi miwili na siku tano”. [Sharaiul-Islam Fi Masaailil-Halali wal Haraam na Ja’far bin Al-hassan Al-Hudhliy 2/250-251, Ch.ya Muassasat Matbua’aty-Ismailiaan].
Hadithi hii ilivyopokelewa na Ibn Abbas R.A na wengi wa Masahaba, kama ilivyopita, na dalili yao ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu : {Basi walemnaowaoa miongoni mwao wapeni mahari yao}. [AN NISAA: 24].
Lakini wanazuoni wa Fiqhi wa Ahlus-Sunna wanaona kuwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi walemnaowaoa miongoni mwao wapeni mahari yao}. [AN NISAA: 24], Inamaanisha Ndoa; kwa sababu maudhui ya Aya tangu mwanzoni mwake mpaka mwisho, ni Ndoa.Vilevile, Mola alitaja aina za wanawake wanaoharamishwa kwa njia ya Ndoa, kisha akaruhusu wengine pale pale kwa njia ya Ndoa, na hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mmehalalishiwa (kuoa wanawake) wasiokuwa hao. Muwatafute kwa mali yenu}. [AN NISAA: 24],Yaani kwa njia ya Ndoa.
Wanazuoni wa Fiqhi wa Madhehebu ya Shia walitoa dalili ya Hadithi ya Jaabir iliyipokelewa na Ahmad katika kitabu chake cha Musnad, akisema: Zilikuwa Muta’a mbili katika zama za Mtume S.A.W, lakini Umar R.A alituzuia tusizitekeleze, basi tukaacha.Vile vile, wakatoa dalili ya Hadithi zinazoruhusu Ndoa ya Muta’a kabla ya kufutwa kwake; kwa sababu kufutwa kwa hukumu hakujathibiti kwao.
Al-Shawkaniy alisema: “Pana jibu linalohusu Hadithi ya Jaabir kuwa: Masahaba walifanya hivi wakati wa Mtume S.A.W, lakini jaabir hakujua hukumu ya kufutwa mpaka Umar R.a, alipoikataza, vile vile Masahaba walifanya hivi bila ya kujua, lakini Umar alipoikataza, watu walikubali. Ingawa jibu hili halifungamani na rai isiyo na nguvu, lakini hupelekea hukumu ya Hadithi sahihi iliyopokelewa na Sabura, nayo ni kutangaza uharamu wa milele. Na kuwa kuwapinga baadhi ya Masahaba kwa hukumu hakuitengui, na wala hakuruhusu katika kuitekeleza, kwani Masahaba walio wengi walielewa Uharamu wake, wakautekeleza, na wakaupokea kwa ajili yetu. Kwa hiyo, Umar R.A alisema katika mapokezi yake na Ibn Majah, kwa Isnaadi sahihi kuwa: Mtume S.A.W, ameturuhusu katika Muta’a mara tatu, lakini aliiharamisha baada ya hapo, na naapa kwa Allah, sijui mtu ye yote anayefuata Muta’a akiwa ameoa, nitampiga mawe, au kunipa mashahidi wanne wanaokiri kuwa Mtume S.A.W, aliihalalisha baada ya kuharamishwa. Abu Huraira R.A, alisema: Katika kauli yake Mtume S.A.W: “Muta’a imeondoshewa Talaka, Eda, na Mirathi”, Imepokelewa na Dar Qutniy, na Al-Hafidh. [Nailul-Awtaar na Al-Shawkaniy 6/164 Ch. Ya Dar Al-Hadiith].
Kwa hiyo, ndoa ya Muta’a ina sifa maalumu.Ilikuwa Ndoa hii katika ndoa za zama za Ujahili, ikawa halali katika Uislamu, kisha ikafutwa. Kwa mujibu wa maelezo hayo, ndoa hii ni batili na haifungiki, na wala haihalalishi tupu za wanawake.Na hii ni kwa maoni ya wanazuoni wa Fiqhi wa Ahlus-Sunna, na kauli ya pamoja iliyopo kwa wafuasi wa Madhehebu ya Malikiy, kwa mtazamo wa kuwa ni aina maalumu ya ndoa ambayo ndani yake kuna baadhi ya mapokezi ya kauli za wanachuoni. Vile vile, katika mkataba huu wa ndoa hii, hakuna masharti na nguzo za ndoa iliyo sahihi, kwa hiyo ni batili; kadhalika kutokuwepo mambo ya lazima kwa ndoa huisababisha kuwa batili.Kama vile: Sharti la kuwepo Walii; sharti la kuwepo Mashahidi; kuainisha muda kwa sababu ndoa haifungamani na muda mfupi; kutaja maneno kama kustarehe na kujistarehesha badala ya kufunga ndoa. Kwa kukosa kwake tamko linalokubalika kisheria.
Ingawa ndoa ya muta’a ni batili, lakini ikipatikana itakuwa na jumla ya hukumu zifuatazo:-
1- Mwanamke wa ndoa ya Muta’a hana talaka, wala Ilai’, wala dhihari, wala lia’ni, na hakuna mirathi kati ya mume na mke, kadhalika hakuna Ihswani (yaani kuwepo uhusiano wa ndoa) kati ya pande mbili, wala hatarejewa mwanamke na mume wa kwanza baada ya kutalikiwa kwa mara ya tatu.
2- Wasipoingiliana, basi hakuna mahari wala Muta’a wala matumizi ya fedha. Mume akimwingilia mke, basi mke ana haki ya mahari, kadiri ya mahari ya ndugu zake, hata ikiamuliwa kiwango maalumu, na hii ni kauli ya wafuasi wa madhehebu ya Shafiy, Ahmadi, na Maliki, kwani kutaja muda husababisha kasoro juu ya mahari. Wafuasi wamadhehebu ya Hanafiy wameelekea kuwa wakati wa kuingiliana, basi mwanamke ana haki ya mahari inayopungua kadiri ya mahari ya ndugu zake, na pia iliyoamuliwa kabla ya hapo, kutokuwepo kiwango maalumu kabla ya hapo, basi ana haki ya mahari kadiri ya ndugu zake, kufikia kiasi cho chote.Wafuasi wa Maliki na Hanbali walielekea kuwa mke ana haki ya kadiri inayoamuliwa na hali ya kuingiliana, na hii ni rai ya Al-Lakhmiy wa Madhehebu ya Malikiy, kwa sababu kasoro yake inapatikana kwa kufungika ndoa hiyo.
3- Mwanamke wa ndoa ya Muta’a akizaa, basi mtoto ni wa mume, hali mume akidhani ndoa hii ni sahihi au siyo, kwa sababu kuna mkataba, na mwanamke katika hali hii ni mke. Muda wa nasaba unahesabika kwa kumwingilia mwanamke,na wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy wanaikubali rai hii.
4- Kwa kumwingilia mwanamke katika ndoa ya Muta’a kunapatikana uharamu wa ukwe wa mume na mke na babu zao na vizazi vyao.
5- Hakuna adhabu ya zinaa kwa pande mbili yaani mume na mke katika ndoa ya Muta’a kwa sababu adhabu ya aina hii huondolewa kwa shaka, na shaka iliyopo hapa ni tofauti ya maoni ya wanazuoni wa Fiqhi. [Rejea: Al-Mughniy 6/393 na 7/11, Ch. Ya Maktabat Al-Kahira].
Kuhusu ndoa ya Muda mfupi, yakipatikana masharti ya mkataba sahihi kama vile: Mashahidi,Tamko la ndoa, na Walii kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa Fiqhi, na kuainishwa kwa muda, basi ina aina mbili:
Kwanza: Kuwa na muda wa kutazamiwa kuufikia, katika hali hii ni batili na haijuzu kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa Fiqhi, na tofauti kati yake na ya Muta’a ni tamko la Ndoa; kuhusu ndoa ya Muda, tamko lake ni ndoa au nikahi, lakini kwa Muta’a ni kustarehe au kujistarehesha’. Vile vile, ndoa ya muda mfupi ni sahihi kwa rai ya Zufar, na sharti la"Muda" halihesabiwi.
Ibn Ali Al-Haddadiy Al-Abbaadiy alisema: “ Sura ya ndoa ya Muta’a ni kumwambia mwanamke: Chukua Dola kumi, kwa mfano, na unistareheshe siku kadhaa.Na hii ni batili kwa kauli ya pamoja. Na sura ya ndoa ya Muda ni kuwa: Mtu amwoe kwa kuwepo mashahidi wawili,kwa muda wa siku kumi au mwezi mmoja, kwa mfano. Zufar alisema: Ndoa ya aina hiyo ni sahihi; kwa sababu ndoa haibatilishwi kwa masharti batili. Na tofauti kati ya aina mbili hapo juu ni: Kutaja tamko la ndoa katika ndoa ya Muda mfupi, na kutotaja katika ya Muta’a. Kwa hivyo, rai ya Zufar ni katika hali ya kujuzisha ndoa ya Muda mfupi pamoja na kuwapo sharti.Na lile sharti halihisabiwi, na ndoa yenyewe inaendelea milele, kwa kuwa asili ya ndoa ni kudumu milele. Na mume akisema kumwambia mwanamke: Ninakuoa kwa sharti nikuache baada ya siku kumi kwa mfano, basi ndoa katika hali hii inajuzu, kwa sababu mkataba wa ndoa ni wa kudumu, lakini sharti lililopo ni kwa muda, basi ndoa hujuzu na sharti hubatilika”. [Al-Jawharatun-Naiyrah na Abu-bakr Muhammad bin Ali Al-haddadiy Al-Abbaadiy 2/18-19, Ch. ya Al-Matbaa’ Al-Khairiyyah].
Pili: Kuwa na muda wa kutotazamiwa kuufikia.Wafuasi wa Madhehebu ya Hanafiy na Hanbal na Abul-Hassan wa malikiya na Al-Balqiniy pamoja na baadhi ya wafuasi wa Madhehebu ya Imamu Shafi, walimili ya kuwa: Muoaji akiweka muda, na muda huo ukawa hautazamiwi kuufikia, basi ndoa ni sahihi, kana kwamba ametaja milele, kwa sababu ndoa kwa kawaida haizidi kuliko hivyo ilivyotajwa, na kutaja muda mrefu hakudhuru. Al-Balqiniy alisema: Katika kauli ya Imam Shafiy iliyopo katika kitabu chake cha AL-UMMU, dalili wazi, na baadhi ya wafuasi wake walimfuata. Ilikuja katika ALFATAAWA ALHINDIYYAH kunakiliwana Shamsul-Aimmah Al-Halawaniy na pia wengi wa wafuasi wa Hanafiy kuwa: Wakiweka muda mrefu usiotazamiwa kufikika kwa mfano miaka elfu moja, basi ndoa inafungika na sharti inabatilika.Na mfano wake kama kwa mfano,wawili hao walioana hadi siku ya Kiyama au kutoka kwa Al-Dajjaal au kuteremka kwa Issa A.S. Baadhi ya wafuasi ya Shafiy walisema: Akimwambia mwanamke: Ninakuoa muda wa maisha yako, basi hii si ndoa ya mutaa’, wala ya muda mfupi kwa sababu muda kama huu ni wa kawaida, na athari yake inabakia baada ya kufa.Wafuasi wa Malik katika madhehebu na wa Shafiy isipokuwa Al-Balqiniy walielekea kuwa: Ndoa ya muda kwa miadi haitazamiwi kuifikia ni batili. [Rejea: Mughny Al-Muhtaaj na Al-Khatiib Al-Shirbiiniy 3/142, Ch. ya Dar Al-Fikr; Hashiyatus-Sawiy Ala Ashrhus-Saghiir 2/387, Ch. ya Dar Al-maarif; Badaii’ Assanaii’, 2/273, Ch. ya Al-Maktabah Al-Ilmiyyah].
Kuhusu ndoa pamoja na kuficha nia ya talaka baada ya muda mfupi si ndoa ya Muta’a wala ya Muda mfupi, lakini ni ndoa yenye nguzo na masharti. Wanazuoni wa Fiqhi, wamehitilafiana katika kujuzu kwake.Wafuasi wa Hanafiy, Malik, Shafiy, na Hanbal katika mapokezi yaliyomo katika kitabu cha Al-Mughny na maelezo yake kuwa: Akimwoa mwanamke kwa nia ya kutoa talaka baada ya mwezi mmoja au zaidi au kwa uchache, basi ndoa hiyo ni sahihi, iwe mwanamke huyo alijua au hakujua, na pia walii wake awe alijua au laa; kwa sababu ya kutokuwepo katika ndoa hii sharti lolote linaloivuruga ndoa hiyo, na wala ndoa hiyo haibatiliki kwa nia, kwa sababu huenda muoajia kanuia asichokifanya, na akakifanya asichokinuia.Na kwa kuwa kuainisha muda ni kunatokana na tamko na wala si kwa nia.
Wafuasi wa Hanbal kwa rai sahihi katika Madhehebu na Al-Awzaaiy, Mwenyezi Mungu amrehemu, walielemea katika hukumu ya kuwa ndoa hii ni batili, kwa kuzingatia kuwa ni aina ya ndoa za mutaa’, na Bahraam wa Malikiyyah ana rai hiyohiyo. Na hasa mwanamke akifahamu jambo lililokusudiwa na mwanamume ndani ya nafsi yake.
Ibn Khalaf Al-Bajiy alisema: “Aliyeoa mwanamke ilhali hataki kuendelea naye, lakini tu anataka kustarehe naye kwa muda maalum kisha amwache, Malik katika mapokezi ya Muhammad alisema: Inajuzu lakini si tendo jema, wala tabia nzuri. Na maana ya hayo, kama alivyosema Ibn Habiib kuwa: ndoa imefungwa kwa kawaida, na mwanamume hakuweka sharti, lakini ndoa ya mutaa’ ni ile yenye sharti ya kuachana baada ya kumalizika muda wake. Malik alisema: Mwanamume huenda akamwoa mwanamke kwa nia ya kutoendelea naye baada ya muda, lakini kutokana na tabia yake nzuri anaona ni vizuri kubaki naye, na huenda akamwoa mwanamke, kwa nia ya kubakia naye na kutokana na tabia yake mbaya anaona ni vizuri kumwacha. Mambo kama hayo hayaathiri katika ndoa, kwa sababu mwanamume ana haki ya kuendelea kuwa na mke wake au kumwacha.Hakika muda ndio unaoitengua ndoa”. [Al-muntaqa Sharh Al-Muwatta’ na Suleiman bin Khakaf Al-Bajiy 3/335, Ch. ya Dar Al-Kitaab Al-Islamiy].
Sheikh Zakariya Al-Ansariy alisema:”Akimwoa bila ya sharti,bali akawa ana nia ya kumwacha baada ya kumuingilia, basi huchukiza, na ndoa huwa ni sahihi, na mke anakuwa halali kutokana na kumuingilia”.
Al-bijermiy katika maelezo yake juu ya rai hii alisema: “Kauli yake (Bali ana nia ya kumwacha baada ya kumuingilia) yaani walikuwa wamekubaliana hivyo kabla ya kufunga ndoa; na kauli yake (Huchukiza) yaani kila jambo ambalo kama lingesemwa lingebatilisha inachukiza kulificha”. [Manhaj Al-Tullaab na Sheikh Zakariya Al-Ansariy kwa maelezo ya Al-Bijermiy 3/368, Ch. ya Dar Al-Fikr Al-Arabiy .Rejea pia Almughniy 7/180].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: Ni wazi kuwa ndoa ya Muta’a, ni batili. Na ubatili wa ndoa ya muda mfupi ni ile inayokuwa na muda wa kutazamiwa kuufikia kwa kawaida, lakini kama muda hautazamiwi kuufikia kuna tofauti, na rai iliyochaguliwa na wanazuoni ni kujuzu kwa ndoa hii. Vile vile, inajuzu ndoa ya kuambatana na nia ya talaka kutokana na rai ya wanachuoni wengi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas